MAITI YA MTU AMBAYE HAKUWEZA KUFAHAMIKA IMEKUTWA IMEFUKIWA KWA MAWE NA UDONGO HUKO MAKOKO KATIKA MANISPAA YA MUSOMA
KAMANDA WA JESHI LA POLISI MKOANI MARA ABSALOM MWAKYOMA AKIWA NA MWANA HABARI GEORGE MARATO |
Maiti ya mtu mmoja ambaye hakuweza kufahamika imekutwa imefukiwa kandokando ya miamba ya milima kwa mawe na udongo katika mtaa wa Nyarigamba Kata ya Makoko Manispaa ya Musoma na kuendelea kuwa na hofu kwa Wananchi juu ya mauaji yanayoendelea kutokea katika maeneo mbalimbali katika siku za hivi karibuni.
Katika taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoani Mara ilisema awali kulikuwepo na uvumi uliohusisha mwili wa marehemu na mwanamke mmoja ambaye amepotea na hajulikani alipo toka tarehe 14.12.2012 katika mazingira ya utatanishi anayeishi katika mtaa wa Ziwani katika kata hiyo ya Makoko.
Taarifa hiyo ilisema baada ya Mwili huo kufanyiwa uchunguzi na madaktari katika hospitali ya Mkoa wa Mara imebainika kuwa mwili huo uliokuwa umefukiwa haujulikani ni wa nani huku ndugu wa Mwanamke aliyepotea wamethibitisha mwili huo sio wa ndugu yao.
"Natoa wito kwa Wananchi wa Musoma na vitongoji vyake pamoja na sehemu nyingine wafike katika Hospitali ya Mkoa wa Mara katika chumba cha kuhifadhia maiti ili kujaribu kuutambua mwili huo ambao umehifadhiwa pale,"alisema Kamanda Mwakyoma.
Mmoja wa shuhuda wa tukio la kufukuliwa kwa mtu huyo Vedastus Masige aliyezungumza na bLOG HII alisema Jeshi la Polisi bado halijaweka nia ya dhati ya kukabiliana na matukio hayo licha kulipotiwa na vyombo vya Habari lakini wamekuwa wakipuuzia huku Wananchi wakiendelea kuangamia.
Alisema hawajasikia Jeshi la Polisi limefikia wapi katika kuchukua hatua juu ya kukabiliana na hali hiyo huku mauaji yakiendelea kutokea na kuwafanya Wananchi wakiishi kwa mashaka na wasiwasi kutokana na hali hiyo inavyoendelea kutokea.
''Tulishuhudia katika siku za nyuma Jeshi la Polisi likihamia Wilayani Serengeti likiongozwa na Kamanda wa Oparesheni wa Jeshi la Polisi Tanzania Chagonja kutokana na kifo cha Mtalii mmoja na waliohusika kukamatwa leo kwa nini wanashindwa kupambana na mauaji yanayokuwa yanatokea mara kwa mara Musoma na Mkoa wa Mara kwa ujumla.
"Haiwezekani kwenye Nchi yetu tuishi kama wakimbizi matukio ya mauaji ya ajabu yamekuwa yakitokea rakini hatua za haraka zimekuwa hazichukuliwi hali ambayo inaendelea kutupa hofu na kuishi kwa mashaka tukiwa katika ardhi yetu inayodaiwa kuwa ni kisima cha Amani,''alisema Vedastus.
Taarifa za kupatikana kwa mwili huo zilitolewa na wavuvi wa dagaa waliokuwa wakianika kwenye jiwe maeneo ya Makoko nje kidogo ya Mji wa Musoma na kusikia harufu ambayo iliwashitua na kuanza kuulizana ni harufu ya kitu gani na inatokea wapi.
"Siku ya kwanza tulisikia harufu lakini tulichukulia ni kawaida lakini muda ulivyozidi kwenda tuliona ikiendelea kuongezeka na kuamua kufatilia kwa kushirikiana na baadhi ya askari wa Jeshi la Wananchi ambao tunaishi nao jirani na kubaini kuna kitu kimefukiwa pembeni ya mlima na kuamua kulitaarifu Jeshi la Polisi,"alisema mmoja wa wavuvi hao aliyekuwa katika eneo la tukio.
No comments:
Post a Comment