Sunday, October 26, 2014

Dk.Slaa asisitiza mkutano lazima tutashiriki.

POLISI YASEMA INATAMBUA MKUTANO WA LEO NI WA CUF NA SII UKAWA KAMA WATAKUWEPO VYAMA VINGINE MABOMU KAMA KAWA:-

Kamanda wa Polisi wa kanda ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova
Wakati Jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, likitoa kibali cha kufanyika kwa mkutano wa Chama cha Wananchi (CUF) leo kwenye viwanja vya Jangwani, limesema halitambui Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuwamo kwenye mhadhara huo.
Limesema kibali hicho kikitumika kinyume, yatakayotokea uwanjani hapo watajua wenyewe.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Umoja huo ulisema utafanya mkutano leo ambapo pamoja na mambo mengine, utasaini makubaliano ya ushirikiano wa vyama wa kusimamisha mgombea mmoja kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.
Vyama vinavyounda Umoja huo ni CUF, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chama cha NCCR-Mageuzi na chama cha NLD.
Kamanda wa Polisi wa kanda ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova, akizungumza na NIPASHE Jumapili jana kuhusiana na taarifa za mkutano huo, alisema kuwa jeshi lake limeuruhusu mkutano wa CUF kwa mujibu wa barua yao waliyoipokea Alhamisi.
Alisisitiza kuwa walioomba kufanya mkutano wa leo ni CUF na siyo Ukawa.
“Baada ya kupokea barua hiyo, jana tulikutana na viongozi wa CUF ambao tuliwauliza kuhusiana na hilo lakini walitueleza kuwa, mkutano huo ni wa chama chao,” alisema na kuongeza:
“Tumeruhusu mkutano wa CUF ambao ndiyo tutaweka ulinzi, siyo taasisi nyingine, tutasubiri yatakayojiri kama ni hatua tutachukua, Ukawa hatuutambui kwenye mkutano huu na hawajatuandikia barua,” alisema.
Aliongeza kuwa, endapo yataingizwa mambo mengine nje ya makubaliano na CUF, wataangalia makosa yatakayotendeka.
Alipoulizwa kama viongozi wa vyama wengine watajitokeza kwenye mkutano huo itakuwaje, Kamanda Kova alijibu kwa kifupi kuwa watajua hapo itakapokea.
Akijibu hoja hizo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, alisema jeshi la polisi halina wasomi na kama wapo hawana kumbukumbu.
“2007 tulisaini maadili ya vyama vya siasa, katika maadili hayo moja ni vyama vya siasa vinaweza kuamua kushirikiana katika shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na mikutano. Hili lilisainiwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kwa niaba ya serikali, msajili wa vyama vya siasa na mkuu wa jeshi hilo nchini,” alisema.
Alisema ndani ya hati hiyo inaeleza ili washirikiane mmoja wao (chama), ataandika barua kwa niaba ya wengine wanapotaka kushirikiana.
“Hichi ndicho kilichofanyika, mmoja wetu amepeleka taarifa polisi ndani ya muda unaotakiwa kwa niaba yetu wote, lakini kwa mujibu wa katiba, tunapotaka kushirikiana ni ruksa,” alisema.
Alitoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo na wawe na amani.
Katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam, wananchi walikuwa wakihamasishwa kujitokeza kusikiliza mkutano huo kwa kutumia waendesha bodaboda waolikuwa wanapita kwenye mitaa nyakati za usiku.
Uhamasishaji huo ni pamoja na kuwaambia wananchi kuwa kutakuwa na mabasi ya bure yatakayowachukua kutoka maeneo yao hadi kwenye viwanja hivyo.
Hali hiyo ya uhamasishaji ilijitokeza katika maeneo ya Tabata - Segerea ambapo bodaboda hizo zilionekana kupita katika baadhi ya mitaa.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI

SASA JAMANI DEMOKRASIA MI NAONA KAMA POLISI WANATUMIKA KUIMINYA : TOA
Bahati Nzumbi's photo.

No comments:

Post a Comment