Tuesday, October 1, 2013

HUYU NDIO MSAIDIZI WA BARACK OBAMA KWENYE TEKNOLOJIA ALIYEKULIA TANZANI




WAKATI anaingia madarakani rasmi Januari 20, mwaka 2009 kuiongoza Marekani, nchi kubwa yenye nguvu za kiuchumi na kisiasa duniani, Barack Obama alikuwa na malengo mengi. Mojawapo ni kuzidi kuipaisha Marekani na kuwasuta waliodhani nchi hiyo haiwezi kuongozwa na mtu mweusi.
Itakumbukwa kwamba, Obama mwenye asili ya Kenya ambaye kwa sasa ni Rais wa 44 wa Marekani, ndiye mtu wa kwanza mwenye asili ya Afrika kuwahi kuiongoza Marekani.
Hivyo, katika kuhakikisha anatimiza ndoto zake, alipanga safu imara ya wasaidizi, miongoni mwao aliibuka kijana mdogo aliyekuwa na umri wa miaka 35 tu, lakini aliyekuwa na kichwa adimu katika utundu wa kazi, hasa kwa upande wa teknolojia.
Huyu si mwingine bali ni Vivek Kundra aliyezaliwa huko New Delhi, India. Huyu alipewa jukumu la kuwa Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Serikali ya Marekani. Kundra, ingawa ana asili ya India, ni ‘Mswahili’ anayeijua vyema Tanzania, kwani amekulia Tanzania.
Historia yake inaonesha kuwa, akiwa na umri wa mwaka mmoja tu, yeye na wazazi wake, walihamia Afrika, katika nchi ya Tanzania. Baba yake alikuwa miongoni mwa maprofesa na walimu waliokuja nchini kufundisha katika shule kadhaa.
Kutokana na mpango huo, Kundra alijikuta akiishi na wazazi wake huko Korogwe, Tanga na pia mkoani Dodoma. Ni huko ndiko alikozama katika Kiswahili, akiifanya lugha yake ya kwanza huku Kihindi na Kiingereza zikiwa lugha za ziada kwake.
Aliishi Tanzania hadi alipofikisha umri wa miaka 11 ambapo wazazi wake walihamia Washington D.C, Marekani.
“Kwa hiyo ninaijua vizuri Tanzania na ninakifahamu vizuri Kiswahili,” anasema Kundra ambaye akiwa Marekani, alihitimu Shahada ya Kwanza katika Saikolojia aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Maryland Park.
Hakuishia hapo, alirudi tena darasani kusoma Teknolojia ya Habari katika Chuo Kikuu cha Maryland, lakini pia alisoma katika Taasisi ya Uongozi wa Siasa ya Sorensin ya Chuo Kikuu cha Virginia.
Kutokana na umahiri wake kitaaluma, Machi mwaka 2011 alitangazwa kuwa mmoja wa waliothibitisha vipaji vya uongozi duniani, akichaguliwa na jopo la wajuzi na wasomi kutoka Mkutano wa Uchumi Duniani (WEF).
Mwaka huo, katika mkutano uliofanyika Amman, Jordan, Kundra alikuwa mwenye furaha kukutana na kijana mwingine aliyepewa heshima kama yake, Susan Mashibe wa Tanzania ‘milionea mtoto’ ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Kampuni ya TanJet, kampuni ya kimataifa na ya kwanza ya aina yake nchini inayoshughulikia masuala ya kiufundi katika ndege binafsi, za biashara na hata za kidiplomasia.
Mwanadada huyu, pia anamiliki kampuni nyingine inayojulikana kama Kilimanjaro Aviation Logistic Center, ambayo inashughulikia taratibu za utuaji na urukaji wa ndege binafsi katika Bara la Afrika.
Aidha, ameanzisha Huduma ya Matengenezo na Ukarabati wa Ndege Kilimanjaro, kwa lengo la kutoa huduma za kisasa, yenye kiwango na salama katika usafiri wa anga wa jumla na ushirika katika eneo la Afrika. Lakini pia Susan ndiye Mwanamke wa Kwanza Afrika Mashariki mwenye Cheti cha Rubani cha FAA na Mhandisi Matengenezo wa Ndege.
Tangu kuanzishwa TanJet mwaka 2003, Mashibe ametunukiwa Tuzo mbalimbali ikiwemo ya Askofu Desmond Tutu ya mwaka 2009 na ile ya Mwanamke Mjasiriamali mwenye Mafanikio ya mwaka 2009.
Tukirudi kwa Kundra, mwaka mmoja kabla ya tuzo ya WEF, alituzwa na taasisi ya teknolojia ya SANS kwa kuwezesha kufichua wizi wa dola za Marekani milioni 300 (Sh bilioni 450) uliokuwa unafanywa kwa njia ya mtandao kwa takribani kila mwaka na baadhi ya watendaji serikalini.
Aidha, Kundra amewahi kutunukiwa Tuzo kemkem kutokana na umahiri wake katika miundombinu ya teknolojia na habari na mawasiliano, akiwa amegundua mifumo kadhaa ya kisasa. Ndiyo maana Chuo Kikuu cha Harvard hakikutaka kuuachia ujuzi wake, na hivyo kuamua kuingia naye mkataba wa kufundisha kwa mkataba chuoni hapo.
Nje ya kazi hiyo, Kundra pia ni Makamu Mwenyekiti wa kampuni kubwa ya masomo ya Salesforce ya Marekani. Majukumu mengine ya kitaaluma aliyokuwa nayo kabla ya kuitwa Ikulu ya Marekani kumsaidia Rais Obama ni kuwa Mkurugenzi wa Miundombinu ya Teknolojia huko Arlington, Virginia mwaka 2001 na miaka mitano baadaye, aliteuliwa na Gavana wa Virginia, Tim Kaine kuwa mkuu wa shughuli za kiteknolojia jimboni humo.
Ilipofika Machi 27, 2007, Meya wa Columbia, Adrian Fenty alimteua Kundra kuwa Ofisa Teknolojia Mkuu wa Columbia.
Je, anazungumziaje kuaminiwa kwake na Rais Obama? Anasema: “Ni heshima kubwa. Sikuwaza kuwa msaidizi wa Rais katika nchi muhimu kama Marekani. Kama unavyojua, nilizaliwa India, nikakulia Tanzania.
Ni mhamiaji tu hapa na ikumbukwe nilikuja Marekani mwaka 1985 nikiwa sijui hata Kiingereza, zaidi ya Kihindi na Kiswahili.
“Lakini bidii katika masomo na nyanja ya utawala, vitu nilivyorithi kutoka kwa wazazi wangu, ndivyo vilivyonifikisha hapa, kiasi cha kuaminika na jamii na hata Rais wa nchi.Namshukuru Mungu kwa kila jema linalotendeka juu yangu. Namshukuru Rais Obama kwa kuwapa nafasi vijana pia.”
Huyo ndiye Vivek Kundra, mtaalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano aliyekulia Tanzania, lakini sasa akifanya vitu vikubwa nchini Marekani.

Source: HabariLeo

No comments:

Post a Comment