NI vigumu kutokea! Lakini safari hii imetokea, mwili wa aliyekuwa mtangazaji wa Abood TV, Julius Nyaisangah ‘Anko J’ ambaye alifariki dunia Jumapili iliyopita mjini Morogoro, ulisafirishwa kwa majeneza mawili.
Usiku wa Jumatatu iliyopita kamera za Risasi Jumamosi, zilishuhudia jeneza lenye rangi nyeupe likiwa limetumika kuusafirisha mwili wa marehemu huyo kutoka Morogoro hadi Hospitali ya Taifa, Muhimbili jijini Dar.
Jumanne iliyopita, saa tatu asubuhi kamera zetu zilishuhudia jeneza lenye rangi ya kahawia (brown) likitumika kuusafirisha mwili huo kutoka Muhimbili hadi Viwanja vya Leaders, Kinondoni, Dar ambako marehemu aliagwa.
Baadhi ya watu walipoulizwa na Risasi Jumamosi wana mawazo gani kuhusu mwili wa marehemu kusafirishwa na majeneza mawili walionekana kushangazwa na tukio hilo.
Mwili wa marehemu ulisafirishwa siku hiyohiyo kwenda Bunda, mkoani Mara alikozaliwa kwa mazishi yaliyofanyika Alhamisi iliyopita.
Risasi Jumamosi lilimtafuta mjumbe mmoja wa kamati ya mazishi ya Anko J aliyeomba kusitiriwa jina lake na kumuuliza kulikoni majeneza mawili yatumike kusafirisha mwili mmoja ambapo alijibu:
“Lile lililotoka na mwili Morogoro lilionekana kukosa ubora halafu lilitengenezwa ‘chapchap’ ndiyo ikaamriwa linunuliwe jingine zuri zaidi.”
Risasi Jumamosi: Sasa lile jeupe lililotoka Morogoro limepelekwa wapi?
Mjumbe: Mh! lile tuliliacha muhimbili ,ndugu watajua cha kufanya.
Kwa Waislam, jeneza linalotumika kubebea mwili wa marehemu ni la wazi na hurudishwa msikitini baada ya mwili kuzikwa kaburini.
Kama mwili utasafirishwa hutumika jeneza la sanduku lakini haliendi kuingia kaburini na huvunjwavunjwa punde mwili unapofika.
Kwa Wakristo, jeneza linalotumika kubebea mwili wa marehemu hutengenezwa kama sanduku na huingizwa kaburini na marehemu akiwemo ndani.
Awali ilidaiwa kuwa, mwili wa marehemu ungesafirishwa kwa ndege kwenda tarime na gharama za usafirishaji zingesimamiwa na wizara ya habari vijana utamaduni na michezo, lakini juzi naibu waziri wa wizara hiyo, Amos makalla alikanusha wizara yake kutoa tamko hilo.
“Wizara haikutoa tamko hilo, wala hatukuwa kwenye kamati ya mazishi ila tulituma mwakilishi,” alisema Waziri makalla.
GPL
No comments:
Post a Comment