Saturday, April 11, 2015

Gwajima bado yuko ngangarii!

Atakiwa kupeleka polisi nyaraka zake, Vimo vielelezo vingine vya mali za kanisa.


Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima.


Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, jana alihojiwa kwa mara ya pili na Jeshi la Polisi kwa takribani saa tano huku akitakiwa kupeleka vielelezo 10 ikiwamo nyaraka ya helikopta anayomiliki.
 
Askofu Gwajima aliwasili katika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa mahojiano hayo saa 1:14 asubuhi akiongozana na Msaidizi wake, Mchungaji Gwandu Mwangasa na Mwanasheria wake, John Mallya.
 
Licha ya juzi kuelezwa kuwa afya ya kiongozi huyo imeimarika, lakini jana Askofu Gwajima alisaidiwa kupanda ngazi na wasaidizi wake huku Mallya akiwa upande wa kushoto na Mchungaji Mwangasa upande wa kulia.
 
Ilipofika saa 6:40, Askofu Gwajima na wasaidizi wake walitoka ndani ya chumba cha mahojiano huku akijikongoja.
 
MWANASHERIA WAKE
Akielezea kilichojiri katika mahojiano hayo, Mwanasheria wake Mallya alisema kuwa Jeshi la Polisi lilimhoji Askofu Gwajima muda mrefu mambo ambayo hayaendani na kosa analotuhumiwa kulitenda.
 
VIELELEZO VYA KUPELEKA
Alieleza kuwa Jeshi la Polisi lilimtaka Askofu Gwajima kuwasilisha vielelezo 10 kituoni hapo Aprili 16, mwaka huu.
 
Alivitaja vitu hivyo kuwa ni hati ya usajili wa kanisa lake, nyaraka za idadi ya makanisa anayomiliki pamoja na  kuwasilisha muundo wa uongozi wa kanisa lake.
 
Viingine ni idadi ya nyumba na mali ambazo kanisa linamiliki, nyaraka ya umiliki wa helikopta anayomiliki na muundo wa Bodi ya Wadhamini wa Kanisa pamoja na majina yao.
 
Kwa mujibu wa Mallya, vingine ni returns (makusanyo) ya kanisa, kumpeleka mtu anayepiga picha za video) katika kanisa lake, waraka ulioandaliwa na Maaskofu wa Jukwaa la Wakristo pamoja na namba ya usajili ya kanisa analomiliki.
 
Hata hivyo, Mallya alisema kuwa Polisi walimhoji Askofu Gwajima masuala ya familia yake na wazazi wake badala ya tuhuma anazotuhumiwa za kumtukana na kumkashifu Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
 
“Ninawashangaa polisi, wamemhoji mteja wangu masuala yanayohusu familia yake na wazazi wake kuliko tuhuma anazotuhumiwa,” alisema Mallya.
 
Mallya alieleza kuwa kutokana na hali hiyo, wamepanga kwenda mahakamani kufungua kesi kupinga kitendo hicho.
 
Katika hatua nyingine, Mallya alieleza kuwa Askofu Gwajima anatarajia kwenda nje ya nchi kutibiwa, lakini hakufafanua zaidi ni nchi gani wala hospitali gani.
 
KAULI YA GWAJIMA
Mara baada ya kutoka katika mahojiano, Askofu Gwajima alieleza kuwa mahojiano kati yake na Jeshi la Polisi yalikwenda vizuri.
 
WAFUASI WAFURIKA POLISI
Wakati Askofu Gwajima akihojiwa ndani, nje ya kituo cha polisi wafuasi wake walifurika wakitaka kufahamu hatma ya kiongozi wao.
 
Kutokana na hali hiyo, Naibu Kamishna wa Polisi, Kamanda Simon Sirro, aliwasihi kutawanyika.
 
“Gwajima yupo katika mikono salama, nendeni mkafanye kazi za kuzalisha mali sasa, mkirundikana wote hapa nani atafanya kazi?” Kamanda Sirro aliwaeleza wafuasi hao.
 
Kamanda Sirro aliwaeleza kuwa Jeshi la Polisi limeshamrejeshea Askofu Gwajima hati yake ya kusafiria, hivyo anaweza kwenda kutibiwa kokote.
 
“Askofu Gwajima yupo ndani anahojiwa akimaliza ataruhusiwa,” alisisitiza.
 
Hata hivyo, mmoja wa wafuasi hao alimjibu Kamanda Sirro: “Akiondoka nasi tutaondoka.” 
 
Naye Kamanda Sirro alijibu: “Makubwa.” Jibu lililowaacha wafuasi hao watapao zaidi ya 100 kuendelea kumsubiri nje.
 
Machi 26, mwaka huu, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, lilimwamuru Askofu Gwajima kujisalimisha polisi kwa tuhuma za kumkashifu Kardinali Pengo.
 
 Machi 27, mwaka huu, Askofu Gwajima alijisalimisha kituoni hapo  lakini wakati akihojiwa alizimia akiwa chumba cha mahojiano kisha kukimbizwa katika Hospitali ya TMJ kwa matibabu. 
 
 Jumanne ya wiki iliyopita, Askofu Gwajima aliondolewa TMJ na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay na kuachiwa bila masharti, lakini alielekezwa kuripoti Alhamisi iliyopita katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment