“Askari
lazima atishe. Popote anapokuwapo wahalifu wajue kuwa kuna mtu hatari dhidi yao.
Kama mhalifu atatiwa woga na uwepo wa polisi, uhalifu utapungua tu na hivyo
kubakiwa na kazi ndogo ya kuwakamata wachache wanaoendelea na vitendo hivyo.”
Omari Mahita
Inspekta
Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu, Omary Mahita amesema askari polisi kwa sasa
wamepoteza hadhi, hawaogopwi na wahalifu na ndiyo sababu kubwa ya kuongezeka kwa
vitendo vya kihalifu kila kukicha.
Mahita
aliyestaafu mwaka 2006, alisema mbali na kuongezeka kwa uhalifu, inafikia hatua
wahalifu wanawaingilia polisi kwa kuvamia vituo vya polisi na kupora silaha
ilhali zamani hakukuwa na matukio hayo.
Hata hivyo,
IGP, Ernest Mangu amejibu kauli hiyo akisema: “Siwezi kutumia mbinu za Mahita
kwa sababu alichokuwa anakabiliana nacho, kwa sasa hakipo.”
Kauli ya
Mahita
Kauli ya
Mahita imekuja miezi minane baada ya askari 10 kuuawa na bunduki zaidi ya 20
kuporwa katika matukio mbalimbali ya uvamizi wa polisi na vituo vya
polisi.
Akizungumza
na mwandishi wetu baada ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Mkurugenzi wa
zamani wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, Dk Mohamed Mhita, Oysterbay Dar es Salaam
juzi, Mahita alisema: “Ili kupunguza vitendo vya kihalifu vinavyozidi kuongezeka
kila kukicha, ni lazima askari warudishe hadhi yao ya kuogopwa na wahalifu
popote walipo.
“Askari
lazima atishe. Popote anapokuwapo wahalifu wajue kuwa kuna mtu hatari dhidi yao.
Kama mhalifu atatiwa woga na uwepo wa polisi, uhalifu utapungua tu na hivyo
kubakiwa na kazi ndogo ya kuwakamata wachache wanaoendelea na vitendo
hivyo.”
Mahita
alikosoa kitendo cha askari polisi kuwa wapole na kueleza kuwa hilo ni suala
lisilotakiwa kabisa kufanywa ndani ya jeshi hilo na polisi... “Unambembelezaje
mhalifu? Hawa ni watu wanaostahili kubanwa kwa kila namna ili kukomesha vitendo
vyao katika jamii. Mhalifu yeyote akiachiwa, madhara yake ni makubwa katika
jamii.”
Licha ya
suala hilo, IGP huyo mstaafu alieleza umuhimu wa doria katika kudhibiti uhalifu
wa kila siku ambao hupunguza amani miongoni mwa jamii na kuwafanya wananchi
washindwe kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na ratiba
waliyojiwekea.
Alitolea
mfano wa vikundi vya uhalifu vilivyojitokea hivi karibuni kama ‘Panya Road’,
‘Mbwamwitu’ na ‘Libya’ kwamba vimekuwapo kutokana na kupungua kwa doria
inayotakiwa ifanywe na jeshi hilo nchi nzima na hasa maeneo ya
mijini.
“Enzi zangu
doria ilipewa kipaumbele. Magari na pikipiki yalikuwa yanazunguka kote katika
jiji hili na kwingineko mikoani karibu kila siku na walikuwa wanaogopeka… kwa
sasa yapo lakini sidhani kama wanafanya kazi kama ilivyokuwa enzi zile,” alisema
Mahita.
“Wahalifu
walikuwa wanajua kuwa polisi wapo kazini muda wote. Lakini sasa hivi mambo hayo
hayapewi uzito unaotakiwa ndiyo maana unaona kikundi kama Panya Road
kinatingisha mji mkubwa kama huu (Dar es Salaam).
“Inawezekana
vipi kikundi kama hicho kikatingisha amani ya jiji hili lenye viongozi wote wa
jeshi?” alihoji Mahita.
Mahita
alikuwa maarufu kwa jina la ‘Ngunguri’ kutokana na kauli yake alipokuwa
akikabiliana na maandamano ya wafuasi wa CUF kwamba kama viongozi wake wako
ngangari basi polisi iko ngunguri kukabiliana nao.
Akizungumzia
uhalifu katika vituo vya polisi, Mahita alisema polisi imekosa kuungwa mkono
hivyo kupunguza ufanisi wake katika kutekeleza majukumu yake.
“Hata jamii
ipo mbali pia… Raia ndiyo wanavamia na kuua askari. Watu hawa wanaishi katika
jamii hiihii. Hivyo ni vyema ikajirudi na kuona kuwa hii ni taasisi muhimu kwa
maisha na mali ya kila mwananchi.”
Akizungumzia
vifo vya askari hao, Mahita alisema kuwa jamii imewasahau na kuwatenga kwani
hakuna anayeshtuka pindi wanapoteza maisha hata kama mauti hayo huwakuta wakiwa
kazini.
IGP
Mangu
Akizungumzia
hoja hizo, Mangu alisema mabadiliko ya jamii na maendeleo ya kiuchumi yamebadili
mbinu za uhalifu.
“Mbinu za
kiuhalifu zimebadilika kiasi cha kulilazimu jeshi pia kubadilika ili kuendana na
mbinu hizo mpya. Haiwezekani jeshi likabaki kama ilivyokuwa miaka 20
iliyopita.
“Jamii ya
wakati wa Mahita ni tofauti na ya sasa. Hata askari hawawezi kuendelea kuwa wale
waliokuwapo. Mazingira na kila kitu vimebadilika. Enzi hizo kulikuwa na uhalifu
wa ulipuaji wa mabomu na utakumbuka ilishatokea huko Arusha na Zanzibar matukio
ambayo hayapo kwa sasa,” alisema Mangu. Alisema ni vigumu kulinganisha vipindi
tofauti vya viongozi na kwamba kufanya hivyo ni sawa na kutowatendea haki kwani
wanakuwa wanaongoza katika mazingira tofauti kwa kila kitu.
“Kubadilika
kwa mbinu na aina za uhalifu kunamlazimu kiongozi husika kuitikia mabadiliko
hayo pia. Mimi siwezi kutumia mbinu za Mahita kwa sababu alichokuwa anakabiliana
nacho hakipo sasa hivi.
Hapakuwa na
mauaji ya albino wakati wake, hili peke yake linaonyesha jamii iliyopo ni
tofauti na iliyokuwapo,” alisema.
“Hata mimi
nikistaafu baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba atakayekuja atapata changamoto tofauti
na hizi ninazokutana nazo au walizokutana nazo watangulizi wangu,”
alisema.
“Rais
Kikwete alikemea mauaji ya polisi kila yanapofanywa... hivi ndivyo
tunavyotakiwa kufanya,” alisema Mangu.
Copied from Paparazi Blog.
No comments:
Post a Comment