FBI waondoka Zanzibar bila polisi kujua
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa
Askari wa Upelelezi wa Marekani (FBI) waliokuja Zanzibar
kusaidia uchunguzi wa kumpata aliyemuua kwa kumpiga risasi, Padri
Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki wameondoka nchini.
Askari hao waliondoka Zanzibar bila kukamatwa mtu
yeyote anayetuhumiwa, licha ya polisi hivi karibuni kutoa mchoro wa mtu
anayedaiwa kumuua padri huyo.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema jana kuwa askari hao waliokuja kushirikiana na wenzao wa Tanzania, wamerudi Nairobi na wanaendelea na uchunguzi wao.
“Hawa jamaa wamerudi Nairobi. Lakini, huwezi kuwaamini sana wanaweza kusema wako watatu kumbe wako 100,” alisema Kamishna Mussa na kueleza kwamba hakumbuki tarehe waliyoondoka nchini.
FBI waliitwa nchini ili kusaidia uchunguzi wa kuuawa kwa Padri Mushi Februari 17 mwaka huu, wakati anakwenda kuongoza ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Teresia lililopo Beit el Raas nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Kamishna Mussa alisema kwamba hadi sasa hawajapata mtuhumiwa ambaye wanaweza kumfikisha mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji hayo.
Mussa mara kadhaa amekuwa akisema kwamba “tunakamata, tunahoji na kuachia” na kueleza kuwa, polisi wamepewa majina mbalimbali baada ya kutoa mchoro wenye taswira ya mtu anayedaiwa kumuua Padri Mushi.
Kuuawa kwa Padri Mushi kulikuja baada ya viongozi wengine wa dini, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Fadhil Soraga kumwagiwa tindikali na kupigwa risasi kwa Padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki Zanzibar.
Tangu kuuawa kwa Padri Mushi kumekuwa na taarifa za kukamatwa kwa baadhi ya watu wakituhumiwa kuhusika na mauaji hayo, lakini polisi wamekuwa wakikanusha.
Serikali iliahidi kwa njia zozote kuhakikisha inawakamata watuhumiwa, huku Rais Kikwete akiahidi kutumia vyombo vya upelelezi vya ndani hata ikiwezekana vya nje kuwakamatwa wahusika.
Chanzo: Mwananchi