Wataalamu kutoka China watua kuchunguza
*Polisi watamba kufichua siri ya milipuko yote
TAARIFA za awali
kutoka kwa makachero wa Jeshi la Polisi nchini zimefanikiwa kubaini
mtandao wa ulipuaji mabomu katika jiji la Arusha, imefahamika. Mpaka
sasa taarifa zinadai mtandao uliohusika na milipuko miwili iliyotokea
kwa nyakati tofauti jijini hapa ulipangwa ndani ya jiji la Arusha.
Mlipuko wa kwanza
ulitokea katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti, Mei 5,
mwaka huu na kuua watu watatu, wakati mlipuko wa pili ulitokea Uwanja wa
Soweto Juni 15, mwaka huu na kuua watu wanne, huku majeruhi wa matukio
yote wakifikia zaidi ya 100.
Akizungumza
katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Arusha (RCC) jana jijini
hapa, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alisema mbinu hizo
zimejulikana kutokana na wananchi waliojitokeza kuwasilisha ushahidi kwa
vyombo vya dola.
Alisema mpaka
sasa ushahidi unaonyesha kuwa mtandao wa waliolipua wa mabomu hayo
ulianzia jijini Arusha, na kikubwa kabisa wanawashukuru wakazi wa Arusha
waliokuwa wakifika kutoa ushahidi wa wahusika.
“Ukweli wa mambo
haya utajulikana hivi karibuni na Serikali itamchukulia hatua mtu yeyote
atakayebainika kuhusika na mtandao huo, bila kujali wadhifa wake. Mambo
haya yamedhalilisha na kufedhehesha Taifa,” alisema Mulongo.
Akiwa ndiye
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, aliendelea kubainisha
kuwa upelelezi wa matuko hayo mawili unaendelea kwa umakini mkubwa na
kikubwa kinachoangaliwa ni kuepuka kukamata watu wasiohusika.
“Tunachukua
umakini ili waliofanya hivi vitendo vya kinyama wasiendelee kutamba,
kwani wanajua tukikamata wasiohusika wao watajiona wameshinda
hawajakamatwa,” alisema Mulongo.
Mwenyekiti huyo
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa aliwataka pia wanasiasa nchini
kutoigeuza milipuko ya mabomu hayo kama njia ya kujitafutia umaarufu wa
kisiasa.
“Kugeuza tukio
hili la kinyama kuwa agenda ya kisiasa kunaidhalilisha Tanzania nje ya
nchi na kuleta athari za kupoteza wageni,” alisema Mulongo.
Mulongo alisema
taarifa za awali za kikachero zinaonyesha kuwa bomu lililorushwa katika
viwanja vya Soweto lilitengenezwa China.
Mkuu huyo wa mkoa
alisema, tayari wataalamu kutoka China wamekwisha wasili jijini Arusha
kwa ajili ya kufanya utambuzi wa taasisi iliyonunua bomu hilo.
Mulongo katika
hotuba yake aliendelea kuwataka wanasiasa kuacha dharau na kueneza
maneno yasiyo na ukweli juu ya Serikali, badala yake aliwataka kuheshimu
taratibu za nchi ili vyombo vya dola visilazimike kutumia nguvu
kukabiliana na watu au kikundi kitakachovunja sheria zilizowekwa.
“Hivi ndugu
zangu, lazima tufike mahali tujiulize hawa wanasiasa wanaotumia uongo na
nguvu nyingi kuchafua nchi huko duniani, wanafanya hivi kwa faida ya
nani?” alihoji Mulongo.
Bomu hilo
lilirushwa katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendelo (CHADEMA),
wakati kikihitimisha kampeni zake za uchaguzi mdogo wa udiwani katika
kata nne jijini Arusha Juni 15, mwaka huu.
Hata hivyo, siku
mbili baada ya mlipuko huo, chama hicho kilitoa shutuma nzito dhidi ya
Jeshi la Polisi na kueleza kuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia
(FFU), ndiye aliyerusha bomu hilo.
Mwenyekiti wa
chama hicho taifa, Freeman Mbowe, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa
chama chake kinao ushahidi wa picha na sauti unaothibitisha kwamba
polisi ndio wahusika wa mlipuko huo.
Hata hivyo, chama
hicho kimegoma kukabidhi ushahidi huo kwa jeshi hilo kwa maelezo kuwa
ushahidi huo hauwezi kutolewa kwa polisi, ambao ni watuhumiwa wa tukio
hilo.
Chama hicho
kilitoa sharti kwa Rais Jakaya Kikwete kuunda Tume ya Mahakama
itakayohusisha majaji waadilifu na kusema kuwa kipo tayari kutoa
ushahidi huo mbele ya tume hiyo na si polisi.
Mbali na bomu
hilo, bomu jingine lilirushwa katika Kanisa la Mtakatifu Joseph
Mfanyakazi, Olasiti na kusababisha watu watatu kufariki ambapo nalo
liligundulika kutengenezwa nchini Urusi.
No comments:
Post a Comment