Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
leo, Ijumaa, Septemba 20, 2013, anatunukiwa Shahada ya Uzamivu (PHD) na
Chuo Kikuu cha Guelph cha Canada kwa kutambua mchango na uongozi wake
katika kuleta mageuzi ya kilimo katika Afrika.
Viongozi
wa Chuo hicho wanasema kuwa wamefanya uamuzi wa kumtunuku Rais Kikwete
kutokana na jitihada zake za kukabiliana na changamoto zinazokabili
kilimo, jitihada zake za kuleta usalama wa chakula na pia majaribio
makubwa ya kuongeza matumizi ya technolojia katika kilimo cha Tanzania
na Afrika.
Rais
Kikwete ambaye amewasili hapa usiku wa jana, Alhamisi, Septemba 19,
2013 akitokea Washington, D.C., Marekani ambako alikuwa kwa siku mbili
akitokea Jimbo la California atakuwa Mtanzania wa kwanza kutunukiwa
shahada ya juu kabisa katika historia ya Chuo hicho.
Chuo
cha Guelph ni moja ya vyuo vikuu vinavyoheshimiwa zaidi katika Canada
na duniani katika Nyanja za kilimo na kilianzishwa rasmi kama Chuo cha
Kilimo cha Jimbo la Ontario Mei Mosi, mwaka 1874.
Chuo
hicho ambacho kimejipatia umaarufu kutokana na ubora wa shughuli zake
za utafiti kimekuwa katika mstari wa mbele kutafuta majawabu ya
changamoto zinazoikabili dunia katika masuala ya kilimo, raslimali za
maji, matatizo makubwa ya magonjwa ya mimea, matatizo ya ukuaji haraka
wa miji duniani na changamoto za biashara za kimataifa.
Katika
miaka ya karibuni kufuatia tishio kubwa kimataifa la ongezeko la bei za
vyakula duniani na hasa katika nchi masikini, mabadiliko ya tabianchi,
ongezeko la uchafuzi wa hali ya hewa, uharibifu wa mazingira, changamoto
za upatikanaji wa maji safi na salama duniani, kazi ya Chuo hicho
imeongezeka sana.
Chuo
hicho kimeichagua Tanzania kama nchi ya kufanya nayo kazi katika Afrika
kukabiliana na changamoto hizo na kimemtambua Rais Kikwete kutokana na
mchango wake mkubwa katika sekta ya kilimo katika miaka yote ya uongozi
wake na mipango yake ya kuboresha kilimo katika Tanzania kama ASDP,
Kilimo Kwanza na SAGCOT ambayo yote inasifiwa sana kimataifa.
Chuo
hicho kina mahusiano ya karibu na Vyuo Vikuu vya Dar es Salaam, Sokoine
cha Mzumbe – Morogoro na UDOM – Dodoma. Kati ya mwaka jana na mwaka
huu, Chuo hicho kimetiliana saini Makubaliano ya Ushirikiano (MOU) na
Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine cha Mzumbe – Morogoro na Chuo Kikuu
cha Dodoma (UDOM).
Mara
nne kati ya Januari, mwaka jana, 2012 na Juni, mwaka huu, 2013, uongozi
wa Chuo hicho ukiongozwa na Rais na Makamu Mkuu wa Chuo, Dkt. Alastair
Summerlee na Makamu wa Rais wa Utafiti Dkt. Kevin Hall umetembelea
Tanzania na kukutana na viongozi wa Serikali pamoja na wale wa Vyuo
Vikuu vya Dar Es Salaam na Sokoine cha Mzumbe, Morogoro.
Mbali na ujumbe ambao unaongozana na Rais Kikwete, sherehe za
kutunukiwa kwa Kiongozi Mkuu huyo wa Tanzania pia zitahudhuriwa na
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa,
Jumuia ya Watanzania wanaoishi Canada pamoja na maofisa wa Ubalozi wa
Tanzania nchini humo.
No comments:
Post a Comment