Saturday, September 7, 2013

Wananchi wamshukia Waziri Muhongo

*Ni kwenye kongamano la wazi


Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
 KONGAMANO la wazi la Wizara ya Nishati na Madini jana liligeuka kuwa mwiba kwa Waziri Profesa Sospeter Muhongo baada ya kusisitiza msimamo wa serikali kuhusu gesi ya Mtwara.
Profesa Muhongo ambaye alikuwa akiwasilisha mipango ya uhakika ya upatikanaji wa umeme nchini aliwalaumu wanasiasa kuwa kikwazo katika mradi huo kwa kuwachochea wananchi kuandamana.



Alisema wananchi wa Mtwara hawana nafasi tena ya kusikilizwa kwa vile walipewa elimu mara kadhaa lakini kutokana na kulaghaiwa na wanasiasa kwa ujira wa Sh 20,000 wamekuwa wakiandamana na kupinga mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

“Maandamano ya wananchi hayawezi kuitingisha Serikali, hatuwezi kusimamisha mradi kwa sababu tumegundua ni ujinga wa baadhi ya wanasiasa kutaka taifa likubaliane na ujinga wao.

“Ni upuuzi mkubwa kudai gesi ni mali ya mikoa ya kusini, ni upuuzi kwa mtu kusema wanamtwara wanahoja eti wakasikilizwe.

“... ni upuuzi tena kwa mwanasiasa kusema ajira kwa vijana ni bomu, nasema hakuna bomu litakalolipuka labda katika familia yake.

“Pia ni upuuzi tena Serikali kuwasikiliza wanasiasa wanaopiga kelele huku hawana takwimu wala njia mbadala ya kupata umeme wa uhakika.

“Nasema kwa kuwa tumewajua wanaopinga mradi tutawashughulikia na hatutaacha kutandaza bomba na ole wao wajaribu, watajuta.

“Tunataka wananchi vijijini wapate umeme hadi asilimia 50 siyo tena leo ni asilimia saba tu wanaopata umeme. Lazima miradi saba itekelezwe ndani ya miaka 20 tuliyojipangia.

“Ni jana (juzi) Rais wa Marekani, Barrack Obama ameondoka nchini ametoa dola bilioni saba kusaidia kupata umeme megawati zaidi ya 10,000 na sekta binafsi zikitoa bilioni tisa,”alisema.

Baada ya kutoa kauli hiyo kulizuka malumbano kati ya washiriki Profesa Muhongo na wakati mwingne washiriki wenyewe kwa wenyewe.

Mshiriki aliyejitambulisha kwa jina la Said Mohamed Manora kutoka mikoa ya Kusini alidaiProfesa Muhongo amewatukana, amewatenga na kutowathamini wananchi wa mikoa hiyo.

Manora alisema Mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa mikoa iliyotelekezwa huku barabara zikijengwa kwa kusuasua tofauti na ilivyo kwa Kanda ya Ziwa.

Alisema Profesa Muhongo ameonyesha dharau kwa wanamtwara akisema anapaswa kutafuta historia yao badala ya kuendelea kuwapuuza.

Hata hivyo Profesa Muhongo aliendelea kutoa msimamo wake kwamba hakuna muda tena wa kuwasikiliza huku akisisitiza gesi ni mali ya Watanzania.

“Narudia kusema itakuwa ni upuuzi gesi hiyo kudai ni yao, mbona hamuuzi korosho huko Mtwara na nani kawaelekeza kuna soko Dar es Salaam,”alisema.

Wakati anajibu ‘mapigo hayo’ kulitokea makundi mawili tofauti ambayo yalinyoosheana vidole; kundi moja likiwa upande wa Profesa Muhongo na jingine likimuunga mkono mshiriki aliyeibua hoja.

Kitendo hicho kilivuruga utulivu katika chumba cha mkutano huo.

Hata hivyo iligundulika kuwa washiriki wengi waliomuunga mkono Manora walikuwa ni wa kutoka mikoa ya kusini na walioungana na Waziri ni watumishi wa wizara hiyo na wale wanaomba kupatiwa miradi ya umeme.

Malumbano hayo yalisababisha washiriki wengi kutoka nje ya ukumbi huku majadiliano ya makundi yakitawala.

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliachim Maswi alimuunga mkono Waziri wake na kuema Serikali haiwezi kukubalina na kile kinachodaiwa na wanamtwara kwa vile kitaligawa taifa na ni hatari.

“Kama hamfahamu naomba niwaeleze kwamba wakati wanamtwara wanadai gesi yao, tulipokea vishawishi vingi kutoka mkoani Mara, kama mnavyojua mimi natoka huko na hivo hivyo waziri.

“Wakurya wenzangu walikuwa wakisema tukubali gesi iwe ya Mtwara na wao dhahabu iwe yao, walisema tukiruhusu hivyo wawekezaji wote watachinjwa haraka hata kabla ya kutoroshwa hapo,”alisema.

Kabla ya tafrani hiyo, Profesa Sospeter Muhongo alisema mipango muda mfupi iliyokuwa ikipangwa awali na Serikali ndiyo iliyosababisha kutopatikana maendeleo ya haraka.

Alisema mipango ya muda mfupi ndiyo imeleta vitendo tunavyoshuhudia hivi sasa kwa Watanzania kama kubomolewa nyumba zao au kuhamishwa katika makazi yao jambo ambalo ni hasara.

“Kama taifa lazima liwe na mipango ya muda mrefu na siyo tena mipango ya miaka michache ambayo inaleta hasara kutokana na mabadiliko.

“Suala la mipango ya muda mfupi halipo katika wizara moja la hasha, karibu wizara zote, hii ni tatizo kwa viongozi wengi, tunapaswa kuiga mipango ya mataifa mengine.

Tanzania itapiga hatua tu tutakapopanga mipango ya muda mrefu kwa kuangalia dunia inakwendaje na kuweka vipaumbele kwani ifikapo 2030 nishati na maji vitakuwa bidhaa adimu maradufu,”alisema.

Profesa muhongo alisema muda umekwisha wa maneno na kilichobaki ni vitendo kwa kuwaajibisha viongozi katika wizara yake kama hawawezi kufanya kazi kwa kiwango cha kimataifa.

Alisema kwa muda aliokaa ndani ya wizara hiyo ameweza kuwafukuza kazi watumishi waliogundulika kujihusisha na rushwa, wizi, utendaji mbovu na ubabaishaji na bado wengine wanafuatiliwa kwa ukaribu.

“Ndani ya wizara ya yangu nasema watumishi wengi watapukutika, siwezi kukaa na watu ambao hawafanyi kazi kwa uadilifu na kiwango cha kimataifa, binafsi najiamini na ninaweza,” alisema.

Profesa Muhongo alisema Tanzania haiwezi kutegemea mabawa ya kizamani yanayosubiria mvua na badala yake tunapaswa kuwa na njia mbadala ya kupata nishati ya uhakika.

Alisema kuwa tayari wizara imeweka kipaumbele ya umeme ni kutumia gesi asilia, makaa ya mawe, maji, jua, upepo na joto ardhi.

Ifikapo Julai 2014 bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam litakuwa limekamilika, alisema.


Chanzo Mtanzania.

No comments:

Post a Comment