Friday, September 20, 2013

wasanii na viingilio vyatajwa Miss TZ


Na Mwandishi Wetu
WAKATI zikiwa zimebaki siku tatu ili Redd’s Miss Tanzania ajulikane, viingilio kwa ajili ya shindano hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa na Watanzania wengi vimetangazwa.
 
Kiingilio cha juu katika shindano hilo linalotarajiwa kufanyika keshokutwa (Jumamosi) katika Ukumbi wa Mlimani City, uliopo Mwenge, Dar es Salaam ni Sh 100,000 kwa viti maalumu, huku viti vya kawaida vikiwa Sh 50,000.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa kinywaji cha Redd’s Original, Victoria Kimaro, ambao ndio wadhamini wakuu wa Redd’s Miss Tanzania alisema, wanaamini viingilio hivyo ni vya kawaida kutokana na ubora wa shindano lenyewe.
 
Victoria alisema, burudani katika shindano hilo inatarajiwa kutolewa na msanii mahiri kutoka Uganda, Mike Ross atakayeshirikiana na Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ pamoja na kundi la Mama Afrika katika kukonga nyoyo za mashabiki watakaojitokeza ukumbini hapo.
 
“Tunaamini kabisa wasanii hawa watakonga nyoyo za mashabiki wa tasnia ya urembo hapa nchini, hivyo napenda kutoa wito kwa mashabiki kujinunulia tiketi mapema ili kuepuka usumbufu,” alisema Victoria.
 
Naye Lady Jadee alisema, kwa kushirikiana na bendi yake ya Machozi wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatoa burudani ya nguvu kwa mashabiki wote watakaohudhuria.
 
“Nawaomba mashabiki wangu na wale urembo kujitokeza kwa wingi ili kufurahia burudani nzuri toka kwangu na bendi yangu ya Machozi, pia wasanii wenzangu waalikwa naamini watafanya vizuri siku hiyo,” alisema.
 
Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency, Hashimu Lundenga ambao ni waratibu wa Redd’s Miss Tanzania alisema, tiketi za shindano hilo tayari zimeshaanza kuuzwa katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
 
Alitaja maeneo ambayo yameteuliwa kuuza tiketi za Redd’s Miss Tanzania kwa mwaka huu ni duka la Shear Illusion lililopo Mlimani City, City Sports Lounge na Steers zilizopo Mtaa wa Samora, Faberk Fashion, Rose Garden Pub na ofisi za Redd’s Miss Tanzania ambazo zote zipo eneo la Mikocheni.
 
“Kwa mara nyingine tena napenda kuwashukuru wadhamini wetu wakuu  kinywaji cha Redd’s Original na wadhamini wenza ambao kwa kweli wamefanya kazi kubwa sana kuhakikisha shindano la mwaka huu linakuwa zuri na lenye tija kubwa.”
 
Lundenga alifafanua kuwa, ili kuwapa fursa watu wengi zaidi tiketi itakayonunuliwa katika vituo vilivyopangwa kabla ya shindano itakuwa ni Sh 80,000 na kutakuwa na ofa kadhaa.
 
Taji la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linashikiliwa na Brigitte Alfred, aliyefanikiwa kulitwaa mwishoni mwa mwaka jana.
 
Shindano la Redd’s Miss Tanzania linadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), huku wadhamini wenza wakiwa kinywaji cha Zanzi, hoteli ya Giragge, Star TV, gazeti la Nipashe, Uchumi Supermarket na Marie Stopes.

No comments:

Post a Comment