Wednesday, November 12, 2014

MBOWE AUNGANA NA LOWASSA

Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amesema serikali haipo makini kutafuta ufumbuzi wa tatizo la ajira kwa vijana na kutaka suala hilo liwe hoja maalum bungeni, serikali kuu, halmashauri na katika baraza la mawaziri, kwani ni janga la taifa.

Akichangia hotuba ya Waziri wa Fedha bungeni juzi kuhusu mapendekezo ya Serikali ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2014/15, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema), alisema ajira ni mkakati na siyo suala la kufumania ambalo linatokea tu na akashauri Rais wa awamu ya tano azingatie suala la ajira kwa vijana.

Akitoa mfano wa vijana 11,000 waliokwenda kufanya udahili wa kupata nafasi 70 za ajira Idara ya Uhamiaji iliyofanyika hivi karibuni Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, alisema tatizo la ajira ni kubwa na hana imani kama serikali ipo makini katika jambo hilo.

“Vijana 11,000 wanawania nafasi 70 za ajira Idara ya Uhamiaji, wabunge hapa tunaliona suala hilo kama mzaha tu, serikali iweke mikakati ya kupata ufumbuzi wa ajira,” alisema.

Alisema suala la ajira limezungumzwa na watu wengi akiwamo kiongozi mmoja mwandamizi sana katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini akaelezwa kwamba anafanya jambo la kuzua.

Ndani ya CCM kiongozi ambaye amekuwa akilizungumzia suala la ajira ni Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa. Mbowe, alitaka serikali kufanya maamuzi magumu na kutambua kuwa utitiri wa vijana ambao hawana ajira mitaani ni bomu linalosubiri kulipuka. 

Mbowe alisema mfumo uliopo sasa wa kila kitu kurundikwa serikali kuu, kama ndiyo inayofikiri kwa niaba ya Watanzania wote katika kutengeneza ajira hautatatua tatizo hilo, alitaka halmashauri zote 133 ziwe na mkakati wa kutengeneza ajira katika maeneo yao.

“Ajira iwe hoja maalum katika bunge hili, serikalini, baraza la mawaziri … tuweke mkakati wa kitaifa wa kutengeneza ajira.

“Hakuna sababu ya kuwa na wakurugenzi na wataalam wa uchumi katika halmashauri kama hawawezi kutengeneza ajira,” alisema.

“Nitawaelekeza hapa namna ya kupata Sh. bilioni 500 mpaka 800 za mikakati ya kupata ajira. Iwapo miradi ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma (PPP), kila wilaya ina utaratibu na mazingira yake, lakini moja inaweza kutengeneza ajira 500,000 kwa mwaka,” alisema.

Alishauri serikali kuanzia Mamlaka ya Majengo (Real Estate Authority - REA) ambayo itahusika kusimamia majengo mijini na kukusanya fedha kwa ajili kusaidia kujenga ajira.

Alisema miradi ya PPP katika halmashauri inaweza kupata kiasi hicho cha fedha na kuwapatia vijana ajira na kuwafanya wasikimbilie mijini baada ya kuona vijijini nako kuna maendeleo.

Alisema bila kufanya hivyo, vijana watalazimika kukimbilia mijini kwa sababu vijijini hakuna maendeleo na hakuna mwelekeo.
Alisema ni aibu kwa Halmashauri za Kinondoni na Ilala kutegemea ruzuku toka serikali kuu wakati inavyanzo vingi vya mapato ambavyo vinaweza kusaidia kutengeneza fedha na ajira kwa vijana.

“Mruhusu halmashauri zitengeneze fedha, zikusanye kodi…huu ni ushauri wa bure tu,” alisema.
Baada ya mchango huo, Naibu Spika Job Ndugai, alisema anakubaliana na Mbowe kwamba tatizo la ajira ni kubwa kuanzia kwa wahitimu wa darasa la saba, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu.

“Mwaka 2015 ajenda ni ajira. Kama kuna mtu anayetaka kura ajue kuwa ajira ni ajenda.  Kila mtu aliye makini na anayetaka chama chake kiongoze ni lazima azungumzia suala la ajira,” alisema.

Akizungumzia suala la ajira nje ya bunge jana, Lowassa, alisema ajira ni bomu ambalo linaanza kupasuka.

Alisema serikali yoyote iliyopo madarakani inapaswa kuzingatia au kutengeneza ajira kwa vijana.

Alisema idadi ya Watanzania ni milioni 48 na kila mwaka wahitimu wa vyuo vikuu wanafikia zaidi ya 40,000, lakini hakuna ajira.

“Lazima serikali ifanye mikakati ya kutengeneza ajira…suala la ajira ni bomu litakalopasuka wakati wowote,” alisema.

Alisema kwa mfano, ujenzi wa kiwanda chochote kile kama kiwanda cha pamba ni lazima uangalie ni kiasi gani cha ajira kiwanda hicho kitazalisha.

Akitoa mfano wa Rais Barak Obama wa Marekani, alisema aliweza kuchaguliwa kuingia Ikulu kwa awamu ya pili kutokana na kutengeneza ajira.


Alisisitiza kwamba ni lazima serikali itengeneze ajira kwa vijana wake.
Mbunge wa Viti Maalum, Sarah Msafiri, aliwataka wabunge na serikali kujiuliza kuhusu tatizo la ajira.
“Lazima tuwe na mkakati wa kitaifa wa kuwasaidia vijana. Zaidi ya vijana 40,000 wanahitimu vyuo vikuu kila mwaka, hivyo, ni lazima wasaidiwe,” alisema.

PAYE KILIO
Baadhi ya wabunge wamelalamikia wafanyakazi kukatwa kodi kubwa kwenye mishahara (PAYE) na kupunguziwa kwa asilimia moja katika bajeti ya mwaka 2014/15 na kwamba kufanya hivyo ni kuwaongezea ushawishi wa kufikiria njia nyingine za kupata fedha.

HAJI
Mbunge wa Konde, Khatib Saidi Haji (CUF), alisema punguzo la asilimia moja kutoka kwenye mshahara wa wafanyakazi ni sawa na kutomfanyia lolote. Alisema kada ya wafanyakazi ndiyo pekee inayolipa kodi kwa asilimia 100 kwa sababu hawana pa kujificha. 

Alisema pamoja na wafanyakazi kupeleka malalamiko yao kwa Muungano wa Vyama Huru vya Wafanyakazi (Tucta) angalau kodi  ishuke hadi asilimia 11, lakini busara imeonyesha ipungue kwa asilimia moja tu.

“Serikali iangalie wafanyakazi wapo katika hali ngumu sana na vishawisi vinaongezeka siku hadi siku. Mambo haya ya kodi kubwa yanawafanya wafikirie njia nyingine za kupata pesa,” alisema.


MATIKO
Esther Matiko (Viti Maalum, Chadema), alisema kodi ya wafanyakazi ndiyo sekta yenye uhakika ya kulipa kodi. Alipendekeza kuwa  angalau wafanyakazi wenye mishahara inayowawezesha kupata Sh. milioni nne kwa mwaka waanze kukatwa asilimia tisa ya kodi.

Aidha, wanaopekea Sh. 330,000 mpaka Sh. 700,000 kwa mwezi waanze kukatwa kodi kwa asilimia tisa ili kutoa unafuu katika kodi zao.

CHILOLO
Kwa upande wake Diana Chilolo (Viti Maalum, CCM), alisema  mfanyakazi kupunguziwa asilimia moja kwenye mshahara wake, haimsaidii kwani  akienda benki kukopa anakatwa, atakimbilia wapi matokeo yake ni kumuumiza.

“Mshahara unakatwa kodi, atabaki na nini, angalieni suala hili upya waondoleeni wafanyakazi kodi,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment