YAANZA NA WAGANGA WA RAMLI 26 WAKAMATWA...TAZAMA MAJINA YAO HAPA
Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga limewakamata waganga wa tiba asilia 26 katika wilaya za Kishapu,Shinyanga na Kahama katika msako mkali wa kuwasaka na kuwabaini waganga wa jadi wanaojihusisha na shughuli za upigaji ramli chonganishi wanaotajwa hujihusisha na mauaji ya albino nchini.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alisema operesheni ya kuwakamata waganga hao iliendeshwa katika wilaya za Kahama, Kishapu na Shinyanga kuanzia Machi mosi hadi Machi 9, mwaka huu ambapo baadhi ya waganga hao wanatuhumiwa kujihusisha na mambo ya ukataji mapanga.
Kamanda Kamugisha alisema, operesheni hiyo ilihusisha kuwapekua, kuwahoji na kisha kuwafikisha mahakamani wale wote waliobainika kujihusisha na upigaji wa ramli chonganishi ambapo baadhi yao walikutwa wakiwa na vifaa vya kupigia ramli hizo wakiwemo wanaojihusisha na ukataji mapanga vikongwe.
Alisema, katika msako huo waganga hao walikamatwa pia wakiwa na nyara mbalimbali za serikali, ikiwemo ngozi za fisi, kicheche, nyani,nyati, simba, nyegere, korongo, digidigi, kitovu cha mbweha na mikia ya nyumbu, pembe na viungo mbalimbali vya wanyama wa aina tofauti tofauti ikiwemo vibuyu vilivyovishwa shanga.
Vifaa vingine ni mafuvu ya mbwa,vioo vya kupigia ramli,ngozi ya kalunguyeye,mwewe,mifupa na ndege pori,visu,vyuma,nyoka,mikuki,shanga na vitu vingine vya ajabu ajabu.
Kamanda Kamugisha aliwataja waganga waliokamatwa, kuwa ni Ester Madirisha (65) mkazi wa Mwalukwa, Selekwa Nicholaus (42) mkazi wa Mwang’osha, Siyantemi Jinasa (41) mkazi wa kijiji cha Ibubu, Fatuma Shija (47) mkazi Ngogwa Kahama, Makandi Guma (51) mkazi wa Ibubu na Gamaweshi Mayala (49) mkazi wa kijiji cha Lubaga.
Wengine waliokamatwa ni, Saimon Lukelesha (34), Jidanda Samanya (20) na John Lubanga (28) wote wakazi wa mkoa wa Tabora, Samwel Zengo (37) mkazi wa Lagana, Jimoka Jitobelo (93) mkazi wa Ibingo, Shija Venji mkazi wa Ibingo Samuye, Milembe Ndahya (50) mkazi wa Isela, Kashinje Nyakali (55) mkazi wa Samuye na Nzela Maige (55) mkazi wa Isela Samuye.
Akifafanua Kamanda Kamugisha alisema, katika msako huo watu wanne walikamatwa wakituhumiwa kwa makosa ya kujihusisha na ukataji mapanga, ambao ni John Sabuni (45) mkazi wa Shinyanga, James Machimanya (34) “Jaji”mfanyabiashara mkazi wa Kishapu, Jackson Charles (55) mkazi wa Shinyanga, Juma Ndodi (50) mkazi wa kijiji cha Buyange.
Wengine waliotajwa kuwa ni Kashinje Kayila (46) “Ntelezu”, Tabu Salamba (43) “Mandago” wote wakazi wa kijiji cha Ngaganulwa kata ya Usanda, Itwelyamhela Shija (28), Jilala Maige (44) wote wakazi wa kijiji cha Singita kata ya Usanda, Nyanzobe Shija (36), Mbula Maduka (57), Masalu Nkuba (53) na Lugonda Kwangu (45) wote wakazi wa Ibadakuli Shinyanga.
Hata hivyo kamanda Kamugisha alisema, mpaka hivi sasa jeshi la polisi linaendelea kumsaka mganga mmoja Milembe Shinji mkazi wa kijiji cha Ibingo ambaye hajakamatwa kutokana na kutoweka nyumbani kwake wakati opereshini hiyo ilipokuwa ikiendelea ambapo upekuzi ulifanyika katika nyumba yake na kukamatwa kwa vifaa kadhaa ikiwemo nyara za serikali.
“Wote hawa baada ya kuwafanyia mahojiano tayari wamefikishwa mahakamani ambako wamesomewa mashitaka yao ya kujihusisha na vitendo vya upigaji ramli chonganishi na ukataji wa mapanga ikiwemo kupatikana na nyara za serikali wanazozimiliki bila vibali vya serikali, operesheni hii bado inaendelea katika maeneo mbalimbali ya mkoa," alisema Kamugisha
No comments:
Post a Comment