Naibu Spika, Job Ndugai, amesema madai yanayotolewa kuwa amezuiliwa kuendesha shughuli za Bunge ni mambo ya kawaida.
Tangu kumalizika kwa mkutano wa Bunge wa 16 na 17 ambao ulijadili kashfa ya uchotaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Bunge kutoka na maazimio nane, Ndugai hajawahi kuonekana bungeni kuongoza shughuli za Bunge.
Hakuhudhruia Mkutano wa 19 na wa 20 unaoendelea hivi sasa., hali iliyozua madai kutoka kwa baadhi ya wabunge na watu wengine kuwa amezuiliwa kuendesha shughuli za Bunge kutokana na msimamo wake wa kuruhusu kujadiliwa kwa kashfa hiyo bungeni.
Baadhi ya watu ambao wamezungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti mjini Dodoma walisema kitendo cha Ndugai kutoa uhuru zaidi wakati wa mjadala wa sakata la Escrow inadaiwa hakikuwafurahisha wakubwa kwani ilipelekea serikali kutikisika.
Ndugai alipoulizwa na NIPASHE jana kwa njia ya simu kuhusiana na taarifa hizo, hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo zaidi ya kuomba asilizungumzie.
Hata hivyo, alisema kwa kifupi: “Naomba uwaambie waachane na hiyo issue (jambo), siwezi kuzungumza lolote, mbona ni la kawaida tu.”
Alipoulizwa kuwa kwa sasa yuko wapi, alisema kuwa alikuwa safarini bila kueleza alikokuwa akielekea.
Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani, alipoulizwa kama anafahamu aliko Ndugai, alisema hafahamu kwa kuwa wabunge hawajajulishwa na ofisi ya Bunge.
Kwa upande wake Mbunge wa Mhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), alisema kiutaratibu Spika wa Bunge, Anne Makinda alitakiwa kuwafahamisha aliko Ndugai lakini kwa bahati mbaya hajatujulisha.
Taarifa za awali kutoka kwa wafanyakazi wengine Bungeni walisema Ndugai ni mgonjwa.
Wafanyakazi hao walisema mara baada ya kikao cha Bunge cha mwezi Novemba mwaka jana Ndugai ambaye ni pia ni Mbunge wa Kongwa, alianza kujisikia vibaya kiafya na hivyo kwenda nchini India kwa matibabu.
Inadaiwa Ndugai ambaye amekaa huko kwa muda mrefu alirejea nchini mwanzo mwa wiki iliyopita na alipitia Dar es Salaam kwa ajili ya kupumzika.
Mwandishi wa NIPASHE alipofika ofisi ya Naibu Spika kuomba kuonana naye, Katibu Muhtasi ambaye jina lake halikufahamika, alisema Ndugai hayupo kwa muda mrefu na hawafahamu aliko.
Chanzo kingine kilieleza kuwa muda mfupi kabla ya Mkutano wa sasa wa Bunge kuanza, Ndugai alikuwa Dar es Salaam akijiandaa na safari ya kwenda nje kwa matibabu.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah, alisema Ndugai ataongoza vikao vya Bunge kuanzia leo.
Dk. Kashililah alisema Ndugai alikuwa amesafiri kikazi nchini Ubelgiji ambako alihudhuria mkutano na alipitia India kufanyiwa uchunguzi wa afya yake, lakini amesharejea nchini.
Katika kipindi ambacho Ndugai hakuwapo, vikao vya Bunge vilikuwa vinaendeswa na Spika Makinda, wenyeviti wa Bunge, Mussa Zungu na Rediana Mng'ong'o.
“Leo Mheshimiwa Ndugai atakuwapo bungeni kwa sababu Spika amebaki pekee yake baada ya Mheshimiwa Zungu kwenda Dar es Salaam kwenye mafuriko na Mheshimiwa Mng’ong’o amekwenda nje ya nchi kuhudhuria mkutano,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment