HOTUBA YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI NA MADINI JOHN JOHN MNYIKA (MB) KUHUSU MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI JUU YA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2012/2013 NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
HOTUBA YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI NA MADINI JOHN JOHN MNYIKA (MB) KUHUSU MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI JUU YA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2012/2013 NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
A: UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Ofisi
ya Waziri wa Nishati na Madini ilianzishwa kwa mujibu wa kipengele cha
21 cha Nyongeza ya Waraka wa Rais uliochapishwa kama Tangazo la Serikali
Na. 494 la tarehe 17 Desemba 2010. Majukumu ya Ofisi hii yameainishwa
katika Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2010
(The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 2010)
lililochapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na.
494A la tarehe 17 Desemba 2010.
Mheshimiwa Spika, Katika
kujadili Mapitio ya Utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2012/2013 na
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka
wa fedha 2013/2014 naomba tuyatafakari maandiko ya katika muktadha wa
uongozi wetu wa leo na hatma ya sekta hizi mbili muhimu za nishati na
madini.
Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha TUJISAHIHISHE katika ukurasa wa pili tutafakari kwamba, naomba kumnukuu ‘ukweli
una tabia moja nzuri sana. Haujali mkubwa wala mdogo; haujali adui wala
rafiki. Kwake wote ni sawa. Pia ukweli unayo tabia ya kujilipiza kisasi
kama ukipuuzwa.Ukiniona nataka kulipiga teke jiwe kwa kuwa nafikiri
kuwa ni dongo au mpira, natumaini utanionya. Lakini nikilipuuza onyo
lako kwa sababu eti wewe ni mdogo au kwa sababu sikupendi, nitalipiga
teke, basi litanivunja dole japo ningekuwa nani. Ukweli haupendi
kupuuzwapuuzwa.
Mheshimiwa Spika, Tuendelee kutafakari maandiko ya Nyerere kwamba ‘Wakati
mwingine, mtu tunayempinga huwa anamakosa kweli, lakini hoja
tunazozitoa ni za kinafsi na hazihusiani kabisa na hoja zake.Nikisema
mbili na tatu ni sita, nakosa. Lakini ni bora kunionyesha kwamba pengine
nilifikiri tunazidisha kumbe tunajumlisha.Ni kweli mbili mara tatu ni
sita;lakini mbili na tatu ni tano, siyo sita. Lakini ukijaribu
kuwashawishi wenzetu wakatae mawazo yangu na kukubali yako kwa kusema
kuwa meno yangu ni machafu ,au natoa kamasi daima, utakuwa unatumia hoja
ambazo hazina maana, Huu ni mfano wa upuuzi; lakini mara nyingi hoja
tunazozitumia kuwashawishi watu wakatae mawazo ya wale tusiowapenda,au
kukubali mawazo yetu, huwa hazihusiani kabisa na mambo tunayojadili’.
Mheshimiwa Spika, Tutafakari maandiko ya Mwalimu Nyerere katika kitabu chake chaUONGOZI WETU NA HATIMA YA TANZANIA uk.
50, nanukuu “Rais Mwinyi ni mtu mwema na mpole, lakini ni kiongozi
dhaifu; au upole wake na udhaifu wake unatumiwa na watu ambao wala si
wema wala wapole kuhatarisha umoja na amani ya nchi yetu, Kipindi chake
cha pili kinakaribia kwisha”.
Mheshimiwa Spika, Tutafakari maandiko mengine ya Mwalimu Nyerere kwamba “lakini
hatulazimiki kuendelea na uongozi mbovu wa chama na Serikali. Wala
tukiendelea na hali hii, bila kubadili uongozi wa Chama na Serikali,
sina hakika kama tutafika huko salama. Masuala muhimu ya nchi yetu
hayatashughulikiwa.Viongozi wetu wataendelea na matendo yao ya kuvuruga
muungano. Matatizo ya kweli ya muungano hayatashughulikiwa, maana hatuna
serikali ya kuyashughulikia.Na masuala mengine muhimu ya uchumi, huduma
za umma, rushwa,chuki za uzawa na ukabila na udini yataachwa yajitatue
yenyewe. Nasema, katika hili kama hiyo sina hakika kama tutafika
salama;na tukifika “salama”, tukiwa na uongozi huu huu wa chama na
serikali, mbele yetu kutakuwa ni giza tupu. Majuto ni mjukuu, huja
baadaye. Tunaweza tukafikishwa mahali tukilinganisha uongozi wa rais
Mwinyi na wa rais wa kesho tukaona kuwa chini ya Ndugu Mwinyi, Pamoja na
udhaifu wake wote, tulikuwa peponi”!
Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere anaendelea kuandika kwamba “Waingereza
wana msemo “Nature abhors vacuum”, “hulka huchukia ombwe” . Hata siasa
huchukia ombwe. Kama uongozi ni mbovu, upo kama haupo au upo kwa mas
lahi ya wenyewe, watatokea watu waujaze uwazi uliopo;hauwezi kuachwa
wazi hivi hivi.Lakini uongozi mbovu ni kama mzoga, unatabia ya
kukaribisha mafisi na mainzi. Tusidhani kuwa hulka ya siasa yetu ni
tofauti na hulka ya siasa ya watu wengine; kwamba sisi tunaweza
kuvumilia uongozi mbovu na tusivune matunda ya hulka ya uongozi mbovu”.
Mheshimiwa Spika, Mwalimu
Nyerere alikuwa akiandika wakati wa awamu ya Rais Mwinyi kuhusu masuala
yanayohusu Muungano; sisi tutafakari maandiko haya katika muktadha wa
uongozi wa sasa wa taifa letu na mustakabali wa sekta nyeti kwa uchumi
wa nchi na maisha ya wananchi za nishati na madini.
B: MASUALA MTAMBUKA
1.0 MAPITIO UJUMLA YA UTEKELEZAJI KWA MWAKA 2012/2013 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2013/2014
Mheshimiwa Spika, tarehe
27 Julai, 2012 niliwasilisha Bungeni maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 na
makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha
2012/2013. Kufuatia maoni hayo, yapo masuala machache ambayo Serikali
imeyazingatia kwenye utekelezaji na mengine mengi ambayo Serikali
haikuyazingatia pamoja na umuhimu wake kwa maslahi ya nchi na maisha ya
wananchi.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani ilitaka kiwango cha bajeti ya Wizara ya Nishati na
Madini kuongezwa, miongoni mwa masuala ambayo serikali imetekeleza ni
pamoja na kuongeza bajeti ya wizara hii kwa kupanga kutumia kwa mwaka
2013/2014 jumla ya shilingi 1,099,434,031,000/= ikilinganishwa na mwaka 2012/2013 ambako kiasi cha shilingi 641,269,729,000/= kilipangwa
kutumika. Aidha napenda kuikumbusha serikali kuzingatia vipaumbele vya
miradi ya maendeleo ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani ilipendekeza katika
Hotuba zake za 2011 na 2012 ili kuweza kuleta maana ya ongezeko hili la
bajeti kwa maana ya kuvipatia vipaumbele uzito unaostahili kwa Kuwekeza
fedha za kutosha kwenye sekta ya umeme na Gesi ili kumaliza kabisa
tatizo la nishati ya Umeme na kupunguza gharama za maisha kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilishauri kuwepo kwa mfumo thabiti wa
kuhakikisha maoni na maazimio yanatekelezwa kwa wakati na kwa ukamilifu.
Lakini serikali imeendelea kupuuza mapendekezo hayo na kutoa ahadi
ambazo haikuwa tayari kuzitekeleza, mathalani ahadi ya Mhe Waziri Mkuu
aliyotoa wakati akiahirisha bunge la bajeti 2011/2012 ya kupunguza
matumizi yasiyo ya lazima ili kuongeza pesa wizara ya Nishati na Madini
lakini tofauti na ahadi yake, Serikali ikaamua kuja na mpango wa kukopa
fedha katika taasisi za fedha ili kulinusuru shirika la umeme Tanzania
TANESCO, ambao nao haujatekelezwa kwa ukamilifu.
Mheshimiwa Spika, pamoja
na hali hiyo ninatambua maoni machache ambayo yalizingatiwa kuhusu gesi
asili, ikiwemo kuendelezwa kwa mchakato wa kuwa na sera na sheria ya
gesi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA ikaitaka
Serikali ieleze hatua ilizochukua juu ya maoni ya kambi rasmi ya
Upinzani Bungeni ambayo hayakuzingatiwa na mengine yaliyotolewa na
Kamati ya Kudumu ya Bunge na michango ya Wabunge kwa nyakati mbalimbali
mwaka 2011 na 2012.
Aidha, ni
Kwa bahati mbaya kabisa serikali haikupenda kufanyia kazi maoni na
ushauri iliyopewa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,kamati ya Bunge na
wabunge mbalimbali kwa nyakati tofauti na ambayo kama yangezingatiwa
kikamilifu yangeweza kuliepusha taifa na matatizo yaliyotokea katika
mikoa ya Lindi na Mtwara na ambayo bado yanaendelea mpaka sasa.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013 makadirio ya mapato na matumizi ya kawaida yanaombewa jumla ya shilingi 107,221,286,000/= kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi 11,612,542,000/= ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa wizara na taasisi zilizochini yake na kiasi cha shilingi 95,608,744,000/= ni kwa ajili ya matumizi mengine (OC). Matumizi haya yanaonekana ni pungufu ya kiasi cha shilingi 2,857,582,000/= kwenye bajeti ya mwaka jana katika fungu hili la matumizi ya kawaida.
Mheshimiwa Spika, upungufu
huu, unaacha maswali, Kambi rasmi ya upinzani Bungeni inaitaka serikali
kuwaeleza watanzania sababu za kupungua kwa bajeti ya mishahara ya
wizara na taasisi zilizokochini yake, ambayo katika mwaka wa fedha
2012/2013 Wizara ya Nishati na Madini ilitengewa shilingi 17,292,347,000/= na kwa mwaka huu wa fedha 2013/2014 serikali inaomba kiasi cha shilingi 11,612,542,000/= ikiwa ni pungufu ya shilingi 5,679,805,000/= Kambi
Rasmi ya Upinzani inataka majibu kwa kuwa wakati wafanya kazi
wakitarajia kupandishwa madaraja na ongezeko la mishahara kutokana na
kupanda kwa gharama za maisha pamoja na mfumko wa bei, bajeti ya
mishahara kwa Wizara na taasisi zilizochini yake inapunguzwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inataka maelezo iwapo punguzo hilo ni kutokana na
kubana matumizi au ni udhaifu katika maandalizi ya bajeti na nini athari
zake kwenye ufanisi wa wizara na taasisi zake? Au wizara imebaini
mianya ya ufisadi ambayo ilikuwepo katika bajeti zilizopita kuhusiana na
fungu la mishahara?
Mheshimiwa Spika, Serikali
hii ya CCM inaonekana kuziba masikio katika kupunguza matumizi yasiyo
ya lazima pamoja na Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, wananchi na wadau
wa maendeleo kulipigia kelele swala hili. Jambo hili limejirudia kwa
upande wa matumizi ya kawaida, ambapo serikali iliomba kiasi cha shilingi 92,786,521,000/= katika Bajeti ya mwaka 2012/2013 na mwaka huu wa fedha 2013/2014 serikali inaomba kiasi cha shilingi 95,608,744,000/= ikiwa ni ongezeko la shilingi 2,822,223,000/=.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai kwa wabunge na Bunge kuungana
pamoja kabla ya kupitisha matumizi haya makubwa na kuitaka Wizara ya
Nishati na madini kubana matumizi kwa kupunguza matumizi yasiyo ya
lazima ili tupate fedha za kuwekeza kwenye nishati .
Mheshimiwa Spika, katika
kuendelea kuonyesha udhaifu na uwezo mdogo wa wizara katika kusimamia
sheria za nchi, kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya Juni 2012 nchi imepoteza
kiasi cha dola za kimarekani 12,634,354.61 sawa na shilingi bilioni
19.71. Hizi ni fedha ambazo hazikukusanywa kutoka kwa makampuni ya
madini kwa kufuata sheria mpya ya madini ya mwaka 2010, kifungu cha
87(1) kuwa mrahaba wa 4% utozwe kabla ya makato na badala yake mrahaba
ukawa ni 3% na kutozwa baada ya makato kama sheria ya zamani ilivyokuwa.
Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 na 2012/2013,
serikali iliathiriwa kwa kiwango kikubwa na mvutano baina ya Watendaji
Waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake kwa upande
mmoja na baadhi ya wabunge kwa upande mwingine katika mvutano ambao
uliambatana na kutuhumiana hadharani kupitia vyombo vya habari juu ya
madai ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka. Baadhi
yamejidhihirisha kufuatia chunguzi na ripoti zilizofanyika na kubaini
kasoro kubwa za kiutendaji hususan kupitia ukaguzi maalum uliofanywa na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Shirika la Umeme
(TANESCO).
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA, inataka Serikali ieleze
hatua iliyofikiwa katika uchunguzi juu ya ununuzi wa mafuta mazito kama
ambavyo tulipendekeza ufanyike. Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kwamba
Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA) nayo iliwahi kueleza kwenye vyombo
vya habari kuwa imeanza uchunguzi ambao ulipaswa kukamilika mwaka 2012;
hivyo tunataka taarifa ya uchunguzi iwekwe hadharani na Serikali ieleze
hatua ilizochukua dhidi ya madai ya ufisadi na matumizi ya madaraka
kupitia mianya ya dharura ya umeme.
2.0 Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge
2.1 Maazimio ya uchangishaji haramu wa fedha wizara ya nishati na madini (‘Sakata la Jairo’).
Mheshimiwa Spika, kwa
kipindi cha mwaka 2011/2012 Bunge lako lilishuhudia mambo kadhaa
yaliyokiuka miiko ya uongozi, ambalo yalilazimu bunge kuunda kamati
teule kuchunguza uhalali wa uchangishaji uliofanyika katika Wizara ya
Nishati na Madini (‘Sakata la Jairo’) na baadhi ya mapendekezo yake
ambayo yalipitishwa kuwa maazimio yalikuwa;
(1). Kamati Teule inapendekeza kwamba Serikali ichukue hatua za
kinidhamu kwa Ndugu David Kitundu Jairo kwa matumizi mabaya ya madaraka,
kukusanya na kutumia fedha za Serikali kinyume cha Sheria, Kanuni na
Taratibu za Fedha za Umma na kuruhusu matumizi mabaya ya fedha za Umma.
(2)Vile vile Serikali iwachukulie hatua za kinidhamu, kwa mujibu wa
Sheria, watumishi wote wa Wizara ya Nishati na Madini waliotajwa kwenye
Taarifa hii kushiriki kwa namna mbalimbali katika mchakato wa
uchangishaji na matumizi ya fedha hizi za umma. Aidha, kwa kuwa kwa
mujibu wa Mwongozo wa Baraza la Mawaziri Waziri ndiye Msimamizi Mkuu wa
Wizara, hivyo suala la uchangishaji halikupaswa kufanyika bila yeye
kufahamu,
(3). Kamati Teule inapendekeza Serikali ichukue hatua zinazofaa kwa Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. William Ngeleja, (Mb.)
(4).,……….. Kamati Teule inapendekeza Serikali ichukue hatua zinazofaa
kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa upotoshaji huo..
,
(5). …… Kamati Teule inapendekeza Serikali ichukue hatua zinazofaa kwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inahoji ni kwanini
hadi sasa Bunge hili limeshindwa kuhakikisha kwamba maazimio haya
yametekelezwa na Serikali? Hakika huu ni uzembe wa wazi wa Bunge
kushindwa kutimiza majukumu yake ya kuisimamia serikali kwa mujibu wa
Katiba.
Aidha, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hatua za
utekelezaji wa maazimio hayo ya Bunge, kwani baadhi ya wahusika bado
wapo ma-ofisini wakiendelea na kazi na wengine wakiendelea kuteuliwa
kushika nafasi zingine katika uongozi na utumishi wa umma kama vile
hakuna liliowahi kutokea.
2.2 MAAZIMIO YA RICHMOND
Mheshimiwa Spika: Itakumbukwa
kwamba taarifa mbili za serikali kuhusu utekelezwaji wa maazimio haya
ziliwasilishwa Bungeni na Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, tarehe 28
Agosti, 2008 na tarehe 11 Februari, 2009 . Taarifa moja ilikabidhiwa na
kujadiliwa na Kamati, ambazo zililitaarifu Bunge kuwa utekelezaji wa
Maazimio 10 kati ya 23 yaliyotolewa na Bunge, yalifanyiwa kazi hadi
mwezi Februari, 2009 na Maazimio 13 bado yalikuwa hayajakamilika.
Mheshimiwa Spika; Bunge
liliazimia kwamba taarifa za utekelezaji wa maazimio yaliyobaki
ziwasilishwe kwa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambayo hata
hivyo katika mwaka 2011, 2012 na mpaka mabadiliko ya muundo wa Kamati
yalipofanyika kamati hiyo haikuwasilisha taarifa yoyote bungeni ya
kueleza kukamilika kwa utekelezaji wa maazimio husika hali ambayo
inahitaji bunge kuingilia kati kuweza kuisimamia Serikali kwa mujibu wa
Katiba ya Nchi Ibara ya 63 (2) na (3).
Mheshimiwa Spika, katika
hali inayozua maswali kuhusu umakini wa Bunge katika kusimamia maazimio
yake mwaka 2011, Mbunge wa Monduli Mheshimiwa Edward Lowassa; aliyekuwa
Waziri Mkuu na kujiuzulu kufuatia kashfa hiyo ya Richmond alichaguliwa
kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama
iliyopewa dhamana na Bunge kufuatilia utekelezaji wa maazimio kuhusu
mkataba kati ya TANESCO na Richmond. Katika hali hiyo, haishangazi
kwamba kwa miaka miwili toka wakati huo, mpaka mabadiliko ya Kamati za
Bunge yalipofanyika; Kamati hiyo katika Taarifa zake zote bungeni
haijawahi kuisimamia Serikali kuhakikisha maazimio husika ya Bunge
yanatekelezwa. Huu ndio uwajibikaji, ndani ya Serikali na uongozi wa
Bunge; vyote vikiongozwa na CCM.
Mheshimiwa Spika, sasa
inajulikana wazi kuwa Mkataba wa TANESCO na Richmond ulirithishwa
kinyemela kwenda kwa Dowans kama inavyoonekana katika nyaraka za
mahakama ambapo Dowans na Richmond zilidaiana huko Marekani; na kuwa
hilo lilifanyika bila kuitaarifu TANESCO kinyume na kifungu cha 15:12
cha Mkataba huo.
Mheshimiwa Spika, Kutokana
na hukumu ya Dowans ushahidi umepatikana na kuwa mashahidi mbalimbali
walioitwa mbele ya Kamati Teule ya Bunge na wakiwa chini ya kiapo
walitoa taarifa za uongo kuwa mkataba kati ya Richmond na Tanesco
ulihamishwa kwenda Dowans Disemba 23, 2006 na hivyo wahusika hao
mbalimbali – wakiwemo wamiliki wa Richmond – walidanganya au kuficha
ukweli mbele ya Kamati Teule na hivyo kuonesha dharau dhidi ya Bunge.
Mheshimiwa Spika; Masuala
haya ni muhimu yakajadiliwa sasa ili kupata undani wa wahusika
wanaopaswa kubeba mzigo wa fidia kwa kampuni ya Dowans badala ya
kubebesha mzigo huo TANESCO na umma wa watanzania. Kushindwa
kuwashughulikia kwa ukamilifu mafisadi wa Richmond na kukwepa kutumia
mianya ya sheria za kimataifa kukana mikataba iliyoingiwa kwenye
mazingira ya ufisadi kwa mara nyingine tena kunaelekea kuligharimu taifa
hivyo wakati umefika sasa wa Bunge kuingilia kati kwa niaba ya
wananchi.
Mheshimiwa Spika; Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Wizara ya Nishati na Madini na Serikali kwa
ujumla kutoa majibu bungeni juu ya hatma ya maazimio 10 yaliyobaki:
Nambari 3,5,7,8,9,10,11,13,14 na 18 ili bunge liweze kuishauri na
kuisimamia serikali kuhakikisha maazimio husika yanatekelezwa kwa
ukamilifu na kwa haraka.
Kambi
Rasmi ya Upinzani, inataka Taarifa ya utekelezwaji wa Maazimio tajwa
yaliyotolewa na Bunge juu ya Mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya
Richmond Development Company LLC badala ya kuwasilishwa kwenye Kamati ya
Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambayo kwa sasa haipo, sasa iwasilishwe
kwenye Bunge zima ili yaweze kujadiliwa na hatima yake iweze
kujulikana.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze kwanini mpaka sasa
haijatekeleza maazimio hayo na bunge liweke muda wa ukomo wa kutekeleza
Maazimio yote ya Bunge yaliyokuwa yamesalia katika sakata hili la
Richmond ili mara moja na daima sakata hili la Richmond limalizwe na
kufungwa baada ya maazimio yote kutekelezwa kwa ukamilifu. Ikiwa
maazimio ya mwaka 2008 utekelezaji wake haujakamilika mpaka mwaka 2013
kwa miaka mitano, nini kitalihakikishia taifa kwamba maazimio mengine
mapya yaliyopitishwa 2011 na 2012 yatatekelezwa kwa wakati na kwa
ukamilifu?
Mheshimiwa Spika: Azimio Na. 3, ambalo liliagiza kwamba “Mkataba kati ya TANESCO naRichmond
Development Company LLC (uliorithiwa na Dowans Holdings S.A.) na ile
kati ya TANESCO na IPTL, SONGAS, AGGREKO na Alstom Power Rentals, ipitiwe
upya mapema iwezekanavyo kama ambavyo Mikataba ya Madini ilivyopitiwa
upya na Serikali”. Iwapo Azimio hili lingetekelezwa kwa ukamilifu wake,
gharama za uzalishaji TANESCO na serikali kwa ujumla zinazotokana na
matatizo katika mikataba zingepungua.
(1) Mheshimiwa Spika, Azimio Na. 5 Mkataba
kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC na sasa Dowans
Holdings S.A umesheheni makosa mengi ya kisheria yanayoashiria udhaifu
mkubwa wa kitaalamu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au
ukosefu wa umakini ama ubinafsi katika kuiwakilisha Serikali. Kwa mfano,
kushindwa kutambua ukosefu wa sifa za kikampuni za Richmond Development
Company LLC; kushindwa kuishauri Serikali kuifanyia kampuni hiyo
ukaguzi wa awali (due deligence) au ukaguzi baada ya uteuzi (post
qualification); kushindwa kutambua tofauti kati ya consortium agreement
na proprietary information agreement; kushindwa kuona dosari kisheria za
proprietary information agreement; kushindwa kuona tofauti kisheria
kati ya Richmond Development Company LLC, RDEVCO,RDVECO na RDC, majina
ambayo wamiliki wa Richmond Development Company LLC walikuwa wanayatumia
kwa kubadilisha badilisha (interchangerbly) kwa makusudi; kushindwa
kuwashauri Wajumbe wa GNT kwamba business card si mbadala wa hati
mahsusi kisheria; kushindwa kuishauri Serikali kuhakikisha kuwa
muhtasari wa majadiliano kati ya Kamati ya Serikali ya Majadiliano (GNT)
na Richmond Development Company LLC ambao ulizingatia baadhi ya maslahi
ya nchi, uwe sehemu ya Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development
Company LLC; kushindwa kuishauri Serikali kutumia fursa iliyokuwepo wazi
ya kuvunja Mkataba baada ya Richmond Development Company LLC kushindwa
kutekeleza sehemu yake ya Mkataba; kushindwa kuhudhuria idadi kubwa ya
vikao muhimu vya majadiliano;n.k. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye
katika majadiliano yake na Kamati Teule alionyesha kutokuelewa kabisa
kilichokuwa kinatendeka na wasaidizi wake, na mwakilishi wa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali Wakili wa Serikali Donald Chidowu, ambaye ushiriki wake
katika GNT haukuwa na tija yeyote, wawajibishwe na Mamlaka ya juu ya
nchi kwa kuchangia kuiingiza nchi katika mkataba wa aibu.
(2)
Mheshimiwa Spika, Azimio Na. 7 lilikuwa “ Kamati Teule inapendekeza kuwa
Wajumbe wote wa GNT ambao ni maafisa waandamizi wa Serikali
wawajibishwe mara moja kwa kushindwa kutumia elimu na ujuzi wao kulinda
maslahi ya Taifa”.
Aidha, Azimio namba 9 lilikuwa linataka mabadiliko ya haraka ya uongozi wa taasisi ya TAKUKURU.
Mheshimiwa Spika, Azimio
Na. 13 “ Kamati Teule inatoa wito kwa Kamati zote za Bunge zihakikishe
kuwa zinapitia mikataba mikubwa na ya muda mrefu ya kibiashara chini ya
sekta zao ili kuliondolea Taifa mizigo isiyo ya lazima. Pale ambapo
upatikanaji wa mikataba hiyo unakwamishwa kwa urasimu usio wa lazima
Kamati zitumie utaratibu uliotumiwa na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na
Biashara ya kuunda Kamati Teule yenye ufunguo wa mikataba iliyofichika”.
Mheshimiwa Spika, Azimio
Na. 14 “Kamati Teule inapendekeza kwamba Waziri wa Nishati na Madini wa
wakati huo Mhe. Dk. Ibrahim Msabaha (Mb) na Katibu Mkuu Ndugu Arthur
Mwakapugi wachukuliwe hatua kali za kinidhamu kwa kuliingiza Taifa kwa
makusudi kwenye mkataba na kampuni ya mfukoni ambao umesababisha hasara
kubwa kwa nchi. Aidha Kamishna wa Nishati Ndugu Bashir Mrindoko naye
achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kushindwa kumshauri Katibu Mkuu mpya
wa Wizara kuhusu udhaifu wa Richmond Development Company LLC ambao
ulijulikana dhahiri na Wizara toka mwaka 2004 kwenye mkataba wa Bomba la
Mafuta. Ndugu Mrindoko ndiye aliyeiandikia barua kampuni hiyo kusitisha
mkataba wake na Serikali mwezi mmoja tu kabla ya mchakato wa zabuni ya
umeme wa dharura haujaanza”.
2.3 Kamati ya wataalamu wa Ofisi ya Spika.
Mheshimiwa Spika, mbali
na maazimio hayo pia kuna uchambuzi uliofanywa na kamati ya wataalam wa
Ofisi ya Spika, kuhusiana na makampuni yanayouza umeme kwa TANESCO
ambayo mikataba yake haipishani na ule wa RICHMOND, taarifa hiyo
iliwasilishwa Bungeni wakati Mhe Harrison Mwakyembe akiwasilisha Taarifa
yake ya Kamati Teule ya RICHMOND ili Waziri atoe ufafanuzi ni kwa
kiwango gani mapendekezo yake Serikali imeyafanyia kazi;
(a) “Uhalali kisheria wa Kampuni ya Aggreko (legal status)
Kwa
mujibu wa maelezo yaliyomo kwenye Mkataba, Kampuni ya Aggreko
International Projects Limited ni Kampuni iliyosajiliwa chini ya Sheria
za nchi ya Scotland. Uchambuzi na utafiti wetu haukuweza kuthibitisha
kuwa Kampuni hiyo kweli imesajiliwa kisheria huko Scotland ili kubaini
kama kulikuwa na udanganyifu kama ule uliofanywa na Kampuni ya RICHMOND,
yaani kutoa taarifa za uongo kuhusu uhalali kisheria wa Kampuni.
(b) Malipo ya Kodi
Kama ilivyo katika Mkataba wa Kampuni ya Richmond, Kifungu cha 3.4
cha Mkataba wa AGGREKO kinatamka kwamba, kodi zote na malipo mengine
yanayotokana na uingizaji nchini na utoaji nchi za nje ya nchi wa
Mitambo ya uzalishaji wa umeme, ikiwa ni pamoja na vipuri na vifaa
vingine vinavyohusika na uendeshaji wa Mtambo huo italipwa na TANESCO.
Aidha, Kifungu hicho kimeweka pia sharti kwamba, pale ambapo bodi au
malipo yoyote yatadaiwa na Mamlaka yoyote ya kodi kutoka kwa AGGREKO,
Kampuni hiyo italijulisha Shirika la TANESCO ambalo litalipa kodi au
malipo hayo kwa mamlaka husika au litairejeshea AGGREKO fedha ambazo
itakuwa imelipa kwa Mamlaka hiyo katika kipindi cha siku 14.
(c) Malipo
Kwa mujibu wa Vifungu vya 4.2 na 4.3 vya Mkataba, Shirika la TANESCO
linawajibu wa kuilipa Kampuni ya Aggreko malipo yafuatayo:-
i. ‘Capacity Charge’ – Dola za Marekani 35.928 kwa Kw kwa mwezi [Tazama Kiambatanisho C cha Mkataba].
ii. Malipo ya Umeme (energy purchase price) – Dola 4.99 kwa Kwh
[Tazama tafsiri ya interim energy purchase price katika uk. wa 3 wa
Mkataba]
(d) Fidia kwa Ucheleweshaji wa Kuzalisha Umeme.
· Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.4.2 cha Mkataba, Aggreko inawajibika
kulipa kwa TANESCO Dola ya Marekani 0.5 kwa Kw kwa siku kwa wiki 4 za
kwanza za ucheleweshaji, na baada ya hapo’ kama ucheleweshaji wa
uzalishaji umeme utaendelea, anawajibika kulipa Dola ya Kimarekani 1 kwa
Kw kwa siku.
· Hata hivyo, malipo hayo ya fidia (liquidated damages) yamewekewa
ukomo chini ya Kifungu cha 10.3 (a) na (c) ambapo hayatazidi Dola za
Kimarekani 350,000 na kwamba, malipo hayo kwa ujumla wake chini ya
Mkataba huo hayatazidi Dola za Kimarekani 500,000.
· Aidha, Kifungu cha 8.8 cha Mkataba wa Richmond kinachoiruhusu
TANESCO kuendesha Mitambo ya Richmond pale ambapo Kampuni hiyoi
itaitelekeza (abandon) Mitambo hiyo, kimeondolewa kwenye mkataba wa
AGGREKO.
(c) Nyongeza ya Mkataba
· Mkataba huo una Nyongeza (Addendum) au (Amendment No.2) ya Januari,
2007 ambayo imebadilisha formula ya kupata ‘capacity payments’, ambapo
muda uliopotezwa na TANESCO kutokana na matatizo ya upatikanaji wa gesi
na pia kutokana na TANESCO kutoomba kupewa umeme kutoka AGGREKO
umepigiwa hesabu kwa ajili ya AGGREKO kulipwa na TANESCO.
· Nyongeza hiyo pia imebadilisha bei ya Umeme unaotolewa na AGGREKO
ambapo, bei mpya sasa ni Dola za Kimarekani 0.0499 x 1000 kwa kila Mwh.
4.1.1 Mkataba Kati ya TANESCO na ALSTOM POWER RENTALS ENERGY LLC
(b) Tarehe ya Kusainiwa kwa Mkataba
Mkataba huo ulisainiwa tarehe 27 Oktoba, 2006
(c) Madhumuni ya Mkataba (Subject Matter)
Mkataba huo ni kwa ajili ya uzalishaji na usambazji wa umeme wa
dharura kutoka kwenye Kinu cha dizeli cha kuzalisha umeme (emergency
supply of power from a diesel – based generating plant in Mwanza with a
capacity of 40 Mw).
(c) Muundo (form) wa Mkataba
Kama ilivyo kwa Mikataba iliyotangulia, Mkataba huu upo katika muundo wa ‘Standard Power Off-take Agreement’
(d) Muda wa Mkataba
Muda wa Mkataba huo ni miezi kumi na mbili (12) kwa mujibu wa Kifungu cha 2.1 cha Mkataba.
(e) Uhalali Kisheria wa Kampuni ya Alstom Power Rentals Energy LLC
Kwa mujibu wa maelezo yaliyomo kwenye Mkataba hususan kwenye Kifungu
cha 5.1 (a) na (b), Kampuni ya Alstom Power Rentals Energy LLC
imesajiliwa chini ya Sheria za Florida, Marekani.
(f) Malipo ya Kodi
Kifungu cha 3.4 cha Mkataba kinatamka kwamba, TANESCO itatumia juhudi
za kibiashara kuhakikisha kwamba Serikali ya Tanzania inatoa msamaha
kwa Alstom wa kutolipa ‘import duties’ na kodi ya ongezeko la thamani
(VAT) kuhusiana na Mtambo au utekelezaji wa majukumu ya Alstom, chini ya
Mkataba huo.
Aidha, Kifungu hicho kinatamka pia kuwa, pale ambapo kodi hizo
zitadaiwa, Alstom itaiomba TANESCO ilipe kodi hiyo au kama italipwa na
Alstom, TANESCO itarejeshea Alstom malipo hayo ya kodi.
(g) Kutii Sheria za Mazingira
Kifungu cha 3.9 cha Mkataba huu kinamtaka Alstom kuhakikisha kwamba,
hatafanya kitendo chochote ambacho kitasababisha kuwepo kwa hali ya
mazingira ambayo inakiuka Sheria za Tanzania.
(h) Malipo ya Umeme
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.3 cha Mkataba, TANESCO inawajibika kulipa
malipo ya ‘capacity charge’ kwa kiasi cha Dola za Marekani 43.8 kwa Kw
kwa mwezi.
(i) Malipo ya Fidia kwa Ucheleweshaji wa Kuzalisha Umeme
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.4 na cha 10.1(a) cha Mkataba, Alstom
anawajibika kulipa kwa TANESCO kiasi cha Dola za Kimarekani 400,000 kama
kiwango cha mwisho cha malipo ya fidia (damages) kwa ucheleweshaji wa
kuzalisha umeme na kiasi cha Dola za Kimarekani 600,000 kama kiwango cha
mwisho cha malipo yote ya fidia (damages).
(j) Dhamana ya Malipo kwa Alstom
Kifungu cha 4.6 cha Mkataba kinaitaka TANESCO kufungua ‘Letter of
Credit’ ya kiasi cha Dola za Kimarekani 3,500,000 kwa kipindi chote cha
Mkataba, kama dhamana ya malipo kwa Alstom.
Aidha, Kifungu cha 4.7 cha Mkataba kinaitaka TANESCO kufungua
‘Standby Letter of Credit’ ya kiasi cha Dola za Kimarekani 14,000,000
kwa ajili ya malipo ya miezi minane (8) ya Mkataba.
(k) Mafuta (fuel)
Kifungu cha 6 cha Mkataba kinatamka kuwa, TANESCO itawajibika kulipia
mafuta ya dizeli yatakayotumika kuendeshea Mtambo wa Alstom wa
kuzalisha Umeme.
(l) Kutolipa Malip ‘Capacity Charges’ Wakati wa Majanga
Kwa mujibu wa Kifungu cha 13.1 cha Mkataba, malipo ya ‘Capacity
Charges’ yanayotakiwa kulipwa na TANESCO yatasitishwa kwa siku 30 iwapo
litatokea janga lolote ambalo litasababisha Alstom kutelekeza majukumu
yake ya kuzalisha na kusambaza umeme.
(m) Kuhamisha (assign) Majukumu
Kwa
mujibu wa Kifungu cha 15.12 cha Mkataba, Alstom au TANESCO inaweza
kuhamisha (assign) sehemu au majukumu yote yaliyomo kwenye Mkataba kwa
Kampuni Tanzu, baada ya kutoa taarifa kwa mhusika wa pili uuzaji
uhamishaji huo wa majukumu. Hata hivyo, mhusika yeyote anayehamisha
majukumu atabaki na wajibu wa kuhakikisha kuwa majukumu hayo
yanatekelezwa ipasavyo na yasipotekelezwa, atawajibika.
4.1.2 Mkataba Kati ya TANESCO na WARTSILA FINLAND OY
(a) Tarehe ya Kusainiwa kwa Mkataba
Mkataba huo ulisainiwa tarehe 20 Juni, 2006.
(b) Madhumuni ya Mkataba (Subject Matter)
Mkataba
huo ni kwa ajili ya uzalishaji na usambazaji wa umeme wa dharura kutoka
kwenye Kinu cha gesi cha kuzalisha umeme (Energy Purchase Contract for
Procurement of Emergency 100 Mw Gas-based Power Generation Plant at
Ubungo, Dar es Salaam.)
(c) Muundo (form) wa Mkataba
Tofauti
na Mikataba yote iliyotangulia kufanyiwa uchambuzi hapo juu, Mkataba huo
upo katika muundo uliowekwa na Kanuni ya Ununuzi wa Umma [The Public
Procurement (Goods, Works, Non-Consultant Services and Disposal of
Public Assets by Tender) Rgulations, G.N. No.97 of 15/4/2005]
zilizotungwa chini ya Kifungu cha 88 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.21
ya Mwaka 2004 [The Public Procurement Act, 2004 (No.21 of 2004)].
Kanuni ya
115(1) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2005, Taarifa ya Serikali
Namba 97 ya Mwaka 2005 inaelekeza kama ifuatavyo:-
“Kwa
kadri inavyowezekana, kila jitihada itafanywa kutumia miundo ya rasimu
za mikataba iliyotayarishwa na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma.” Tafsiri na
msisitizo ni wetu.
Ili kuondoa tatizo la tafsiri, Kanuni hiyo iliyoandikwa kwa lugha ya Kingereza inasomeka kama ifuatavyo:-
“Every effort shall be made to utilize as for as possible, the sample Standard Contract documents prepared by the Authority.”
(d) Muda wa Mkataba
Muda wa
Mkataba (contract period) ni miezi 21, kwa mujibu wa Kifungu cha G.C.C
1.1 (aa) na GCC 8.1[Tazama Uk.1 na 2 wa ‘Special Conditions of Contract]
(e) Uhalali kisheria wa Kampuni ya WARTSILA FINLAND OY
Kwa
mujibu wa maelezo yaliyomo kwenye Mkataba, Kampuni hiyo imesajiliwa
chini ya Sheria za Finland. Hatukuweza kufanya utafiti wa kina
kuthibitisha kuwa maelezo hayo ni sahihi, isipokuwa tumefanya hivyo kwa
Kampuni moja tu ya RICHMOND.
(f) Malipo (Contract Price)
Kwa
mujibu wa Kifungu cha 2.1 cha Mkataba, TANESCO anawajibika kulipa kiasi
cha Euro 57,550,000/= kama malipo ya huduma ya kupatiwa umeme wa
Megawatt 100 kutoka kwenye Kinu cha kuzalisha umeme cha WARTSILA.
(g) Utaratibu wa malipo
Kwa
mujibu wa Kifungu cha 2.2 cha Mkataba, TANESCO anawajibika kufanya
malipo ya huduma ya umeme kwa kufungua ‘Letter of Credit’ ya kiasi cha
Euro 51,795,000/= kwa jina la WARTSILA.
(h) Dhamana ya Utekelezaji (Performance Bond)
Chini ya
Kifungu cha 3.1 cha Mkataba, WARTSILA anawajibika kutoa dhamana ya
utekelezaji wa kazi (Performance security/bond) ya kiasi cha 10%ya
malipo anayostahili kulipwa, kabla ya kuanza kazi.
(i) Malipo ya Kodi
§ Kwa
mujibu wa Kifungu cha 14.4 (GCC), uk. wa 3 wa Special Conditions of
Contract, kodi zote ambazo WARTSILA anapaswa kulipa zitasamehewa (be
exempted) au zitalipwa na TANESCO.
§ Aidha,
chini ya Kifungu hicho pia, kodi na malipo yote yanyohusu mishahara ya
watumishi wa kigeni wa Kampuni ya WARTSILA zinapaswa kulipwa na TANESCO.
(j) Taratibu za Usuluhishi
Chini ya
Kifungu cha 6.2.3 taratibu zitakazotumika wakati wa Usuluhishi ni za
Mahakama ya Kimataifa ya usuluhishi ya London, chini ya Sheria za
Uingereza.
Tunadhani kifungu hiki si kwa manufaa na maslahi ya TANESCO.
(k) Malipo ya bonus
Chini ya Kifungu cha 26.3 cha Mkataba (Taz. Uk. wa 5 wa SCC malipo ya bonus hayaruhusiwi.
(l) Kipindi cha Matengenezo (Defect liability period)
§ Kwa
mujibu wa Kifungu cha 27.2 cha Mkataba (Uk. wa 5 wa SCC), kipindi cha
matengenezo ni miaka miwili (2) baada ya kukamilika kwa ufungaji wa
Mtambo.
§ Tunadhani kwamba, Kifungu hiki ni kwa manufaa na maslahi ya TANESCO.
4.1.3 Mkataba Kati ya TANESCO na SONGAS LIMITED
(a) Tarehe ya Kusainiwa kwa Mkataba
Mkataba huo umesainiwa tarehe 11 Oktoba, 2001.
(b) Madhumuni ya Mkataba (Subject Matter)
Mkataba
huo ni kwa ajili ya uzalishaji na usambazji wa nishati ya umeme kutokana
na gesi ya Songosongo (Power purchase relating to the Songosongo
gas-to-electricity)
(c) Muundo (form) wa Mkataba
Mkataba huo upo katika muundo wa ‘Standard Power Purchase Agreement’.
(d) Muda wa Mkataba
Kwa
mujibu wa Kifungu cha 4.1 cha Mkataba, muda wa Mkataba ni miaka ishirini
(20), na unaweza kuongezwa kwa makubaliano kati ya TANESCO na SONGAS.
(e) Uhalali Kisheria wa Kampuni ya SONGAS LIMITED
Kampuni
ya SONGAS LIMITED ni Kampuni ya kitanzania iliyosajiliwa chini ya Sheria
ya Makampuni, Sura 212, Toleo la 2002 [The Companies Ordience (Cap.212)
of the Laws of Tanzania, R.E, 2002] (Tazama Kifungu cha 5.1 cha
Mkataba)
(f) Malipo ya Kodi
Kwa
mujibu wa Kifungu cha 15.1 cha Mkataba, SONGAS LIMITED inatakiwa kulipa
kodi kulingana na masharti yaliyomo kwenye Mkataba wa Utekelezaji
(Implementation Agreement) ulioingiwa kati yake na Serikali ya Tanzania.
(g) Malipo ya Umeme
Kwa
mujibu wa Kifungu cha 2.1(a)(i) na (ii) cha Mkataba, kikisomwa pamoja na
Vifungu 9.2 na 9.5, TANESCO anawajibika kulipa malipo yafuatayo kwa
SONGAS:- ‘Capacity Charge’ – Dola za Kimarekani 6,638,600 ‘Energy
Charge’ – kwa kiasi kitakachotokana na ‘formula’ iliyowekwa na Kifungu
cha 5 cha Nyongeza F ya Mkataba.
(h) Usuluhishi
§ Kifungu
cha 3.10 cha Mkataba kinatamka kwamba, TANESCO na SONGAS wamekubaliana
kutotekeleza masharti na matakwa ya Kifungu cha 20(2) cha Sheria ya
Umeme, Sura 131, Toleo la 2002 [Electricity Act, (Cap.131) of the Laws
of Tanzania, R.E 2002], na badala yake kusuluhishwa migogoro baina yao
kwa kutumia utaratibu uliowekwa na Mkataba.
§ Kwa kuwa kinahusu makubaliano ambayo yanavunja sheria, Kifungu hicho hakina uhalali wowote wa kisheria.
(i) Kuvunjwa kwa TANESCO
Kwa
mujibu wa Kifungu cha 4.3(a) cha Mkataba, kikisomwa pamoja na Kifungu
cha 17.12, TANESCO haiwezi kuvunjwa kwa Sheria au kuhamisha majukumu
yake yaliyoainishwa kwenye Mkataba, isipokuwa tu kwa kuzingatia masharti
yaliyowekwa na Kifungu cha 8.7 cha Mkataba wa Utekelezaji
(Implementation Agreement).
(j) Uuzaji Umeme wa SONGAS
Kwa
mujibu wa Kifungu cha 4.1(b), iwapo TANESCO watakataa kuongeza muda wa
Mkataba baada ya muda wa awali wa miaka 20 kumalizika, SONGAS
wataruhusiwa kuingia Mkataba na mtu yoyote anayetaka kuuziwa umeme.
(k) Haki ya Kununua Mradi
Chini ya
Kifungu cha 4.8 cha Mkataba, TANESCO na T.P.D.C wamepewa haki ya kununua
Mradi huo wa SONGAS iwapo SONGAS atakiuka masharti ya Mkataba.
Mapendekezo Mengine
Pamoja na
mapendekezo ya hapo juu, tunashauri na kupendekeza pia kuwa, kuna
ulazima kwa Mikataba mikubwa ambayo inahusu maslahi na manufaa ya Taifa
kama vile Mkataba wa IPTL kuwasilishwa Bungeni, kwa utaratibu wa dhana
ya demokrasia ya uwajibikaji (accountability in a Parliamentary
democracy) kwa ajili ya ushauri wa Bunge.
Tunapendekeza
na kushauri vilevile kuwa, pale ambapo kuna ulazima wa kutumia rasimu
ya Mkataba ambayo ni tofauti na ile iliyotayarishwa na Mamlaka ya
Ununuzi wa Umma, mabadiliko muhimu yafanywe katika rasimu hiyo ili
masharti yaliyomo ambayo hayafai yaondolewe na yale ambayo ni kwa
manufaa ya Taifa letu yawekwe. Wanasheria watumike katika kuitekeleza
jambo hili.
Tunashauri
na kupendekeza vilevile kuwa, Mikataba yote ya umma ifanywe kwa
kuzingatia misingi ya kibiashara na si vinginevyo, na kwamba, Taasisi na
Mashirika yote ya Umma lazima yatekeleze na kufuata utaratibu, masharti
na matakwa yaliyowekwa na Sheria ya Ununuzi wa Umma, Namba 21 ya mwaka
2004, pamoja na Kanuni zilizotungwa chini ya Sheria hiyo.
Aidha,
tunapendekeza na kushauri kwamba utoaji Mikataba utumike kama njia au
chombo cha kutekeleza Sera za Taifa na malengo ya jamii, badala ya
kutumika kama chombo cha kuchota rasilimali za Taifa na kuongeza
umaskini wa wananchi wa nchi hii.
Aidha,
tunashuri pia kwamba, pale inapotokea ukiukwaji wa masharti ya Mkataba
unaofanywa na Mwekezaji basi hatua mwafaka zichukuliwe, ikiwa ni pamoja
na kudai malipo ya fidia iwapo kuna kifungu cha Mkataba kinachotoa haki
hiyo.
Kwa
kuzingatia kuwa Mikataba mibovu kati ya TANESCO na Makampuni mbalimbali
ambapo Makampuni hayo yanalipiwa kodi yote na TANESCO imekuwa ni chanzo
cha bei kubwa za umeme katika nchi yetu, na kwa kuzingatia kuwa Mikataba
hiyo inasababisha Sera muhimu za Taifa, kama vile, Sera ya Kupiga vita
Umaskini, Sera ya Huduma Bora kwa Jamii, Sera ya Taifa ya Nishati
inayolenga kusambaza nishati ya bei nafuu vijijini n.k. kutotekelezeka,
tunashauri kuwa Mikataba hiyo ipitiwe upya ili irekebishwe, kwa maslahi
na manufaa ya Taifa letu.
Mwisho,
kwa kuzingatia ukweli kwamba, Mikataba hiyo mibovu, kwa kiasi kikubwa
inadidimiza uchumi wa nchi yetu, tunapendekeza Serikali ichukuwe hatua
muafaka zinazofaa ili kuondoa hali hiyo ambayo inalipeleka Taifa letu
‘shimoni’[1].
Mheshimiwa Spika, hali
hiyo ya kuachwa kutekelezwa kwa maazimio ya Bunge la Tisa ya Mwaka
2008, hayahusu tu Richmond bali pia juu ya Kashfa ya Mgodi wa Kiwira
aliyomgusa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na baadhi ya mawaziri kama
ambavyo hotuba hii itaeleza kwa ufupi wakati wa kutoa maoni kuhusu sekta
ya madini. Serikali wakati inaendelea kuchukua hatua kuhusu kashfa hii
ni muhimu ikarejea maelezo ya ziada na vielelezo zaidi vilivyotolewa
wakati wa kusomwa kwa orodha ya mafisadi (List of Shame) Septemba 15
mwaka 2007 katika uwanja wa Mwembe Yanga.
Mheshimiwa Spika, Aidha,
matokeo ya Bunge kuzembea kuisimamia Serikali kukamilisha utekelezaji
wa maazimio ya Bunge ya mwaka 2008 yamesababisha udhaifu wa Serikali
katika kutekeleza maazimio ya Bunge ya mwaka 2011 kuhusu “Sakata la
Jairo” kama nilivyoeleza katika Hotuba hii lakini pia kuhusu uchunguzi
juu ya Sekta ndogo ya Gesi Asili na Mpango wa Dharura wa Umeme kama
nitakavyoeleza wakati nawasilisha maoni kuhusu sekta ya gesi ya nishati.
C. NISHATI
3.0 SEKTA NDOGO YA GESI ASILIA TANZANIA
Mheshimiwa Spika, sekta
ndogo ya gesi asilia ni sekta ambayo kutokana na ukubwa wa hazina
iliyokwishapatikana na inayokisiwa kuwepo itakuwa ni kubwa sana katika
shughuli za uchumi kwa nchi yetu. Lakini Sekta ya gesi asilia imegubikwa
na utata mwingi ambao kwa njia moja au nyingine unatokana na kutokuwepo
kwa sera na sheria mahususi ya gesi. Na hivyo kusababisha utendaji wake
kutokuwa na mdhibiti (regulator) wa kuhakikisha maslahi ya taifa,
mwekezaji na mlaji yanaangaliwa.
Mheshimiwa Spika, Utafutaji
na uzalishaji wa mafuta na gesi( Upstream); shughuli zote za utafutaji
wa mafuta na gesi nchini unatawaliwa na Sheria ya Utafutaji na
Uzalishaji Mafuta ya mwaka 1980 (The Exploration Act,1980). Shughuli ya
usafirishaji na uuzaji (down stream) hii hutawaliwa na sheria ya EWURA
sura 414 kwa kuwa kwa sasa sheria ya gesi nchini haipo. Hivyo basi,
makubaliano katika mkataba baina ya wadau hutakiwa kuwasilishwa EWURA
kwa mapitio tu, na baada ya kujiridhisha EWURA hupanga bei za gesi.
Mheshimiwa Spika, mkataba
wa ubia ndiyo mwongozo mkuu wa mahusiano yote yanayohusu uzalishaji na
ugawanaji wa mapato ya gesi baina ya TPDC na mbia yeyote. Lakini kwa
makusudi wabia na TPDC wamekuwa hawafuati matakwa yaliyomo kwenye PSA na
mfano mzuri ni Pan African Energy[2].
Mheshimiwa Spika, utakumbuka
moja ya mapendekezo ya kamati ndogo iliyoundwa na Bunge lako tukufu
toka kwenye iliyokuwa kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini ilipendekeza
na Bunge kukubali, kuwa nina nukuuu ‘’ipo haja ya kudurusu Sera ya
Nishati, kuandaa Muswada wa gesi asili wenye kutoa majibu ya maswali
magumu ya Watanzania wa leo na wa miaka 50 ijayo…
Majukumu
kati ya asasi moja na asasi nyingine yaainishwe bayana na kutenganishwa
kwa lengo la kuleta ufanisi na kuongeza tija. Aidha, mipango mkakati na
kabambe iandaliwe ili kuibua miradi ya miundombinu na mahitaji ya
rasilimali. Taifa likichelewa kuweka nyenzo hizi muhimu, likaruhusu
majadiliano na mikataba kuchukuwa nafasi, kipindi si kirefu yatashuhudia
manun’guniko kuwa nchi imeuzwa na mivutano kati ya wananchi na
wawekezaji na ya wananchi na Serikali yao itajitokeza kwa nguvu sana
jambo ambalo ni vyema likaepukwa mapema[3]’’
Mheshimiwa Spika, mapendekezo
haya yalitolewa Bungeni Novemba 17, 2011 na kupitishwa kuwa azimio la
bunge. Sasa ni mwaka mzima na miezi sita, hadi tunashuhudia maandamano
na malalamiko ya wazi toka maeneo ambapo gesi asili imegunduliwa.
Mheshimiwa Spika, Licha
ya ukweli kwamba gesi asili ilianza kutafutwa toka mwaka 1952 na
iligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini mwaka 1974 na baadae mwaka 1982,
wakati wote huo hakuwahi kuwa na sera mahususi ya gesi mpaka mwishoni
mwa mwaka 2012 zaidi ya miaka 30 baadae ndipo serikali imeanzisha
mchakato wa kutunga sera ya Taifa ya gesi asili.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imedhihirisha udhaifu mkubwa wa kisera na kiutendaji kwa kuzingatia
kuwa mikataba kadhaa ya uchimbaji na utafutaji wa gesi imeshatiwa saini
kati ya serikali na wawekezaji bila kuwa na sera wala sheria inayotoa
mwongozo juu ya namna Taifa linavyopaswa kuthibiti rasilimali hii
adhimu. Uwepo wa sera na sheria ya gesi asilia ungetoa mwelekeo juu ya
namna gani serikali ingeshirikiana na wakazi wa maeneo yaliyogunduliwa
gesi, pamoja na wadau wengine katika kutafuta,kugundua na kuvuna,
kusafirisha, kununua na kutumia gesi asilia.
Mheshimiwa Spika, Serikali
bila uwepo wa sera na sheria hiyo, tayari imefunga mkataba na kampuni
ya Statoil, Ophir, British Gas, Artumas, Shell, Texaco, Agip, PetroBras
na kadhalika. Ni wazi kwamba mikataba husika imeingiwa bila muongozo
wowote wa kisera wala kisheria mahususi. Aidha, licha ya makosa hayo na
wakati mchakato wa sera uko karibu kukamilika Serikali imefunga mkataba
mwingine kwa Kampuni nyingine kufanya utafutaji kwenye Ziwa Tanganyika.
Jambo hili linazidisha wasiwasi kama kweli Serikali ina nia ya dhati ya
kuhakikisha sekta hii ya gesi inanufaisha Taifa na watu wake.
Kitendo cha
Serikali kuendelea kuingia mikataba na makampuni ya kutafuta gesi asilia
bila ya kukamilisha kwanza sera na sheria ni sawa na kuweka mkokoteni
mbele ya punda.
Mheshimiwa Spika; Waziri
Mkuu akiwa ndiye msimamizi na mdhibiti wa shughuli za kila siku za
Serikali ndani na nje ya Bunge, anapaswa kutoa maelezo kuhusu hali
inayoendelea hivi sasa katika sekta ndogo (sub sector) muhimu kwa nchi
yetu ya gesi asili kuhusu mazungumzo yanayoendelea na makampuni
mbalimbali ya kimataifa na mikataba inayozidi kusainiwa huku kukiwa na
ombwe la kisera na udhaifu wa kiuongozi katika sekta hizo nyeti hali
ambayo itakuwa na athari za muda mrefu sana kwa taifa.
Mheshimiwa Spika, Ucheleweshwaji
wa sera na sheria katika sekta ya gesi asilia unachangiwa na wizara
yenyewe kwa watendaji wake kuwa na udhaifu katika kuweka mifumo ya
kuifanya sekta hiyo kuwa endelevu na yenye manufaa kwa nchi. Hili
linathibitishwa na ukweli kwamba TPDC imeshindwa kusimamia kwa ukamilifu
sekta hii ya gesi asilia kwani hata mikataba iliyopo inayotaka kampuni
inayofanya utafiti baada ya muda Fulani kuchimba kisima kipya; lakini
hadi sasa kwa mfano tangu Kampuni ya Songas kuchukua visima
vilivyochimbwa na TPDC haijawahi kuchimba visima vipya kwa kadiri ya
mahitaji.
Mheshimiwa Spika, mfano
mwingine ni kampuni ya Pan African Energy Tanzania (PAT) kukosa sifa za
uaminifu ambapo Kamati ilishauri Mkataba wa Pan African Energy Tanzania
(PAT) usitishwe. Aidha, utekelezaji wa kuvunja mkataba huu ulipaswa
kwenda sambamba na kuhakikisha kuwa taratibu za kisheria na za kimkataba
zinazingatiwa, uwepo wa usalama wa visima na mitambo na uwepo wa
uhakika wa huduma ya upatikanaji wa gesi nchini. Hili lilikuwa ni
pendekezo namba 4 la kamati iliyochunguza uendeshwaji wa sekta ndogo ya
gesi asilia hapa nchini na baadae kuwa azimio la Bunge. Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni
kwanini mpaka sasa Serikali haijatekeleza azimio hilo? Aidha, ni lini
Bunge litachukua hatua ili kuepusha uzembe kwa upande wa chombo hiki
muhimu? Aidha ni lini mabilioni yote ya mapunjo yenye mwelekeo wa
ufisadi yatarejeshwa?
Mheshimiwa Spika, kuhusu
gesi asilia, tarehe 15 Julai, 2011 Kambi Rasmi ya Upinzani ilieleza
kuwa, nchi yetu imejaliwa utajiri wa gesi asilia katikati ya lindi la
umaskini wa wananchi na kwamba Taifa letu lina fursa ya kuwa nchi
kiongozi katika gesi Afrika na kushindana Kimataifa ikiwa tutaweka
mstari wa mbele uzalendo,upeo, umakini na uadilifu katika sekta ya
nishati kuepusha laana ya rasilimali.
Mheshimiwa Spika, hata
hivyo, mapitio ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2011/2012, yalionesha
Serikali kutochukua hatua thabiti kushughulikia ufisadi na udhaifu wa
kiuongozi katika sekta ndogo ya gesi asili.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitaka hatua za haraka kuchukuliwa katika
mwaka wa fedha 2012/2013 ili kuepusha rasilimali kuwa chanzo cha
migogoro na kuhatarisha pia usalama wa nchi lakini kwa sababu ya udhaifu
wa serikali hii kutosikiliza ushauri kitendo hicho kilisababisha vurugu
na uharibifu wa mali kwa mikoa ya Lindi na Mtwara.
Mheshimiwa Spika, ushahidi
wa hili unapatikana katika ushauri ambao serikali ilipewa kwa nyakati
mbili tofauti lakini ikashindwa kuzuia vurugu za Lindi na Mtwara. Tarehe
27 Julai 2012 nikiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu
mapitio na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya nishati na
madini nilishauri “Mapitio ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha
2011/2012, yanaonekana bado serikali haichukui hatua thabiti
kushughulikia ufisadi na udhaifu wa kiuongozi katika sekta ndogo ya gesi
asili hivyo hatua za haraka zisipochukuliwa katika mwaka 2012/2013 na
kuendelea rasilimali inaweza kuwa chanzo cha migogoro na kuhatarisha pia
usalama wa nchi”. Lakini pamoja na angalizo hili serikali
haikuchukua hatua yeyote na matokeo yake sote tunayafahamu, kambi rasmi
ya upinzani inahoji ni nani mpaka sasa amewajibika kutokana na hali
hiyo?
Mheshimiwa Spika, wakati
wa mchakato wa kutoa maoni juu ya rasimu ya gesi , pamoja na kwamba
mchakato huo haukufanyikakiwa ufanisi katika maeneo mengine muhimu kama
Chuo Kikuu cha Dar es salaam(UDSM) ambacho kina kozi mbalimbali za
masuala haya na ambako tungepata ushauri mzuri na wa kitaalamu kutokana
na wadau hao kutokujua na hivyo kutokujitokeza .
Mheshimiwa Spika,
miongoni mwa wananchi waliojitokeza kutoa maoni ni pamoja na wananchi
waliofunga safari kutoka Mtwara hadi Dar es salaam kuja kutoa maoni yao
juu ya rasimu ya gesi. Miongoni mwa mapendekezo aliyotoa mwananchi huyo
(jina linahifadhiwa) mbele ya viongozi wa serikali alishauri serikali
kujua matatizo yanayotokea katika sekta ya madini ili tuhusianishe na
gesi asilia.
Mheshimiwa Spika, Pamoja
mwananchi huyo kuwakilisha mikoa ambayo ndiko hasa nishati hiyo
inakopatikana, mwananchi huyo alipendekeza kutengwa kwa asilimia kumi
(10%) ya mapato yatokanayo na gesi kwa ajili ya kuboresha maeneo
rasilimali hiyo inapopatikana. Akapendekeza kijengwe Chuo Kikuu Mtwara
kitakachofundisha watanzania elimu ya gesi na pia vijengwe viwanda
vitatu kwa faida ya wana mtwara. Mapendekezo ambayo pia yamewahi
kutolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA kwa mwaka
2011 na 2012, katika hali kama hii ya kushindwa kutimiza wajibu na
kusababisha migogoro, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ikiri
kuwa imeshindwa kuiongoza sekta hii.
Mheshimiwa Spika, Kamati
ya kudumu ya bunge ya nishati na madini ilitoa mapendekezo ya
kukamilishwa kwa sera na sheria ya gesi kwa haraka na umakini mkubwa.
Kamati pia ilishauri serikali kuonyesha katika sera na sheria hiyo ya
gesi asilia jinsi ambavyo mapato yanayotokana na gesi asilia yatakavyo
simamiwa, mapendekezo hayo ya kamati yalizingatia wingi wa upatikanaji
wa nishati hii kwa sasa katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, katika
hali ya kushangaza serikali imeendesha mchakato mzima wa kutengeneza
rasimu ya gesi asilia bila kuwa na ushiriki mkubwa wa wananchi kinyume
na mapendekezo ya kamati ya kudumu ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, hakukuwa
na uhamasishaji wa kutosha kwa wananchi katika kutoa maoni juu ya
rasimu ya kwanza ya gesi iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini na
ndio maana mahudhurio katika sehemu ambako mijadala iliendeshwa yalikuwa
madogo sana. Kwa mfano katika ukumbi uliopo Makumbusho ya Mwalimu
Nyerere waliohudhuria siku ya kwanza hawakufika hata 25 na siku ya pili
hawakuzidi watu 30. Pia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM),
wanafunzi na wadau wa gesi kutoka taasisi hiyo muhimu ya elimu ya juu
hawakujitokeza kwa sababu ya uhamasishaji hafifu na hivyo kupelekea
kuahirishwa kwa zoezi hilo katika suala la msingi linalohusu uchumi wa
watanzania. Lakini pia suala hili kwa wakati huo lilitakiwa liwe ni
mjadala wa kitaifa ndani ya vyuo vikuu vingi nchini na jamii kwa ujumla
ikihusisha pia mikoa yote ambako kuna uvunaji au utafutaji wa gesi
asilia ili kupanua dhana ya kuwashirikisha wananchi katika maswala
yanayohusu rasilimali za Taifa kinyume na uhalisia wenyewe.
Mheshimiwa Spika, Kufuatia
kasoro zilizoanza kubainishwa na wabunge na wadau mbalimbali katika
toleo la tatu la rasimu ya gesi; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kutoa maelezo ni kwanini haikuzingatia baadhi ya maoni muhimu
ya wadau yaliyotolewa mara baada ya kutolewa kwa rasimu ya kwanza ya
Sera hiyo. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA
inataka mchakato wa kupitia rasimu ya tatu ya sera hiyo upanue wigo wa
ushirikishwaji wa wananchi katika mikoa yote ambayo utafutaji wa gesi
asilia umeanza au unatarajiwa kuanza pamoja na mikoa yote itakayofikiwa
na miradi ya uendelezaji wa gesi asilia.
Ikumbukwe
kwamba udhaifu wa Serikali katika kuwezesha ushirikishwaji wa wananchi
katika mipango na miradi ya maendeleo na matumizi mabaya ya muda mrefu
ya rasilimali za nchi ni kati ya sababu zilizochangia migogoro katika
maeneo ambayo uendelezaji wa miradi ya gesi asilia umeanza hususani
katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuwashirikisha wananchi na kutoa
taarifa za kutosha na kwa wakati juu ya suala hili la gesi asilia na
rasilimali nyingine za taifa ili kuondoa mkanganyiko unaojitokeza kwa
wananchi juu ya mchakato mzima wa uwekezaji kwenye rasilimali za Taifa,
rasimu ya sera haikidhi haja irudishwe upya kwa wananchi ikiwemo kwenye
mikoa yote yenye utafutaji unaoendelea na maeneo ya matumizi
yanayotarajiwa.
Mheshimiwa spika, kwa
mujibu wa michango mbalimbali iliyotolewa na wabunge wakati wa mjadala
wa kuchangia bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini 2012/2013 waheshimiwa
wabunge pia walitaka kujua kama taifa mipango ambayo serikali imeweka
kufuatia kugundulika kwa kiasi kikubwa cha gesi, kama rasilimali watu
kwa maana ya wataalamu waliobobea, idadi ya wataalamu tunaowaandaa
kwenda sambamba na uhalisia wa uhitaji wa wataalamu wenyewe katika sekta
ya gesi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia kuitaka serikali
kufanya maandalizi ya kutosha ya kuwekeza katika suala la rasilimali
watu ili kuondoa matatizo yanayoweza kujitokeza hivi karibuni kutokana
na uhaba wa wataalamu katika fani hiyo.
3.1 Ugawaji wa Vitalu vipya vya utafutaji wa gesi na mafuta.
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka
2012/13, baada ya kupokea ushauri wa Kamati kuhusu kusitisha ugawaji wa
vitalu vya utafutaji gesi, Serikali iliahidi kwa kusema kuwa “zoezi
la kugawa vitalu vipya kwa ajili ya utafutaji wa mafuta umesitishwa
mpaka hapo sera ya Gesi Asilia na sheria ya Gesi Asilia nchini
itakapokamilika na kuanza kutumika”
Mheshimiwa Spika, Jambo
la kushangaza ni kwamba wakati sera ya Gesi Asilia ipo kwenye rasimu na
ndio kwanza wabunge tumeletewa kutoa maoni, Serikali tayari imetangaza
kwa mujibu wa vyombo vya habari na tamko la TPDC tarehe 18.5.2013 kuanza
mzunguko mwingine wa leseni za utafutaji Mafuta na Gesi kwenye Bahari
kuu na Ziwa Tanganyika Kaskazini. Kutoa leseni kwenye kitalu ya
utafutaji ni hatua ya kuelekea kutoa mkataba wa uvunaji.
Zabuni hii
mpya ya leseni za vitalu vya utafutaji imetolewa wakati kuna maamuzi ya
Bunge kuzuia ugawaji huu mpya mpaka sera ya Gesi Asilia na Sheria ya
Gesi vikamilike. Haraka hii ya serikali kugawa vitalu bila sera wala
Sheria inatoka wapi.
Mheshimiwa Spika, uharaka
huu unaifanya Kambi Rasmi ya Upinzani iwe na mawazo kwamba Wizara
iliidanganya Kamati ya Kudumu ya Bunge, je ilifanya hivyo kwa maslahi ya
nani? Tunamtaka Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge sababu za kuidanganya
kamati inayofanyakazi kwa niaba ya Bunge.
Wizara ya
Nishati na Madini imekuwa ikitoa ufafanuzi potofu kwamba tangazo la sasa
halina athari kwa kuwa maamuzi ya utoaji wa leseni yatafanyika mwaka
2014 baada ya kuwa na sera na sheria. Hata hivyo, ufafanuzi huu wa
Wizara hauzingatii ukweli kuwa, hata zabuni ya maombi ikiwemo vigezo,
utaratibu na masuala mengine ilipaswa kutolewa kwa kuzingatia misingi
mipya inayopaswa kuwekwa kupitia mchakato wa katiba mpya na maandalizi
ya Sera na Sheria ya Gesi Asili.
Katika muktadha huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kutengua tangazo hilo mpaka baada ya kukamilika kwa mchakato
wa katiba mpya na maandalizi ya sera na sheria mpya sio tu kwenye sekta
ndogo ya gesi asilia bali katika sekta nzima ya nishati ikiwemo juu ya
masuala yanayohusu mafuta.
Vinginevyo,
watanzania wataamini kwamba hatua hiyo imefuatia msukumo uliotokea baada
ya ziara ya Rais wa China nchini Tanzania; hasa kwa kuzingatia namna
ambavyo, pamoja na vitalu vilivyotangazwa kwenye zabuni ili kutolewa kwa
ushindani, vipo vitalu ambavyo vimebakishwa mikononi kwa TPDC ambavyo
mazingira ya mchakato wa utolewaji wake yanaacha maswali.
Mheshimiwa spika, Katika
hatua ya sasa Wizara ya Nishati na Madini ijielekeze katika kusimamia
mikataba ambayo tayari nchi yetu imeingia mpaka sasa kwa maslahi ya nchi
na kupitia upya mikataba mibovu. Aidha, katika kutekeleza azma hiyo,
Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Wizara ya
Nishati na Madini kutoa kwa Bunge taarifa ya uchunguzi wa mikataba hiyo
iliyokamilika toka mwaka 2012 lakini imeendelea kufanywa kuwa siri mpaka
hivi sasa.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
pia serikali kuweka wazi kwa watanzania wote mikataba hiyo na mingine
ambayo serikali imeisaini inayohusu rasilimali za Taifa hili. Aidha
inatoa mwito kwa wananchi kuhakikisha kwamba masuala ya uwazi katika
mikataba yanapewa kipaumbele katika katiba mpya, sera na sheria.
Mheshimiwa spika,
Kitendo ambacho serikali ilikuwa inakifanya kupitia Shirika la
Maendeleo ya Petrol (TPDC) cha kugawa vitalu vipya nane vya gesi wakati
bado sera na sheria ya gesi haijakamilika ni ushahidi tosha kuwa kuna
watu wachache katika serikali wameanza kulichukulia suala hili la gesi
asilia kwa manufaa ya watu binafsi.
Mheshimiwa spika, Wizara
ya Nishati na Madini katika bajeti yake ya miaka iliyopita imekuwa
ikitenga fedha nyingi kwa ajili ya mishahara na posho kitengo cha sheria
cha Wizara. Jambo hili la kugawa vitalu vipya nane vya gesi wakati sera
na sheria kuhusu gesi havijakamilika linadhihirisha siyo tu udhaifu
katika idara hii ya ushauri wa kisheria bali pia mazingira yanayoashiria
mianya ya matumizi mabaya ya raslimali za umma katika zoezi hili. Kambi
Rasimi ya Upinzani Bungeni inalichukulia jambo hili kuwa ni udhaifu
ambao hauwezi kuvumilika hata kidogo na tunaitaka wizara ieleze sababu
hasa za kuendesha zoezi hili kinyume na maoni na mapendekezo ya kamati
ya kudumu ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, Mwalimu
Nyerere aliwahi kusema kwamba chama lege lege huzaa serikali legelege;
udhaifu huu wa wizara unaweza kutafsiriwa kwamba unachangiwa na ushiriki
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupewa na kukubali hisa toka kwa moja ya
makampuni yanayojihusisha na utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini,
kampuni ya Ophir energy. Kwa mujibu wa taarifa rasmi za Bunge za
tarehe 08.11.2012 ni kuwa wakati CCM ikipewa hisa wapo pia baadhi ya
watanzania ambao waligawiwa sehemu ya hisa hizo kwa ajili ya CCM
Aidha,Katibu
Mkuu wa CCM Abdurahaman Kinana anatajwa na vyanzo mbalimbali kwamba
amewahaki kuwa Mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya Artumas
ambayo iliingia mkataba na Serikali wa kuzalisha Mega Watt- 300 za umeme
Mtwara eneo la Mnazi Bay. Mkataba huo ulikuwa wa misingi ya
mabadilishano ya gesi kwa nishati ya umeme (gas for power). Kwamba
Artumas ingechimba na kuuza gesi asilia na kuilipa serikali kwa pamoja
na mambo mengine kuizalishia umeme wa 300MW. Baadae mwaka 2010 Artumas
baada ya kufaidika vya kutosha kutokana na uvunaji na uuzaji iliacha
kuendeleza mradi huo kwa kisingizio cha madai ya mdororo wa Uchumi mwaka
2009 na kuuza hisa zake kwa kampuni ya Wentworth ya Ufaransa.
Mheshimiwa Spika, Ushiriki
huu wa viongozi waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi na chama hicho kwenye
shughuli ambazo zinaitia hasara serikali unazua mazingira ya kwamba CCM
inasababisha unyonywaji wa Taifa na wananchi, na hivyo ni dhahiri si
mwafaka kuendelea kuongoza nchi hii. CCM na baadhi ya viongozi wake
wamekuwa wakifaidika kutokana na ombwe la kisera na kisheria katika
sekta hii na nyingine muhimu. Katika hali kama hii, maneno ya Mwalimu
Nyerere yanapaswa kuongezewa nukuu mpya kwamba “chama cha mafisadi huzaa
serikali ya mafisadi”.
3.2 Haki ya Wananchi kumiliki rasilimali asilia
Mheshimiwa
Spika, Wakati Katiba yetu inatambua haki ya kumiliki mali na hifadhi ya
mali hiyo na inakataza unyang'anyi wa mali kwa lengo la kuitaifisha au
kwa malengo mengine, haki za wananchi kumiliki rasilimali zao za asilia
kama ardhi, madini, mafuta, gesi asilia, misitu na wanyama pori, uvuvi,
n.k., zimekuwa haziheshimiwi na mamlaka za kiserikali kwa hoja kwamba
rasilimali asilia hizo ni mali ya umma.
Mheshimiwa Spika, Dhana
ya mali ya umma ni dhana yenye asili yake katika ukoloni. Ni dola ya
kikoloni ya Kijerumani ndio ilikuwa ya kwanza kutangaza kwamba mali
asilia zote katika koloni lao la Tanganyika ni mali ya Mfalme wa
Kijerumani. Baada ya Wajerumani kushindwa Vita ya Kwanza ya Dunia na
kunyang'anywa makoloni yao ya Afrika, dola ya kikoloni ya Waingereza
iliyokabidhiwa Tanganyika, walitangaza kwamba rasilimali asilia zote ni
mali ya umma chini ya mamlaka na udhibiti wa Gavana wa kikoloni. Dhana
hii ilipokelewa bila mabadiliko yoyote ya msingi baada ya uhuru na ndio
imekuwa msingi mkuu wa sera za rasilimali asilia za nchi yetu kwa muda
wote wa uhuru wetu. Jambo hili ni hatari kwani mali ya umma maana yake
ni mali isiyokuwa na mwenyewe, na ndio maana wenye nguvu wanatumia
mwanya huo kupora wasio na nguvu.
Mheshimiwa Spika, Kama
ilivyokuwa wakati wa ukoloni, utekelezaji kivitendo wa dhana ya mali ya
umma wakati wote wa uhuru umekuwa ni kuwanyang'anya wananchi rasilimali
asilia zilizoko kwenye maeneo yao na kuzimilikisha mamlaka za Serikali
(wakati wa miaka ya uchumi-dola), au kuzimilikisha kwa wawekezaji wa
kigeni katika zama hizi za soko holela kwa kisingizio cha huria.
Mheshimiwa Spika, Matokeo
ya mfumo huu ni kwamba milki na mamlaka ya maamuzi juu ya matumizi ya
rasilimali asilia yameondolewa mikononi mwa wananchi na kuhamishiwa
kwenye mikono ya warasimu wa Serikali. Sio hio tu, wananchi wamejikuta
wakiondolewa kwa nguvu kutoka kwenye maeneo yao ili kuwapisha wamiliki
wapya wa rasilimali hizo, yaani wawekezaji wa kigeni au wa ndani. Kwa
sababu hiyo, uchumi wa wananchi umeanguka, umaskini umeongezeka na
matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu yameongezeka.
Mheshimiwa Spika, Dhana
ya mali ya umma katika umilikaji wa rasilimali asilia imehakikisha
kwamba maeneo yenye rasilimali asilia hayapati faida na manufaa
yanayotokana na uwepo wa rasilimali hizo katika maeneo yao. Mrahaba,
kodi na tozo nyingine zinazotokana na matumizi au mapato ya rasilimali
hizo yanapelekwa kwenye mamlaka za Serikali Kuu. Kwa upande mwingine,
madhara yanayotokana na matumizi ya rasilimali hizo Kama vile uchafuzi
wa mazingira na mabadiliko ya matumizi ya rasilimali husika,
yanawaangukia wananchi wa maeneo ziliko rasilimali hizo.
Mheshimiwa Spika, naomba
nieleze mtazamo na msimamo wa Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na
CHADEMA kuhusiana na umiliki pamoja na uendelezaji wa Raslimali zetu
asilia,ni kwamba:
i. Wananchi
hawatanyang'anywa rasilimali zao asilia na mamlaka za Serikali kwa ajili
ya matumizi na watu au taasisi nyingine bila kwanza Wananchi
watakaoathiriwa na unyang'anyi au matumizi hayo kutoa ridhaa yao baada
ya kupatiwa taarifa zote na kamili zinazohusu matumizi yanayotarajiwa ya
rasilimali hizo na athari za matumizi hayo kwa mazingira, kiuchumi na
kijamii (the right of prior informed consent). Wananchi Kama wamiliki wa
msingi wa rasilimali asilia, watakuw
ii.Wananchi
wana haki ya kulipwa mrahaba kwa ajili ya matumizi ya watu au taasisi
nyingine ya rasilimali asilia za Wananchi, wakati mamlaka za Serikali za
mitaa, Majimbo na Serikali Kuu zitakuwa na haki ya kutoza kodi mapato
yatakayotokana na matumizi ya rasilimali hizo.
3.4 BOMBA LA GESI TOKA MTWARA HADI DAR ES SALAAM
Mheshimiwa Spika, Pamoja
na ushauri wa kambi rasmi ya upinzani bungeni wakati wa kuwasilishwa
kwa bajeti ya wizara 2012/2013 kuitaka Serikali kuwasilisha Bungeni na
kuweka wazi kwa umma mkataba wa mradi husika ili Bunge liweze kuishauri
na kuisimamia Serikali kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ibara ya 63; kuanzia katika hatua za awali kuhakikisha kwamba
maslahi ya Taifa yanalindwa katika hatua zote na pia wananchi
wananufaika kutokana na fursa za uwekezaji huo mkubwa lakini bado
serikali haikutilia maanani ushauri huu. Matokeo yake siyo tu
kusababisha mkanganyiko kwa wakazi wa Lindi na Mtwara bali pia kuacha
maswali mengi kwa watanzania juu ya nini hasa nia ya serikali kwa
kuficha mikataba inayohusu rasilimali hizi za Taifa kwa wananchi wake na
hata kwa chombo cha kuwakilisha wananchi kama Bunge.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali isiendelee
na ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar Es Salaam hadi
kwanza; Mosi, iweke wazi kwa Bunge mikataba yote inayohusu uendelezaji
wa gesi asilia ikiwemo ya ujenzi wa Bomba hilo. Pili, ikutane na
wananchi kuwashirikisha na kuhakikisha manufaa kwa taifa na kwao.
Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa
na CHADEMA imeshangazwa na hatua ya Waziri wa Nishati na Madini Prof.
Sospeter Muhongo tangu kuibuka kwa mgogoro huo amejikita zaidi katika
kutoa kauli kupitia vyombo vya habari badala ya kwenda kukutana na
wananchi hatua kwa hatua na kuwezesha ufumbuzi kupatikana. Aidha,
manufaa kwa wananchi wa Lindi na Mtwara ambayo taarifa yake imechapwa
kwenye vyombo vya habari yaletwe kama taarifa rasmi bungeni ikiwa na
ulinganisho baina ya shughuli za kijamii zilizofanywa na makampuni tajwa
pamoja na miradi iliyotekelezwa na Serikali kufuatia mapato katika
sekta hii tangu mwaka 2004 na thamani halisi ya mapato ambayo makampuni
tajwa na Serikali wamepata.
Mheshimiwa Spika, pamoja
na ujenzi wa mitambo miwili ya kusafishia gesi asili Mnazi Bay na Songo
Songo kama sehemu ya mradi huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inarudia
kuitaka Serikali kueleza ni miradi ipi iliyotengewa fedha inayoambatana
na mradi huo ambayo imepangwa kuwanufaisha wananchi wa Mikoa ya Lindi na
Mtwara na imetengewa kiasi gani cha fedha katika mwaka huu wa fedha
2013/2014 ili kuharakisha msukumo wa maendeleo kwa mikoa hiyo ya Kusini
ambayo imesahaulika kwa siku nyingi na hivyo siyo tu kuharakisha
maendeleo kwa mikoa ya Kusini bali pia kuhakikisha usalama wa mradi huo
mkubwa kwa manufaa mapana ya jamii ya kitanzania.
Mheshimiwa Spika, kuanza
kwa ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi asilia pamoja na bomba la
kusafirisha gesi hiyo hadi Dar es salaam na usambazaji wa umeme katika
vijiji 52 vinavyopitiwa na bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Lindi
haikidhi wala kujibu kilio cha wananchi wa Mtwara na Lindi cha kutaka
ugunduzi wa gesi asilia katika mikoa hiyo uweze kunufaisha mikoa hiyo
kimaendeleo kutokana na kuwa nyuma kimaendeleo miaka 52 baada ya uhuru
wa Taifa hili.
Mheshimiwa Spika, wakati
waziri akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2012/2013 ya Wizara ya
Nishati na Madini tarehe 27-07-2012 aliliambia bunge hili kuwa,
kusainiwa kwa mkataba wa mkopo kati ya Tanzania na China kwa ajili ya
kusafirisha Gesi asili na ujenzi wa Bomba la kusafirishia gesi toka
Mnazi BAY hadi Dar es saalam na kusainiwa kwa mikataba mingine mitano
(5) na mkataba wa uzalishaji na ugawanyaji wa mapato ya mafuta na Gesi
asili kuwa ni miongoni mwa jitihada ambazo serikali imechukua katika
jitihada za kukabiliana na tatizo sugu la umeme hapa nchini, hata hivyo
kama ulivyo utaratibu wa serikali mikataba hii inaendelea kuwa siri.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali na Wizara ya
Nishati na Madini kuainisha miradi hiyo na kuitengea fedha ili wananchi
wa mikoa ya kusini waweze kunufaika na rasilimali hiyo kwani kwa muda
mrefu sana wamekuwa wavumilivu wakisubiria utekelezwaji wa ahadi za
kuwapelekea maendeleo kwa miaka mingi bila kuyaona wala kuyapata.
Kambi
rasmi ya Upinzani , inaitaka serikali isitishe ujenzi wa Bomba hilo
kwanza iende ikajadiliane na wananchi wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani
na wakubaliane jinsi ya kuendelea na mradi huo ndipo ujenzi wa bomba
hilo uweze kuendelea , kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeamua kumaliza
tatizo la msingi kwani serikali ikiendelea bila kujali madai ya wananchi
hawa na kuamua kutumia mabavu kujenga hakuna atakayekuwa mshindi kati
ya serikali na wananchi hawa. Ni rai yetu kuwa serikali itaweza kuiona
busara hii ili gesi iweze kuwanufaisha watanzania wote yaani wa Mtwara
na wale wa maeneo mengine.
4.0 MAFUTA
4.1 MFUMO WA UAGIZIAJI MAFUTA KWA UFANISI
Mheshimiwa Spika, Marekebisho
ya Sheria ya petrol (Petroleum Supply Act 2008) kifungu cha 33(1)
kinatamka kuwa uagiziaji wa bidhaa za petroli lazima ufanyike kwa
ufanisi na kwa kigezo cha unafuu mkubwa wa gharama na kufafanuliwa zaidi
na kifungu cha 33(2) ambacho kinaeleza ufanisi wenyewe ikiwa ni pamoja
na :-
a) Uagiziaji wa pamoja wa kushirikiana (Joint Procurement)
b) Uagiziaji wa ushindani (Compitative Procurement)
c) Uagiziaji wa shehena kubwa (Bulk Procurement)
d) Kwa
kutumia fursa ya viwango vya kiuchumi (Taking advantage of economic
Scale). Pia Sheria imetoa fursa ya kubadili kwenye aina nyingine za
uagiziaji utakao onekana unatija zaidi.
Mheshimiwa Spika,
sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA) sura
ya 414 pamoja na Petroleum Conservation Act (cap 392) zimeongeza
majukumu ya kudhibiti na kuratibu uagiziaji mafuta kutoka nje. Pia mfumo
wa ununuzi na usafirishaji wa mafuta kwa pamoja umependekeza kuwa na
mratibu (Petroleum Importation Co-ordinator - PIC) wa kukusanya taarifa
za mahitaji na kutayarisha zabuni.
Mheshimiwa Spika, Kampuni
hii , iliratibiwa na EWURA lakini ilisajiliwa kwa masharti ya sheria ya
makampuni na hivyo kuifanya kuwa kampuni binafsi inayomilikiwa na Umoja
wa Makampuni yanayoagiza na kusafirisha mafuta nchini (TAOMAC).
Uendeshwaji wa Kampuni hiyo upo chini ya bodi na Mwenyekiti wa bodi
uteuliwa na mkutano wa wanahisa.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani imekuwa ikieleza jinsi gani Wizara inavyoshindwa
kusimamia mambo ya msingi kwa mujibu wa sheria na kanuni za uwepo wake.
Mfano dhahiri ni kitendo cha Mhe Waziri kuteua Mwenyekiti wa Bodi ya PIC
kwa kutumia Nafasi yake na mbaya zaidi kumteua Ndugu James Andindile
ambaye ni Kamishna msaidizi-Wizara ya Nishati ni dhahiri kuwa Wizara
itashindwa kufanyakazi yake ya usimamizi.
Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka
Mhe.Waziri alieleze Bunge ni kwa vipi ana uwezo wa kuingilia utendaji
wa Kampuni Binafsi kwa kuteua Mwenyekiti wa Bodi? Ni mfumo gani umewekwa
wa kuhakikisha Wizara inafanya usimamizi?
Mheshimiwa Spika, ili kuepusha watanzania kubebeshwa mzigo wa gharama kubwa ya mafuta katika Kikao
cha Arobaini na Mbili – Tarehe 9 Agosti, 2011,kulitolewa hoja ya
dharura kuhusu uhaba wa mafuta baada ya michango kadhaa ya waheshimiwa
wabunge na hatimae Serikali ilitoa kauli yake. Baada ya mjadala huo
Bunge lilifanya uamuzi. Hata hivyo hakukuwa na ufuatiliaji wa karibu
baada ya maazimio. Hali hii ni moja katika kasoro kubwa ambayo
kuanzia mwaka huu Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA
ilitaka irekebishwe. Katika Kamati zote zilizopo za sekta hakuna Kamati
ambayo inafuatilia maazimio yote ya Bunge ili Serikali kusimamiwa kwa
zile ahadi au maazimio tuliyoyapitisha hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, Kamati
ya Nishati na Madini ya Bunge la Tisa iliweza kupendekeza kwa Serikali
mara nyingi sana kuhusu suala la TPDC kupitia kampuni tanzu ya COPEC
kuanzisha biashara ya mafuta. Kamati ya Nishati ya Bunge la Tisa
ikazungumzia pia Bulk Procurement piaStrategic Reserve. Masuala yote haya yamehojiwa na Kambi Rasmi ya Upinzani mwaka 2011 na 2012
Mheshimiwa Spika, baada ya kushindwa kuchukua hatua hatimaye Serikali ikaleta ahadi nyingine, nanukuu “leo
hii tarehe 9 Agosti, 2011, Serikali kupitia EWURA imeipa leseni Kampuni
ya COPEC ambayo ni Kampuni Tanzu ya Serikali kupitia TPDC kuanza
kufanya biashara ya mafuta mara moja.
Naomba
kurudia. Leo hii tarehe 9 Agosti, 2011 Serikali kupitia EWURA imeipa
leseni COPEC ambayo ni Kampuni Tanzu ya Serikali kupitia TPDC kuanza
kufanya biashara ya mafuta mara moja”.
Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka 2011/2012 wa fedha Wizara ya Nishati na Madini, COPEC ilikuwa
imepangiwa shilingi milioni 20 tu kwa ajili ya kampuni hiyo kuanza
kufanya biashara. Ukweli ni kwamba kampuni hiyo haikuwa na miundombinu
yoyote ya kuiwezesha kufanyabiashara kama Serikali ilivyoagiza.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ilieleze Bunge toka ilipopatiwa leseni ya biashara hadi sasa COPEC imeongeza tija ipi katika biashara ya mafuta kwa watanzania?
Mheshimiwa
Spika, Waziri aliahidi mbele ya bunge kuanza kwa mpango wa utekelezaji
uingizaji wa mafuta wa pamoja (Bulk procurement) mwezi January 2012.
Wizara ieleze kuanza kwa utaratibu huu umeokoa kiasi gani cha pesa
kilichokuwa kinapotea kabla ya kuanza kutumika kwa utaratibu huu mpya na
sababu za mpango huo kushindwa kushusha bei ya mafuta kinyume na ahadi
za Serikali.
5.0 UMEME
Mheshimiwa
Spika, Bado kunaendelea kuwepo na utata kuhusu mgawo wa umeme katika
maeneo mengine ya nchi huku serikali ikikanusha kuhusu mgawo wakati
watanzania wakiendelea kupewa nishati hiyo kwa mgawo kwa nyakati
mbalimbali. Aidha Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini akiwasilisha
makadirio ya Bajeti ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka 2012/1013
aliliambia bunge lako tukufu kuwa “hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni 2012 lengo la kuondoa mgao wa umeme lilifikiwa kwa asilimia 100”.
Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inalitaka shirika la umeme Tanzania
(TANESCO) na Wizara ya Nishati na Madini kuwaambia ukweli watanzania
kuhusu mgawo wa umeme kwa kuzingatia hali mbaya ya shirika hilo kifedha
ambayo imeripotiwa na vyombo vya habari hivi karibuni kwa sehemu
ikichangiwa na wingi wa mikataba mibovu ya miaka mingi ya ukodishaji wa
mitambo ya umeme na hali ya sasa ya ununuzi wa ziada wa mafuta ya
kluendeshea mitambo ya dharura.
Mheshimiwa Spika, kitendo
cha kutowaambia wananchi ukweli kuhusu mgawo wa umeme wakati wananchi
wakipata nishati hiyo kwa mgawo huku wakipewa sababu ambazo zinaonekana
hazina ukweli kinazidi siyo tu kushusha heshima na hadhi ya serikali kwa
wananchi wake bali pia kinadhihirisha udhaifu uliopo katika mfumo wa
kiutendaji wa serikali pamoja na mashirika yake likiwemo shirika la
umeme Tanzania (TANESCO).
Mhesimiwa Spika, mradi
wa kuboresha mifumo ya umeme katika jiji la Dar es salaam ambayo
imekuwa ndio kisingizio kikubwa cha mgawo wa umeme hali ambayo inazua
maswali mengi kwa watanzania. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kazi hiyo
ilianza katika bajeti ya 2011/2012 na mpaka sasa tatizo la kukatika kwa
umeme bado linaendelea kitendo ambacho kinatafsiriwa kuwa kazi hiyo
bado haijakamilika miaka miwili tangu kuanza kwa kazi hiyo iliyogharimu
shilingi billion 120. Watanzania wanapenda kujua ni lini hasa kazi hii
itakamilika ili kupunguza kero ya mgawo wa umeme kwa Dar es salaam na
Tanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, kitendo
cha serikali kutoa ahadi hewa zisizo tekelezeka na kutochukua hatua
stahiki dhidi ya watumishi wa serikali wanaoihujumu TANESCO imekuwa ndio
chanzo cha kuzorotesha ufanisi wa shirika hili na kufanya liendelee
kuendeshwa kwa hasara. Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni imekuwa ikishauri
mara kadhaa juu ya kufikishwa mahakamani kwa watumishi wote wa serikali
na mafisadi wote wanaohujumu uchumi wakiwemo wale wa TANESCO, Kiwira,
Meremeta, Richmond n.k lakini inaonekana kuwa ni utaratibu wa serikali
hii au udhaifu wa serikali katika kushughulikia watuhumiwa hao wa
uhujumu uchumi.
Mheshimiwa Spika, kutokana
na udhaifu wa Serikali ya CCM katika kuchukua hatua, kama ilivyokuwa
katika kusamehe baadhi ya wezi wa EPA na kuzimwa kwa sakata la Richmond
lililosababisha hasara ya mabilioni ya fedha. Hali hiyo imechangia
kuzaliwa kwa sakata jipya la DOWANS linalopelekea TANESCO kutakiwa
kuilipa kampuni hii ya DOWANS ambayo ilirithi mkataba wa kampuni hewa ya
Richmond zaidi ya shilingi 97,000,000,000 kunazidi kulipatia taifa
mzigo mkubwa. Hii ni kwa sababu kodi za wananchi na malipo ya wateja
zinazotumika katika kashfa zote hizo na kuwasababishia wavuja jasho wa
taifa hili kuwa na ugumu wa maisha pamoja na kwamba waliahidiwa maisha
bora kwa kila mtanzania.
Mheshimiwa spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali kutoa taarifa kwa Bunge
lako tukufu ikieleza sababu zinazowafanya wasimfikishe Mahakamani
aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco Eng. William Mhando, siyo tu kwa
matumizi mabaya ya ofisi yaliyosababisha TANESCO hasara ya zaidi ya
bilioni 6,000,000,000 kwa kila mwezi baada ya kukatisha mkataba wa
ununuzi wa mafuta kwa ajili ya IPTL kutoka kwa BP waliokuwa wakiuza kwa
bei nafuu na kuanza kununua kwa kampuni za Oryx na Camel oil ambayo
gharama yake ilikuwa juu bali pia kwa kukiuka miiko ya maadili ya
viongozi wa umma?
Mheshimiwa spika, katika
mjadala wa bajeti ya mwaka 2012/2013 kulijitokeza pia wasiwasi wa namna
TANESCO inavyojiendesha. Bunge liliiomba Wizara ya Nishati na Madini
ichunguze kwa kina suala la mapato ya TANESCO na jinsi yanavyotumika.
Ilionekana TANESCO kwa mwezi inapata takribani Billion 60 au Billion 70.
Mishahara ya wafanyakazi wa TANESCO peke yake ni takribani Billion kumi
na moja. TANESCO inatumia fedha nyingi sana kununua umeme kutoka
makampuni yanayotumia umeme hususani wa dharura na kukodisha mitambo ya
kufua umeme wa dharura. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
serikali kupitia wizara ya Nishati na Madini itoe majibu juu ya
uchunguzi unaohusu uendeshaji wa shirika hili.
Mheshimiwa spika, Mnamo
tarehe 18 Julai, 2011 serikali kupitia Waziri Mkuu Mizingo Pinda
iliahidi kupunguza matumizi yasiyo ya msingi ya serikali ilikupata fedha
ambazo zilitegemewa kuliongezea Shirika la Umeme la TANESCO ili liweze
kutekeleza mpango wa umeme wa dharura na kuliongezea shirika hilo uwezo
wa kujiendesha. Hata hivyo ahadi hiyo ilichukua sura mpya baada ya
serikali kushindwa kutekeleza tamko lake la kwanza na kutoa ahadi
nyingine tena ya kupata fedha kwa kukopa ambayo mpaka sasa utekelezaji
wake bado unasuasua.
Mheshimiwa spika, Mnamo
13 Agosti, 2011 serikali ilitoa ahadi ya kuisaidia TANESCO kuweza
kukopa bilioni 408 kutoka kwenye mabenki, lakini mpaka sasa ni jumla ya
dola za marekani milioni 65 ambazo ni sawa na billion 104 tu ndizo
TANESCO imeweza kukopa tena kwa kuchelewa. Hii ni kwa mujibu wa taarifa
ya serikali kama ilivyoainishwa na Wizara katika ripoti yake ya
utekelezaji kwa Kamati ya Nishati na Madini TANESCO ilipokea fedha hiyo
mwezi Januari mwaka huu (2013). Ahadi hizi zisizotekelezeka zimekuwa
kikwazo kikubwa cha maendeleo ya sekta hii muhimu ya umeme ndiyo maana
mpaka sasa ni sehemu ndogo sana ya Watanzania wameunganishwa na huduma
hii muhimu ya umeme.
Mheshimiwa spika, katika
mwaka wa fedha 2012/13 kamati ya kudumu ya bunge ya nishati na madini
ilitoa mapendekezo kazaa kwa lengo la kuboresha sekta ya umeme,
mapendekezo hayo ya kamati pamoja na yale yaliyotolewa na Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni mengi hayajafanyiwa kazi na serikali na hata yale
ambayo yamefanyiwa kazi utekelezaji wake ni kwa kiwango kidogo. Aidha
mapendekezo ambayo hayajafanyiwa kazi ni kama ifuatavyo:
(i)
kuanzishwa kwa mfuko wa kuendeleza nishati ya umeme nchini kwa lengo la
kutumia mfuko huo kama mtaji (Equity) ili fedha zake zitumike katika
kuboresha huduma ya upatikanaji wa umeme nchini na pia kukopa kutoka
vyombo vingine vya fedha.
(ii). Kamati
pia ilishauri wizara kutenga fedha za kutosha katika uzalishaji,
usambazaji na usafirishaji wa umeme kwani vinategemeana. Cha kushangaza
katika bajeti ya serikali ya mwaka 2013/2014 haijatengwa fedha yoyote
ile kwa ajili ya kuboresha njia za usafirishaji umeme mbali ya kuwepo
kwa asilimia 22.5 ya upotevu wa umeme unaozalishwa inayosababishwa na
miundombinu chakavu ya umeme.
(iii).
Kamati baada ya kuona ugumu na gharama ambayo TANESCO itapata katika
kusafirisha mafuta toka bandarini kwenda Nyakato Mwanza ilishauri tangu
kwenye bajeti ya mwaka 2011/2012 na kurudia ushauri huo katika bajeti
2012/2013 kwamba mradi huu uhamishiwe sehemu ambayo yatapatikana mafuta
ya uhakika na mitambo hiyo itumie mafuta ya dizeli ili kuweza kunusuru
gharama ambazo nchi itaingia baadaye na kupelekea ufanisi wa mitambo
hiyo kuwa mdogo.
(iv) Pia
Kamati iliitaka serikali kuiwezesha TANESCO kumiliki mitambo yake badala
ya kutegemea mitambo ya kukodi ambayo inaligharimu shirika hilo fedha
nyingi linazolipa kwa makampuni yanayomiliki kama capacity charge.
Mheshimiwa Spika, Katika
hoja hii Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaamini kwamba kamati
ilifanya uchunguzi wa swala hili kabla ya kutoa ushauri kwa serikali.
Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa mchanganuo
wa gharama ambazo TANESCO itazipata katika kusafirisha mafuta mazito ya
mitambo ya kufua umeme inayo jengwa Nyakato Mwanza.
Mheshimiwa spika, katika
hoja hii serikali imejaribu kueleza jitihada yake ya kujenga mitambo
mbalimbali ya kufua umeme wa gesi ikiwemo ile ya Kinyerezi, Ubungo na
Mwanza.
Mheshimiwa spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kueleza bayana namna
mitambo hii inayojengwa itakavyokuwa mbadala wa mitambo ya kukodi kuliko
kuendelea kijisifia inajenga mitambo wakati kuna baadhi ya mitambo
imekamilika lakini bado mitambo ya kukodi haipungui na TANESCO inazidi
kulipa capacity charge.
Mheshimiwa spika, umeme
vijijini, zaidi ya bilioni50 ambazo REA imetengewa, kiasi hiki ni
kikubwa, hivyo kitendo cha Wizara kutenga fedha kwa ajili ya kupeleka
umeme vijijini bila kutaja idadi na majina ya vijiji vitakavyonufaika na
miradi ya fedha hizo linatoa mwanya wa kutumia vibaya fedha za
serikali. Hali hii imejitokeza pia katika Taarifa za Serikali za mwaka
wa fedha 2012/2013 ambapo hakuna vijiji vya kutosha vilivyooneshwa
kunufaika na hivyo kuleta mkanganyiko mkubwa katika utekelezaji wa
miradi hii vijijini.
Mheshimiwa Spika, pia
tunamtaka Waziri aelezee juu ya mradi uliotengewa fedha na Serikali
katika bajeti mwaka wa fedha 2011/2012 mradi uliohusu taa za mwanga bora
vijijini ambao ulitakiwa kutekelezwa Bukombe, Kahama, Biharamulo na
Chato. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe majibu kwa nini
mradi huo haukutekelezwa wakati fedha za mradi huo zilitengwa? Pamoja na
majibu hayo Kambi Rasmi Bungeni pia inaitaka Wizara kueleza juu ya
mradi mwingine ambao ulifahamika kwa jina la “TANZANIA AFFORDABLE RURAL
ELECTRIFICATION PLAN” ambao ulitakiwa utekelezwe Bukombe na Kibondo,
hasa juu ya hatua iliyofikiwa hadi sasa.
Mheshimiwa Spika, TANESCO
imefika hapo ilipo sasa kutokana na kutokuwa makini katika uingiaji wa
mikataba mbalimbali na makampuni yanayoiuzia umeme. Kamati ya wataalam
wa sheria ya Bunge wakati wa sakata la RICHMOND ilishauri yafuatayo
kuhusiana na mikataba:“kuna ulazima kwa Mikataba mikubwa ambayo
inahusu maslahi na manufaa ya Taifa kama vile Mkataba wa IPTL
kuwasilishwa Bungeni, kwa utaratibu wa dhana ya demokrasia ya
uwajibikaji (accountability in a Parliamentary democracy) kwa ajili ya
ushauri wa Bunge kuwasilishwa Bungeni….. Aidha, Kwa kuzingatia kuwa
Mikataba mibovu kati ya TANESCO na Makampuni mbalimbali ambapo Makampuni
hayo yanalipiwa kodi yote na TANESCO imekuwa ni chanzo cha bei kubwa za
umeme katika nchi yetu, na kwa kuzingatia kuwa Mikataba hiyo
inasababisha Sera muhimu za Taifa, kama vile, Sera ya Kupiga vita
Umaskini, Sera ya Huduma Bora kwa Jamii, Sera ya Taifa ya Nishati
inayolenga kusambaza nishati ya bei nafuu vijijini n.k. kutotekelezeka,
tunashauri kuwa Mikataba hiyo ipitiwe upya ili irekebishwe, kwa maslahi
na manufaa ya Taifa letu”.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inamtaka Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge katika
ufanyaji kazi wake ni mikataba mingapi ya uzalishaji wa umeme na kuiuzia
TANESCO, Madini au Gesi imefungwa bila ya kuzingatia ushauri au
mapendekezo yaliyokwishatolewa Bungeni? Kama imefanyika je jukumu la
Bunge kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 63 ina maana
gani?
Mheshimiwa Spika, matumizi
mabaya ya raslimali za umma hayako katika mikataba ya kukodi mitambo ya
umeme tu, bali katika ununuzi wa huduma za kisheria. Hivyo, narudia
kutoa mwito kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali aeleze ni kiasi cha fedha
kilichotumika kwenye kuendesha kesi za Dowans na IPTL mpaka sasa na
hatua zilizochukuliwa dhidi ya mawakili wa TANESCO na makampuni binafsi
yanayotuhumiwa kusababisha mzigo mkubwa wa gharama za kesi ambazo
serikali inashindwa kwa nyakati mbalimbali.
Mheshimiwa Spika,
Izingatiwe kuwa kwa mwaka wa fedha 2011/2012 pekee jumla ya shilingi
bilioni 10 zimetumika kwa ajili ya gharama za kuendesha kesi hizo kwa
kuilipa kampuni ya Rex Attorneys na Makampuni mengine ambayo kwa nyakati
mbalimbali yamekuwa yakiiwakilisha serikali na TANESCO na kushindwa
katika mahakama za kitaifa na kimataifa.
Mheshimiwa
Spika, kufuatia mfululizo wa TANESCO kushindwa mahakamani huku mabilioni
ya walipa kodi na wateja wake yakitumika, Kambi Rasmi ya Upinzani
inayoongozwa na CHADEMA inapendekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu
za Serikali (NAO) na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA)
wachunguze tuhuma za ufisadi na ubadhirifu kwa Shirika la Umeme
(TANESCO) kwenye matumizi ya mabilioni katika idara ya sheria na ununuzi
wa huduma za kisheria kutoka makampuni binafsi unaofanywa na TANESCO.
Ukaguzi na
uchunguzi huo ufanywe kuhusu matumizi na ufanisi wa huduma za kisheria
ambazo TANESCO imekuwa ikizipata kutoka kwenye makampuni binafsi katika
kesi kubwa za kimataifa ikiwemo ya Dowans na IPTL kwa kurejea pia maoni
niliyoyawasilisha bungeni tarehe 27 Julai 2012.
Mheshimiwa Spika, katika
hotuba ya Kambi Rasmi bungeni mwaka jana ilitaka Serikali kutoa maelezo
ya kina kuhusu matumizi ya kifungu cha 1005 cha Kitengo cha Sheria
ambacho kina kasma ya 229900 ambayo kwa mwaka wa fedha 2012/2013
kimetengewa kiasi cha Shilingi Bilioni 4 kama gharama za utetezi wa
Serikali katika kesi ya IPTL ikiwemo kwa ajili ya kuilipa kampuni ya
Mkono & Co. Advocates.
Aidha, Kambi
Rasmi ya Upinzani iliitaka Serikali kueleza jumla ya fedha zilizotumiwa
na Wizara kati ya mwaka 1995 mpaka 2011 kwa ajili ya kulipa makampuni
binafsi ya uwakili kwenye kesi kubwa za kitaifa na za kimataifa pamoja
na kutaja orodha ya makampuni hayo.
Mheshimiwa Spika, pia
Serikali ilitakiwa ieleze mkakati wa kudhibiti ongezeko la gharama za
kisheria ambazo ni mzigo mkubwa kwa mashirika ya umma na wananchi walipa
kodi kwa kuwa yamekuwepo mazingira ya kesi kuendelezwa kwa muda mrefu
na kugeuzwa kuwa vitega uchumi vya watu wachache. Nilitaja Mifano ya
kesi zilizodumu kwa muda mrefu ni ya IPTL ambayo Serikali inawakilishwa
na Mkono and Co. Advocates na ile ya Dowans ambayo Serikali imekuwa
ikiwakilishwa kwa nyakati mbalimbali na Rex Attorneys.
Mheshimiwa Spika, Waziri
wa Nishati na Madini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wanapaswa kulieza
Bunge sababu za kuacha kutoa majibu kuhusu suala hilo mpaka hivi sasa.
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua hatua ambazo Serikali imechukua
juu ya matumizi hayo.
Mheshimiwa Spika, mwaka
2011 Benki ya Standard Hong-Kong ambayo ni mdeni mkuu katika sakata la
IPTL ilifungua kesi ya madai katika mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi
(ICSID case Na. ARB/10/20) inayodai kiasi cha dola za Kimarekani milioni
225, pamoja na riba katika kuendesha kesi hiyo. Kampuni ya uwakili ya
Mkono (inayomilikiwa na Nimrod Mkono Mbunge wa CCM) ilipewa zabuni ya
kuitetea Serikali katika shauri hilo, na kwa kujiamini iliishauri
Serikali kuwa kesi hiyo tutashinda pamoja na wanasheria wengine kuwa na
maoni kinzani kuhusu suala hilo. Kampuni ya Mkono imekuwa ikiishauri
Serikali isifanye usuluhishi nje ya mahakama ya ICSID wakati wadai
kupitia kwa Mfilisi wa Mali na Madeni za IPTL (RITA) wanakubali
kusuluhishwa nje ya mahakama. Je, mpaka lini Serikali itaendelea kuingia
gharama hizo na ni kiasi gani Serikali imelipa kwa kampuni hiyo na
zingine mpaka hivi sasa?
5.1 MPANGO WA UMEME WA DHARURA
Mheshimiwa spika, itakumbukwa
kuwa Bunge lako tukufu lilipitisha mpango wa umeme katika mkutano wake
wa nne. Serikali ililiambia Bunge hili usafirishaji wa gesi kutoka
Songosongo hadi, Somanga hadi Dar es salaam ungeongezwa ndani ya miezi
kumi na mbili ili majenereta yaliyokuwa yamenunuliwa kutumika katika
mfumo wa gesi yafanye kazi ndani ya miezi kumi na mbili. Aidha
ilikusudiwa pia kuwa mpango huo ulilenga kushusha gharama za uzalishaji
wa umeme hapa nchini. Ikiwa sasa ni mwaka mmoja na zaidi umepita fedha
zinazidi kutengwa kwa ajili ya kununulia mafuta mazito ya kuendeshea
majenerata, kwa sehemu kubwa ikiwa ni kwa ajili ya mitambo ya kufua
umeme.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa kauli kuhusu sababu za
ucheleweshaji katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na
kushindwa kubadilisha mfumo wa majenereta kutumia gesi badala ya mafuta,
na kama kweli dharura iliyokuwepo bado ipo au imekwisha?
Mheshimiwa Spika, miongoni
mwa miradi ya dharura iliyotakiwa kuwa imekamilika ni pamoja na mradi
wa Jacobsen awamu ya pili ambao ulitakiwa kutekelezwa kuanzia mwezi
Januari hadi disemba 2012 ambao ungezalisha mega-watt 150 na kuendeshwa
na fedha za mkopo. Tunapenda kupata ufafanuzi kuhusu miradi hii ya umeme
wa dharura miradi mingapi imekamilika, kiasi gani cha pesa kimetumika
na kama taifa tunadaiwa kiasi gani cha fedha ambazo hadi sasa zimekopwa
kwa ajili ya miradi ya umeme kwa vile ni miongoni mwa maeneo ambayo nchi
hii imekuwa ikiingia gharama kubwa lakini ikishindwa kumaliza tatizo
hili na kuchangia katika deni la Taifa ambalo sasa linafika trilioni 22.
Aidha Mheshimiwa Spika, moja
ya mambo ambayo serikali iliahidi kuyafanyia kazi katika mpango wa
umeme wa dharura ni kununua mitambo yake, napenda kunukuu maneno ya
mheshimiwa waziri mkuu “Mheshimiwa spika ushauri mlioutoa ni wa msingi sana, moja mumesema serikali nunueni mitambo, ”Kambi
Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali kuliambia bunge hadi sasa
tangia kupitishwa kwa mpango wa umeme wa dharura ni mitambo mingapi ya
kuzalisha umeme ambayo inenunuliwa na tayari imeshaanza kuzalisha umeme.
Pia serikali iliambie bunge lako tukufu ina mpango gani kuhusu mitambo
ambayo tumekuwa tunakodi kwa maana ya mitambo ya Symbion miaka miwili,
na mitambo ya Aggreko ambayo yote tumekuwa tunalipa capacity charge, je
serikali imeandaa njia gani mbadala zaidi ya ambayo tumekuwa tukitumia?
Mheshimiwa
Spika katika mpango wa umeme wa dharura, mashirika ya mifuko ya jamii
kama NSSF nayo yaliruhusiwa kuwekeza katika sekta hii ya umeme, Kambi
Rasmi ya Upinzani inataka kupata ufafanuzi kuhusu mipango inayoendelea
juu ya nia hiyo ya mifuko ya jamii kuwekeza katika sekta ya umeme hapa
nchini.
5.2 SYMBION POWER AFRICA LLC, TANESCO NA KUANZISHA KAMPUNI MPYA YA UMEME KUSINI MWA TANZANIA (SECO).
Mheshimiwa
Spika, kutokana na andiko la kinadharia ‘conceptual proposal’la kujenga
mtambo wa kufua umeme katika mji wa Mtwara na usambazaji wake
lililoandikwa na kuwasilishwa Wizara ya Nishati na Madini ,TANESCO na
TPDC mnamo tarehe 07 Septemba 2012 na baada ya andiko hilo kupitiwa kwa
kina na TANESCO kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, mnamo
tarehe 12 Februari 2013 Symbion Power Africa LLC waliandaa
/waliwasilisha MOU baina yao na Tanesco ili iweze kusainiwa kwa ajili ya
kuanzisha kampuni ya kuzalisha umeme chini ya kinachoitwa ‘Special Purpose Company’ (SPC) ,Kampuni hiyo itajulikana kama “Southern Electric Company” (SECO) ambayo
inaanzishwa chini ya utaratibu wa PPP .Kwa mujibu wa MOU ni kuwa
Kampuni hii itakuwa ni kwa ajili ya kujenga ,kumiliki na kuendesha
mitambo inayotumia gesi kuzalisha umeme 600 MW katika miji ya Mtwara na
Dar Es Salaam.
Aidha ,kampuni hiyo ‘mpya’ ya SECO itajenga
,kumiliki na kuendesha mtandao wa usafirishaji na usambazaji wa umeme
kutoka kusini mwa Tanzania kwenda kwenye Gridi ya Taifa , Kaskazini mwa
Msumbiji na Malawi ( ….AND to build,own and operate transimission and
distribution networks that will link power plants in the south to the
Tanzania grid, northern Mozambique and Malawi (“the project”))
Mheshimiwa Spika, MOU hii iliingiwa baada ya Symbion kufanya mazungumzo na Shirika la umeme la Msumbiji ‘Electricite de Mozambique’ (EDM) kwa ajili ya kuwauzia umeme eneo la kaskazini mwa Msumbiji katika maeneo ya Pemba na Nacala, hii ni baada ya EDM kuonyesha kuwa watakuwa tayari kununua umeme kutoka Symbion Tanzania.
Aidha kwa
mujibu wa MOU hiyo ni kuwa tayari Symbion wameshasaini makubaliano na
Wizara ya Nishati ya Malawi kwa ajili ya kuanzisha uchunguzi kuhusiana
na mradi huo wa umeme kutoka nje , kipengele E cha MOU kinasomeka hivi,
nanukuu “Symbion has signed an agreement with the Ministry of Energy
in Malawi that provides for the investigation of a cross border project”
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa MOU kipengele cha 2.1 ni kuwa Symbion ndio watakuwa na jukumu
la kufanya upembuzi yakinifu kwa gharama zao wenyewe na kuwasilishwa
TIC kupitia kampuni ya ‘Special Purpose Company’ (SPC) kwa ajili ya kupatiwa hati ya PPP. Aidha, kampuni ya Special Purpose Company (SPC) itapewa hadhi ya kuwa ‘mwekezaji wa kimkakati’ ‘strategic Investor’ .
Aidha , kwa
mujibu wa kipengele cha 2.2 cha MOU ni kuwa umbembuzi yakinifu huo
utahusisha pia kuhusiana na mtaji unaohitajika kuwekezwa na SPC kwa
ajili ya mtambo wa kuzalisha 300MW kwa kutumia gesi pamoja na mtambo wa
kuzalisha 300MW Kinyerezi DSM kwa kutumia gesi.
Mheshimiwa Spika, kipengele
cha 2.4 cha MOU kinasema kuwa upembuzi yakinifu huo utahusisha pia
uwezekano wa kuhamisha mara moja baadhi ya mitambo ya kuzalisha umeme
kutoka mtambo wa kuzalisha umeme wa Symbion Ubungo na kupelekwa
Mtwara,lengo likiwa ni kuongeza ufanisi kwa muda mfupi huko Mtwara.
Kwa mujibu
wa kifungu cha 2.5 ni kuwa upembuzi yakinifu huo pia utahusisha utoaji
wa mafunzo ya kina kuhusiana na uendeshaji wa mitambo ya kisasa ya
uzalishaji,usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini Marekani kwa ajili
ya utawala wa baadae wa SPC .
Mheshimiwa
Spika, kambi rasmi ya upinzani inasikitishwa sana na tabia ya Serikali
hii ya CCM kutokana na tabia yake ya kuendelea kupuuza maazimio ya Bunge
hili ,kwani itakumbukwa kuwa Moja ya maazimio ya Bunge kuhusiana na
Richmond ilikuwa ni kuhusisha Kamati za Bunge katika kuingia mikataba na
makampuni ya kuzalisha umeme , sasa hapa sio kuzalisha tu bali ni
kuanzisha kampuni nyingine .
Aidha ,
tunataka kujua ni kwanini serikali hii ya CCM imeamua kusaini MOU ya
aina hii bila kuishirikisha kamati ya Bunge au Bunge , tena huu ni
mkataba wa kwenda kuuza umeme nje ya nchi wakati sisi tuna shida kubwa
ya umeme.
Je? hii haiwezi kwenda kuwa Richmond nyingine?
5.3 MIRADI MIKUBWA YA UMEME NCHINI 2013/2014
5.3.1 Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Mheshimiwa Spika, wakala
huyu alianzishwa kwa sheria Na 8 ya mwaka 2005 na alianza kazi rasmi
oktoba mwaka 2007, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya
Nishati ya mwaka 2003. Lengo likiwa ni kuwapatia wananchi waishio
vijijini nishati bora. Pamoja na umuhimu wa wakala huyu bado serikali
haijaonyesha kwa vitendo kuwa ina nia ya kusaidia wakala huyu ili aweze
kutimiza majukumu yake kikamilifu na hasa linapokuja suala la kuupatia
fedha kama zinavyoombwa na zinavyopitishwa na Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, Takwimu
zinaonyesha kuwa serikali imekuwa haitimizi wajibu wake wa kuipatia REA
fedha kama zinavyotengwa na kuidhinishwa na Bunge hili , kwa mfano
mwaka 2008/2009 zilipitishwa shilingi bilioni 20.00 ila zilitolewa shilingi bilioni 12.06 sawa na asilimia 60. Mwaka 2009/2010 zilipitishwa shilingi bilioni 39.55, zilizotolewa ni bilioni 22.14 sawa na asilimia 56. Mwaka 2010/2011 zilipitishwa bilioni 58.883, zilizotolewa zilikuwa bilioni 14.652sawa na asilimia 25. Mwaka 2011/2012 zilipitishwa bilioni 71.044,zilitolewa bilioni 56.748 sawa na asilimia 80 na mwaka 2012 /2013 zilipitishwa bilioni 53.158, zilitolewa bilioni 6.757 sawa na asilimia 13.
Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka huu wa fedha 2013/2014 wakala unahitaji kiasi cha shilingi
bilioni 366.9 kwa ajili ya kutekeleza miradi sita ya nishati vijijini
ambayo ni pamoja na awamu ya pili ya kusambaza umeme vijijini bilioni 200, mradi wa kupunguza gharama za miundombinu na usambazaji wa umeme vijijini bilioni 10, kupeleka umeme katika makao makuu ya wilaya mpya 13 bilioni 70, mradi wa kusambaza umeme kwenye maeneo yaliyopitiwa na njia kuu bilioni 75, mradi wa Global Village Energy Partinership bilioni 10.4 na mradi wa kuhamasisha na kuongeza matumizi ya nishati jadidifu bilioni 1.5.
Kambi rasmi
ya Upinzani, inaitaka serikali kutenga fedha kama zilivyoombwa na wakala
yaani bilioni 366.9 kwa mwaka huu wa fedha na sio kutenga kiasi cha
shilingi bilioni 91 za ndani na bilioni 62 za nje, kama Kifungu 3001,
kasma 3113 zinavyoonyesha, kwani wakala huyu asipopewa fedha kulingana
na mipango ilivyo atashindwa kufikia lengo la kusambaza umeme kwa
asilimia 30 Vijijini
Aidha, Kambi
rasmi ya Upinzani, inataka kujua fedha zilizotengwa kwa ajili ya REA
2012/2013 asilimia 87 zimeenda wapi ? Mbona hazikupelekewa REA kama
Bunge lilivyokuwa limeamua?
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA, haikubaliani na pendekezo la
Waziri aliloliwasilisha mbele ya kamati ya Bunge (randama uk 22) la
kuongeza tozo ya shilingi 100 kwenye kila lita moja ya mafuta ya petrol
kwa ajili ya nishati Vijijini kwani huku ni kumwongezea mwananchi mzigo
wa gharama za maisha, badala yake tunaendelea kusisitiza kuwa fedha
zilizoongezwa kwenye kila lita moja ya mafuta ya taa mwaka 2011/2012 kwa
hoja kwamba ni kuzuia uchakachuaji shilingi bilioni 600 kwa mwaka
zipelekwe zote REA kwani watumiaji wakuu wa mafuta ya taa wapo vijijini
na nusu zipelekwe TANESCO. Aidha makampuni ya madini yalipe kodi na tozo
za mafuta wanayosafirisha na wanayotumia.
5.3.2 Thermal Power Operation Bilioni 273.207
Mheshimiwa Spika, mradi
huu ni kwa ajili ya kuhudumia vituo vya uzalishaji umeme ambavyo
vimeungwa kwenye Gridi ya Taifa na kununua vipuri vyake wakati kina cha
maji kwenye mabwawa ya kufua umeme kitakapopungua kutokana na ukame. Kwa
mwaka huu fedha zilizotengwa ni kwa ajili ya kununua mafuta ya
kuendeshea mitambo ya dharura ya kufua umeme na kununua umeme kutoka kwa
wazalishaji hao binafsi.
Mheshimiwa Spika, Mnamo
tarehe 28.07.2012 Naibu Waziri wa Nishati na Madini (nishati)
Mhe.Simbachawene wakati akiwasilisha maoni juu ya hotuba ya bajeti
alisema kuwa tatizo la mgao wa umeme nchini ni la kupangwa mezani,
nanukuu (hansard uk.488) ‘………..lakini kila unapokaa siku mbili
unaombwa kukubaliana na mgawo wa umeme na mkizungumza mezani mgawo
unatoweka .Kumbe umeme wa Tanzania ni suala la kuzungumza mezani halafu
mnakubaliana kuwa unakuwepo mgao au haupo;hii haikubaliki’
Mheshimiwa Spika, Kambi
rasmi ya upinzani inaona kuwa hata suala la kutenga fedha nyingi kiasi
hiki kwa ajili ya mafuta ya kuendeshea mitambo binafsi ya kuzalisha
umeme wa mafuta nalo ni jambo la kupangwa mezani, kwani kama tukiamua
kuwekeza kwenye vyanzo vingine vya umeme hakika tusingekuwa tunatumia
fedha nyingi namna hii kwa ajili ya umeme wa mafuta nchini tena kutoka
kwa wazalishaji binafsi.
Mwenendo wa
wizara hii ni kutenga mabilioni ya fedha kila mwaka , Kwa mfano mwaka
2011/2012 zilitengwa bilioni 204.643, mwaka jana 2012/2013 tulitenga
bilioni 51.3 (lakini serikali ikatumia kiasi cha shilingi bilioni 242.96 randama uk.4) na
mwaka huu wa fedha tunatenga bilioni 273.207 kwa ajili ya kununulia
mafuta ya mitambo ya kuzalishia umeme. Yaani kwa miaka 3 tu taifa
limeunguza fedha kiasi cha shilingi bilioni 720.81.kwa ajili ya
kulipa makampuni binafsi, hivi Mchuchuma,Liganga, Stiglersgorge,
inahitaji uwekezaji wa kiasi gani?
5.3.3 MRADI WA UMEME IGUNGA
Mheshimiwa Spika, kutokana
na mradi wa umeme ambao unaendelea katika Wilaya ya Igunga kumekuwepo
na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wa vijiji vya Mbutu, Mwamakona,
Bukama, Igunga na vijiji vingine ambavyo mradi huu unapita kutokana na
kutokuridhishwa na kiwango cha fidia ambacho walilipwa ili kuweza
kupisha na kuachia ardhi yao, nyumba zao na mazao yao kwa manufaa ya
mradi huo .Wapo waliolipwa shilingi laki sita, milioni moja nk
Kambi rasmi ya upinzani, imepokea
malalamiko ya wananchi juu ya viwango vidogo vya fidia kwani na madai
yao ya kutoona tathimini iliyofanywa kulingana na mali zao na pia
hawakulipwa kwa njia ya hundi pamoja na kutakiwa kufungua akaunti bali
walilipwa kwa fedha taslimu. Hivyo, tunataka kujua juu ya yafuatayo;
i. Ni lini wananchi hawa watalipwa kiasi halisi kulingana na ardhi na mali zao?
ii. Ni kwanini wananchi hawa walilipwa fedha taslimu na sio kwa njia ya hundi kama ulivyo utaratibu wa malipo wa serikali?
5.3.4 SERIKALI NA MADENI YA SHIRIKA LA UMEME TANZANIA (TANESCO)
Mheshimiwa Spika kambi
rasmi ya upinzani bungeni, inaishangaa serikaLi hii ya CCM kwa kukosa
dira ya kuongoza nchi hii, hali hii inatokana na serikali yenyewe kuwa
sehemu ya kudhoofisha Shirika lake yenyewe huku ikitaka kuwaaminisha
watanzania kwamba inashughulikia matatizo ya kupatatikana kwa umeme
nchini.
Mheshimiwa Spika, miongoni
mwa matatizo yanayokwamisha shirika la umeme Tanzania kujiendesha ni
pamoja na madeni ambayo yamekuwa sugu kutoka kwa makampuni mbalimbali,
watu binafsi , mashirika , katika hali ya kushangaza idara za serikali
zikiwemo pia Wizara za Serikali ambayo inajinadi kuweka mpango wa
kumaliza tatizo la umeme wakati ikishindwa kulipia hata bili zake za
umeme.
Taasisi za
serikali ambazo zinaonekana kuwa ni wadaiwa sugu hadi kufikia mwazi
Januari 2013 ni pamoja na Zanzibar State Fuel inayo daiwa kiasi cha
shilingi 46,136,823,543/=, Jeshi la wananchi wa Tanzania (TPDF)
linadaiwa shilingi 13,839,849,487/=, Jeshi la Polisi linalodaiwa
shilingi 8,994,752,654/= Wizara ya maji inadaiwa shilingi
4,997,245,027/= DAWASA inadaiwa shilingi 4,114,828,175/= na Jeshi la
MAGEREZA linalodaiwa shilingi 3,530,850,068/= pamoja na mifano hii
michache wadai wengine ni pamoja na Regional Water Engineers, Muhimbili
Medical Centre, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Hospitali za serikali,
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Radio Tanzania.
Kwa mjibu wa taarifa rasmi za TANESCO zilizopo ni kuwa shirika linadai jumla ya Tsh 83,773,824,632/= hadi mwezi januari 2013 kutoka kwa wadaiwa ambao ni wizara na taasisi za Serikali hii ya CCM .
Kambi rasmi ya upinzani bungeni, inaitaka
serikali kueleza sababu za kulihujumu shirika la umeme Tanzania kwa
kutolipa bili za umeme, lakini pia ikumbukwe kuwa kila mwaka bunge hili
Tukufu linapitisha bajeti kwa Wizara husika zenye vifungu vya matumizi
mengine (0C) ambayo hutumika kufanyia shughuli nyingine zikiwemo kulipia
bill za umeme na gharama za wizara husika , tunataka wakati wa
majumuisho serikali itoe maelezo kwanini imeshindwa kulipa hadi sasa,
fedha hizo zinafanya kazi gani na lini serikali italilipa shirika la
umeme Tanzania ili kuepukana na matatizo ambayo serikali inayasababisha
yenyewe.
6.0 MADINI
Mheshimiwa Spika, sekta
ya madini ni miongoni mwa sekta ambazo, kama serikali ikiamua kutumia
vizuri rasilimali hii ni miongoni mwa rasilimali ambazo kama zikitumika
kwa masilahi ya Taifa zinaweza kulitoa taifa katika lindi hili la
umasikini. Hata hivyo inaonekana kuwa bado sekta hii kama ilivyo kilio
cha watanzania walio wengi na wenye mapenzi mema na taifa hili bado
haijaweza kuchangia pato la Taifa kwa kiwango kinachotakiwa.
Mheshimiwa Spika, Kwa
mujibu wa vyanzo mbalimbali hazina ya madini iliyothibitika hadi sasa
ni pamoja na Dhahabu tani 222, Nikel tani milioni 209, shaba tani
milioni13.65, chuma tani milioni 103, Almasi tani milioni 50.9,
Limestone tani milioni 313, magadi soda tani milioni109, chuma tani
milioni 103, jasi tani milioni 3, phosipahate tani milioni 577, na makaa
ya mawe tani milioni 911. Lakini pamoja na kuwepo kwa hazina hii
mchango wa sekta hii katika uchumi wa Taifa na maendeleo ya jamii
haukidhi matarajio ya wananchi. Aidha miongoni mwa vitu vinavyofanya
sekta hii kutochangia vyema ukuaji wa uchumi ni pamoja na misamaha
katika ulipaji wa kodi ya madini. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaishangaa serikali hii ya CCM kwa kushindwa kufuta misamaha inayotoa
kwa makampuni ya uchimbaji wa madini hapa nchini licha ya kwamba jambo
hili limekuwa linapigiwa kelele na wadau walio wengi. Kama taifa
tunajiuliza na kutaka majibu toka kwa serikali ni nini nia hasa siri ya
serikali katika kuendelea kutoa misamaha hii ya kodi.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa ripoti ya kodi katika madini iliyotolewa na shirika laInternational Centre for Tax and Development (ICTD) iliyotolewa
mwezi April 2013 inaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo
zinapata pato dogo la mapato ya ndani yanayotokana na madini kwa wastani
wa 1:1.3 ikilinganishwa na nchi ya Botswana ambayo inawastani wa 1.32:1
ikifuatiwa na nchi ya Chile. Aidha ripoti hiyo inaonesha kuwa Tanzania
ingeweza kufikia kiwango cha nchi ya Chile kama ingekuwa na viwango vya
kutoza kodi kama nchi ya Chile kwa sekta ya madini na kuchangia kukua
kwa pato la Taifa endapo ongezeko ya kodi ya thamani, kodi ya
kusafirisha na kodi ya mapato zinazotokana na madini zingechangia
kupanda kwa pato la Taifa (GDP).
Mheshimiwa Spika, Swala
la mrahaba limeonekana kutopatiwa jawabu halisi kwani kiwango cha
asilimia 4% kinachotozwa kwa sasa baada ya kufanyika marekebisho bado ni
kidogo. Pamoja na kwamba kamati ya Jaji Mark Bomani kupendekeza kuwa
tozo la mrahaba lizingatie ukokotoaji kwa kigezo cha gross value badala
ya net back value pendelezo hilo halitekelezwi kwa ukamilifu. Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuboresha mazingira ya
utoaji wa mrahaba pamoja na kodi, ikizingatiwa kuwa baadhi ya makampuni
hayafuati sheria ya mpya ya madini ya mwaka 2010 inayotaja kiwango kipya
cha mrahaba (Royalty), na kuchukua hatua nyingine za ziada kwa
kuzingatia mapendekezo tuliyotoa 2011 na 2012 hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ieleze kwanza ni makampuni
gani ambayo hayajaanza kutumia sheria hii mpya, pili ni hatua gani
imechukuliwa dhidi ya suala hili lakini pia viwango vya kodi na mrahaba
vinavyotozwa vilingane na viwango vinavyotozwa katika nchi nyingine kama
Botswana.
Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa mchango wa sekta ya madini katika maendeleo na huduma za
jamii (Corporate social responsibility); Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaamini kuwa sekta ya madini inayo kazi ya kuhakikisha maendeleo na
huduma za jamii. Katika kufanikisha adhima hii ripoti ya Jaji Mark
Bomani ilipendekeza miongoni mwa mambo mengine ni pamoja na wawekezaji
kutoa huduma za jamii ili kuimarisha uhusiano na jamii zinazozunguka
migodi, wawekezaji washiriki katika mashauriano ya mashauri ili wajue
vipaumbele na mirahaba inayokwenda halmashauri itumike katika kuboresha
huduma za jamii.
Mheshimiwa Spika, pamoja
na mapendekezo hayo lakini hali ya halmashauri ambako makampuni ya
uchimbaji wa madini yanakopatikana bado ni wilaya maskini sana.
Halmashauri za Kahama, Geita, Tarime hazifanani na thamani ya madini
yanayopatikana katika maeneo yao. Pamoja na hayo kuna mkanganyiko katika
sheria ya Local Authority Finance Act dhidi ya mikataba na kusababisha
halmashauri kukosa haki zake. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
serikali kueleza hatua zaidi za makusudi ambazo inachukua kuhakikisha
wananchi wa maeneo hayo na watanzania kwa ujumla wananufaika na
rasilimali za nchi hii kwa maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kushughulikia
mkanganyiko huo wa kisheria.
Mheshimiwa Spika, naomba kunukuu tulichokisema mwaka 2011/2012 kuhusiana na ujanja wa makampuni makubwa ya madini “Mheshimiwa
Naibu Spika, Ili kuongeza kiwango cha mapato ikiwemo ya kodi kutokana
na uchimbaji wa madini; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kutekeleza mikakati ya kupenya kuta za umiliki na mitaji (capital and
ownership structures) zilizojengwa kwa muda mrefu na makampuni ya
kimataifa kwa kutumia mianya ya udhaifu wa kisheria na ushawishi wa
kifisadi uliosababisha mikataba mibovu katika sekta ya madini nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kueleza bayana hatua ambazo imechukua kufuatia Ripoti ya Tume/Kamati
mbalimbali ambazo ziliundwa na Serikali kwa nyakati mbalimbali kwa
kutumia fedha nyingi za walipa kodi lakini mapendekezo yake bado
hayajatekelezwa kwa ukamilifu wake. Mathalani ripoti za karibuni za
Kamati ya Masha na ile ya Bomani (2008) zilieleza bayana namna ambavyo
makampuni makubwa ya madini yamekuwa yakitumia sehemu kubwa ya uwekazaji
wao kama mkopo (debt financing). Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua
kwamba makampuni hayo yamekuwa yakitumia mianya hiyo ya kisheria na
kimikataba kuwezesha wamiliki na wanahisa kupata faida mapema kuliko
kuweka mtaji kwa kuwa riba ya mikopo huondolewa katika kukokotoa kodi.
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Serikali iwaeleze Watanzania ni trilioni
ngapi za mapato tumezikosa kati ya mwaka 1995 mpaka 2010 katika kipindi
cha miaka 15 ya kuachia mianya ya upotevu wa mapato kwa kuruhusu
asilimia kubwa ya mikopo kuwa mitaji. Aidha, ni hatua gani zimechukuliwa
kwa waliohusika kuliingiza Taifa katika mikataba mibovu iliyoruhusu
makampuni hayo kujitangazia hasara kila mwaka huku yakipata faida
kubwa”.
Mheshimiwa Spika, matatizo
ya wachimbaji wadogowadogo wa madini, kimekuwa ni kilio cha muda mrefu
kwa taifa hili. Kwa mujibu wa mapendekezo ya kamati ya Jaji Bomani
kuhusu namna ya kuboresha mazingira ya wachimbaji wadogowadogo wa
madini, kamati ilishauri muda wa leseni kuongezwa kufikia miaka 10 ili
kuwawezesha wachimbaji hao waweze kupata mikopo kutoka taasisi za fedha.
Wachimbaji kusaidiwa mbinu kwa ajili ya kupata mtaji wa kufanya
shughuli za uchimbaji, kuchangia katika mfuko wa wachimabji
wadogowadogo, kuwekwa kwa utaratibu wa kisheria kwa ajili ya kuwakatia
bima wafanyakazi wao na kuanzisha taasisi za fedha kwa ajili ya mikopo
kupitia SACCOS zao.
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa taarifa ya kamati ya kudumu ya bunge ya Nishati na Madini
kuhusu utekelezaji wa majukumu ya wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka
wa fedha 2011/2012 pamoja na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka
wa fedha 2012/2013, kamati ilithibitisha matatizo ya wachimbaji
wadogowadogo kuwa ni pamoja bajeti ndogo inayotengwa kwa wachimbaji,
elimu kutotolewa kwa wachimbaji, uhaba wa maeneo ya uchimbaji kwa vile
maeneo yao yamechukuliwa na wawekezaji wakubwa, ukosefu wa masoko ya
kuuzia bishaa zao na kodi kubwa, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni
inaitaka serikali kueleza hatua ilizofanya katika kutekeleza mpango
mkakati wake hususan katika matatizo yafuatayo;
(a) Serikali
imeongeza kiasi gani cha fedha kwenye bajeti ya wachimbaji
wadogowadogo, ni utaratibu gani umewekwa ili fedha hizo ziwafikie
walengwa?
(b) Kuna
mkakati gani wa kuhakikisha wachimbaji hao wanapata mafunzo ya uchimbaji
na masuala yanayolenga kuongeza thamani ya madini yao?
(c) Maeneo
gani na kanda zipi ambapo wachimbaji hawa wametengewa maeneo kutokana na
maeneo yao kuchukuliwa na wawekezaji wakubwa?
(d) Serikali imeweka mfumo gani katika kuhakikisha mchango wa uchimbaji mdogo unajulikana kwenye pato la Taifa?
(e) Ili
kuongeza thamani ya madini, kuna mkakati gani wa wa kuhakikisha kazi hii
inafanyika hapa nchini na kuongeza siyo tu thamani bali ajira kwa
watanzania?
(f) Hatua
gani zimefanywa na serikali kuhakikisha soko na bei ya madini inakuwa
imara na mikakati gani imewekwa ili kuhakikisha umeme unapatikana katika
maeneo ya wachimbaji wadogowadogo?
Mheshimiwa Spika, sasa
ni takriban miaka sita toka kuwasilishwa kwa ripoti ya Mheshimiwa Jaji
Mark Bomani kwa Rais. Baada ya kuwasilishwa pia hapa Bungeni na Kamati
husika na Bunge likaijadili na mapendekezo yake yakawa ni maazimio ya
Bunge. Lakini hadi sasa maazimio ya Bunge bado hayatekelezwa kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, Katika
mapendekezo ya tume ya Jaji Bomani ambayo pia yaliridhiwa na Bunge lako
tukufu na kupitishwa kama Azimio la Bunge ni pamoja na kufutwa misamaha
ya kodi, kwa badiliko alilotoa Waziri wa Fedha la kufuta utekelezaji wa
GN 99 kuanzia Julai 2009 kwa makampuni. Marekebisho haya yanahusu
kampuni za madini zilizoingia mkataba na Serikali kuanzia July 2009. Kwa
nini ufutaji wa misamaha hii usiyaguse makampuni yaliyokuwepo kabla ya
kamati ya Jaji Bomani haijaanza kazi?
Mheshimiwa Spika, ukweli
ni kwamba msamaha ambao unaendelea kutolewa hadi sasa kwa makampuni
hayo ya mafuta unaukosesha mfuko wa barabara mabilioni ya fedha na huko
makampuni hayo ndiyo yanaharibu kwa kiasi kikubwa barabara zetu. Kambi
Rasmi ya Upinzani inamtaka Mhe Waziri alieleze Bunge ni kwanini maazimio
ya Bunge hadi leo hii hayajatekelezwa kikamilifu?
Aidha, Mheshimiwa Spika, mapendekezo mengine ya kamati ya Mheshimiwa Jaji Bomani yalikuwa ni:
1. Serikali
kumiliki hisa ndogo kama kwa kampuni ya Williamson Diamonds Limited
ambapo Serikali ina hisa 25%, hali ambayo si sawa kwa umiliki wa kigeni.
Upo umuhimu wa ushiriki wa kutosha wa watanzania katika umiliki wa hisa
za kampuni za uchimbaji mkubwa.
2. Shughuli
zote za uchimbaji wa vito, na Kampuni za uchimbaji wa kati wa madini
mengine, zimilikiwe ama kwa 100% au kwa kiasi kisichopungua 50% na
wananchi wa Tanzania.
3. Shughuli zote za wachimbaji wadogo zimilikiwe na kuendeshwa na watanzania tu.
Mheshimiwa Spika, ni
matarajio ya Kambi Rasmi ya Upinzani, Serikali itawaeleza watanzania
utekelezwaji wa maazimio hayo ya Kamati ya Mhe.Jaji Bomani ambayo
yaliridhiwa na Bunge yametekelezwa kwa kiwango.
Mheshimiwa Spika, Utaratibu
unaotumika katika kuingia mikataba ya uchimbaji wa madini umewekwa wazi
katika Sheria ya Madini ya mwaka 2010. Sehemu ya 23 ya Sheria hiyo
inaelezea kuhusu kuanzishwa kwa bodi itakayojulikana kama Bodi ya
Ushauri ya Sekta ya Madini. Bodi hii inamshauri Waziri anayesimamia
madini kuhusu masuala ambayo yako chini ya Sheria ya Madini ya mwaka
2010 ambayo yanatakiwa kufikishwa kwenye Bodi.
Mheshimiwa Spika, Wizara
ya Nishati na Madini imeonyesha udhaifu wa kumnyima hata Mkuguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhakikia mikataba ambayo Serikali imefunga
na wachimbaji ili “kubainisha taratibu ambazo zinafuatwa na Wizara
katika kutekeleza matakwa ya sheria hii kwa vile mikataba hii ya
Uchimbaji ni ya watu binafsi na ni siri kwa watu wengine wasiokuwa
sehemu ya mikataba hiyo. Kutokana na usiri huo, sikupewa haki ya
kuipitia mikataba hiyo na hivyo kuzuia wigo wa ukaguzi wangu”[4].
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaliomba Bunge katika mjadala huu utakaoendelea
kupitisha azimio mahususi kuilazimisha Wizara kuwajibika kwa kuendelea
na utekelezaji wa mikataba yote ambayo, kwa njia moja au nyingine
imekiuka sheria na pia imekiuka maazimio na ushauri unaotolewa na Bunge.
Kwa njia hii tutakuwa tumetimiza wajibu wetu wa Kikatiba wa Kuisimamia
na kuishauri Serikali.
Mheshimiwa spika, mchango
wa sekta ya madini katika pato la taifa bado ni mdogo mno ukilinganisha
na jinsi nchi yetu ilivyojaliwa rasilimali hii na uchimbaji unaoendelea
sehemu mbalimbali katika nchi yetu. Kwa ujumla madini tuliyojaliwa
hayawafaidishi watanzania kwa kiwango kilichotegemewa zaidi ya
kuwaingiza kwenye matatizo ya uchafuzi wa kimazingira ugumu wa maisha.
6.1 STAMICO
Mheshimiwa Spika, Shirika
la Madini (STAMICO) linaimarishwa upya na serikali baada ya kuondolewa
kutoka kwenye orodha ya mashirika ya umma yanayotakiwa kufutwa mwezi
Machi, 2009. Hivyo lilipewa majukumu makuu manne, ambayo ni:
a. Kuwekeza katika utafutaji,uendelezaji na uchimbaji wa madini
b. Kusimamia hisa za serikali katika migodi
c. Kuratibu uendelezaji wa wachimbaji wadogo nchini, na
d. Kutoa
huduma za kibiashara katika sekta ya madini, huduma hizo ni uchorongaji
wa miamba, utafutaji wa madini na utoaji ushauri katika masuala ya
madini.
Mheshimiwa Spika, taarifa
ya shirika liyowasilishwa kwenye kamati ya madini na nishati, inaeleza
kuwa Bodi ilimaliza muda wake mwezi Juni, 2012. Hivyo basi shirika hilo
halina bodi hai. Kwa mujibu wa taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti ameongelea
kitendo cha Mwenyekiti wa Bodi kuingilia moja kwa moja utendaji wa
shirika hilo kiasi kwamba, shirika limekuwa likimlipa posho ya mafuta
Mwenyekiti huyo sawa na lita 100 za mafuta kila wiki, asilimia 40 ya
posho ya mafuta kama fedha za matengenezo kila wiki na shilingi
500,000/= kwa mwezi kama fedha za mawasiliano.
Mheshimiwa Spika,
msuguano huu wa kiutendaji kati ya mkurugenzi mtendaji na Mwenyekiti wa
bodi kwa kiasi kikubwa inadumaza utendaji wa shirika. Hivyo basi, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwachukuliwa hatua za kinidhamu
Wenyeviti wenye tabia kama hii kwani malipo hayo ni aina nyingine ya
matumizi mabaya ya raslimali za umma ambayo yanapaswa kudhibitiwa.
Mheshimiwa Spika, STAMICO
ndiyo yenye dhamana ya uendelezaji wa Mgodi wa Buhemba, kwani tangu
mwezi Julai, 2011 shirika lilipewa leseni ya utafutaji wa madini juu ya
eneo la mgodi wa zamani wa dhahabu wa Buhemba, mkoani Mara kwa kumiliki
asilimia 40 za mgodi huo.
Mheshimiwa Spika, kutokana
na ukweli kwamba mgodi huu wa Buhemba ndio uliokuwa ukimilikiwa na
kampuni ya MEREMETA kampuni ambayo mbali ya kuiingiza nchi kwenye kashfa
bali pia iliwaacha wananchi/ wachimbaji wadogo wa eneo la Buhemba
wakiwa na malalamiko ya kutokulipwa fidia kwa kutwaliwa maeneo yao.
Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuelewa je STAMICO inamkakati gani wa
kwanza kuchukua mali zilizokuwa zinamilikiwa na MEREMETA? Na pili madai
ya wananchi wanayalipa vipi kwa pamoja na mbia wake?
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa ushauri ulipotolewa na Mkaguzi kuhusu ushiriki wa Sekta
ya Umma na Sekta binafsi kugubikwa na mapungufu makubwa ambapo faida
inakuwa kwenye upande wa pili zaidi na Serikali. Mfano ni ubia wa SONGAS
Ltd, IPTL ltd, Kiwira Coal Mines (TANPOWER LTD), TICTS na kadhalika.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iwahakikishie watanzania ni
kwa kiwango gani ubia huo wa STAMICO na MANJARO RESOURCES Pty Ltd kutoka Australia utakuwa na tija kwa taifa?
6.2 WAKALA WA UKAGUZI WA MADINI-TMAA
Mheshimiwa Spika, wizara ya nishati na madini 08 desemba, 2011 ilitoa taarifa kwa umma kuhusu maendeleo ya sekta ya madini.
Mrabaha
uliolipwa na migodi mikubwa ya dhahabu katika kipindi hicho cha kuanzia
mwaka 1998 hadi 2010 ilikuwa ni Shilingi Bilioni 341.57, wakati hadi
kufikia mwaka 2010 kulikuwa na Watanzania 6,129 walioajiriwa rasmi
kwenye migodi mikubwa 6 ya dhahabu. PAYE wanayolipwa ya kati ya asilimia
14 mpaka 30 kutegemea kiwango cha malipo.
Mheshimiwa Spika, ili
kufanya ulinganisho ulio sahihi wa kama kweli mchango wa sekta ya
madini kwenye kodi unatokana na mrahaba au kodi ya PAYE wanayolipa
waajiriwa hao 6,129 ilitakiwa tuambiwe ni kiasi gani, kwani kuna
uwezekano mkubwa PAYE inazidi kwa mbali fedha inayoingia itokanayo na
mrahaba.
Mheshimiwa Spika, Wakala
wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ndiye mwenye dhamana katika
kudhibiti uzalishaji wa madini na ukusanyaji maduhuli yatokanayo na
mrahaba kwa kampuni za uchimbaji madini. Hata hivyo, TMAA haina udhibiti
wowote katika uzalishaji na uthamanishaji wa madini kwa wachimbaji
wadogo na wa kati ambao wameachwa kueleza wenyewe kiasi cha madini
wanachozalisha.
Mheshimiwa Spika, kutokana
na ukweli huo, ni kwa vipi Wizara inataka kuliaminisha Bunge kuwa
takwimu za madini hasa dhahabu zilizozalishwa hapa nchini kuwa ni
sahihi?
Mheshimiwa Spika, mapungufu
haya kwa kiasi kikubwa yanatokana na ukweli kwamba “control mechanism”
kwa wachimbaji wadogo wakati wa kutoa leseni umegubikwa na matumizi
mabaya na udanganyifu ambapo watu wachache wamehodhi maeneo mengi na
kuajiri wachimbaji wadogo na kinachopatikana kutokana na machimbo hayo
Serikali inanyimwa taarifa. Pia kushindikana kwa udhibiti ni viwanja
vidogo vya ndege vilivyotapakaa hapa nchini ambavyo TMAA haina udhibiti
navyo.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa hiyo ni kwamba Serikali imechukua hatua zingine za kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini ni pamoja na:
1. Kutenga maeneo maalum ya wachimbaji wadogo;
2. TANSORT kuhamishia rasmi shughuli zake hapa nchini kutoka Uingereza mwezi Agosti, 2010;
3. Upigaji
marufuku wa usafirishaji nje ya nchi madini ghafi ya Tanzanite yenye
ukubwa unaoanzia gramu moja na kuendelea mwezi Aprili, 2010;
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ilieleze Bunge tangu kitengo hicho
cha kuchambua almasi kirudishwe hapa nchini toka Uingereza ni kiasi gani
cha fedha kimepatikana kutokana na kazi zake hizo?
Mheshimiwa Spika, yamekuwepo
madai ya wachimbaji wadogo wadogo ambao ndiyo wazawa kunyimwa leseni
katika maeneo yao ya uchimbaji na maenea yao kugawiwa kwa wanaojiita
wawekezaji na wao wakihamishwa hamishwa pasipo kupatiwa maeneo mbadala.
Mheshimiwa Spika, Kuna
matatizo mengi ya wachimbaji wadogo wadogo katika maeneo ya Kalalani
Tanga, Mgusu, Nyarugusu, Mtakuja Geita, Winza Mtakanini Mpwapwa,
Simangulu Chamwino, North Mara, Rwamgasa, Kasema,Kilindi Nyamongo na
kadhalika. Hivi karibu ni wachimbaji wapatao 400 wa kijiji cha
Nkongilangi wanaochimba eneo la Machimbo ya Sekenke-Iramba Magharibi,
ambao toka mwaka 1982 wamekuwa wakiomba leseni lakini hawapatiwi majibu
ya maombi yao. Mwaka 2007 waliomba tena na kuambiwa leseni imetolewa kwa
kampuni ya WASEKE, kwa mshangao mkubwa mwaka 2011 alikuja mtu anayedai
kuwa ndiye mmiliki wa eneo hilo la uchimbaji mdogo la kijiji cha
Nkongilangi aitwaye “JOHN BINA”. Na hapo ndipo matatizo na unyanyasaji
ulipoanzia na kusababisha uporaji na vifo kutokea[5].
Mheshimiwa Spika, katika
mazingira kama hayo, wachimbaji wadogo wapatao 3000 kwa ushirika wao
wilayani Maswa baada ya kulipia ada ya maombi yao imechukua takriban
miezi minne baadae wakajibiwa kuwa eneo hilo tayari lilikuwa na mmiliki
toka mwaka 2002. Lakini baada ya kuangalia coordinates zilizosemwa
kwenye barua na zile zilizoko kwenye ramani, ni kwamba leseni PL
4233/2007 ambayo mmiliki wake ni SAVANNAH EXPL. Ltd iliyotolewa tarehe
02/05.2007 na eneo lake liko Luguru na Luguru ni kijiji kilicho ndani ya
wilaya ya Bariadi na sio Maswa. Huu ni mkakati unaotumiwa na watendaji
Idara ya Madini kwa kushirikiana na wenye dhamana katika Serikali
kuwanyima haki wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwaeleza wachimbaji fedha
zilizotengwa kiasi cha shilingi bilioni moja kama kianzio cha Mfuko wa
kuendeleza Wachimbaji wadogo nchini, kama hotuba ya Waziri Mkuu Mhe.
Mazengo Pinda alivyosema Bungeni wakati akiwasilisha mapitio na
makadirio ya matumizi ya fedha yake na Ofisi ya Bunge kwa mwaka
2010/2011 zilipewa wachimbaji wadogo wa wapi?
Mheshimiwa Spika, aidha,
kwa mujibu wa maneno ya Mhe Naibu Waziri Madini wakati akijibu swali
tarehe 22 April 2013 alisema “SERIKALI inatarajia kukamilisha taratibu
za Mfuko rasmi wa kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini, ili
kuwawezesha kupata mikopo, ikiwa ni pamoja na kuwapatia mikopo ya vifaa
vya kuchimbia kwa kanda zote nane zinazochimba madini nchini”.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inauliza mfuko huo ambao umekwisha tengewa fedha na
hapa Naibu Waziri anasema inatarajia kukamilisha taratibu rasmi za mfuko
huo, hii maana yake nini? Na mfuko huo utaendeleza wachimbaji gani
wakati ambapo maeneo mengi wana malalamiko ya leseni na wanafukuzwa ovyo
kama mifano ambayo tumeitoa hapo juu.
Mheshimiwa Spika, Kwa
wale walio na maeneo ya kuchimba madini wamekuwa wakifanya kazi katika
mazingira magumu kutokana na kuwa na mtaji mdogo unaowafanya washindwe
kupata zana bora kwa ajili ya uchimbaji. Aidha, watoto wa walalahoi
wamekuwa wakiajiriwa katika migodi mbalimbali nchini mbali ya kuwa na
sheria inayopinga ajira kwa watoto hususan katika maeneo ya migodini.
Mheshimiwa spika, Kitendo
cha serikali kupandisha kodi mara kawa mara kwa wachimbaji au
wawekezaji wadogo wadogo ni kufanya wawekezaji wadogo wasimudu kushiriki
kikamilifu katika kuwekeza ndani ya sekta ya Madini wakati serikali
inajigamba kuwasaidia wawekezaji hao huku serikali ikipandisha kodi
kutoka 80,000/= hadi 1,000,000/= kwa wachimbaji hao.
Mheshimiwa spika, Jambo
hili ambalo pia lililalamikiwa na wabunge wengi limeonekana
limetafsiriwa kuwa ni mkakati wa makusudi wa kuwafukuza wawekezaji
wadogo wadogo katika sekta hii na kutoa mianya kwa wawekezaji wenye pesa
zao kuendelea kuwekeza katika sekta hii ya madini. Kambi rasmi ya
upinzani bungeni inaitaka serikali kieleze kwa kina ni kwa jinsi kani
itawasaidia wachimbaji wadogo kama gharama za uendeshaji wa migodi hiyo
zinapanda bila kuzingatia hali halisi ya wachimbaji hao. Hii ni hatari
sana kwani tunafanya wazawa washindwe kunufaika na sekta hii moja kwa
moja.
Mheshmiwa spika, Katika kuboresha sekta hii ya madini kamati ilishauri mambo yafuatayo yafanyike:
Ø Serikali kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kushiriki katika shughuli za kutoa huduma(supply)mbalimbali migodini
Ø Sheria ya ajira kwa watoto isimamiwe ipasavyo
Ø Migodi mikongwe ilipe kodi(corporate tax)
Ø Kuwepo kwa soko la pamoja la madini
Ø Kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika kila kanda na kusimamia vizuri zoezi la ugawaji wa leseni
Ø Serikali
iwasaidie wachimbaji wadogo iliwaweze kapata mikopo ya kuwawezesha
kuanzisha viwanda vidogo vitakavyowasaidia kuongeza thamani ya madini
yao
Ø Serikali kukomesha biashara haramu ya madini
Hata hivyo
serikali haijayafanyia kazi kwa ukamilifu mapendekezo hayo ya kamati
katika mwaka wa fedha 2012/2013 na bado sekta hii inakumbwa na hali
ileile na kuifanya iendelee kutokuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa
nchi.
Mheshimiwa spika, Taarifa
ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa fedha za serikali ulioishia 30 Juni,
2012 inaonesha kuwa Wizara ya Nishati na Madini imeliingizia taifa
hasara ya zaidi ya shilingi 20,000,000,000 katika sekta ya madini.
Hasara hiyo kama ilivyooneshwa kwenye taarifa ya CAG ilisababishwa na
malimbikizo ya maduhuli ambayo hayakuonyeshwa Sh.1,645,582,899.Taarifa
za fedha zilizowasilishwa na Wizara hazikuonyesha malimbikizo ya
maduhuli yenye jumla ya Sh. 1,645,582,899/- kama ilivyotakiwa na Mkaguzi
na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
Mheshimiwa spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani bungeni inashangaa ni kwa sababu gani hasa bado
sheria ya zamani inaendelea kutumika wakati tayari sheria ya mwaka 2010
imeshaanza kufanya kazi. Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka
Wizara ieleze kwanini hali hiyo imejitokeza na hatua gani inachukua
dhidi ya watendaji waliohusika katika kulipatia hasara hiyo?
Kambi Rasmi ya Upinzani pia
inaitaka serikali kutumia sheria mpya ya kukusanya mrahaba katika
kampuni za madini na hivyo makampuni yote yaliyolipa mrahaba huo kwa
kutumia sheria ya zamani yalipe sehemu iliyobakia kwa mujibu wa sheria
mpya.
Pamoja na
hayo tunaitaka serikali ilitaarifu bunge lako tukufu kuhusu malimbikizo
ya maduhuli ambayo hayakuoneshwa kwenye taarifa za mahesabu ya wizara
hii, tunataka tujue serikali inampango gani na fedha hizi ambazo ni
zaidi ya 1,000,000,000/=.
Mheshimiwa spika, mambo
mengine yanayo sababisha hasara katika sekta ya madini ni pamoja na
kutokuwa na udhibiti wa mapato ya wachimbaji wadogo wa madini na
kutokuwa na udhibiti katika viwanja vya ndege. Udhibiti mdogo katika
sekta hii ya madini kumesababisha kupotea kwa mapato mengi ambayo nchi
ingeyapata kutokana na madini yanayosafirisha bila kulipa kodi na
biashara haramu ya madini inayoendelea nchini.
Mheshimiwa Spika, Pia
kwa mujibu wa taarifa ya CAG hukuna ushirikianao kati ya wizara na TRA
na hivyo kodi nyingi zinashindwa kukusanywa kutokana na TRA kukosa
taarifa sahihi juu ya vyanzo vya mapato vya wizara hiyo.
Mheshimiwa spika, utekelezaji
wa ahadi nyingine za Waziri wa Nishati na Madini katika bajeti ya
2012/2013; Waziri wa Nishati na Madini katika majumuisho yake aliahidi
Bunge kuwa kuna madini ya VANADIUN na PGE yanayopatikana katika madini
ya Copper na Nickel. Hilo atalifanyia kazi suala la wawekezaji
wanaochukua leseni ya Copper na Nickel kwani kuna upatikanaji wa madini
ya VANADIUM na PGE ambayo inasemekana kuwa yanathamani kubwa kuliko
Copper na Nickel. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka
serikali kueleza juu ya utekelezaji wa suala hili kama waziri
alivyoahidi bungeni wakati wa kuhitimisha hotuba ya bajeti ya wizara
yake ya mwaka wa fedha 2012/2013
Mheshimiwa spika, katika
suala la mkopo wa billion 8.9 kwa wachimbaji wadogo kwamba ni kwa vipi
wachimbaji wadogo wangepewa mikopo hiyo wakati kwa wakati huo leseni
nyingi na maeneo yote wamepewa wawekezaji wakubwa, Mh. Waziri aliliambia
bunge kuwa lesini hizo zinaisha muda wake, na zikiisha muda wake
wawekezaji wakubwa wanaacha nusu ya eneo walilokuwa wanamiliki na hivyo
maeneo haya wanapewa wachimbaji wadogo wadogo.
Mheshimiwa spika, katika
suala hilohilo la wachimbaji wadogo wadogo ilijitokeza pia hoja kutoka
kwa wabunge, waliomuuliza Waziri wa Nishati na Madini jinsi gani mkopo
wa billion 8.9 uliopangwa kuwanufaisha wachimbaji wadogo wadogo nchini
utagawiwa kwa wachimbaji husika. Waziri alijibu wanatakiwa waunde vyama
vyao kila mkoa na wawe na chama chao kitaifa ambako ndiko mkopo huu
utaelekezwa.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka serikali itupe takwimu sahihi mpaka sasa tathmini ikoje juu ya
leseni za wawekezaji wakubwa kuisha muda wake na wawekezaji wadogo
kupewa maeneo husika na je mkopo wa billion 8.9 umewanufaisha wachimbaji
wadogo wadogo wangapi mpaka sasa? Na Kama wachimbaji wadogo
hawajanufaika na mkopo huu serikali itueleze fedha hizi zilizotengwa
katika mwaka wa fedha 2012/2013 kwa ajili ya kazi hii zimefanyiwa nini?
Mheshimiwa spika, kuhusu
madeni ambayo wawekezaji katika sekta ya madini wanadaiwa na serikali,
Naibu Waziri Wa Nishati na Madini wakati wa mjadala wa bageti ya mwaka
2012/2013 alipokuwa anajibu hoja ya madeni ambayo wawekezaji katika
sekta ya madini walikuwa wanadaiwa tangu mwaka 1997 hadi mwaka 2005
aliliahidi bunge kwamba kampuni ya BARRICK ambayo ndiyo kampuni pekee
iliyokuwa inakataa kulipa deni lake atalifanyia kazi swala hilo na
kuhakikisha wanalipa.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali ieleze kama madeni yote
yamelipwa kwa kuzingatia sheria mpya ya madini ambayo pamoja na mambo
mengine inataka mirahaba kulipwa kwa asilimia nne [4%] kabla ya makato
ya makato ya Kodi. Na kama kuna makampuni hayataki kutii sheria hii mpya
ya madini kwa nini serikali isiyafutie leseni ya kufanya kazi za
uchimbaji wa madini nchini ? Kwa sababu nchi haiwezi ikavumilia
wawekezaji ambao hawatii sheria za nchi.
Mheshimiwa spika, Pia
Naibu Waziri alikiri mbele ya bunge lako tukufu kuwa mgodi wa BUZWAGI
haujalipa kodi ya kampuni yaani (Corporate tax), na kuahidi kuwa mgodi
wowote mpya utaoanza kuanzia wakati huo serikali itaanza kuwa na share
ya 15% kama hisa za kubeba (free carried interest).
Tunaitaka
serikali ilieleze bunge lako tukufu na umma wa watanzania kwa ujumla
wake kama mgodi huo umelipa kodi hiyo na serikali imejipangaje kumiliki
hisa kwenye migodi inayotegemewa kuanzishwa na hii ambayo imeanzishwa
kwa ajili ya kuwa na udhibiti wakati kwa kuzingatia masharti ya sheria
ya madini ya mwaka 2010 ambayo inatoa haki hiyo ya Serikali kuwa na
hisa.
6.3 UCHIMBAJI MADINI AINA YA URANI
Mheshimiwa Spika, Kwa
kuwa swala la uchimbaji na utafutaji wa madini ya aina yeyote lipo
chini ya wizara ya nishati na madini , na kwa kuwa swala la uchimbaji wa
madini ya aina ya urani kama taifa tunahitaji kuwa na angalizo kubwa
ikiwa ni pamoja na kutochimba madini hayo ya aina ya urani kutokana na
uhatari wake kwa maisha ya binadamu, na kwa kuwa kambi rasmi ya upinzani
kwa mara kadhaa ndani ya bunge hili imekuwa ikitoa maoni yenye nia
njema na maisha ya watanzania na viumbe vingine na kwa kuwa tatizo la
serikali kutokubali kufanya maamuzi ya kubadili mtazamo wa kutegemea
uchumi wa urani na kujikita katika uchumi wa rasilimali mbadala ambazo
taifa letu limebarikiwa kuwa nazo.
Mheshimiwa Spika, katika
eneo la mbarang’andu katika wilaya ya Namtumbo ambapo kampuni ya Game
Frontiers iliyojipatia kitalu hicho kwa ajili ya uwindaji kwa mujibu wa
sheria imeamua kufanya biashara ya kuruhusu utafiti wa uchimbaji madini
aina ya urani kinyume na taratibu za uendesahji wa vitalu vya uwindaji.
Mheshimiwa Spika, katika
bunge hili mnamo Tar 28/07/2012 zilitolewa taarifa hapa ndani ya bunge
hili kwa vielelezo kutoka kwa msemaji wa kambi rasmi ya upinzani bungeni
kuhusu maswala ya ardhi Mhe. Halima Mdee juu ya kampuni ya Game
Frontiers kukodisha kitalu chake cha uwindaji kwa ajili ya utafutaji wa
madini ya urani katika eneo la mbarang’andu katika wilaya ya Namtumbo.
Mheshimiwa Spika, lakini
pia msemaji wa kambi rasmi ya upinzani alitaka kupata ufafanuzi kwa
Waziri juu ya maagizo yaliyotolewa na Naibu Spika wakati wa majumuisho
ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, maagizo husika
yalitaka Wizara ya Nishati na Madini, wakati wa kupitisha makadirio ya
mapato na matumizi itoe maelezo juu ya mkataba ulioingiwa tarehe 23
Machi, 2007 kati ya Uranium Resources PLC na Western Metals Limited na
Game Frontiers of Tanzania Limited. Mkataba ambao, pamoja na mambo
mengine una ihalalishia Game Frontiers Limited kupata malipo toka kwa
makampuni yanayofanya utafiti katika kitalu cha uwindaji katika kijiji
cha Mbarang‘andu.
Mheshimiwa Spika, majibu ya waziri yalikua kama ifuatavyo nanukuu …..“Mheshimiwa
Spika, lingine lililoulizwa na Kambi ya Upinzani hasa Mheshimiwa Mdee,
huu mkataba wa siri, kweli tumeufuatilia mkataba wa siri, ule wa
uchimbaji wa uranium”…. Kuonesha waziri alikiri mbele ya bunge na kuahidi kulitafutia ufumbuzi swala hilo, na kuwa ataleta taarifa kwa mtoa hoja.
Mheshimiwa Spika, kwa
mara nyingine tena kambi rasmi ya upinzani bungeni inataka kujua ni
vipi wizara ya nishati na madini imeshughulikia swala la kampuni ya
uwindaji ya Game Frontiers kukodisha kitalu chake cha uwindaji kwa ajili
ya utafutaji wa madini ya urani katika eneo la Mbarang’andu wialayani
Namtumbo, lakini pia serikali iwaambie watanzania kwa hatua ilizochukua
za kuchimba urani ni vipi itaweza kuwalinda dhidi ya madhara ya
uchimbaji wa madini hayo?
6.4 MGODI WA KIWIRA
Mheshimiwa Spika, kati
ya kashfa ambazo ziliikumba serikali ya awamu ya tatu ya Rais Mkapa
ilikuwa ni pamoja na kubinafsishwa kwa mgodi huu wa Kiwira
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa kumbukumbu za bunge lako tukufu, bunge lilipitisha maazimio
yake juu ya taarifa ya kamati ya Nishati na Madini kuhusu ubinafisishaji
wa mgodi wa kiwira kufuatia mapendekezo yaliyokuwa yameelekezwa
serikalini kwa ajili ya hatua stahiki, miongoni mwa maazimio ya bunge
ambayo hayakufanyiwa kazi na serikali yalikuwa ni pamoja na;
i. Urejeshwaji wa vifaa na mali ambavyo vimeibiwa au kuhamishwa kutoka kwenye miundombinu ya mgodi wa kiwira
ii. Bilioni
17 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ukarabati wa miundomninu ya
mgodi, serikali ilitakiwa kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha hizo
kupitia kwa Mthibiti na Mkaguzi wa Hesabu za serikali ili kujua matumizi
halisi na halali ya fedha za umma
iii.
Serikali kufuatilia uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU wa shilingi milioni
50 zilizotolewa kutoka mfuko wa Consolidated Holdings Corporation
iv. Kuwalipa wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira mafao yao na stahiki zao kwa wafanyakazi ambao CAG alithibitisha kuwa hawakulipwa
v. Serikali kukamilisha haraka zoezi la kukabidhiana mgodi huo
vi. Serikali
kueleza kigezo kilichotumika kuwalipa viongozi waandamizi kiasi cha
shilingi milioni 80 wakati wafanya kazi wa kati walilipwa kati ya
shiligi milioni 8 na wafanya kazi wa chini wakilipwa shilingi milioni
moja na nusu.
Mheshimiwa
Spika, jambo lingine ambalo halijafanyiwa kazi lilikuwa ni hili la
malipo yaliyolipwa mara mbili, kwa mjibu wa hansard za bunge , maoni ya
wabunge yalikuwa ni … “niligusie hili la dola milioni nne na laki nane
na sitini na tano ambazo ni sawa na bilioni tano na laki sita, serikali
imekiri…imefanya double payment jambo ambalo ni kosa la jinai, …
mwenzangu anadai tuachane nayo, haiwezekani” lakini katika hali ya
kustaajabisha hadi hivi leo haijulikanai hatima ya fedha hizo
zilizolipwa mara mbili. Ni maoni ya kambi rasmi ya upinzani kuwa
serikali ihakikishe maoni yote yanafanyiwa kazi , fedha za walipa kodi
haziwezi kupotea hivihivi kwa wajanja wachache.
Kambi rasmi ya Upinzani, inataka maelezo ya kina kuhusiana na mambo yafuatayo;
i. Fedha za
mwaka jana zilitengwa Bilioni 40 na zilitumika Bilioni 28 kulipa fidia,
je fedha hizo alilipwa nani na zilikuwa ni kwa ajili gani?
ii. Mwaka huu tumetenga tena bilioni 20 je, ni kwa ajili ya kuendelea kufidia ufisadi huu ? au ni kwa ajili ya kazi gani?
7.0 HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Maoni
yetu juu ya mapitio ya utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka 2012/2013 na
makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2013/2014 yanaonyesha
kwamba chanzo cha hali tuliyonayo hivi sasa ni cha muda mrefu. Bunge la
tisa likiongozwa na Spika Samuel Sitta halikuweza kukamilisha
kurekebisha hali hiyo, ikiwemo kukwepa kukamilisha kwa wakati maazimio
ya Bunge ya mwaka 2010. Bunge la kumi, likiongozwa na Spika Anna Makinda
katika kipindi chake cha kwanza cha miaka miwili na nusu, halijaweza
kukamilisha utekelezaji wa maazimio ya mwaka 2008 na maazimio yake ya
mwaka 2011 na 2012. Bunge hili, bado linalo nafasi ya kurekebisha hali
hii kuanzia sasa katika kipindi chake cha miaka miwili na nusu
iliyobaki.
Mheshimiwa Spika, mwalimu nyerere katika kitabu chake cha TUJISAHIHISHE ukurasa wa pili (2) aya ya 4 kinasema nanukuu “Makosa
yetu mengine hutokana na woga; woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa japo
tunajua kuwa kakosa,au kumtetea mdogo anayelaumiwa na wakubwa japo
tunajua kuwa hana makosa. Na msingi wa woga pia ni unafsi. Pengine
twaweza kuwa hatuna cheo cochote ambacho tunaogopa kupoteza; pengine
huwa hatuna wala tama yoyote ya kupata cheo Fulani. Lakini woga unaweza
kutokana na tamaa ya kila bindamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi
wote tunayo tama hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza
ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio
wengi kwa walio wachache, au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa
kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha,
wasije wakatuchukia. Huu ni unafsi mbaya sana. Ni kweli kwamba
demokrasia haiwezi kudumu ikiwa wachache hawatakubali matakwa ya wengi,
lakini matakwa ya wengi hujulikana katika majadiliano au mazungumzo ya
wazi wazi.
Mheshimiwa Spika, lakini pia katika ukurasa wa tatu (3) aya ya pili anasema nanukuu“Kadhalika,
matakwa ya wachache hujulikana katika majadiliano na na mazungumzo.
Bila wale wachache kusema wazi wazi matakwa yao, majadiliano hayana
maana. Wakati mwingine, hata baada ya majadiliano, wachache japo
wamekubali kutii uamuzi wa wengi wanaweza kuendelea kuamini kwamba
mawazo yao ni sawa, na ya walio wengi yamepotoka. Demokrasia inawapa
haki, na ukweli unawapa wajibu wa kuendeleza mawazo yao mpaka wengi
waone kuwa ni ya kweli.Bila hivyo maendeleo katika mawazo hayawezekani,
kwani mara nyingi wazo zuri hutokana na mtu mmoja tu. Mwanzo laweza
likapigwa, pengine kwa nguvu kabisa,na walio wengi, lakini hatimaye
wengi hulikubali. Huu ndio msingi wa maendeleo katika mawazo ya
binadamu”.
Mheshimiwa Spika, Katika
sekta za Nishati na Madini, kama ilivyo katika sekta nyingi nchini;
tumefika hapa tulipo kwa sababu ya udhaifu wa Serikali inayoongozwa na
Rais Kikwete, uzembe wa Bunge na ulegelege wa CCM. Kambi Rasmi ya
upinzani inayoongozwa na CHADEMA inataka kama taifa; TUBADILIKE,
TUWAJIBIKE, TUJISAHIHISHE.
Mheshimiwa Spika, Naomba kuwasilisha.
John John Mnyika(Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-
Wizara ya Nishati na Madini
22.05.2013
No comments:
Post a Comment