SOMA HOTUBA YOTE YA SUGU ALIYOISOMA LEO BUNGENI NA KUFANYA BUNGE KUHAIRISHWA
Penulis : mtandao-net on Monday, May 20, 2013 | 2:15 PM
MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA JOSEPH O. MBILINYI (MB) KUHUSU
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI
NA MICHEZO KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya kanuni za Bunge toleo la mwaka 2013)
1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Dira ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni “kuwa na taifa
lililohabarishwa vizuri, lina vijana wenye uwezo na malezi bora,
linathamini utamaduni wake na linakuwa mahiri katika michezo ifikapo
mwaka 2025.” Aidha, ‘dhamira’ ya wizara hii ni ‘kuendeleza utambulisho
wa taifa kwa kuwezesha upatikanaji mzuri wa habari, kuwawezesha vijana
kiuchumi na kukuza utamaduni na michezo kwa umma kwa maendeleo ya
kijamii na kiuchumi.’
Mheshimiwa Spika,
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Serikali hii ya CCM
imeshindwa kutekeleza dira na dhamira iliyotajwa katika maandiko ya
kisera ya Wizara. Badala yake, chini ya usimamizi wa Wizara hii,
Tanzania imegeuka kuwa taifa lisilotaka watu kuhabarishwa vizuri juu ya
matendo ya watawala. Tanzania imegeuka kuwa taifa linalofungia magazeti
yanayofichua ufisadi, uchafu na matumizi mabaya ya madaraka miongoni mwa
viongozi, watendaji na watumishi wa Serikali hii ya CCM. Tanzania
imegeuka, chini ya usimamizi wa Wizara na Serikali hii ya CCM, kuwa
taifa linaloteka nyara wanahabari, kuwatesa kwa kuwang’oa kucha na meno,
kuwatoboa macho, kuwamwagia tindikali na hata kuwaua. Tanzania sio nchi
inayoandaa vijana wake tena. Haiwapi tena elimu bora wala kuwapatia
maarifa, uwezo na malezi bora; ni nchi isiyowawezesha wala kuwathamini
vijana wake; ni nchi inayoruhusu vijana wake kunyonywa na kutoendelezwa;
na ni taifa ambalo limeachia utamaduni utambulisho wake kama taifa
kupotea kabisa. Aidha, katika fani ya michezo ya aina zote, Tanzania
imeporomoka kutoka taifa lililokuwa linaheshimika kimataifa katika miaka
ya sabini na kuwa alichokiita rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ‘kichwa
cha mwendawazimu’ ambacho kila kinyozi anajifunzia kunyolea!
2. UHURU WA UHARIRI NA USALAMA WA WANAHABARI
Mheshimiwa Spika,
Kwa masikitiko makubwa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalitaarifu
Bunge lako tukufu kwamba sasa Tanzania imeingia rasmi katika orodha ya
fedheha (The List of Shame) ya mataifa ambayo taaluma ya habari ni
taaluma ya hatari kwa wale wote wanaoitumia kama sehemu ya wajibu wao
kwa taifa na kama ajira yao. Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Kulinda
Waandishi wa Habari Ulimwenguni (the Committee to Protect Journalists -
CPJ) iliyotolewa mwaka huu 2013, kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa
CPJ mwaka 1992, Tanzania imeingizwa kwenye orodha ya nchi 20 ambazo ni
hatari kwa waandishi wa habari kufanya kazi zao kutokana na hatari ya
kuuwawa kwa mwaka 2012 (20 Deadliest Countries in 2012). Kwa mujibu wa
taarifa hiyo, ilishikilia nafasi ya 7 ulimwenguni kati ya nchi 20
zinazoongoza kwa kuhatarisha maisha ya waandishi wa habari.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa taarifa ya CPJ, tishio kubwa kwa waandishi wa habari
duniani ni kuuwawa kwa kutekwa na kuteswa na/au kutishiwa maisha. Aidha,
Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama ni washiriki wakubwa wa
mauaji ya waandishi wa habari. Kwa mujibu wa takwimu za CPJ, kati ya
waandishi waliouwawa mwaka 2012, karibu ya 20% waliuwawa ama na maafisa
wa serikali au na majeshi yake. Karibu idadi hiyo hiyo ya waandishi wa
habari waliuawa kwa sababu ya kufuatilia taarifa za kiuchunguzi na za
hatari. Taarifa hiyo inaonyesha kwamba hadi kufikia Aprili 2013,
waandishi wa habari wapatao 30 tayari wamekwishauawa ulimwenguni wakati
wakitimiza wajibu wao; wakati mwaka 2012 waandishi wa habari 103
waliuwawa ulimwenguni kote.
Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya CPJ inaungwa mkono na ushahidi wa matukio mengi
yanayodhihirisha kwamba maisha ya waandishi wa habari wa Tanzania yako
hatarini kutokana na vitendo na vitisho kutoka kwa Serikali na watendaji
wake ambao hawataki kusikia ukweli dhidi yao ukianikwa hadharani.
Kudhihirisha kauli hii tunaomba kumnukuu mwanahabari mahiri na mmoja wa
wahanga wa vita dhidi ya wanahabari na uhuru wa habari hapa nchini, Mzee
Ndimara Tegambwage:
“Mwaka 2006, waliojiita wananchi wakazi wa jiji la Mwanza, walikusanywa
na wenye uwezo kufanya maandamano makubwa kwa walichoita ‘kupinga
mwandishi Richard Mgamba kuandika uongo’ na kudai kwamba alikuwa Mkenya
na ‘siyo raia wa Tanzania.’ Desemba 2009, mwandishi Frederick Katulanda
wa Mwanza, alivamiwa nyumbani. Wavamizi walikuwa wakipaza sauti na kudai
kuwa ana nyaraka za akaunti za benki za Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Walikuwa na mapanga. Walikuwa wakichagizana kwa kusema, “Kata kichwa!
Kata kichwa!” Waliondoka na mafaili. Walimwachia kilema mguuni na makovu
mikononi.
“Mwezi Septemba, 2010 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, katika eneo la
Nyambiti, Jimbo la Sumve wilayani Kwimba, mkoani Mwanza, mwandishi
Frederick Katulanda alivamiwa na kupigwa na watu wapatao 15 waliojiita
“Green Guard” - wa “chama cha kijani.” Katika “kumshughulikia,”
Katulanda anasema, walikuwa wakionyesha kuwa na ujuzi mkubwa wa judo na
karate huku wakidai kuwa anawaandika ‘vibaya’ Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Mwaka 2011 mwandishi Richard Massatu alikutwa amekufa katika eneo la
Igoma, jijini Mwanza. Vyombo vya habari viliripoti kuwa macho yake
yalikuwa yametobolewa na kuwekwa gundi aina ya super glue; mguu wa
kushoto na mbavu vilikuwa vimevunjika. Vyombo vya habari viliripoti kuwa
Massatu aliyekuwa mmiliki na mhariri mkuu wa gazeti la Kasi Mpya (sauti
ya umma), alionekana mara ya mwisho usiku wa kifo chake akiwa na
maofisa wa polisi na usalama katika baa iitwayo Cross Park katika eneo
la Igoma.
“Tarehe 3 Januari, maiti ya mwandishi Issa Ngumba iliokotwa katika pori
la mlima Kajuruheta, kijiji cha Mhange, wilayani Kakonko katika mkoa wa
Kigoma.Ngumba alikuwa mwandishi wa habari wa Redio Kwizela. Tangu mwezi
uliopita Machi, mwandishi wa habari Erick Kabendera anayeishi Dar es
Salaam, anaishi kwa wasiwasi. Wazazi wake waishio Bukoba, wamehojiwa na
‘ofisa usalama’ kwa kile kilichoitwa ‘uhalali wa uraia wao.’
“Kuuwawa kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Luninga cha ITV,
John Lubungo ambaye alikuwa mfuatiliaji mahiri wa habari zinazohusu
wafanyabiashara au biashara haramu ya dawa za kulevya ambayo inadaiwa
kufanywa na watu wakubwa nchini, wakiwemo vigogo serikalini. Kuna orodha
ndefu ya waandishi wa habari waliotishwa na wanaoendelea kutishwa;
waliopigwa na polisi na askari magereza (Ukonga, Dar es Salaama) kwa
tuhuma mbalimbali; waliotishiwa maisha kwa simu na hata kwa kufuatiliwa
na watu wasiowafahamu.”
Kwa sababu ya uadilifu na kutopenda kujikweza, Mzee Tegambwage hakutaja
shambulio la tindikali na mapanga dhidi yake na mwandishi mwenzake Saed
Kubenea wa gazeti la Mwanahalisi, ambalo baadae lilifungiwa na Serikali
hii ya CCM.
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yake wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Katiba na
Sheria ya tarehe 3 Mei mwaka huu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
ilielezea kwa kirefu jinsi ambavyo Serikali hii ya CCM imekuwa tishio
kwa maisha ya waandishi wa habari na kwa uhuru wa habari katika nchi
yetu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilirejeaRipoti ya Timu Maalum ya
Uchunguzi Iliyoteuliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF) Kuchunguza Mazingira Yaliyopelekea Kuuawa kwa
Mwandishi wa Habari Daudi Mwangosi Septemba 2, 2012 Katika Kijiji cha
Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani Iringa, iliyotolewa na Baraza la
Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), taasisi
mbili huru zinazojihusisha na masuala ya habari Tanzania.
Kwa mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, matokeo ya uchunguzi wao “...
yanadhihirisha bila wasi wasi kwamba polisi kwa makusudi waliwavurumisha
waandishi waliotoka Iringa wakati wakikusanya habari za shughuli za
CHADEMA katika kijiji cha Nyololo. Zaidi ya hapo, Daudi Mwangosi
mwenyewe aliuawa akiwa mikononi mwa polisi huku wakisimamiwa moja kwa
moja na Kamanda (wa Polisi wa Mkoa wa Iringa SACP Michael) Kamuhanda.”
Ripoti hiyo inaelezea jinsi Marehemu Mwangosi alivyouawa: “Alipoangalia
nyuma, Daudi Mwangosi aliona kikundi cha polisi wakimpiga mwandishi mkuu
wa gazeti la Nipashe wa Iringa, Godfrey Mushi.... Wakati mwandishi
Godfrey Mushi akiwa bado anapigwa na polisi, marehemu Mwangosi
aliwakimbilia akiwaomba waache kumdhuru zaidi Mushi kwa kuwa alikuwa
mwandishi tu. Polisi hawakumsikiliza. Badala yake wakamburuta mwandishi
huyo ambaye tayari alikuwa amepoteza fahamu na kumweka kwenye gari lao
na wakamgeukia Daudi Mwangosi mwenyewe, wakampiga kwa nguvu mpaka
akapoteza fahamu.”
Hata amri ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Mafinga Mwampamba kuwataka askari
polisi waache kumpiga marehemu Mwangosi haikusikilizwa na askari hao.
Ili kujiokoa, marehemu Mwangosi alimkumbatia OCS Mwampamba na “baadaye
kumwangukia miguuni mwake kuepuka kipigo zaidi.” Kwa mujibu wa Ripoti ya
MCT/TEF, “picha za mgando zinaonyesha polisi mmoja akipiga bomu la
machozi tumboni mwa marehemu Mwangosi kwa karibu kabisa.” Bomu hilo
liliusambaratisha mwili wa marehemu Mwangosi aliyekufa papo hapo. Kwa
sababu marehemu Mwangosi alikuwa chini ya miguu ya OCS Mwampamba, “naye
pia alijeruhiwa vibaya.”
Mheshimiwa Spika,
Sio MCT/TEF pekee zilizofanya uchunguzi wa mauaji ya Marehemu Mwangosi.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nayo ilitoa Taarifa ya Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Uchunguzi wa Tukio Lililopelekea
Kifo cha Daudi Mwangosi Kilichotokea Septemba 2, 2012 Kijijini Nyololo,
iliyobaini kwamba Marehemu Mwangosi “... alizingirwa na askari, aliteswa
na hatimaye ... alipigwa bomu na kufa papo hapo.” Aidha, kwa mujibu wa
Taarifa hiyo, “... Tume imejiridhisha kuwa tukio la lililopelekea kifo
cha Daudi Mwangosi limegubikwa na uvunjwaji wa haki za binadamu na
ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.” Taarifa ya Tume inafafanua kuwa,
“... Tume imejiridhisha kuwa Jeshi la Polisi limevunja haki ... ya
kuishi, haki ya kutoteswa na kupigwa, haki ya usawa mbele ya sheria na
haki ya kukusanyika na kutoa maoni.”
Mheshimiwa Spika,
Siku moja baada ya mauaji ya Daudi Mwangosi, Jeshi la Polisi lilianza
kampeni kubwa ya kujaribu kuficha ukweli juu ya kuhusika kwake, kwa
kuhamishia lawama kwa watu wengine wasiohusika na mauaji hayo. Kwa
mfano, Kamanda Kamuhanda alinukuliwa na vyombo vya habari akidai kwamba
marehemu Mwangosi alifariki “kutokana na kitu kizito kilichotupwa na
waandamanaji.” Aidha, siku iliyofuata Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la
Polisi Paul Chagonja alidai kwamba baada ya ghasia kudhibitiwa,
marehemu Mwangosi alikimbilia walipokuwa polisi na “kitu kama bomu
kikarushwa na kundi la watu wanaokimbia hovyo na kumlipua Mwangosi.”
Njama hizi za kuficha ukweli zimeumbuliwa na Ripoti ya MCT/TEF
inayobainisha kwamba marehemu Mwangosi “aliuawa chini ya usimamizi wa
moja kwa moja wa RPC Michael Kamuhanda.” Ripoti hiyo pia imeelezea kwa
kirefu jinsi Jeshi la Polisi lilivyotoa taarifa zinazokinzana juu ya
kuhusika kwake na mauaji ya Mwangosi. Hivyo, kwa mfano, wakati Waziri wa
Mambo ya Ndani Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi alidai tarehe 4 Septemba
2012 kwamba marehemu aliuawa na bomu la machozi ambalo ‘halikulipuliwa
kitaalamu na polisi’, Kamanda Kamuhanda alitokea kwenye televisheni siku
iliyofuata “akitangaza habari za kuwatupia lawama wafuasi wa CHADEMA
kwa kutupa kitu kizito kilicholipuka na kumuua Mwangosi....”
Mheshimiwa Spika,
Hata Taarifa ya Uchunguzi wa Kifo cha Mwandishi wa Habari wa Channel Ten Bw. Daudi Mwangosi,
iliyoandaliwa na Kamati iliyoundwa na Mheshimiwa Nchimbi na kuongozwa
na Jaji Stephen Ihema imethibitisha kuhusika kwa Jeshi la Polisi na
mauaji ya Marehemu Mwangosi. Baada ya kuzunguka huku na huko ikijaribu
kulisafisha Jeshi la Polisi kutoka kwenye lawama ya kumuua Marehemu
Mwangosi, Taarifa ya Kamati hiyo inasema: “Hapakuwepo na uhalali wa
kutumia Bomu la Kishindo kwani lengo la ulipuaji wake ni ili watu
waogope na kukimbia.” Aidha, Kamati hiyo inakiri kwamba “hapakuwepo
umuhimu wa kutumia Bomu la Kishindo kwa sababu hata ingekuwa ukamataji
tayari askari polisi wapatao sita walikuwepo eneo la tukio.” Kwa misingi
hiyo, “… Kamati imeona kwamba … tukio la kuuawa Bw. Daudi Mwangosi na
kuumizwa baadhi ya askari polisi halikustahili kabisa.”
Mheshimiwa Spika,
Kuna uthibitisho mkubwa kwamba Serikali hii ya CCM na Jeshi la Polisi
wamekuwa wanawalenga kuwaua au kuwaumiza waandishi wa habari wanaoandika
zisizowapendeza viongozi wa Serikali au Jeshi la Polisi. Kwa mfano,
Ripoti ya MCT/TEF inaashiria kuwa sababu ya Marehemu Mwangosi kuuawa ni
kwamba yeye “... ndiye mwandishi pekee aliyemuuliza RPC (Kamuhanda)
‘maswali magumu’ kiasi cha kumkera kiongozi huyo wa jeshi la polisi.”
Ripoti hiyo inafafanua kwamba “baada ya mkutano huo na waandishi, ...
baadhi ya polisi ... waliwaonya wasiende Nyololo kwa ajili ya kukusanya
habari za shughuli za kisiasa za CHADEMA kutokana na uwezekano wa
kutokea kwa hali hatarishi.” Aidha, “baada ya mkutano wa waandishi wa
habari wa asubuhi katika ofisi za RPC (Kamuhanda), ... askari mmoja
mpelelezi alimfuata Mwangosi na kumwambia: ‘Ina maana gani kwenda
Nyololo kuandika habari za Chadema ambazo zinaweza kuishia na kifo
chako?’” Vile vile, Ripoti ya MCT/TEF inabainisha, ni “... wazi kwamba
Polisi walikuwa wanawawinda waandishi wa Iringa ambao walikuwa
wakiwajua.”
Mheshimiwa Spika,
Siku tatu baada ya mauaji ya Daudi Mwangosi, Mkurugenzi wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai katika Jeshi la Polisi Robert Manumba alitoa kauli kwa
vyombo vya habari kuhusu matukio ya kuuawa kwa waandishi wa habari
ambapo alisema “….matukio ya aina hii yapo na yataendelea kuwepo.”
Katika kuthibitisha kwamba Serikali hii ya CCM ina sera isiyo rasmi ya
kulenga kuwadhuru waandishi wa habari wanaowaandika watawala vibaya na
hata kuwaua, kauli ya DCI Manumba imerudiwa tena na Mkuu wa Mkoa wa
Arusha Magessa Mulongo wakati wa sherehe za Mei Mosi mwaka huu jijini
Arusha. Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Mkuu huyo wa Mkoa
aliwatahadharisha waandishi kwa kuwaambia kwamba “unapoingia katika
mkakati wa kumdhalilisha kiongozi wa Serikali unaiweka roho yako
rehani…. Kuweni makini.”
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yake kwenye mjadala wa Wizara ya Katiba na Sheria, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni iliyaita matamshi ya DCI Manumba na Mkuu wa
Mkoa Mulongo kuwa ni ‘matendo ya kigaidi’ kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia
Ugaidi, 2002, ambayo inafafanua ‘matendo ya kigaidi’ kuwa ni pamoja na
vitisho vinavyohusu mtu kusababishiwa maumivu au majeraha makubwa
kimwili, kuhatarisha maisha ya mtu na vinavyohusu usalama wa umma
ambavyo vimelengwa au ambavyo kwa hulka au muktadha wake vinaonekana
vimelengwa kutishia umma au sehemu ya umma.
Kwa mara nyingine tena Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali
kutoa kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama tafsiri hiyo ya
Sheria ya Kuzuia Ugaidi ni sahihi au la. Na kama ni sahihi, Kambi Rasmi
ya Upinzani inataka kujua ni kwa nini DCI Manumba na Mkuu wa Mkoa
Mulongo bado hawajakamatwa na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi hadi sasa?
Kama tafsiri hiyo sio sahihi, basi Serikali hii ya CCM itamke mbele ya
Bunge lako tukufu kwamba ni sera yake rasmi kwamba waandishi wa habari
wanaoiandika Serikali au viongozi wake vibaya ‘wanaweka roho zao
rehani’!
Mheshimiwa Spika,
Kauli ambazo zimetolewa na Serikali hii ya CCM ndani ya Bunge lako
tukufu zinathibitisha kuhusika kwa Serikali katika, kama sio kupanga
basi angalau kubariki, mauaji yanayofanywa na vyombo vya usalama vya
Serikali kwa waandishi. Na moja ya kauli za Serikali ambazo
zimeifadhaisha na kuisikitisha sana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni
ile iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Serikali na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge, Mh. William Lukuvi pale alipomsifu
Kamanda Kamuhanda wakati wa mjadala wa Wizara ya Mambo ya Ndani: “Katika
kitabu hiki cha Kambi ya Upinzani, wamekutaja sana (Kamuhanda),
hawawezi kukupongeza. Huko Iringa Kamanda unafanya kazi nzuri sana,
usitetereke na makamanda wako wa huko Iringa.”
Ikumbukwe, Mheshimiwa Spika, kwamba mtu anayesifiwa kwa ‘kufanya
kazi nzuri sana kule Iringa’ ni yule yule ambaye aliyelaumiwa na Tume ya
Haki za Binadamu – ambayo Makamishna wake wote ni wateule wa Rais kwa
mujibu wa Katiba – kuwa alikiuka sheria za nchi yetu na misingi ya
utawala bora kufuatia tukio la mauaji ya Marehemu Mwangosi! Mtu
anayeshauriwa na Waziri Lukuvi kwamba ‘asitetereke’ ni yule yule ambaye
MCT/TEF imemhusisha na usimamizi wa moja kwa moja wa mauaji ya Mwangosi.
Needless to say, mtu huyu bado yuko huru na hajachukuliwa hatua yoyote licha ya mshangao mkubwa kitaifa na kimataifa!
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi
mbele ya Bunge lako tukufu kama kauli ya Mheshimiwa Lukuvi kuhusu
kuhusika kwa Kamanda Kamuhanda na Jeshi la Polisi katika mauaji ya
Marehemu Mwangosi ndio msimamo rasmi wa Serikali hii ya CCM. Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kuliambia
Bunge lako tukufu ni nini msimamo wake rasmi juu ya Taarifa ya Tume ya
Haki za Binadamu na Ripoti ya MCT/TEF kuhusu kuhusika kwa Jeshi la
Polisi na Kamanda Kamuhanda katika mauaji ya Marehemu Mwangosi. Kwa
maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kimya cha Serikali hii ya CCM
juu ya maswali haya muhimu ni ushahidi dhahiri kuwa mauaji haya ni
sehemu ya mkakati ulioasisiwa na Serikali hii ya CCM wa kuwanyamazisha
waandishi wa habari kwa nia moja tu: kufifisha uhuru wa kupata na kutoa
habari muhimu zinazohusika kashfa za ufisadi na matumizi mabaya ya
madaraka serikalini.
Mheshimiwa Spika,
Miezi sita baada ya Jeshi la Polisi kumuua Daudi Mwangosi, mwandishi
mwingine mwandamizi na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),
Absalom Kibanda, alitekwa nyara na kuteswa vibaya nje ya nyumba yake
baada ya nyendo zake kufuatiliwa na polisi na watu wengine wanaodhaniwa
kuwa watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS). Badala ya
kuchukua hatua za dhati kuwachunguza na kuwakamata wale wote
waliohusika na tukio hilo la kigaidi, Jeshi la Polisi likishirikiana na
Idara ya Usalama wa Taifa, maafisa waandamizi katika Ofisi ya Rais Ikulu
na viongozi waandamizi wa CCM chini ya Naibu Katibu Mkuu wake
Mheshimiwa Mwigulu Nchemba na baadhi ya waandishi habari maslahi,
walianzisha kampeni kubwa ya kuipakazia CHADEMA na Mkurugenzi wake wa
Ulinzi na Usalama Wilfred Lwakatare kwa madai ya kuhusika na ugaidi
kutokana na ushahidi wa kutunga!
Mheshimiwa Spika,
Kwa vile njama dhidi ya CHADEMA na Bw. Lwakatare zimegonga mwamba baada
ya Mahakama Kuu ya Tanzania kuyatupilia mbali mashtaka ya ugaidi dhidi
yake, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kutoa
taarifa rasmi mbele ya Bunge lako tukufu juu ya waliohusika na jaribio
la kumuua Bw. Kibanda. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali hii ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu juu ya
kuhusika kwa Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Ikulu na CCM
katika kutengeneza ushahidi wa uongo dhidi ya CHADEMA na Bw. Lwakatare
ili kuwapumbaza Watanzania wasihoji shambulio la kigaidi dhidi ya Bw.
Kibanda.
Kutoa taarifa ya uongo kwa lengo la kuanzisha mashtaka ya jinai
mahakamani au kutengeneza ushahidi wa uongo kwa lengo la kuipotosha
mahakama ni makosa ya jinai yenye adhabu ya kifungo cha miaka saba kwa
mujibu wa Sheria ya Adhabu ya Tanzania. Ni muhimu kwa ukweli wa
jambo hili kujulikana sio tu kwa ajili ya kuwawajibisha kijinai
wahusika, bali pia kwa lengo la kulinda demokrasia na utawala wa sheria
katika nchi yetu. Kama alivyosema Chris Conybeare, Katibu Mkuu wa Chama
cha Mabaraza ya Habari Duniani (WAPC) katika ujumbe wake kwa Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Dk. Fenella Mukangara
juu ya mauaji ya Marehemu Mwangosi: “Waandishi wa habari wanapouawa
demokrasia pia inakufa.”
3. MAELEZO NA UHURU WA HABARI
Mheshimiwa Spika,
Idara ya Habari (MAELEZO) ilikasimiwa majukumu na mali za lililokuwa
Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA) na Sheria ya Kufuta Shirika la
Habari la Tanzania, Na. 7 ya mwaka 2000. Wakati SHIHATA ilikuwa na
ukiritimba wa kukusanya habari pamoja na mamlaka ya kusajili waandishi
wa habari, ukiritimba huo na mamlaka ya usajili wa waandishi wa habari
yalifutwa kabisa kama sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa Tanzania, 1991 (‘Tume ya Nyalali’), iliyobaini kwamba Sheria ya SHIHATA ilikuwa inakiuka misingi ya uhuru wa mawazo na uhuru wa habari.
Kwa sababu hiyo, majukumu mapya ya Idara ya Habari, kama
yalivyofafanuliwa katika kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Kufuta SHIHATA,
ni pamoja na kutoa, kuendeleza na kuhamasisha uanzishwaji na uendeshaji
wa za kukusanyia na kusambaza habari; kukusanya na kusambaza habari na
kuishauri Serikali juu ya masuala yanayohusu usambazaji habari na
utendaji wa mashirika ya habari. Idara ina ofisi katika baadhi ya mikoa
ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika,
Tofauti na SHIHATA, Idara ya Habari haina na haijawahi kupewa jukumu la
kisheria la kuwa msimamizi wa vyombo vya habari na wanahabari nchini.
Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa SHIHATA, Idara hii imekuwa inawauzia
waandishi wa habari vitambulisho (press cards) ambavyo vimekuwa
vinatumika kama vitambulisho cha kazi kwa waandishi wa habari hapa
nchini. Vitambulisho hivyo vimekuwa vinauzwa kwa shilingi za Tanzania
elfu ishirini, lakini Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina taarifa kwamba
bei ya vitambulisho hivyo imepanda mwaka huu hadi kufikia shilingi elfu
thelathini. Aidha, vitambulisho hivyo hutolewa kila mwaka katika Ofisi
za MAELEZO Dar es Salaam na hivyo kusababisha gharama na usumbufu mkubwa
kwa waandishi wa habari walioko mikoani.
Mheshimiwa Spika,
Vitendo hivi vya Idara ya Habari ni kinyume cha Sheria ya Kufuta
SHIHATA. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali hii ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu Idara ya
Habari imetoa wapi mamlaka ya kusajili waandishi wa habari kwa
kuwalazimisha kununua vitambulisho vya uandishi habari. Aidha, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya
Bunge lako tukufu kama kuna masharti yoyote ya kisheria yanayolazimu
waandishi wa habari wasajiliwe na MAELEZO kwa kupatiwa vitambulisho vya
kazi na Idara hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Sio tu kwamba Idara ya Habari imejitwalia mamlaka ya kusajili waandishi
wa habari kwa kuwalazimisha kununua vitambulisho vya taaluma yao, lakini
pia imeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa kupanuka kwa demokrasia na
uhuru wa habari katika nchi yetu. Historia yake inaanzia miaka ya mwanzo
ya utawala wa kikoloni wa Kiingereza wakati walipotunga Sheria ya
Magazeti ya 1928. Chini ya Sheria hiyo, wakoloni walidhibiti ukuaji wa
vyombo vya habari vya wenyeji wa Kiafrika kwa kuviwekea masharti ya
kusajiliwa baada ya kutoa dhamana ya fedha taslimu.
Marekebisho ya Sheria hiyo yaliyofanywa mwaka 1952 yaliweka masharti
magumu zaidi ya usajili wa magazeti pamoja na kuongeza kiwango cha
dhamana kutoka pauni za Kiingereza 160 hadi pauni 520. Kwa mujibu wa
Martin Sturmer katika kitabu chake The Media History of Tanzania,
wakati magazeti ya Wamisionari na yale yaliyokuwa yanaunga mkono sera
za utawala wa kikoloni katika Tanganyika hayakudaiwa kulipa dhamana,
magazeti yaliyokuwa na mrengo wa upinzani wa sera za dola ya kikoloni
yalilazimika kulipa dhamana hiyo.
Baadae mwaka 1955 dola ya kikoloni iliongeza udhibiti zaidi wa vyombo
vya habari kwa kuingiza katika Sheria ya Adhabu vifungu vipya
vilivyokataza uchapishaji wa jambo au taarifa yoyote lenye uwezo wa
kuleta chuki dhidi ya serikali ya kikoloni au watendaji wake. Kama
anavyosema Sturmer, kutokea hapo sheria hiyo ya uchochezi ndio imekuwa
kizingiti kikubwa kwa uhuru wa magazeti katika Tanzania. Haiwezi kuwa
ajabu kwamba wahanga wa kwanza wa sheria hiyo ya uchochezi walikuwa
mabwana Kheri Rashidi Baghdelleh na Robert Moses Makange waliokuwa
wahariri wa gazeti la Mwafrika; na mhariri wa gazeti la Sauti ya TANU aliyejulikana kama Julius Kambarage Nyerere!
Mheshimiwa Spika,
Kitu cha ajabu ni kwamba sheria iliyotungwa na wakoloni wa Kiingereza
kwa lengo la kuwadhibiti wenyeji wa Kiafrika wasidai uhuru au kuanika
uchafu na uonevu wa dola ya kikoloni haikufutwa mara baada ya uhuru.
Badala yake, sera za habari za dola ya uhuru sio tu zilipokea na
kuzidisha masharti ya kisheria dhidi ya uhuru wa habari kwa kutunga Sheria ya Magazeti
ya mwaka 1976 iliyoongeza makali ya sheria ya uchochezi, bali pia
zilitaifisha magazeti na vyombo vingine vya habari binafsi vilivyokuwepo
wakati wa uhuru.
Hivyo, kwa mfano, Shirika la Utangazaji la Tanganyika (TBC)
lilitaifishwa kwa Sheria ya Bunge ya tarehe 16 Machi 1965 na kubatizwa
jina jipya la Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Aidha, tarehe 5
Februari, 1970, gazeti binafsi la The Standard lilitaifishwa na Serikali. Na ilipofika tarehe 26 Aprili, 1972, The Daily News,
gazeti jipya la Serikali lilianzishwa kwa kuunganisha The Standard na
gazeti la The Nationalist lililokuwa linamilikiwa na TANU. Hivyo basi,
kama anavyosema Sturmer katika historia yake ya vyombo vya habari
Tanzania, “kufikia mwaka 1976 Serikali ya Nyerere ilishafanikisha lengo
lake kuu la sera ya habari – kuwa na udhibiti juu ya vyombo vyote vikuu
vya habari....”
Mheshimiwa Spika,
Utaratibu huu wa udhibiti juu ya vyombo vya habari kwa kutumia Sheria ya Magazeti
ulishambuliwa na Tume ya Nyalali kwa kukiuka matakwa ya ibara ya 18 ya
Katiba inayotoa uhuru wa mawazo na uhuru wa habari. Kwa maneno ya Tume
hiyo, Serikali inakiuka uhuru wa mawazo na wa habari “... kwa
kujihusisha na kuchuja habari zinazotolewa kwa wananchi.” Tume
ilipendekeza marekebisho makubwa katika Sheria ya Magazeti “... ili
kuruhusu uhuru mkubwa zaidi wa habari na wa mawazo na kulegeza uchujaji
wa habari.” Mapendekezo haya ya Tume ya Nyalali hayajatekelezwa hadi leo
hii, zaidi ya miaka ishirini na mbili tangu Tume hiyo iwasilishe
Taarifa yake kwa Rais Ali Hassan Mwinyi.
Mheshimiwa Spika,
Wakati Tanzania imebakia mateka wa sera za habari za kikoloni na za
utawala wa kiimla wa chama kimoja, jirani zetu wa Kenya na marafiki zetu
wa Zimbabwe wamepiga hatua kubwa katika kupanua uhuru wa habari. Hivyo,
kwa mfano, Katiba Mpya ya Jamhuri ya Zimbabwe iliyopitishwa kwa kura ya
maoni ya wananchi wa nchi hiyo mwezi Februari mwaka huu inatoa uhuru wa
mawazo ambao unajumuisha uhuru wa kutafuta, kupokea na kusambaza mawazo
na habari nyingine; uhuru wa mawazo ya kisanii na wa utafiti wa
kisayansi na uhuru wa taaluma.
Aidha, Katiba hiyo inatoa uhuru wa habari ambao ni pamoja na ulinzi wa
vyanzo vya habari vya waandishi wa habari; na uhuru wa uanzishaji wa
vyombo vya utangazaji ambavyo havitakiwi kuwa chini ya udhibiti wa
serikali au maslahi ya kisiasa au kibishara. Vile vile, Katiba Mpya ya
Zimbabwe inavilazimu vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Serikali kuwa
huru kuamua mambo gani ya kutangaza; kutokupendelea na kutoa fursa sawa
kwa ajili ya kutangaza maoni tofauti na mawazo yanayokinzana.
Mheshimiwa Spika,
Katiba Mpya ya Zimbabwe inatoa pia uhuru wa taarifa (access to
information). Hivyo, kwa mfano, kila raia au mkazi wa kudumu wa
Zimbabwe, ikiwa ni pamoja na makampuni na vyombo vya habari, ana haki ya
kupatiwa taarifa yoyote inayodhikiliwa na Serikali au na taasisi au
shirika lolote la serikali katika ngazi zote, kama taarifa hiyo
inahitajika kwa ajili ya maslahi ya uwajibikaji kwa umma. Zaidi ya hayo,
kila mtu, ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari vya Zimbabwe, ana haki
ya kupatiwa taarifa inayoshikiliwa na mtu yeyote, pamoja na Serikali,
kama taarifa hiyo inahitajika kwa ajili ya kufurahia au kulinda haki
yake. Kama ilivyo kwa Zimbabwe, Katiba Mpya ya Kenya nayo pia imetoa
uhuru mpana wa habari kwa wananchi wa Kenya.
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ni fedheha kwamba nchi
yetu iliyokuwa ya kwanza kupata uhuru katika ukanda wa Afrika Mashariki,
Kati na Kusini inaelekea kuwa ya mwisho katika masuala ya uhuru wa
habari kwa watu wake. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali
hii ya CCM kulieleza Bunge lako tukufu ni lini italeta muswada wa sheria
kwa lengo la kufuta urithi huu wa fedheha wa sheria za kikoloni ili
Tanzania iendane na karne mpya ya uhuru wa habari na wa mawasiliano.
Mheshimiwa Spika,
Kwa sasa vyombo vya habari vya Serikali yaani, Radio na Television za
Taifa ndio vinatoa matangazo kwa wananchi kuhusu kile kinachoendelea
Bungeni. Kwa bahati mbaya ni kwamba Radio ya Taifa ambayo inasikilizwa
na watanzania wengi wa hali ya chini na kati katika maeneo mengi ya
mijini na vijijini wanashindwa kusikiliza mijadala inayoendelea Bungeni,
kwani matangazo yanakatishwa pindi kipindi cha maswali na majibu
kinapomalizika. Matangazo ya mjadala wa Bunge yanaendelea kurushwa
kwenye Television ya Taifa hadi Bunge linapoahirisha shughuli zake kwa
siku.
Mheshimiwa Spika,
Huku ni kutowatendea haki watanzania wengi kwa kuwapa fursa kusikiliza
nini wawakilishi wao wanachokiongea katika mijadala mbalimbali Bungeni.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaona sasa ni muda mwafaka kwa sekta binafsi
nazo kufanyakazi hiyo ambayo inaonyesha imevielemea vyombo hivyo vya
serikali na kuondoa ukiritimba uliopo wa kurusha matangazo ya Bunge.
3.2 Matangazo ya serikali kwenye vyombo vya habari
Mheshimiwa Spika,
Suala la matangazo ya serikali katika vyombo vya habari si kwamba
limekuwa likitumika kuminya uhuru wa habari katika baadhi ya vyombo vya
habari hususan vinavyoonekana kuwa vinafanya utafiti katika habari zake
kwa masuala mbalimbali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na hivyo kuweka
hadharani mapungufu na uchafu wa Viongozi waliopewa dhamana na wananchi.
Mheshimiwa Spika,
Suala hilo la matangazo badala ya kuviimarisha vyombo vya habari ili
viweze kusimama na kufanyakazi bila ya kuingiliwa, sasa linatumika kama
njia ya kufifisha uhuru wa kutafuta na kutoa habari na kuvifanya vyombo
vya habari kuachana na uhandishi wa uchunguzi na hivyo kukiuka haki za
walaji za kupata taarifa kwa mujibu wa Ibara ya katiba ya 18 (d).
Mheshimiwa Spika,
Sasa kumezuka mtindo mwingine wa kuhamishia raslimali za Serikali kwenye
chama kwa ajili ya kuiokoa CCM na wanasiasa wengine. Tutatoa mfano hai
wa hivi karibuni kabisa. Kwa wafuatiliaji wa habari katika vyombo vya
habari, bila shaka watakumbuka kuwa siku ya Mei Mosi, Gazeti la CCM
linaloitwa Uhuru, lilikuwa na kurasa 79, ikiwa ni ongezeko la karibu
mara tatu ya gazeti hilo linavyotoka kwa siku za kawaida kama halina
matangazo.
Kinachoweza kuwa kimewasikitisha wafuatiliaji makini wa masuala ya
habari ni kwamba matangazo hayo hayakuwa ya watu au kampuni binafsi
yalikuwa ni matangazo ya serikali na taasisi zake, kwa maana ya kwamba
yaligharimu mamilioni ya shilingi za walipa kodi wa Tanzania, ambayo
kimsingi yalipotumika ‘hovyo’ kama tutakavyoonesha kwa hoja hapa;
Mheshimiwa Spika,
Tatizo hapa si tu kwamba gazeti hili ni la CCM, bali pia kuna masuala ya
msingi kadhaa ambayo kwa kweli mtu yeyote makini, anayejua biashara ya
matangazo, hasa kutangaza kupitia vyombo vya habari, anapaswa kuzingatia
mara zote kabla hajaamua kutumbukiza mamilioni kwa ajili ya
kujitangaza;
Kwanza, kama chombo hicho ni gazeti, basi linapaswa kuwa na wasomaji
wengi na pia mzunguko mkubwa sokoni kwa maana ya kuwafikia watu wengi
kutokana na kusambaa maeneo mengi ndani (na nje ikibidi) ya nchi.
Mfuatiliaji yeyote makini wa vyombo vya habari anajua wazi kuwa gazeti
hilo la CCM, halina sifa hizo.
Kama serikali na taasisi zilizotumia gazeti hilo la CCM kama njia ya
kujitangaza zingekuwa makini na matumizi halali ya fedha za Watanzania,
lazima zingezingatia kanuni za kawaida kabisa; yaani kuhakikisha
wanapata wasomaji na soko kubwa katika bidhaa na huduma zao
wanazotangaza, hivyo wangepaswa kutangaza katika magazeti yanayosomwa na
yenye mzunguko mkubwa.
Mheshimiwa Spika,
Kinachoonekana hapa ni kwamba, baada ya njia nyingine za kifisadi za
kupata fedha kuisaidia CCM kushtukiwa, sasa zimebuniwa mbinu nyingine za
kifisadi za kusaka fedha kwa ajili ya chama hicho, mojawapo ikiwa ni
hii ya utoaji wa matangazo kwa vyombo vya habari vya CCM, visivyokuwa na
sifa stahili. Haya ni matumizi mabaya ya matangazo yenyewe na fedha za
umma!
Ni namna ile ile ya kutoa zabuni kwa Kampuni ya CCM, ifanye upanuzi wa
eneo la bandari kwenye eneo la CCM, bila makampuni yenye uwezo
kushindanishwa ili kupata moja iliyo makini na yenye vigezo vya kufanya
kazi husika.
3.3 TCRA NA UANGALIZI WA VYOMBO VYA HABARI VYA KIELEKTRONIKI
Mheshimiwa Spika,
TCRA ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia vyombo vya elkroniki kama Radio na
Televisdion, lakini imeshindwa kabisa kusimamia vyombo hivyo
walivyovipatia leseni ya kufanyakazi, kwani baadhi ya vituo ukisikiliza
vinafanya uchochezi wa kisiasa, kidini, ukabila wa wazi lakini vimeachwa
hadi matatizo ya udini yaliposhika kasi ndio Serikali ikaanza kukimbia
kuchukua hatua.
Mheshimiwa Spika,
Hivi sasa intaneti haitawaliwi na sheria yoyote nchini, baadhi ya
vipindi vya redio na televisheni havizingatii maadili ya Kitanzania,
maeneo mengi ya vijijini hayana huduma ya televisheni. Kambi Rasmi ya
Upinzani inasema kuwa huu ni udhaifu wa wazi kwa mamlaka hiyo iliyopewa
jukumu la kusimamia. Hivyo basi tunaitaka Serikali itoe kauli kuhusiana
na udhibiti wa TCRA katika suala hilo.
ka 2013)
3.4 SHIRIKA LA UTANGAZAJI TANZANIA (TBC)
3.4.1 TBC na matukio muhimu ya Kitaifa
Mheshimiwa Spika,Ikiwa imepita takribani miaka mitano tangu Mhe.
Raisi alipozindua rasmi Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mwezi mei
2008. Kwa kuwa, pamoja na uchakavu na ukosefu wa vifaa TBC imeweza
kupanua masafa yake ya utangazaji karibu nchi nzima ,na kwa kuwa hili ni
shirika la umma, ni matumaini makubwa kwa watanzania kuwa TBC ingekua
mstari wa mbele katika kuripoti na kutangaza matukio muhimu
yanayoendelea katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Kwa masikitiko makubwa TBC imekua nyuma katika
kuripoti matukio muhimu na badala yake imekua ikiweka vipindi
visivyoendana na matukio yanayolikabili taifa. Hii ni dharau kwa
watanzania wengi hasa ukizingatia kuwa hili ni shirika la umma na si la
mtu binafsi hivyo wajibu wake mkubwa ni kumpa taarifa mtanzania kwa
wakati hata pale inaposhindwa kutoa taarifa ama kuwepo eneo la tukio
basi lazima programu zake ziendane na hali halisi.
Mheshimiwa Spika, Kwa masikitiko makubwa wakati wa ajali ya meli
ya MV Skagkit iliyotokea mwaka jana, 2012, wakati kuna taarifa za awali
za ajali, TBC ilikua ikiweka na kupiga muziki wa taarabu bila ya
kuzingatia uzito wa ajali ile, hata siku iliyofuata kwa ajili ya
shughuli za uokoaji TBC iliendelea kuweka programu ambazo hazikuendana
na uzito wa tukio lile licha ya kuwa mamia ya watanzania walipoteza
maisha na huku tafrani ikizuka kwa baadhi ya watanzania ambao ndugu zao
walikua katika tukio lile.
Mheshimiwa Spika,Katika kuonesha kuwa TBC haijifunzi kutokana na
makosa, ama labda imekosa uongozi wenye weledi na umakini tangu kuisha
kwa ajira ya mkurugenzi wao makini Tido Muhando, mwezi wa April 2013
ambako kulikua na mlipuko wa bomu Arusha,tukio ambalo lilikuwa kubwa
kwenye historia ya nchi yetu kwani ni mara ya kwanza tukio kama hilo
kutokea, TBC iliendelea na urushaji wa matangazo na vipindi tofauti huku
televisheni na vituo vingine vya binafsi vilikuwa vinajulisha taifa
kuhusiana na tukio hilo.
Mheshimiwa Spika, Tukiwa katika mijadala ya muhimu ya mustakabali
wa taifa letu, ambapo tunajadili na kupitisha bajeti kwa ajili ya
watanzania, TBC hukata matangazo ya vipindi vya Bunge wakati
uwasilishaji wa hoja muhimu ukiendelea. Wakati wa hotuba ya Mambo ya
ndani, wakati msemaji mkuu wa kambi ya upinzani anakaribia kuanza kusoma
maoni ya Kambi ya Upinzani , TBC walikata matangazo na kuweka sherehe
za Mwenge.
Mheshimiwa Spika,Pamoja na hayo yote, TBC bado inaendelea na kauli mbiu yake ya 'Ukweli na Uhakika' kauli
ambayo haiendani na uhasilia wa uratibu wa vipindi vyake vya matangazo
na uwasilishaji wa taarifa kwa umma. Mara nyingi kwenye mijadala na hoja
nzito ambazo Serikali inakua ina hali mbaya, matangazo ya bunge hukatwa
kwa kisingizio kuwa mitambo au matatizo ya kiufundi yametokea, mbona
matangazo au hitilafu za ufundi hazitokei katika sherehe za Mwenge?Ama
hitilafu kwenye kuonesha ujio wa rais wa China ? TBC inatumika na
imeendelea kutumiwa na Serikali ya CCM katika kuminya haki ya mtanzania
ya kupata habari si kwa sababu ya ufinyu wa bajeti peke yake bali
kuwaridhisha watawala. Lazima TBC ibadilike na kujua kuwa ina dhamana
katika kupeleka habari na taarifa sahihi kwa umma kwa wakati na si kwa
kuendeshwa kama roboti.
4.0 MASUALA YA VIJANA
4.1 UUNDAJI WA BARAZA LA VIJANA LA TAIFA
Mheshimiwa Spika, suala la mchakato wa uundwaji wa Baraza la
Taifa la Vijana, sasa umekuwa si tu wimbo bali zimwi la muda mrefu
linaloiandama serikali ya CCM na imeshindwa kabisa kuepukana nalo.Sera
ya zamani ya maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 ilitamka kwamba
kutaanzishwa Baraza la Vijana na suala hilo kurudiwa katika Sera mpya ya
mwaka 2007; hata hivyo Serikali imekuwa ikiwepa kuhakikisha kwamba
matakwa hayo ya sera tajwa yanatekelezwa pamoja na kuwa suala hilo
linahusu mustakabali wa maendeleo ya vijana nchini. Kambi Rasmi ya
Upinzani inatambua kwamba katika ilani za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010
vyama mbalimbali viliahidi kuhakikisha kwamba Baraza la Vijana la Taifa
linaundwa.
Mathalani, CHADEMA katika Ilani yake 2010-2015 kipengele 6.4.1 (viii)
ilitamka “Kwa kuwa vijana ndio kundi kubwa hapa nchini, na kwa kuwa uhai
wa muda mrefu wa taifa letu upo mikononi mwa vijana, Serikali ya
CHADEMA itawezesha vijana kuunda Baraza la Vijana (BAVITA) ambalo
limekwamishwa na Serikali ya CCM kwa muda mrefu”.
CCM nayo kupitia ilani yake ya katika kipengele 80 (k) “Kuhamasisha
ushiriki wa vijana katika ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwa ni pamoja na
kukamilisha uanzishaji wa Baraza la Vijana”.Hivyo, Kambi Rasmi ya
Upinzani inatarajia kwamba wabunge wa pande zote katika suala hili la
kuanzishwa kwa Baraza la Vijana la Taifa kuungana kuwa kitu kimoja
kuisimamia Serikali itekeleze Sera na ahadi badala ya kuitetea kwa
udhaifu iliyouonyesha.
Mheshimiwa Spika; Katika Hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo juu ya mapitio ya
utekekelezaji kwa mwaka 2010/2011 na makadirio ya mapato na matumizi kwa
mwaka 2011/2012 tulihoji ni lini hasa Serikali ingewezesha kuanzishwa
kwa Baraza la Vijana la Taifa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani ilirudia
tena kuhoji suala hili wakati wa mjadala wa mapitio ya utekelezaji kwa
mwaka 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2012/2013.
Hata hivyo, kwa nyakati zote hizo Serikali katika majumuisho imekuwa
irudia tena ambayo imekuwa ikitolewa kwa miaka zaidi ya miaka 17 ya
kukamilisha mchakato wa kuanzishwa kwa baraza la Vijana la Taifa; bila
utekelezaji kamili na wa haraka.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inayo taarifa kwamba
kufuatia hali hiyo mwezi Januari 2013 mbunge wa Ubungo, Mheshimiwa John
Mnyika aliwasilisha kwa Katibu wa Bunge muswada binafsi wa sheria
kuwezesha kuundwa kwa Baraza la Taifa la Vijana. Katika Hotuba yake juu
ya mapitio ya utekelezaji kwa mwaka 2012/2013 na makadirio ya mapato na
matumizi ya mwaka 2013/2014 ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kiongozi wa Kambi
ya Upinzani Mheshimiwa Freeman Mbowe alihoji ni lini Serikali
itawasilisha bungeni miswada binafsi ya wabunge ukiwemo muswada huo.
Mheshimiwa Spika; kwa mujibu wa Kitabu cha hoja za wabunge na
majibu ya Serikali kuhusu Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na
Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2013/2014 juu ya muswada huo “Ofisi ya
Katibu wa Bunge imemwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupata
ufafanuzi kama Muswada unaohusu uanzishwaji wa Baraza la Vijana la Taifa
hautakuwa na athari zozote za kiwango cha matumizi ya fedha kutoka
Mfuko Mkuu wa Hazina kama ilivyoanishwa katika Kanuni ya 95 ya Kanuni za
Kudumu za Bunge toleo la mwaka 2007”.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inayo taarifa kwamba
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa ushauri kuwa muswada huo hauwezi
kuchapishwa katika gazeti la Serikali kwa kuwa umekiuka masharti ya
ibara ya 99 ya Katiba ya Nchi. Kambi Rasmi ya Upinzani ina taarifa kuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa ushauri huo kwa kuwa muswada
unalenga pamoja na mambo mengine kupitia kifungu cha 31 kipengele cha
kwanza kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa madhumuni ya
kugharamia shughuli za baraza la vijana la taifa, mipango ya baraza na
kutekeleza miradi ya vijana kwa ajili ya maendeleo ya vijana.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kueleza iwapo katika kutoa ushauri huo ilizingatia kwamba kifungu cha 31
kipengele cha pili cha muswada huo kinataja vyanzo mbalimbali vya fedha
za mfuko ikiwemo kutaja kuwa fedha za mfuko zitatokana na fedha
zilizotengwa na Serikali na Bunge kwa ajili ya Baraza kwa mujibu wa
Ibara ya 135 kifungu cha pili cha katiba ya Nchi.
Mheshimiwa Spika; Ibara ya 135 (2) ya Katiba ya Nchi inatamka
kuwa “fedha ambazo hazitawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali
ni zile zote ambazo zimetajwa na sheria ya kwamba zitumike kwa shughuli
maalum au ziwekwe kwenye mfuko mwingine kwa ajili ya matumizi maalum”.
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka ufafanuzi kutoka kwa Serikali ni kwanini
haikutoa ushauri wa kufanya ibara hiyo ya Katiba ya Nchi kutumika
kuwezesha kuanzishwa kwa Baraza la Vijana na Mfuko wa Maendeleo ya
Vijana bila kufungwa na Ibara ya 99 ya Katiba kifungu cha kwanza ambacho
kimeweka masharti kuwa “Bunge halitashughulikia jambo lolote kati ya
mambo yanayohusika na ibara hii isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba
jambo hilo lishughulikiwe na Bunge na pendekezo hilo la Rais liwe
limewasilishwa kwenye Bunge na Rais.”
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kuwa Kifungu
cha pili kinataja mambo yanayohusika na ibara hiyo ya 99 ni pamoja na
muswada wa sheria kwa ajili ya “kuagiza kwamba malipo au matumizi ya
fedha yafanywe kutokana na Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au mfuko
mwingine wowote au kubadilisha kiwango hicho kwa namna nyingine yoyote
isipokuwa kupunguza”. Hata hivyo, kwa zaidi ya miaka 17 maraisi na
mawaziri wenye dhamana wamekuwa wakiacha kutumia madaraka hayo ya
kikatiba kuleta muswada bungeni wa kuwezesha kuundwa kwa Baraza la
Vijana la Taifa; hivyo kitendo cha Serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu
kuendeleza vikwazo hata kwa muswada binafsi wa mbunge kuhusu suala hilo
kunaashiria ukosefu wa nia njema kwa upande wa Serikali katika mchakato
wa kuundwa kwa Baraza la Vijana la Taifa.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa mwito kwa
Serikali na Uongozi wa Bunge kuwezesha muswada wa Baraza la Taifa la
Vijana kuwasilishwa kwenye mkutano huu wa kumi na moja wa Bunge
unaoendelea iwe ni kupitia muswada binafsi, muswada wa kamati au muswada
wa Serikali kwa kuwa tayari maoni yameshakusanywa kwa miaka mingi
kinachohitajika sasa ni utekelezaji wa Sera na ahadi.
Kambi rasmi ya upinzani, Tunataka kujua msimamo wa Serikali katika bunge
hili, ituambie muda mahsusi (time frame) lini hasa mchakato wa uundwaji
wa baraza hilo utakamilika na hatimaye kuanza kufanya kazi kwa Baraza
la Vijana la Taifa kwa ajili ya maslahi ya vijana wa nchi hii. Iwapo
Serikali ya CCM itaendelea kupiga dana dana muswada wa sheria wa kuundwa
kwa chombo hiki muhimu kwa maendeleo ya vijana; Kambi Rasmi ya Upinzani
bungeni inayoongozwa na CHADEMA itawahamasisha vijana nchi nzima
kuelekeza nguvu na uwingi wao katika kuishinikiza Serikali sikivu ya
CCM, kufanya mabadiliko yenye kuwezesha matakwa ya vijana kutekelezwa
kwa wakati.
4.2 Sekta ya maendeleo ya vijana
Mathalani katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka jana, kazi pekee ambazo
zimekuwa zikipewa kipaumbele na sekta hii ni kukimbiza mbio za mwenge na
kuratibu maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa. Aidha kwa mwaka jana,
sekta hii, kwa mujibu wa maelezo ya wizara, ilifanya uratibu wa mafunzo
ya kuwawezesha vijana kuwa na mawazo ya kimkakati ya ubunifu na
ujasiriamali katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Mara, Morogoro, Geita,
Njombe, Kigoma na Arusha!
Kambi ya Upinzani Bungeni inaitaka wizara kulieleza bunge lako hili kwa
takwimu na maelezo ya kina ni kiasi gani mbio za Mwenge ambazo zimekuwa
zikitumia mabilioni ya fedha ‘kuingiza’ mamilioni ya fedha, zimeweza
kuwasaidia vijana wa Tanzania kupambana na tatizo kubwa linalowakabili
la ukosefu wa ajira na ujira wenye staha. Je, wizara inaweza kutoa
takwimu hapa kuonesha namna ambavyo mabilioni ya fedha waliyotengewa
mwaka jana kwa ajili ya uratibu wa mafunzo ya ubunifu na ujasiriamali,
wameweza kufundisha vijana wangapi na katika maeneo yapi hasa ya
utaalamu na taaluma, kwa kiwango gani ili kuweza kuwajengea uwezo wa
kuajiriwa na kujiajiri kwa ajili ya kupata ujira wenye staha.
4.3 Mikataba, mipango, sera na utekelezaji
Mheshimiwa Spika, Mwaka mzima baada ya serikali kusimama hapa
bungeni na kulipatia bunge lako matumaini na kutoa ahadi kemkem wakati
wa kupitisha Azimio la Mkataba wa Kimataifa wa Vijana wa Afrika, hadi
sasa wizara hii imeendelea kusuasua na kuzidi kutoa ahadi juu ya ahadi
kuhusu kuweka utaratibu wa kisheria wa utekelezaji wa mkataba huo.
Mheshimiwa Spika, Baada ya bunge hili katika mkutano wake wa
mwezi Februari mwaka jana kupitisha azimio hilo, katika hotuba ya bajeti
mwaka jana, wizara hii ilisema kuwa, kwa kushirikiana na Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeanza kuchukua hatua za kuandaa muswada
wa sheria ya utekelezaji wa mkataba huo.
Mheshimiwa Spika, Lakini katika kuonesha kuwa serikali hii
haikuwa wala haina nia ya dhati kuweka utaratibu wa kisheria ili
kusaidia utekelezaji wa azimio hilo, katika malengo yake ya utekelezaji
wa mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2013/14, imeshindwa kabisa
kuzungumza chochote juu ya suala hilo.
Kambi rasmi ya Upinzani, inaona kuwa huu ni mwendelezo tu wa
serikali hii ya CCM kuendelea na utamaduni wake wa
kuwatelekeza,kuwapuuza na kuwadharau vijana wa nchi hii.Aidha , tunataka
kujua ni lini wizara italeta mswada huo hapa Bungeni kwa ajili ya
kupitishwa na Bunge na kuwa sheria.
4.4 Mbio za Mwenge wa Uhuru
Mheshimiwa Spika,mara kadhaa sasa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni
imekuwa ikihoji maswali anuai kuhusu jambo hili lakini bahati mbaya
yamekuwa yakitolea majibu yasiyokidhi haja. Nasi kwa ajili ya kutimiza
wajibu wetu wa kuwasemea Watanzania wasiokuwa na sauti ndani ya mhimili
huu, tutaendelea kukumbushia na kuhoji hadi majibu mujarabu
yakakapotolewa.
Mathalani, katika moja ya malengo ya utekelezaji wa mpango wa bajeti wa
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni ukimbizaji wa Mwenge
wa Uhuru. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, si tu kwamba imekuwa ikihoji
maana nzima ya kuendelea kutumia mabilioni ya walipa kodi maskini kwenye
mbio za mwenge, badala ya kuuweka makumbusho na kuufanya kuwa moja ya
vivutio vya kiutamaduni.
Mheshimiwa Spika, mtu yeyote makini hawezi kuona mantiki ya mbio
za mwenge ambazo zimekuwa zikitumia mabilioni ya fedha kuzunguka nchi
nzima kuzindua miradi ya mamilioni ya watu binafsi! Kama vile bar,
nyumba za kulala wageni na mingineyo.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha tumeendelea kutenga
fedha kwa ajili ya kukimbiza mwenge, randama ya wizara inaonyesha kuwa
,kijifungu 210319 zinaombwa shilingi 3,000,000 ‘kwa ajili ya kulipa
matibabu na bima kwa wakimbiza Mwenge wa uhuru’,kijifungu 210315
zinaombwa shilingi 64,200,000 ‘kwa ajili ya kulipa posho za kujikimu kwa
wakimbiza mwenge wa uhuru, kijifungu 220302 zinaombwa shilingi
57,750,000 ‘kwa ajili ya kununulia dizeli ya magari mawili
yatakayotumika kwenye sherehe za uzinduzi na kilele cha mbio za mwenge
wa uhuru’,.
Aidha, kijifungu 220604 sare, wizara inaomba kiasi cha shilingi
8,886,000 ‘kwa ajili ya sare za wakimbiza Mwenge kitaifa’, kijifungu
220708 zinaombwa shilingi 25,000,000 ‘kwa ajili ya kukodi ndege kwa
shughuli za mbio za Mwenge wa uhuru’, kijifungu 220709 ,zinaombwa jumla
ya shilingi 7,200,000 zinaombwa kwa ‘ajili ya ununuzi wa vifaa vya
mkutano wa tathimini ya mbio za mwenge wa uhuru’,kijifungu 221005
zinaombwa shilingi 78,500,000 ‘kwa ajili ya posho ya safari za kikazi
ndani ya nchi kwa wakimbiza mwenge kitaifa’ ,kijifungu 221406 zinaombwa
shilingi 15,000,000 kwa ajili ya ‘...kuandaa tuzo ...wakati wa mbio za
mwenge’,
Mheshimiwa Spika, Pamoja na kutengwa kwa fedha zote hizi kiasi cha shilingi 259,536,000
pesa ambazo zingewekezwa kwenye mfuko wa kuwakopesha vijana zingeweza
kuwakwamua kwenye tatizo la ajira, serikali inaomba fedha hata kwa ajili
ya kukodi ndege kwa ajili ya kukimbiza mwenge , mwaka huu tutashuhudia
mwenge ukikimbizwa angani! bado mwenge umeendelea kupoteza mwelekeo
Mheshimiwa Spika, katika kuthibitisha kuwa Mwenge umepoteza mwelekeo katika mwaka huu wa fedha katika kijifungu 230600 ‘matengenezo ya mashine’ katika kijifungu 230605 ‘mikataba ya matengenezo kutoka nje’ randama uk.86 inasema
‘mwaka 2013/2014 sh.366,000 zinaombwa kwa ajili ya kupata wataalamu nje
ya wizara kwa ajili ya kutoa huduma ya matengenezo ya chombo cha Mwenge
wa uhuru’. Unaweza kuona kuwa chombo hiki kinatafutiwa mtaalamu
kutoka nje ya wizara na malipo ya mtaalamu huyo ni shilingi laki tatu!
Hii ni dalili ya wazi kuwa chombo hiki yafaa kikawekwa kwenye jumba letu
la makumbusho.
Kambi Rasmi ya Upinzani, haikubaliani na serikali kutumia kiasi cha
shilingi 259,536,000 kwa ajili ya posho za kukimbiza mwenge, tunataka
fedha hizi ziingizwe kwenye programu za maendeleo ya vijana ili waweze
kujiajiri na mwenge uwekwe kwenye jumba la makumbusho, kwani umekuwa ni
kero kwa wananchi vijijini kuchangishwa fedha za mwenge bila hata kujua
zinaenda kufanya nini.
5.0 USIMAMIZI WA MICHEZO NA MUSTAKABALI WAKE KWA TAIFA
Mheshimiwa Spika, Pamoja na hazina ya wanamichezo nchini, lakini
michezo mingi nchini haipewi kipaumbele na serikali.Mara kadhaa vyombo
vya habari vimekua vikiupa kipaumbele mchezo wa soka kana kwamba michezo
mingine haina tija kwa taifa. Leo hii kuna michezo ambayo kama ikipewa
uzito wa kutosha italeta taifa hili heshima katika medani za kimataifa.
Mheshimiwa Spika,Labda kwa kuwa tumeshindwa kuwekeza kwenye
michezo mingine kwa vipaumbele ambavyo vinaweza kuiweka Tanzania katika
ramani ya michezo, hii imefanya michezo hiyo kufa na hazina ya taifa ya
vipaji mbalimbali nayo kufa bila kutumika. Mfano katika michezo ya 30 ya
Olimpiki iliyofanyika jijini London, Uingereza Julai mwaka 2012,
Tanzania ilipeleka jumla ya wanamichezo 7 ambao hawakuambulia medani
yoyote .
Mheshimiwa Spika,Wakati Afrika ya Kusini ilipeleka wanamichezo
125 kwa jumla ya michezo 17,sisi tulipeleka 7 tu. Kuna jambo kuu la
kujifunza kutokana na jinsi ambavyo Serikali, sikivu , ya CCM inaendesha
nchi yetu. Jambo ambalo linastaajabisha na lenye maswali mengi yasiyo
na majibu, Je Wizara hii ina kazi gani? Ina mikakati gani ya jumla
katika kusimamia vyama vya michezo nchini ili viwe na tija? Je wizara
hii ina uchungu na fedha za kodi za wananchi hii kwa matumizi yasiyo na
tija katika sekta ya michezo? Je taifa hili limekosa kutumia michezo
kama njia mojawapo ya kutangaza jina la Tanzania na kuliweka katika
ramani ya dunia kwa kuwa na wanamichezo bora na si bora wanamichezo?
Kambi rasmi ya Upinzani, inapendekeza kwa msisitizo mkubwa kuwa
katika kipindi hiki ambacho taifa letu lipo katika mpasuko na mgawanyiko
wa masuala mbalimbali kuanzia udini,mchakato wa katiba nk , katika
kipindi hiki ambacho mshikamano na umoja wetu kama taifa upo katika
hatari ya kusambaratika, jambo ambalo linaweza kutuunganisha kama taifa
moja lililobakia ni michezo .
Hivyo basi tuhakikishe kwamba timu ya taifa ya mpira wa miguu
inaandaliwa vya kutosha na tuweze kuingia kwenye fainali za kombe la
dunia ifikapo 2014, tuna kazi ndogo ya kuifunga Morocco kwao, tunatakiwa
kuifunga Ivory coast hapa kwetu, tunaamini inawezekana kama mipango
madhubuti ikiwekwa sasa.
5.1 Chama cha Riadha Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2012, katika mashindano ya taifa ya
riadha kulikua na changamoto kubwa ya wanariadha kushiriki katika
mashindano ya taifa bila ya maandalizi ya kutosha, huku baadhi ya
wanariadha wakishiriki katika mashindano bila ya kuwa na viatu. Haya ni
mashindano ya taifa, Chama cha Riadha (RT)nchini, kimeyandaa bila ya
kuwa na mikakati ya kitaifa ya kuhakikisha kuwa vigezo na viwango
vimefuatwa.
Aidha , chama hiki kimekuwa kikilalamikiwa sana na wadau wake kutokana
na hisia kwamba kunakuwa na upendeleo katika kutuma wanariadha ambao
wamekuwa wakiwakilisha taifa letu katika michezo mbalimbali ya
kimataifa.
Kambi rasmi ya upinzani, inataka kujua serikali imechukua hatua
gani dhidi ya viongozi wa chama hiki ambao badala ya kusimamia riadha
wamekuwa hawafanyi hivyo , aidha kuna mikakati na mipango gani ya kuinua
kiwango cha riadha hapa nchini ili kurudhisha heshima ya taifa kwenye
mchezo huu maarufu duniani kote?
5.2 Mapato ya viwanja vya Taifa.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa randama uk 102 katika mapato kuna
kifungu 140259 ambacho kinahusu mapato ya viwanja vya michezo (uhuru na
Taifa) makadirio yalikuwa kukusanya shilingi 400,000,000 kwa
mwaka 2012/2013 ila mapato halisi yaliyokusanywa kutokana na asilimia 15
ya mapato yote yanayokusanywa kutokana na kutumika kwa kiwanja hicho
mpaka februari 2013 yalikuwa 329,814,400 tu.
Kambi rasmi ya upinzani, inataka kujua mapato hayo yalikusanywa
kutokana na michezo mingapi na fedha hizo zilitumika katika kufanya kazi
gani za kuendeleza michezo hapa nchini.
5.3 Malipo kwa makocha wa kigeni.
Mheshimiwa spika, katika mwaka huu wa fedha serikali imetenga
kiasi cha shilingi bilioni 1.230 katika kifungu 6004-280518 (Baraza la
Michezo la Taifa –Makocha)(chanzo:randama, jedwali namba 8) kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC),Aidha kwenye fungu hilo hilo 6004 kwenye matumizi ya kawaida (chanzo randama ;jedwali namba 6) zimetengwa jumla ya shilingi milioni 586,079,000 kwa ajili ya mishahara na matumizi mengineyo zimetengwa shilingi 1,917,960,000
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa randama ya wizara uk.93 kijifungu 270800 ‘ruzuku kwa asasi na vituo’ zimetengwa jumla ya shilingi 1,564,382,000 na katika kijifungu kidogo cha 270813 ‘Baraza la Michezo la Taifa’ zimetengwa shilingi 1,524,382,000 kwa ajili ya ‘mishahara ya Makocha wa Kigeni’
na matumizi ya Baraza la michezo la Taifa. Aidha katika mwaka wa fedha
2012/2013 kwenye kijifungu hiki zilitengwa jumla ya shilingi 823,546,000 tu kwa ajili ya mishahara kwa makocha wa kigeni.
Wakati kichwa cha habari cha kasma hii na kijifungu hiki kikisema ni
‘ruzuku kwa asasi na vituo’ , ruzuku inayokwenda kutolewa ni kiasi cha shilingi milioni 40 tu
kama ambavyo inaonekana kwenye kijifungu 270839 kituo cha michezo
Arusha shilingi milioni 20 na kijifungu 270840 kituo cha michezo Songea
shilingi milioni 20.
Kambi rasmi ya upinzani, inaona kuwa fedha hizi ni nyingi sana
kwa ajili ya mishahara na marupurupu ya makocha wa kigeni, hivyo basi
tunataka kujua yafuatayo;
i. Ni makocha wangapi watalipwa na ni wa michezo gani?
ii. Wanapewa marupurupu gani kama stahili zao?
iii. Kwanini serikali na wizara hii isiwapeleke makocha wa kitanzania
mafunzoni nje ya nchi ili waweze kutumikia taifa lao pindi wakimaliza
masomo yao?
6.0 BARAZA LA KISWAHILI TANZANIA
Mheshimiwa Spika,Wizara inao wajibu wa kuimarisha, kukuza na
kuendeleza lugha yetu ya Kiswahili kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano
ikiwa ni pamoja na uratibu na kuhakikisha ustawi na maendeleo ya
utumiaji wa Kiswahili kwa kushirikiana na asasi zile ambazo zinahusika
na uendelezaji wa lugha hii hapa nchini. Baraza lina wajibu wa
kuhakikisha kuwa matumizi ya Kiswahili yanapewa kipaumbele katika maisha
ya kila siku ya mtanzania, ikiwemo katika shughuli za kitaifa na
kimataifa ambazo viongozi wa taifa letu wanahudhuria.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na nyimbo ambazo Serikali ya CCM imekua
ikiziimba mara kwa mara kuwa inataka kukuza lugha ya Kiswahili ili
kuutangaza utamaduni wa Tanzania katika jumuia ya kimataifa ni aibu
kubwa kwa taifa letu pale ambapo viongozi wake waandamizi wanapokuwa
watumwa wa lugha za nchi za Magharibi!
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa Serikali ya CCM imeamua kuimarisha
uhusiano wa kidiplomasia na nchi ya China, ni kitendo cha kusikitisha na
aibu kuona kuwa wakati wa ziara yake nchini, Raisi wa China, alihutubia
na kuzungumza kwa ufasaha lugha ya taifa lake wakati Rais wa Tanzania
na Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wakitumia lugha ya
Kiingereza. Swali la kujiuliza, kama Raisi wa nchi pamoja na waziri
wake wanaona ugumu kutumia lugha ya taifa wakati mgeni wao ametumia
lugha ya taifa lake wakati walengwa wa ujio ule na wageni wengi
waliokuwa katika uzinduzi wa Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere
wengi walikua ni watanzania, je itakuaje kwa mwananchi wa kawaida leo?
Lugha ya Kiswahili haiwezi kukua wala kupewa umuhimu na mataifa mengine
ikiwa viongozi wa Serikali wanaonesha hadharani utumwa wa utamaduni wa
nchi za magharibi, lazima kwa nguvu zote Bunge na taifa tukatae aina hii
ya utumwa kwa maana kuwa hata Serikali inayotakiwa kuhimiza matumizi ya
lugha ya Kiswahili na kukitangaza, wamekua mstari wa mbele kutumia
lugha ya Kiingereza.
Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani tunajiuliza
hivi, Hata kama Serikali ya CCM imeshindwa kulinda tembo wetu basi hata
Kiswahili mshindwe kukilinda? Tunarudia tena, huu ni utumwa!
Haukubaliki! Tutumie na kukitangaza Kiswahili kwenye dhifa na hafla za
kimataifa, kwa kuwa Kiswahili ndiyo urithi wetu.
7.0 USIMAMIZI WA HAKI ZA WASANII NA USHIRIKI WA SERIKALI KATIKA UTEKELEZAJI
Mheshimiwa Spika, Sheria ya hakimiliki inayotumika sasa katika
kusimamia hakimiliki na hakishiriki za wasanii , ni sheria iliyopitishwa
na Bunge inayojulikana kama Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki namba 7
ya 1999. Hii iliiondoa sheria ya awali Sheria ya Hakimiliki namba 61 ya
1966. Sheria hii imeendelea kutumika baada ya kutungwa kanuni
mbalimbali mwaka 2000 na kuanza kutumika zikiwemo sheria iliyounda
COSOTA. COSOTA ilianza kwa kuwa na bodi iliyokuwa mchanganyiko wa
wajumbe waliochaguliwa na wasanii na wajumbe walioteuliwa na Waziri wa
Viwanda na Biashara. Na hali hii ya kuwa na wawakilishi wasanii katika
COSOTA iliendelea mpaka baada ya uchaguzi mkuu wa chama hicho 2007,
ambapo Waziri hakuweza kuteua Mwenyekiti wa bodi ya chombo hicho na
hivyo kuzuia Bodi kuweko.
Mheshimiwa Spika,hata alipoulizwa na Mh. Martha Mlata kwenye
bunge la bajeti 2008 aliahidi kushughulikia na hakufanya hivyo hata
akaulizwa tena bunge la bajeti 2009. Hivyo hatimaye 2011 ikateuliwa Bodi
ambayo haikuwa na muwakilishi kutoka wasanii japokuwa COSOTA iliendelea
kukusanya mirabaha ‘kwa niaba ya wasanii’.
Kambi rasmi ya upinzani, inataka kujua ni kwanini bodi hii haina
mwakilishi wa wasanii kama sheria inavyotaka? Lini mwakilishi huyo
atateuliwa na wizara?
7.1 Kulinda kazi za wasanii
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2001, ilitengenezwa kamati iliyoitwa
National Anti Piracy Committee ikiongozwa na Mwenyekiti John Kitime,
iliyokuwa chini ya COSOTA, kazi yake kubwa ni kuwezesha kutengeneza
sheria na kanuni za kuwezesha kazi za audio na video kuwa na stika za
mapato. Kazi hii ilifanyika na kukamilika na kanuni hizo zilipita kwa
usimamizi wa Waziri Mh. Juma Ngasongwa kabla tu ya uchaguzi wa mwaka
2005, lengo likiwa ni kupata sapoti ya wasanii.
Mheshimiwa Spika, Baada ya jitihada za hapa na pale, Serikali kwa
kupitia TRA wameleta stika mpya, ambazo Tatizo moja tu hapa ni kuwa TRA
kazi yao ni kukusanya kodi tu na sio kulinda hakimiliki, hivyo stika ya
TRA ni stika ya kukusanya kodi na italeta mkanganyiko katika
utekelezaji wa taratibu za hakimiliki. Je, wizara imepanga mikakati gani
kuhakikisha kuwa kazi za sanaa hazidurufiwi, kuuzwa na kusambazwa bila
ya ridhaa za wasanii nchini? Kambi rasmi ya upinzani bungeni inarudia
kuitaka Serikali kuifumua COSOTA na kuunda chombo kipya kitachokuwa na
uwezo wa kusimamia kazi za sanaa.
7.2 Nyimbo za wasanii na Mapato kwao.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2003 zilipitishwa kanuni zilizoagiza
wenye vyombo vya utangazaji nchini ziwalipe wanamuziki kutokana na
matumizi ya nyimbo zao mbalimbali ambazo wanazitumia kwenye vipindi
mbalimbali. Ni jambo la kushangaza kuona kuwa Serikali ya CCM
inayojitapa kuwa na utawala wa sheria inashindwa kudhibiti vyombo vya
habari na utangazaji ambavyo vimeendelea kutumia kila aina ya ubabe na
njia za kiunyonyaji ili visilipe fedha hizi kwa wasanii. Leo hii wasanii
wanalazimishwa kuandika barua kuwa wametoa nyimbo zao kwa vyombo hivyo
zipigwe bila kulipia na kutokana na mazingira yaliyotengenezwa,
wanamuziki wanajikuta ni lazima wahonge! ili nyimbo zao zipigwe ili
waweze kupata soko la kazi zao.
Mheshimiwa Spika,Wizara hii ambayo inasimamia TBC, televisheni na
redio ya Taifa, imeshindwa kuvichukulia hatua za kisheria vyombo vyake
ambavyo vimekua moja wapo ya wakiukaji wa sheria hii. Ni kejeli kwa
taifa, ni kejeli kwa wasanii wanaopata shida kujikwamua kimaisha. TBC
leo inapiga na kucheza nyimbo za wasanii bila kuwalipa, huku wizara
inayotakiwa kusimamia vyombo hivi inashuhudia sheria zilizopitishwa na
bunge hili zinavunjwa.
Mbaya zaidi TBC inauza CD na kanda za nyimbo zilizoko katika maktaba
yake bila kutoa hata senti kwa wanamuziki waliorekodi nyimbo hizo, iko
wapi tofauti yao na maharamia wengine? Leo hii wizara inawezaje kusema
kuwa wao ni wasafi? Ni aibu kwa wizara, ni aibu kwa watendaji wake, ni
aibu kwa serikali , sikivu, ya CCM!
7.2 Harakati za kudai haki za wasanii.
Mheshimiwa Spika, sanaa imeendelea kufanywa mtaji wa biashara na
watu wachache ambao wanatumia nguvu waliyo nayo katika jamii na uwezo
wao wa kifedha katika kukandamiza maslahi ya wasanii hapa nchini. Katika
harakati za kutafuta haki za wasanii hapa nchini, mimi binafsi pamoja
na wasanii wengine wachache, tulianzisha harakati za kudai haki kwa
kupitia programu maarufu iliyojulikana kama 'Anti Virus' chini ya 'Vinega' ikiwa
na lengo na juhudi za kudai haki za wasanii dhidi ya ukandamizaji
unaofanywa na wajanja wachache kwenye muziki, ambao wametumia nafasi
kama njia ya kutumia mitaji yao ya fedha kuwaendesha wasanii jinsi
wanavyotaka wao.
Mheshimiwa Spika, Kama ilivyo kawaida, wasanii wengi walidharau
jitihada zetu na kutotuunga mkono. Leo hii katika tasnia ya muziki, kuna
mgogoro mkubwa uliofuka moto kati ya msanii maarufu Lady Jaydee dhidi
ya wamiliki wa radio ya Clouds FM hatua iliyosababisha nyimbo za
wanamuziki wa kizazi kipya maarufu kama 'Bongo Flavour' kutopigwa
kwa siku moja katika kituo hicho. Sasa, ukiangalia kilio cha Lady
Jaydee ni kilio kilekile kilichopelekea VINEGA kuingia vitani.
Mheshimiwa Spika, kama msemaji mkuu wa kambi ya upinzani bungeni,
na mwenye dhamana na uchungu na tasnia ya sanaa nchini, niweke wazi kwa
umma wa watanzania kuwa, tumefikia hapa tulipo si kwa kuwa na sheria
kandamizi tu bali pia kwa kukosekana kwa umoja wa wasanii nchini. Wakati
tukiwa na juhudi za kutetea maslahi ya watanzania kupitia Anti Virus,
ni wasanii wachache ambao walituunga mkono na wengi wao wakibeza
jitihada zetu, wakiwemo hawa ambao leo wanalalamika kuwa wananyonywa
haki zao. Wengine walifikia hatua ya kusema kuwa tumepewa fedha ili
kuzima harakati tulizozianzisha.
Mheshimiwa Spika, Umoja wa wasanii hasa wa muziki wa kizazi kipya
nchini, unasimamiwa na chombo halali kinachojulikana TUMA-‘Tanzania
Urban Music Association’, lakini kutokana na ujanja wa watu wachache,
waliudhoofisha umoja huu kwa kuanzisha kampuni iliyosajiliwa kama TFU-
‘Tanzania Flavour Unit’ iliyowalaghai wasanii kuwa ni muungano wa
wanamuziki wa Bongo Fleva na kuhodhi majukumu ya TUMA ambacho ni chama
halali cha kusimamia wanamuziki wa Bongo Fleva. Mpaka tunapoongea leo
hii, hata Studio iliyotolewa na Mheshimiwa Raisi, bado ipo katika mikono
ya TFU pamoja na Serikali kuamuru irudishwe katika mikono ya Serikali
ili ikabidhiwe kwa wasanii wote chini ya chama halali cha TUMA. Sasa
tunataka wasanii wote nchini waache uoga na unafiki na wajiunge na vyama
vyao halali ili viwatete haki zao.
Mheshimiwa Spika,Kumekuwa na upotoshaji mkubwa wa utetezi wa haki
za wasanii kwa kuwa wanaotuhumiwa kunyonya haki za wasanii wameweza
kutajirika na kuneemeka kwa kupitia jasho na mgongo wa wasanii. Hawa
hawa wanaotuhumiwa kuhujumu wasanii ndio wanatumia nafasi yao kuupotosha
ukweli wa tuhuma dhidi yao. Wanatumia fedha na rasilimali walizo nazo
katika kunyanyasa wasanii, kuwakandamiza, kuwapokonya haki zao na
kuwadhalilisha kuwa bila wao, wasanii wasingekua kitu.
Mheshimiwa Spika, Leo hii wasanii wanaishi kwenye hali ngumu,
umasikini mkubwa lakini bado wanatolewa maneno ya kashfa na dharau na
Serikali imeendelea kukaa kimya. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,
inaitaka Serikali kuacha siasa kwenye kutatua migogoro ya taifa hili.
Siasa zimetumika sana katika kuzima jitihada za wanyonge kwenye taifa
hili, leo hii wananchi hawana imani na Serikali kwa kuwa imeonesha wazi
imeshindwa! Kushindwa kwa Serikali katika kutatua migogoro ya wasanii
kwa kutotekeleza makubaliano mbalimbali yanayoafikiwa kati yake na
wasanii, yameshusha hadhi yake kwa wasanii. Swali kubwa kwa Serikali
sikivu ya CCM, Je mnasubiri migogoro mingapi ili mjue kuwa wasanii
hawatendewi haki? Je mnasubiri vikao vingapi vya upatanishi na
usuluhihishi ili mjue kuna tatizo? Ama mnataka wasanii wagombane,
wapigane, wauane ili mjue kuwa kuna tatizo?
Mheshimiwa Spika,Leo hii, Serikali bila ya kukaa na wadau wa
muziki wa dansi, taarabu, bongo fleva, hip hop, mnanda na mahadhi
mengine na kuwasikiliza kwa makini wamejikuta wanajihusisha na mambo
ambayo hawajui. Watendaji wa Serikali wameendelea kuwaingiza mkenge
viongozi wa Serikali katika masuala ya sanaa nchini. Hivi karibuni,hapa
Dodoma, bila ya kuwa na taarifa muhimu juu ya unyonyaji wa haki za
wasanii, waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda, alishiriki katika tamasha la
kudai haki za wasanii ambalo liliandaliwa na baadhi ya watu ambao kwa
muda mrefu wamekua wakituhumiwa kuwa ni wanyonyaji wa kazi za wasanii.
Kiongozi mkuu wa Serikali, unashiriki katika kupiga mihuri na
kuhalalisha mikakati ya kimafia ya kuua umoja wa wasanii bila ya kuwa na
taarifa sahihi. Je, waziri mkuu ana taarifa kuwa walioandaa tamasha la
kudai haki za wasanii ndio walalamikiwa namba moja nchini dhidi ya haki
za wasanii hasa wa muziki? Tuinataka Serikali na wanasiasa wote kuacha
kutumia wasanii kwa faida zao binafsi bali wasaidie kutatua matatizo
halisi ya wasanii ili waondokane na umasikini.
8.0 UTAMADUNI NA MALIKALE NCHINI
Mheshimiwa Spika,Zipo njia mbalimbali ambazo zinatambulisha
utamaduni wa mtanzania kwa mataifa mengine. Utamaduni wetu unatambuliwa
kwa kupitia lugha, mavazi, vyakula, sanaa, maadili na malikale za taifa
letu. Leo hii ukiangalia makumbusho ya taifa, haina vitu vya msingi vya
kufanya makumbusho kuwa chanzo cha kuliingizia taifa fedha za kigeni kwa
njia ya utalii. Sehemu nyingi nchini ambazo zinaelezea utamaduni wetu
na asili ya taifa letu, kama Bagamoyo, Kilwa Masoko, Kilwa Kivinje,
Isimila, Zanzibar haziwekwi katika mazingira ya kuyatunza kwa ajili ya
kuelezea asili ya taifa letu.
Leo hii , Serikali ya CCM ikijitetea kuhusu kuboresha ama kutunza
malikale za taifa letu ikiwemo majengo ya kale, itajigamba kuwa
imeyapaka rangi. Lakini ni maajabu kuona majengo yale, yamepakwa rangi
nyeupe, chokaa hali inayoyafanya majengo haya kuwa na rangi za kijani
zenye ukungu inapokuja suala la ukarabati wake. Ukiangalia marekebisho
ya majengo hayo, yamefanyika na kuondoa uasilia wa majengo hayo kama
yalivyokua zamani,.
Kambi rasmi ya Upinzani, inaiuliza Serikali je,imeshindwa
kutafuta wataalamu wa majengo wenye kuweza kurekebisha na kuyatunza
majengo katika hali ilokuwa bila ya kuyaharibu zaidi? Ni mikakati ipi
ambayo Serikali imejiwekea kwa mwaka huu wa fedha wa 2013/2014 katika
kuyatunza na kuyatengeneza majengo ya kale ili kutunza utamaduni wa
taifa letu?
10.0 UCHONGAJI WA VINYAGO NA THAMANI YAKE KWA TAIFA
Mheshimiwa Spika,Kama kawaida Serikali ya CCM imeendelea kutawala
huku kukiwa hakuna utaratibu mzuri wa kusimamia maslahi ya wachongaji
wa vinyago hapa nchini. Wachongaji wa vinyago ambao wamesaidia kwa kiasi
kikubwa kutangaza utamaduni wa taifa letu kwa kutumia kazi zao za sanaa
hapa nchini hasa katika kutangaza utalii.
Kwa taarifa tulizonazo kutoka kwa wachongaji vinyago ni malalamiko ya
kazi zao za sanaa kununuliwa na kisha kusafirishwa kuelekea nchi za nje
ambapo huko hupigwa mihuri kuwa imetoka katika nchi za jirani. Hii imeua
soko la vinyago hapo nchini na kukandamiza maslahi ya wachongaji hawa
ambao ni hazina kwa taifa letu. Wachongaji vinyago wana umuhimu mkubwa
katika kulinda utamaduni wa nchi yetu kwa kuwa ni urithi tuliopewa na ni
lazima Serikali iweke mikakati ya kuhakikisha kuwa soko la vinyago
ndani na nje ya nchi linamufaisha mchongaji kimapato.
Kambi rasmi ya upinzani bungeni, inaitaka Serikali kutoa kauli
hapa bungeni ina mkakati gani uliowekwa kwa mwaka huu wa fedha katika
kuhakikisha kuwa wachongaji vinyago wananufaika kwa kazi zao hasa
ukizingatia kuwa, soko la ndani la vinyago halina faida ya kutosha na
usimamizi wa kina. Vinyago ambavyo vinachongwa Tanzania vimeendelea
kuuzwa nje ya nchi na kuzipatia nchi hizo mapato makubwa na baadhi ya
kazi hizo hazitambuliwi kuwa zinatoka nchini.
11.0 USIMAMIZI WA HAKI ZA WASANII KATIKA UUZAJI WA MIITO YA SIMU
Mheshimiwa Spika,Biashara ya miito ya simu, inayofanywa na
makampuni ya simu nchini ni biashara ya siri ya kimafia inayohitaji
kuwekwa wazi kwani kuna ukwepaji mkubwa wa kodi na haki za wasanii,
ambapo pamoja na waliojiunga kihalali kutopata haki yao wako wale
wanaokuta nyimbo zao zinatumika bila kujua zimepelekwa huko na nani na
kwa mikataba ipi. Leo vyombo vyote vya Serikali vinavyotakiwa kusimamia
sheria na kanuni za hakimiliki zinakaa kimya huku wasanii wakipokwa haki
zao, taifa likipoteza mapato na kuubariki wizi huu wazi wazi.
Mheshimiwa Spika,Hivi karibuni tumeshuhudia Serikali ya CCM
kupitia wizara yake yenye dhamana ya kufuatilia biashara ya miito ya
simu, wizara ya mawasiliano, sayansi na teknolojia imeshindwa kutoa
majibu ya ufuatiliaji wa tozo na mapato ya miito ya simu, Mmeshindwa
kutimiza wajibu wenu kwa wananchi lakini pia mmeshindwa kutimiza wajibu
wenu katika kutekeleza matakwa ya katiba ya nchi hii, kuulinda uhuru na
haki za wananchi wake kama ambavyo muasisi wa taifa hili alijitahidi
kufanya.
12.0 TASNIA YA FILAMU NA MCHANGO WAKE KATIKA KUKUZA UCHUMI NCHINI
Mheshimiwa Spika,Tasnia ya filamu nchini imeendelea kukua kila
siku huku kukiwa na usimamizi mdogo wa Serikali katika kuhakikisha kuwa
sekta hii inatumika vizuri kama chanzo cha kukuza ajira nchini lakini
pia kama moja ya njia ya kuwaongezea wananchi kipato na Serikali kukuza
uchumi kwa kupitia kodi mbalimbali. Leo hii, soko la filamu nchini
Nigeria limeweza kuingiza takribani kiasi cha dola 250 milioni kwa mwaka
kama mapato ya filamu zinazotengenezwa kwa soko lao la Nollywood, je
Serikali kupitia wizara hii imefanya tathmini gani kwa kupitia mamlaka
za mapato na kujua soko la filamu kwa mwaka linaingiza kiasi gani hapa
nchini? Kambi rasmi ya Upinzani, inaitaka Serikali ya CCM kuacha kufanya
kazi kwa mazoea sasa na badala yake ivisimamie vyombo husika
kuhakikisha kuwa sekta ya filamu inapewa kipaumbele pia na thamani ili
kuweza kukusanya kodi na kupunguza umasikini nchini. Tasnia ya filamu si
tu inaweza kuliingizia soko hili fedha bali pia ikipewa thamani
inauwezo mkubwa kwa kutatua tatizo la ajira hapa nchini. Kwa kuwa mpaka
sasa, Tanzania imeshatoa filamu nyingi na soko lake kupanuka katika nchi
za Afrika Mashariki na kati, je tasnia hii mpaka sasa imeweza kuzalisha
ajira ngapi? Kambi rasmi ya upinzani, inaitaka wizara kuja na takwimu
rasmi za ajira zilizotokana na tasnia hii kufikia mwezi Machi mwaka huu.
Mheshimiwa Spika,Tanzania ambayo imebarikiwa kwa kuwa na vivutio
mbalimbali vya utalii, ikiwemo Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama za
Serengeti, Ngorongoro, Manyara, Mikumi pamoja na hifadhi za wanyama kama
Selous, Tarangire, maziwa makubwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa,
sehemu zenye asili ya utumwa kama Bagamoyo, Zanzibar, Kilwa Masoko,
misitu mikubwa, mito na vivutio mbalimbali; ina nafasi kubwa ya kutumika
kama moja ya 'film destinations' duniani kama ambavyo nchi nyengine
imewekeza.
Mheshimiwa Spika,Nchi mbalimbali zimeweza kujiingizia fedha za
kigeni kila mwaka kutokana na kutumia vivutio walivyo navyo na mandhari
ya nchi zao kupitia tasnia ya filamu. Nchini Afrika Kusini, tasnia ya
filamu ina thamani ya kiasi cha takribani randi 12 bilioni sawa na
shilingi trilioni 2.17 za kitanzania huku ikichangia kiasi cha shilingi
1.4 bilioni kwenye uchumi wa taifa na ongezeko la kiasi cha shilingi
milioni 400 kwa mwaka katika kipindi cha miaka minne toka mwaka 2008
walipoamua kufanya mabadiliko ya tasnia ya filamu. Zaidi , tasnia ya
filamu imeweza kuongeza soko la ajira kwa kutoa karibu ajira 30,000.[1]Afrika
kusini imeweza kutumia sekta hii kwa kwa kutumia mandhari waliyo nayo
ambayo inafanana na mandhari za takribani nchi 57 ulimwenguni na
kutumika kutengeneza filamu zenye mafanikio Hollywood. Ipo haja ya
wizara hii kwa kushirikiana na wizara ya maliasili na utalii kufanya
tathmini ya kina na kutengeneza mazingira ya kutumia vivutio tulivyo
navyo ili kuifanya Tanzania sehemu bora zaidi Afrika kwa ajili ya
kutengeneza filamu kwa kupitia mandhari zake. Lazima Serikali itengeneze
mkakati endelevu wa kuendeleza sekta ya filamu nchini kwa kuitangaza
Tanzania katika anga za kimataifa kama 'film destination' bora zaidi
Afrika.
13.0 MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI 2013/2014
Mheshimiwa Spika, katika makadirio ya mapato na matumizi ya
wizara hii kwa mwaka wa fedha 2013/14, jumla ya shilingi 21,
328,045,000, zimeombwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya
maendeleo.
Aidha, kama ilivyo ada ya miaka yote kwa bajeti za serikali hii ya CCM,
katika wizara zote, fedha za matumizi ya kawaida ni nyingi kuliko fedha
ambazo zinatarajiwa kutumika katika miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Suala linaloweza kumuumiza mdau yeyote ambaye
angependa kuona wizara hii ikisonga mbele ni pale ambapo miradi ya
maendeleo imetengewa sh. 600,000,000 pekee, wakati kuna kiasi cha
takriban bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya kitu kinachoitwa ‘matumizi
mengineyo’.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inahoji hayo matumizi mengineyo
yasiyojulikana au kuelezwa hapa mbele ya bunge lako lakini yanatengewa
karibu nusu yote ya bajeti ya matumizi ya kawaida, ni nini na yapi?
Mheshimiwa Spika, Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
.............................. .........
Joseph Osmund Mbilinyi (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-Wizara ya Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo.
20.05.2013
No comments:
Post a Comment