Wednesday, May 29, 2013

MAMA ALIYEJIFUNGUA WATOTO WATANO ARUHUSIWA KURUDI NYUMBANI KUTOKA HOSPITALI

Bi Jane Mlelwa aliyekaa kitandani akiwa amebeba mmoja wa  wawatoto watano aliowazaa kabla ya watototo hao kufa wote(Picha na maktaba)
Hawa ndio watoto aliojifungua katika hospital ya Mkoa wa Ruvuma na kesho wakafaliki dunia (Picha na maktaba)
..........................................................................
Na Nathan Mtega,Songea


 MWALIMU Sophia Mgaya(28) mkazi wa Ruhuwiko mjini Songea mkoani Ruvuma aliyejifungua watoto watano kwa wakati mmoja kwa njia ya upasuaji mnamo Mei 25 mwaka huu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma iliyopo mjini Songea na watoto hao kuishi kwa muda wa masaa kumi kabla hawajafariki dunia ameruhusiwa kutoka hospitalini hapo.

Akizungumza na Demashonews kwa njia ya simu Sophia Mgaya akiwa nyumbani kwake Ruhuwiko mjini Songea alisema alilazimika kuomba kutoka wodini kwa sababu alikuwa akijisikia uchungu anapowaona wanawake wenzake wodini humo wakiwakumbatia watoto wao baada ya kujifungua huku wa kwake wote wakiwa wamefariki dunia baada ya kuzaliwa. 

Alisema kuwa muda wote aliokuwa hospitalini hapo baada ya watoto wake kufariki huku akiwa bado anauguza kidonda cha upasuaji aliofanyiwa alikuwa akilia muda wote anapowaona wanawake wenzake waliojifungua wakiwakumbatia na kuwanyonyesha watoto wao hivyo akaamua kuomba aruhusiwe kutoka hospitalini hapo. 

 ‘’Niliomba kuruhusiwa kutoka hospitali na kwenda kujiuguza kidonda nyumbani kwa sababu ya uchungu na majonzi niiiyokuwa nikiyapata wodini hapo ninapowaona wanawake wenzangu waliojifungua wakiwakumbatia na kuwanyonyesha watoto wao huku wa kwangu wakiwa wameshazikwa”alisema Bi.Mgaya 

Aidha aliushukuru uongozi wa hospitali hiyo pamoja na wafanyakazi wote kwa namna walivyomuhudumia yeye pamoja na watoto wake watano waliozaliwa na kuishi kwa muda wa masaa ya kumi ambapo alisema kuwa yote yaliyotokea anaamini kuwa ni mapenzi ya Mungu.

Mganga Mkuu mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma Dkt.Benedict Ngaiza akizungumza na mwandishi wetu  kwa njia ya simu kuwa waliamua kuridhia ombi la mama huyo kuondoka hospitalini hapo baada ya kujiridhisha kuwa anaendelea vizuri kwa sababu walifanya kila walichoweza kukoa uhai wake na watoto lakini watoto walifariki baada ya masaa kumi. 

Wakizungumza baadhi ya wananchi waliomshuhudia mama huyo na watoto wake baada ya kuzaliwa na  kabla hawajafariki walisema kuwa kuna kila sababu kwa kila mwenye uwezo wa kumsaidia mama huyo kwa namna yoyote afanye hivyo
Bi.Marietha Ngonyani na Lusi Haule wakazi wa mjini Songea waliwaomba wananchi mbali mbali kujitolea kumsaidia mama huyo kwa sababu bado anauguza kidonda cha upasuaji aliofanyiwa na pia tukio hilo limemuathiri kisaikolojia pia hivyo anahitaji faraja. 

No comments:

Post a Comment