Saturday, May 18, 2013

NOAH SASA RUKSA KUBEBA ABIRIA KWA MASHARTI...

Gari aina ya Noah.
Baada ya kilio cha muda mrefu cha baadhi ya wasafirishaji, Serikali imeruhusu magari aina ya Noah kubeba abiria nchini.

Serikali imeiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), kutoa leseni hizo kwa masharti, kwa sababu magari hayo hayakuwa yameundwa kubeba abiria.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, alitangaza hayo bungeni jana wakati alipowasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
“Wizara imepokea malalamiko mengi kutoka mikoa kadhaa juu ya hatua za Sumatra kuzuia magari madogo aina ya Noah kutoa huduma za usafirishaji wa abiria,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza:
“Sababu zinazotolewa na Sumatra ni za msingi kwamba magari hayo hayakuundwa kubeba abiria kibiashara, kwani hayana uwezo mkubwa wa kubeba abiria wengi, hivyo kwa nauli elekezi za Sumatra, kamwe hayawezi kupata faida mpaka kwa kukiuka masharti ya leseni na hayana madirisha yanayofunguka sehemu ya nyuma ya gari.”
Dk Mwakyembe alisema hoja hizo ni za msingi, lakini kwa kuzingatia hali ngumu ya usafiri iliyopo nchini, iliyoilazimu Serikali iruhusu pikipiki za magurudumu mawili na magurudumu matatu kubeba abiria, inaagiza Sumatra kuchukua hatua kadhaa kuziruhusu Noah kubeba abiria.
Alizitaja hatua hizo ni kuandaa utaratibu wa kutoa leseni kwa Noah kwa sharti la kurekebisha madirisha yake ya nyuma, kubeba idadi ya abiria itakayotajwa na Sumatra na kwa nauli elekezi za mamlaka hiyo ambazo zitatangazwa baada ya kuwashirikisha wamiliki wa magari hayo.
“Kuhakiki leseni za udereva siyo tu kwa madereva wa Noah, bali pia kwa madereva wa pikipiki za magurudumu mawili na matatu.
“Kutoruhusu biashara ya Noah ndani ya majiji ambayo tayari yamechukua hatua mahsusi kuzuia matumizi ya magari madogo, mbali na teksi, yasiyoweza kubeba zaidi ya abiria 18,” alisema.

No comments:

Post a Comment