Mchungaji Bonnke |
MKUTANO wa Injili ambao inatarajiwa kuwa utahubiriwa na
mhubiri maarufu duniani, Reinherd Bonnke wa Ujeruman, umeanza jioni leo (Agosti
21) jijini Dar es Salaam, huku Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la “Ufufuo na
Uzima”, Josephat Gwajima akipewa nafasi ya kuomba amani itawale katika mkutano
huo na nchini kwa ujumla.
Gwajima, maarufu kama “Mzee wa Misukule” baada ya
kukaribishwa jukwaani (madhabahuni) umati wa watu ulishangilia kwa nguvu. Mwenyekiti
wa Kamati inayoratibu mkutano huo ni Askofu Magnus Mhiche. Mhiche ni makamu wa
askofu mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG).
Hata hivyo, ilielezwa kuwa mkutano huo utafunguliwa rasmi
kesho (Alhamis) baada ya kuwasili kwa Bonnke anayetarajiwa kutua nchini usiku
huu. Taarifa iliyotolewa mkutanoni ilisema Bonnke alichelewa kuwasili kutokana
na ratiba ya ndege aliyosafiri nayo kubadilika.
Kanisa la “Ufufuo na Uzima” ni miongoni mwa makanisa yenye
wafuasi wengi jijini Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa, kupewa nafasi ya kuombea
amani mkutano huo, kunatoa nafasi kwa waumini wa kanisa hilo ambalo kwa muda
mrefu lilikuwa kama limetengwa na makanisa ya Kipentekoste, kuhudhuria mkutano
huo.
Mchungaji Gwajima akiombea amani Taifa |
Mbali na Askofu Mhiche, wengine katika kamati ya maandalizi
ya mkutano huo ni; Katibu wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (PCT),
Askofu David; Mwenyekiti wa PCT, mkoa wa Dar es Salaam na ambaye ni Mchungaji
Kiongozi wa Kanisa la EAGT Mito ya Baraka, Bruno Mwakibolwa, Mchungaji Emmanuel
Mwasota, Mchungaji Bathlomew Sheggah, na Mchungaji E. Ntepa.
Hivi karibuni Gwajima alipewa nafasi ya kuomba kwa ajili ya
amani katika kongamano la maombi lililoratibiwa na PCT mkoa wa Dar es Salaam na
kufanyika katika Kanisa la Efatha Mwenge. Kanisa hilo linaongozwa na Mtume na
Nabii Josephat Mwingira. Kama ilivyo kwa Gwajima, Mtume na Nabii Mwingira naye
kwa muda mrefu amekuwa akitazamwa na Wapentekoste kama “sio mpentekoste
halisi”.
Baada ya tukio hilo kulitolewa kauli tofauti na viongozi wa
PCT. Mwenyekiti wa PCT mkoa wa Dar es Salaam, Mchungaji Mwakibolwa pamoja na
Katibu wa PCT Taifa, David Mwasota walisema kuwa, Mwingira na Gwajima walikuwa
“wamerekebisha” mambo fulani ya kiimani, hivyo kustahili hata kujiunga katika
PCT.
maelfu ya watu waliohudhulia mkutano |
Mwakibolwa alikaririwa akisema kuwa, haoni kama kuna tatizo
la kiimani kwa Mwingira na Gwajima kwani amewaona wote wananena kwa lugha.
Mwasota yeye alikaririwa akienda mbali zaidi ambapo alidai kuwa, Mwingira hana
tatizo tena na mchakato unafanyika wa kujiunga na PCT ila Gwajima kulikuwa na
mambo kidogo ya kurekebisha kiimani.
Hata hivyo, siku chache baadaye Mwenyekiti wa PCT Taifa, Askofu David Batenzi katika mahojiano
na Fungukasasa.blogspot.com alisema kuwa, kilichotokea ni kwamba PCT mkoa wa
Dar es Salaam waliomba tu kufanyia kongamano hilo katika Kanisa la Efatha kama
ambavyo wangeomba kufanyia katika ukumbi unaomilikiwa na kanisa Katoliki, na
jambo hilo halimaanishi kitu kingine.
Alikana kuwepo kwa mchakato wa mmojawapo wa watumishi hao
kupeleka maombi ya kujiunga katika PCT. Alisema kuwa, kwa utaratibu wa kujiunga
na PCT mwombaji hujaza fomu kisha huangaliwa misingi yake ya kiimani kama ni ya
Kipentekoste au la.
No comments:
Post a Comment