SIKU chache baada ya kukamatwa kwa
askari feki wa usalama barabarani, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, imewakamata watuhumiwa saba wa ujambazi, wakiwa na sare za
Polisi, huku mwingine akijifanya ofisa Usalama wa Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaa,
Suleiman Kova alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na sare za
Polisi jozi mbili.
Watuhumiwa hao ni Khamis Mkalikwa (40),
Magila Werema (31), Nurdin Bakari (46), Materu Marko (32), Louis Magoda
(34), Amos Enock (23) na Amiri Mohammed (45), wote wakazi wa jijini Dar
es Salaam.
Sare hizo, kwa mujibu wa Kamanda Kova,
ni zenye cheo cha Sajenti wa Kituo, huku jozi moja ikiwa na jina
linalosomeka SSGT A.M Mduvike.
Watuhumiwa hao walikamatwa jana katika
eneo la Kiluvya, baada ya askari kuweka mtego, ambao ulifanikiwa
kuwanasa. Alisema watu hao walikuwa wakitumia silaha, sare za jeshi la
Polisi na redio ya mawasiliano katika uhalifu wao na hivyo kuwafanya
baadhi ya watu kutupia lawama Jeshi la Polisi kwa kujihusisha na
uhalifu.
Alisema watuhumiwa hao, wanahusishwa na
uhalifu katika maeneo ya Boko, Tegeta, Mbweni, Bahari Beach, na maeneo
mengine ya jiji. Alisema watu hao ni hatari zaidi.
Watuhumiwa hao walikuwa wakitumia gari
aina ya Cresta GX, 100 yenye namba T 546 BWR na baada ya kuona
wamezingirwa na askari maeneo hayo, walifyatua risasi moja hewani,
lakini askari walipambana nao na kufanikiwa kuwakamata.
“Mbali na vitu hivyo pia wamekamatwa na
bastola moja aina ya Brown yenye namba B.3901, ambayo ilikuwa na risasi
nne na ganda moja, tunawashikilia kwa upelelezi na baada ya kukamilika
watafikishwa mahakamani,” alisema Kova.
Katika hatua nyingine, Kamanda Kova
alisema wanamshikilia mtuhumiwa Alquine Masubo (42) maarufu kama Claud,
kwa kosa la kujifanya ofisa wa Usalama wa Taifa.
Claud ambaye ni mkazi wa Yombo Buza,
alikamatwa akiwa na vielelezo mbalimbali pamoja na nyaraka za idara
hiyo, ambapo baada ya kuhojiwa alikiri kuwa yeye si mfanyakazi wa idara
hiyo.
Kova alisema mtuhumiwa huyo
alipopekuliwa zaidi, alikutwa na bastola aina ya Browing yenye namba A.
956188-CZ83 ikiwa na risasi 12 ndani ya kasha lake.
“Alipopekuliwa nyumbani kwake alikutwa
na bastola nyingine aina ya Maknov yenye namba BA4799 ikiwa na risasi 19
na kitabu cha mmiliki chenye namba CAR 00071678, ikiwa na jina la
P.1827 LT COL Mohammed Ambari, jambo ambalo haliwezekani kwa mtu mmoja
kumiliki silaha mbili,” alisema Kova.
Mtuhumiwa huyo pia alikutwa na
kitambulisho cha Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) chenye namba 7001- E.
1075 na kompyuta mpakato aina ya Toshiba.
“Huyu ni tapeli wa siku nyingi na
taarifa zake tulikuwa nazo, anatumia kivuli cha idara ya usalama wa
taifa kufanya utapeli, lakini sasa ndiyo mwisho wake na wananchi wamjue”
alisema.
No comments:
Post a Comment