BAADA ya
kuwa wametengwa kwa muda mrefu na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania
(PCT), ikidaiwa kuwa huduma zao zina utata, hatimaye Kiongozi Mkuu wa Huduma ya
Efatha, Mtume na Nabii Josephat Mwingira pamoja na Kiongozi Mkuu wa Kanisa la
“Ufufuo na Uzima”, Mchungaji Josephat Gwajima, maarufu kama “Mzee wa Misukule”,
‘wametakaswa.’
Kuthibitisha
kuwa Wapentekoste sasa hawana tatizo tena na huduma ya watumishi hao
wanaoongoza makanisa yenye wafuasi wengi (mega churches), Jumamosi ya Julai 20,
2013 PCT Mkoa wa Dar es Salaam wakishirikiana
na PCT Taifa, waliandaa maombi maalum
kwa ajili ya kuombea amani ya Taifa,
ambayo
yalifanyika katika Kanisa la Efatha, lililoko Mwenge, jijini Dar es
Salaam na kuhudhuriwa na Wapentekoste kutoka madhehebu mbalimbali, wakiwemo wa
Kanisa la “Ufufuo na Uzima” wakiongozwa na Gwajima mwenyewe.
Wengine
walioshiriki ni Katibu Mkuu wa PCT Taifa, Askofu David Mwasota. Huyu pia ni
askofu mkuu wa Kanisa la Naioth Gospel Assembly. Wengine ni Askofu Mkuu wa
Kanisa la Church of God of Prophecy, Erick Mwambigija na Mwenyekiti wa PCT Mkoa
wa Dar es Salaam, Askofu Bruno Mwakibolwa. Mwakibolwa pia ni mchungaji kiongozi
wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Mito ya Baraka,
Dar es Salaam. Kitaifa Kanisa la EAGT linaongozwa na Askofu Moses Kulola.
Mtume na Nabii Mwingira na mkewe, Eliakunda
walishiriki kikamilifu katika maombi hayo, huku kwa nyakati tofauti wakipata
nafasi ya kutoa neno. Eliakunda alizungumza huku akitiririsha machozi.
Askofu
Mwakibolwa aliliambia gazeti hili kuwa, hayo ni matokeo ya maombi ya
Wapentekoste ya siku 40 kwa ajili ya amani ya Tanzania yaliyoanza Julai Mosi,
mwaka huu ambayo yanayotarajiwa kuhitimishwa Agosti 11, mwaka huu. “Tunaomba
kwa ajili ya kuja pamoja kama kanisa. Tunataka kanisa liwe na umoja,” alisema
Mwakibolwa katika mahojiano na gazeti hili kwa njia ya simu, juzi Ijumaa.
Kwa muda wa
miaka mingi, hapa nchini huduma za kitume na kinabii katika Upentekoste
zimekuwa hazipewi nafasi kubwa kutokana na sababu mbalimbali. Staili ya
kuhubiri ya Mtume na Nabii Mwingira, ambayo huambatana na mizaha na vitendo
vyenye kuibua maswali mengi, imewafanya baadhi ya Wapentekoste kutoiamini
huduma ya mtumishi huyo.
Miongoni mwa
vitendo hivyo ni; kupuliza spika wakati wa kuombea wagonjwa na kumwagia maji
watu wakati wa kuwabatiza badala ya kuwazamisha kwenye maji mengi.
Vitendo vya
mifano hiyo na vingine ambavyo hufanywa madhabahuni na Mtume na Nabii huyo
maarufu anayetajwa kuwa miongoni mwa watumishi wenye utajiri mkubwa nchini,
vinachochea baadhi ya Wapentekoste kuihukumu huduma yake kuwa iko nje ya
misingi ya imani ya Kipentekoste.
Gwajima yeye
pamoja na mambo mengine amekuwa akituhumiwa na Wapentekoste kuwa na imani
inayodaiwa kuwa ni potofu, kutokana na mafundisho yake ya “kufufua misukule.”
Baadhi ya Wapentekoste wamekuwa wakitilia shaka huduma na mafundisho hayo na
hivyo kuhitimisha kuwa mafundisho ya mtumishi huyo yako kinyume na misingi ya
imani ya Kipentekoste.
Upinzani
ambao Mwingira na Gwajima wamekuwa wakiupata kutoka kwa Wapentekoste wenzao ni
sawa na ule ambao aliwahi kukabiliana nao Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel
Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe kwenye miaka ya mwishoni mwa 1990 hadi
mwanzoni mwa 2000.
Katika
kipindi hicho huduma ya Askofu Kakobe ambayo ilikuwa ikikokota makundi ya
waumini kutoka makanisa mbalimbali, yakiwemo ya Kipentekoste, ilikuwa ikipigwa
vita kali na Wapentekoste wenyewe, na wakati mwingine Kakobe kutuhumiwa kutumia
ushirikina.
Ili ‘kumtakasa’ Askofu Kakobe kulifanyika
kongamano kubwa kanisani kwake Mwenge, ambalo liliwashirikisha watumishi wa
Mungu mbalimbali wa makanisa ya Kipentekoste, wakiwemo wenye ushawishi mkubwa,
Askofu Moses Kulola na Emmanuel Lazaro. Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa kauli
za kuvunja ‘roho ya utengano’ na kutuhumiana mambo mbalimbali ya hovyo, lakini
baada ya kongamano hilo Kakobe hakujiunga na PCT hadi leo.
Akizungumzia tukio hilo la Wapentekoste
‘kumtambua’, Mtume na Nabii Mwingira alisema kuwa, anawapongeza viongozi wote
wa PCT kwa ujasiri wa kukubali kufanyia maombi kanisani kwake.
Hata hivyo,
alisema: “Wote ambao mmekubaliana na jambo hili la umoja ili liweze kwenda ni
lazima mkubali ‘kufa’. Kwahiyo hapa hakuna hata mmoja ambaye atatoka, lazima
muweke saini watumishi wa Mungu kwenye kitabu changu (kitabu cha wageni).
Wekeni saini zenu wote kama ishara ya kukubali ‘kufa’. Kwa kuwa jambo hili ni
la Mungu mwenyewe, hakuna ambaye atalizimisha, lazima kanisa la Mungu liwe na
umoja.”
Kutengwa na
kupigwa vita kwa mitume na manabii kuliwasukuma kuanzisha umoja wao
uliojulikana kama Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania ambao ulikuwa chini ya
uenyekiti wa Mwingira. Hata hivyo, umoja huo ulishindwa kuendelea kutokana na
kilichoelezwa baadaye kuwa ni viongozi wa umoja huo “kutaka ukubwa na
kupandisha chati huduma zao”.
Baada ya
umoja huo kusambaratika Mwingira alijiunga katika umoja wa mitume na manabii wa
Afrika. Mara kwa mara mitume na manabii kutoka nchi mbalimbali za Afrika
wamekuwa wakifika katika Kanisa la Efatha kuhubiri na kutoa huduma za kinabii.
Wanachama wa umoja huo wa mitume na manabii wa Afrika wana utajiri mkubwa.
Dalili za
Mwingira kuanza kutambuliwa na Wapentekoste kama Mpentekoste mwenzao halisi,
zilianza kuonekana mwanzoni mwa mwaka huu alipoalikwa na PCT kushiriki katika
mkutano mkubwa wa Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF), uliofanyika katika Ukumbi
wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Kurasini, jijini Dar es Salaam na
kuhudhuriwa na maaskofu wapatao 177.
Mkutano huo ulikuwa
unazungumzia madhila mbalimbali ambayo yanawakabili Wakristo ikiwemo baadhi ya
Wachungaji kukamatwa na kuwekwa mahabusu na hata kufikishwa mahakamani kwa
‘kosa’ la kuchinja wanyama kwa ajili ya kitoweo; kutishwa, kujeruhiwa na kuuawa
kwa viongozi wa dini ya Kikristo pamoja na kuchomwa moto na kuharibiwa kwa
nyumba za ibada za Kikristo
Kauli ya PCT
Katika
mahojiano na mwandishi wa habari hizi, Katibu Mkuu wa PCT, Askofu David Mwasota
alisema: “Kwa ujumla hawa akina Mwingira na Gwajima ni Wapentekoste wenzetu.
Hawana ujanja wa kwenda kwingine zaidi ya huku kwani imani wanayoiendesha ni ya
Kipentekoste. Mchakato unaendelea wa kuwapokea kuwa wanachama wa Baraza la
Makanisa ya Kipentekoste (PCT).
Hata hivyo,
kuna vitu fulani fulani ambavyo wanapaswa kuvikamilisha ndio wawe wanachama.
Lakini Mwingira kwa sasa yuko vizuri hivyo muda wowote anaweza kuwa mwanachama
mwenzetu.
Kwa upande
wa Gwajima kikwazo kikubwa kwa msingi wa imani yetu ni suala la misukule. Tulijaribu
kumuuliza kama mambo ya misukule ni msingi wa imani ametujibu kuwa yeye ‘anafufua’
nafsi na sio msingi wa imani. Hivyo huyu naye muda wowote akiishakamilisha
vigezo atakuwa mwanachama. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa Kanisa la
Kipentekoste linakuwa na umoja wa kweli”.
Alipoulizwa
kama anamtambua Mwingira kuwa ni mtumishi wa Mungu, Askofu Mwasota alijibu:
“Kwa hakika wote hawa Mwingira na Gwajima ni watumishi wa Mungu.”
Gazeti hili
lilipomtafuta Askofu Mwasota ili afafanue zaidi hakuweza kupatikana, baada ya
kuelezwa kuwa baada ya ibada hiyo alisafiri nje ya nchi.
Mwenyekiti
wa PCT Mkoa wa Dar es Salaam, Askofu Bruno Mwakibolwa alipoombwa na mwandishi
wa habari hizi kuzungumzia juu ya PCT ‘kuwatakasa’ Mwingira na Gwajima na
mtazamo wake kuhusu utumishi wao, alisema:
“Tofauti
lazima ziwepo, ila ninachojua umoja wa Kanisa ni jambo la muhimu, lazima
watumishi tuungane kumhubiri Yesu na watu waokoke. Nilichokiona Mwingira
amenena kwa lugha na Gwajima amenena kwa lugha, hivyo hawa ni wenzetu na kazi
inaonekana”.
Alipoombwa
kwa msisitizo kujibu iwapo Mwingira ni Mtumishi wa Mungu, Askofu Mwakibolwa
alijibu: “Kinachotakiwa ni kumhubiri Yesu, mimi kama mwenyekiti wa PCT mkoa wa
Dar es Salaam nimefanikisha kuwaunganisha watumishi wakubwa kama hawa, hivyo
nikiwa na jambo la kuhubiri Yesu nikiwashirikisha watumishi kama hawa kazi
inakuwa rahisi, hivyo ni wenzetu, hawa ni Wapentekoste”.
Baadaye
Mwakibolwa katika mahojiano na gazeti hili kwa njia ya simu alisema: “Ni kweli
maombi hayo tuliandaa PCT mkoa wa Dar es Salaam pamoja na PCT Taifa. Haya ni
matokeo ya maombi ya siku 40 tunayoyafanya. Unajua lengo letu ni kuona tunakuja
pamoja kama Wapentekoste. Tunaomba amani na kuona kanisa linakuja pamoja.
Unajua tangu
nimekuwa mwenyekiti wa PCT mkoa wa Dar es Salaam ninaona Mungu anatuleta
pamoja. Wewe bila shaka unafahamu hata TAG hawakuwa wanachama wa PCT lakini leo
ni wanachama. Kama tunakaa na Wakatoliki kwenye Jukwaa la Wakristo (TCF)
kwanini tusikae na hawa wenzetu?”
Alipoulizwa
kuwa kwenye jukwaa wanakutana taasisi zinazowaunganisha Wakristo wanaopishana
katika baadhi ya mambo ya msingi kiimani, lakini Mwingira na Gwajima wamekuwa
wakilalamikiwa kuwa huduma zao zinaendeshwa kinyume na Upentekoste, sasa kwa
kauli yake inamaanisha watumishi hao wamebadilika na kuendesha huduma zao
Kipentekoste halisi, Askofu Mwakibolwa alisema:
“Mimi sioni
kama kuna tatizo, nimewaona wakikemea dhambi na nimewaona wakinena kwa lugha.
Unajua kama nilivyokueleza, tunataka tumhubiri Yesu Kristo tukiwa na unyoofu wa
moyo, tuwe na upendo kama ilivyoandikwa katika Zaburi 33.”
Andiko hilo
linasema: “Mpigieni BWANA vigelegele, enyi wenye haki, Kusifu kunawapasa
wanyofu wa moyo.”
Mwingira aendeleza mizaha
Katika hali
iliyoonesha kuwa Mwingira ni mtumishi asiyeishiwa mizaha, wakati akitoa neno la
shukrani kwenye ibada hiyo ya kuombea Taifa, huku akicheka alimrushia utani
Mchungaji Gwajima akisema: “Nina mashaka na usukuma wa Gwajima, maishani kwangu
sijawahi kuona msukuma mfupi kama huyu (Gwajima). Nahisi kwa kuwa usukumani
kuna machimbo ya dhahabu nahisi Wapare ‘walifanya fujo’.”
Mwingira hakufafanua
kuhusu Wapare kufanya fujo. Inaaminika kuwa wanaume Wapare ni wafupi. Mwingira
ni Mngoni. Kijadi Wangoni na Wasukuma ni watani. Gwajima hakuonekana kujali
mzaha huo na badala yake alionekana kama mtu anayemtafakari Bwana.
Maombi yenyewe
PCT wameitisha
maombi kwa ajili ya kulilia amani ya nchi. Maombi hayo ambayo ni kwa makanisa
yote ya Kipentekoste nchini yalianza Julai, mosi mwaka huu na yanatarajiwa
kuhitimishwa Agosti 11, mwaka huu.
Uamuzi wa
kufanyika kwa maombi hayo nchi nzima ulifikiwa katika Mkutano Mkuu wa PCT
uliofanyika mjini Dodoma, hivi karibuni. Mkutano huo ndio uliwapa nafasi ya
kuendelea na uongozi Askofu Mwasota (Katibu) na Askofu David Batenzi
(Mwenyekiti).
Ibada hiyo
iliyofanyika Efatha Mwenge kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa nane mchana,
ilihudhuriwa na idadi kubwa ya waumini wa madhehebu ya Kipentekoste.
Ibada hiyo
iliongozwa na Askofu Mwasota akishirikiana na watumishi wengine. Gwajima
aliombea viongozi wa Taifa na mke wa Mwingira, Eliakunda aliombea kanisa liwe
na umoja. Kabla ya kuomba alimwaga machozi akisema amekuwa akikerwa mno na hali
ya kanisa kukosa umoja.
No comments:
Post a Comment