KULIA: Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es Salaam. KUSHOTO: Dk Harrison Mwakyembe. |
Kuanzia
sasa viongozi wote serikalini watakaopita kwenye viwanja vya ndege
nchini, watakuwa wakikaguliwa kama abiria wengine, isipokuwa Rais,
Makamu wake, Waziri Mkuu, Jaji Mkuu na Spika wa Bunge.
Waziri
wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema ipo tabia ya viongozi wenye
madaraka, kukiuka utaratibu na kupita katika viwanja vya ndege bila
kukaguliwa.
Alisema
kutokana na hali hiyo, amewaambia watumishi wanaofanya kazi katika
viwanja hivyo, hususan Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere
(JNIA) viongozi wasiokaguliwa ni Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Jaji
Mkuu na Spika wa Bunge.
Alitoa
msimamo huo wiki iliyopita kupitia kipindi cha Jenerali on Monday,
kinachorushwa na Televisheni ya Channel Ten. Alisema viongozi wengine
wote, wakiwamo mabalozi na mawaziri lazima wakaguliwe.
Dk
Mwakyembe alisema aliwaambia viongozi wasiopenda kukaguliwa, wasipande
ndege. Alisema pamoja na baadhi kuona ni usumbufu, inawezekana
wakajikuta wamesahau vitu hatari, kama vile risasi na wakaenda
kugundulika nje ya nchi ikawa tatizo.
Alitoa
mfano kwamba aliwahi kupigiwa simu na mmoja wa mabalozi, akilalamika
kwamba vijana wake wamemkagua uwanja wa ndege. Alisema alimjibu kwamba
wanatimiza wajibu wao.
Katika
mahojiano yaliyojikita juu ya tatizo la dawa za kulevya nchini, Dk
Mwakyembe alisisitiza kwamba hatua alizoanza kuchukua kudhibiti
upitishaji dawa hizo kwenye viwanja vya ndege, siyo moto wa kifuu wala
nguvu ya soda.
“Ninachokifanya
hapa ni kile ambacho kinapaswa kufanywa…na hili la dawa za kulevya
katika viwanja vya ndege, nitalikomesha,” alisema. Alisisitiza kwamba
udhibiti huo ni kwa viwanja vyote vya ndege nchini.
Dk
Mwakyembe alisema, “kwa sasa mizigo yote inayoingia katika eneo hilo,
lazima ikaguliwe, kwani huo sio mzaha, sio moto wa kifuu wala nguvu ya
soda.”
Kwa
mujibu wa Waziri, mizigo inayoingia imekuwa haikaguliwi. Alisema katika
kutekeleza ukaguzi huo wa mizigo inayoingia, imenunuliwa mitambo kwa
ajili hiyo.
Kuhusu wanaomeza dawa za kulevya, alisema wamekuwa wakigundulika kutokana na ufuatiliaji kuanzia kwenye ndege.
Alitoa
mfano kwamba kwa sasa endapo abiria atapanda ndege katika uwanja wa
ndege wa Dar es Salaam, mathalani kwenda Dubai, akipewa chai au pombe,
akakataa kunywa, kwa vyovyote huyo lazima akaguliwe zaidi.
Katika
hilo, aliwaasa vijana wa Tanzania kujiepusha na hali hiyo, kwani pindi
akishuka kwenye uwanja wowote, namba yake ya kiti itashikiliwa na
atakaguliwa ipasavyo, kubaini kama amemeza dawa.
Hatua ya
Mwakyembe kuamua kuvalia njuga dawa za kulevya, inatokana na kile
ambacho kinaelezwa kuwa ni kuchafuka kwa Tanzania, kutokana na baadhi ya
watanzania kukamatwa nje ya nchi, wakisafirisha dawa hizo, wakiwa
wamezipitisha uwanja wa ndege.
Dk Mwakyembe alieleza kuwa hatua yake ya kuvalia njuga suala hilo, inaungwa mkono na serikali kwa ujumla.
Hivi
karibuni waziri huyo alifanya ziara ya ghafla katika uwanja wa ndege wa
Mwalimu Nyerere na kubaini kuwa tatizo si vifaa vya ukaguzi, bali ni
baadhi ya wafanyakazi wasio waadilifu.
Msemaji
Mkuu wa Serikali ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO),
Assah Mwambene alisema hivi karibuni serikali imeanzisha mkakati wa
kutokomeza wimbi la dawa za kulevya kwa kudhibiti viwanja vya ndege na
sehemu mbalimbali za mipakani, zinazotumiwa kupitisha.
Picha na zirro blog.
No comments:
Post a Comment