Kanisa la Minara Miwili, Unguja ambako Sista huyo na wenzake wanafanyia kazi. |
Watawa wa
kike wa Shirika la Moyo Safi wa Maria, Mgolole, Morogoro, wanaofanya
kazi katika Parokia ya Minara Miwili, Unguja, wameiomba Serikali
kuongeza ulinzi kwenye maeneo ya kiimani.
Wametoa mwito huo, baada ya jana kuvamiwa na kundi la watu kwenye
makazi yao na kumpiga mmoja, Irene Mwenda na kumvua shela kichwani.
Tukio hilo japo lilihusisha majirani; nyumba ya watawa ya Bububu na
majirani wa karibu na nyumba hiyo, waliodai kuku wao aling’atwa na mbwa
wa watawa hao, watu wengine waliingilia ugomvi huo wakiwa na wenye kuku
na kubishana na watawa hao, jambo lililosababisha ugomvi na hata baadhi
yao kumpiga mtawa huyo na kumvua shela.
Mtawa Mkubwa wa Nyumba ya watawa hao visiwani, Sista Gaspara,
alimwambia mwandishi jana kuwa tukio hilo halikuwa kubwa kiasi cha
Polisi kuingilia kati.
Lakini, alisema ilibidi wapige simu Polisi baada ya kuona kundi la
watu, wengi wakiwa vijana na silaha za jadi yakiwamo mawe, wakizungumza
kwa jazba na matusi, wakidai kuku wao aling’atwa na mbwa wa watawa na
bila kusubiri mazungumzo na namna ya kulipwa, walianza kumpiga mtawa
mmoja.
“Ilikuwa saa 11 jioni jana (juzi), tulikuwa tumerudi kutoka shughuli
za ibada nje ya hapa nyumbani, tulipofika likaja kundi la vijana na
watoto wakidai mbwa wetu amemng’ata kuku wao, wakati Sista Mwenda
akiuliza imekuwaje mbwa ang’ate kuku kwa kuwa huwa tunawafungia ndani,
mmoja alimpiga sista ngumi chini ya jicho na sehemu zingine za mwili,”
alidai Sista Gaspara.
Alidai Sista Mwenda alitaka vijana wale wasiohusika na kuku waondoke,
ili wasijae sana pale na abaki mmiliki wa kuku ili wazungumzie tukio
hilo na namna ya kumfidia, maana nyumba ya watawa ina uzio na kuku huyo
alirukia ndani kwa kuwa milango ilikuwa imefungwa.
Sista Gaspara alidai kuwa kinachosikitisha si kipigo dhidi ya mtawa,
kwa kuwa hakuna damu iliyomwagika ila maumivu ya kawaida aliyopata na
kutibiwa katika hospitali ya Jeshi ya Kibweni, lakini kibaya ni namna
walivyopandisha jazba kuhusu tukio hilo na kitendo cha kumvua mtawa
shela na kuitupa.
Katika utaratibu wa Kanisa Katoliki, shela anayovaa mtawa inabeba
maana halisi ya kiimani ya utawa wake, hivyo kitendo cha kuvuliwa
kitambaa ni sawa na kuvuliwa utawa. Hata hivyo, waliiomba Serikali
kuongeza elimu ya maadili shuleni, wazazi kufunza nidhamu watoto wao na
jamii nzima kuheshimu maadili na kuishi kwa amani na utulivu.
Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wa Zanzibar, Yusuf Ilembo,
alithibitisha kutokea tukio hilo lakini akasema ulikuwa ni ugomvi wa
kawaida wa majirani kwa majirani, hivyo pamoja na kwamba Polisi
ilishirikishwa, lakini uliisha kiujirani.
“Ni kweli suala limetokea, lakini ni ugomvi mdogo wa jirani na
jirani, kuku aliingia nyumbani kwa watawa, pale wanafuga mbwa,
akang’atwa, wenye kuku walikwenda kudai, ndipo ugomvi ukatokea mmoja
akampiga mtawa ila hakuna damu iliyomwagika,” alisema Ilembo.
No comments:
Post a Comment