KATIBU
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdul-rahman Kinana amemfungulia kesi
Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema),
Kutokana na kumtuhumu
anajihusisha na ujangili na biashara haramu ya pembe za ndovu.
Kinana
amefungua kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutokana
na kitendo cha Mbunge huyo kutoa tuhuma hizo dhidi yake kwa nyakati
tofauti nje na ndani ya Bunge, pia alikataa kuzikanusha na kumuomba
radhi.
Inadaiwa
kuwa Aprili 21 mwaka huu Msigwa ambaye ni Waziri Kivuli wa Maliasili na
Utalii alitoa tuhuma hizo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika
Shule ya Msingi Mbuguni wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.
Aidha
alizitoa bungeni wakati akiwasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani katika
Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka
2013/2014. Katika hati ya madai, Kinana anadai kuwa kutokana na tuhuma
hizo ameharibiwa tabia yake, uaminifu, hadhi yake kitaaluma na weledi na
kumfanya achukiwe na kudharauliwa katika jamii.
Anadai
kuwa kabla ya tuhuma hizo alikuwa katika hatua za mwisho za mchakato wa
mazungumzo ya mradi wa ubia wa kilimo cha mboga na mwekezaji kutoka
kampuni ya nje, lakini tuhuma hizo zimesababisha kampuni hiyo kuvunja
majadiliano hayo.
Kinana
anadai kuwa sababu iliyotolewa na kampuni hiyo kuvunja mazungumzo hayo
ni kutajwa kwake na mbunge huyo kuwa ni jangili anayejishughulisha na
biashara hiyo.
Kwa
mujibu wa hati ya madai, Mradi huo ulikuwa na thamani ya Dola za
Marekani milioni nne, Hisa za ushiriki wa Kinana zilikuwa ni asilimia 25
katika kipindi cha miaka mitano hivyo anatathmini kuwa amepata hasara
ya Sh milioni 350.
Kinana
anaiomba Mahakama hiyo imwamuru Msigwa amlipe fidia ya Sh milioni 350
kama hasara rasmi, pamoja na fidia ya maudhi na fidia ya hasara ikiwemo
gharama za kesi.
Aidha
anaiomba Mahakama imwamuru amlipe riba kwa kiwango kitakachopangwa na
Mahakama, tangu tarehe ya hukumu hadi malipo ya mwisho, imwamuru kufuta
tuhuma dhidi yake na kumuomba radhi kwa kuchapisha katika magazeti
mawili ya Kingereza na mawili ya Kiswahili yanayosambazwa nchini.
Pia
Mahakama itoe zuio la kudumu kumzuia Msigwa, au wakala wake kutoa au
kuchapisha taarifa zozote za kashfa dhidi yake. Katika hati ya madai
amenukuu baadhi ya kauli za Msigwa, ikiwemo "Kinana (naomba waandishi wa
habari mnisikie na nyie Usalama wa Taifa mkapeleke habari) hana sifa za
kupita barabarani na kuwaambia Watanzania waiamini CCM. Kinana mikono
yake si misafi."
"Hata
kwenye Nassaco, Shirika la Meli Tanzania kuna harufu ya ufisadi ndani
yake; ajibu hoja...Kinana meli zake ndizo zinazohusika kubeba pembe za
ndovu nchini. hajajibu hoja hizo! Kwa siku nchi hii tembo 67 wanauawa.
"Hao
ndio wanaokifadhili Chama Cha Mapinduzi, halafu wanakuja eti
kuwashawishi Watanzania muwasikilize na kwamba Chama Cha Mapinduzi eti
ni kizuri."
".Haya
mambo ninayoongea ni hatari kwa sababu haya yote ni majangili ni
organized Crime. Ni mtandao wa Kimafia, uko duniani kote, unaweza
ukatuua lakini wabunge tumesimama tunawatetea..."
Chanzo, HabariLeo.
No comments:
Post a Comment