Thursday, June 20, 2013

Wabunge Chadema wasimulia mkong’oto Soma hapa Ilikuaje


Mbunge wa Singida Mashariki,Tundu Lissu akiwaonyesha waandishi wa habari miwani yake aliyodai kuvunjiwa na polisi. Lissu alipata dhamana katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati, jijini Arusha jana baada ya kukamatwa juzi. Picha na Moses Mashalla 
Arusha/Dar es Salaam. Wabunge wanne wa Chadema, ambao waliachiwa na polisi kwa dhamana wamesimulia mateso waliyoyapata wakiwa rumande baada ya kukamatwa juzi.
Vigogo hao; Mbunge wa Mpanda Mjini Said Amour Arfi, Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mustapha Akunaay (Mbulu) na Joyce Mukya (Viti maalumu), walikamatwa juzi baada ya wao na wafuasi wa chama hicho kutawanywa kwa mabomu ya machozi na polisi kwenye Viwanja vya Soweto, Arusha.
Wabunge hao waliachiwa baada ya kujidhamini wenyewe huku watu wengine 65 waliokamatwa pamoja nao wakiachiwa baada ya kudhaminiwa.
Wote wanatakiwa kuripoti kwenye kituo hicho Julai 22, mwaka huu na wataelezwa hatma ya suala hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja alisema jeshi lake linaendelea kuwasaka Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha, Godbless Lema na kuwaonya kuwa wanatakiwa kujisalimisha mara moja.
Chagonja alisema Mbowe na Lema wanatafutwa kwa kosa la kufanya kusanyiko lisilo halali katika viwanja hivyo vya Soweto walipokuwa wakitaka kuomboleza vifo vya watu watatu; Judith Moshi, Ramadhan Juma na Amir Ally waliofariki dunia baada ya kuumizwa kutokana na mlipuko wa bomu, Jumamosi iliyopita.
Pia aliwaamuru Mbowe na Lema kuwasilisha mara moja ushahidi wa kuwahusisha polisi na shambulio la bomu na kama hawana imani na Polisi, basi wawasilishe ushahidi wao kwa Rais Jakaya Kikwete.
Lissu
Lissu, ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alilalamikia kitendo cha polisi kumwagia maji ya kuwasha baada ya kumkamata.
“Walinimwagia maji ya kuwasha kwa mfululizo nikalazimika kulala chini kifudifudi huku nikiwa nimefunika macho kukwepa yasiingie maji. “Kuna askari walitaka kunipiga lakini niliokolewa na mwenzao mmoja aliyenikinga nisishambuliwe. Kwa kweli ilikuwa hali ya hatari,” alisema.
Alisema polisi hao waliomkamata walivunja miwani yake kwa makusudi akisema aliikabidhi kaunta ikiwa haijavunjika.
“Wakati naingia mahabusu nilikabidhi miwani yangu lakini ajabu wakati tukiachiwa ilikuwa imevunjika.” Alilalamikia hatua ya polisi kuwashambulia kwa mabomu, kuwamwagia maji ya kuwasha walipokuwa wakiwatawanya watu waliokusanyika Soweto akisema awali, waliwaruhusu.

source Gazeti la mwanainchi

No comments:

Post a Comment