Moja ya majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). |
Suala la uwepo wa rushwa ya ngono kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) limetinga bungeni.
Lilijitokeza jana wakati Mbunge wa Kilwa
Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), alipomaliza kujieleza bungeni akiomba
kura kwa wabunge wamchague awe mjumbe kwenye taasisi hiyo.
Baada ya Mbunge huyo kumaliza kujieleza,
alisimama Mbunge wa Viti Maalumu, Naibu Waziri wa Jinsia na Watoto, Ummy
Ally Mwalimu aliyemhoji atatoa mchango gani katika kupambana na
changamoto kwenye chuo hicho, ikiwamo rushwa ya ngono na ukatili wa
kijinsia, ili kusaidia watoto wa kike wasome vizuri.
Kabla
ya Mangungu kujibu swali hilo, Mbunge wa Chakechake, Mussa Haji Kombo
(CUF), aliomba Mwongozo wa Spika kutaka muuliza swali afute kauli yake
kwani ni ya udhalilishaji na inaweza kuleta matatizo. Hata hivyo, Spika
Anne Makinda aliingilia kati na kusema hakuna haja ya kufuta kauli hiyo
kwa vile ndiyo hali halisi iliyopo.
Akijibu swali hilo, Mangungu alisema atasaidiana na wenzake kuhakikisha wanakomesha suala hilo.
Katika uchaguzi huo, Mbunge wa Kisarawe,
Suleiman Jaffo (CCM) alichaguliwa kuwa mjumbe kwenye Jukwaa la Kibunge
la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC-PF)
katika uchaguzi uliofanyika bungeni.
Akitangaza matokeo, Spika Makinda alisema
Jaffo aliibuka kidedea baada ya kupata kura 74 na kuwashinda wapinzani
wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere (Chadema) aliyepata kura
56 na Mbunge wa Busanda, Lorensia Bukwimba (CCM) aliyepata kura 51.
Kura 182 zilipigwa na moja kuharibika.
Pia Spika Makinda alimtangaza Mangungu
mshindi na kuwa mjumbe wa Baraza la Udom kwa kupata kura 137 dhidi ya 38
za mpinzani wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Pudenciana Kikwembe (CCM).
Kura 177 zilipigwa na mbili kuharibika.
Upande wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) aliyeibuka mshindi ni Mbunge wa Babati Vijijini, Jitu Soni (CCM)
ambaye hakuwa na mpinzani baada ya Mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu
(CCM) kujitoa.
Pia Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana
(CCM) aliibuka kidedea kwa ujumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi
na Teknolojia, Mbeya, baada ya kukosa mpinzani.
Chanzo:ziro99blog
No comments:
Post a Comment