Saturday, August 10, 2013

POST HIII IMENIGUSA SANA. NAOMBA MUISOME JAMANI,

 INASOMEKA HV:

Ni siku nyingi kidogo, mwaka 1979, lakini ni
tukio ambalo liliniuma sana. Ilikuwa vigumu
sana kulisahau na lilinifanya nijiulize,
inakuwaje Mungu anakuwa mkatili kiasi kile.
Lakini bila shaka ilikuwa ni wakati ule wa
ufahamu mdogo. Hivi sasa ninafahamu mengi
na hasa baada ya kujifunza maarifa haya ya
utambuzi.
Ilikuwa ni mwaka 1979 nikiwa nasafiri
kutokea Dar es salaam kwenda Arusha. Sijui
ilikuwaje, lakini ilitokea. Tuliondoka Dar es
salaam saa 12.30 jioni. Wakati ule mabasi
yalikuwa yakisafiri jioni na usiku, sio kama
siku hizi.
Nilikuwa ninakwenda Arusha kwenye usaili
kwa ajili ya ajira, nikiwa ndio kwanza
nimemaliza kidato cha nne. Niliajiriwa moja
kwa moja serikalini, kwani siku zile ajira
zilikuwa ni za kumwaga. Hata hivyo
sikuridhishwa na kazi niliyokuwa nafanya,
hivyo niliomba kazi kwenye kampuni moja
kule Arusha na niliitwa kwa usaili.
Tulifika mji unaoitwa Korogwe ambao wakati
ule ulikuwa ndio mji maarufu kwa hoteli zake
katika barabara yote ya Segera hadi Moshi na
Arusha. Tulipofika Korogwe basi letu
lilisimama kwa ajili ya abiria kupata chakula.
Niliingia kwenye hoteli moja ambayo
nakumbuka hadi leo kwamba ilikuwa ikiitwa
Bamboo. Niliagiza chakula na kula haraka
kutokana na muda mfupi wa kula uliotolewa
na wenye basi la TTBS ambalo ndilo nililosafiri
nalo.
Wakati wa kulipa ndipo niliposhangaa na
kuogopa. Niliingiza mkono mifukoni na
kukuta kwamba sikuwa na hela. Nilianza
kubabaika na mwenye hoteli alisema hawezi
kukubali ujinga huo, "Abiria wengine wahuni
bwana, anakula na kujifanya kaibiwa,
ukikubaliana nao kila siku hasara tu" Mwenye
hoteli alisema kwa kudhamiria hasa.
Kulizuka zogo kubwa, huku mwenye hoteli
akisema ni lazima anipeleke polisi. Ni kweli
alimtuma mmoja wa watumishi wake
kwenda kituo cha polisi ili nishughulikiwe……
Hapo Hotelini kulikuwa na bwana mmoja
aliyekuwa amekaa pembeni na mkewe na
watoto wao wakila. Yule bwana alipoona vile
alimtuma mhudumu mmoja aniite. Niliondoka
pale kaunta nilipokuwa nabembeleza na kuja
kwa yule bwana.
Alikuwa ni kijana mtu mzima kidogo,
mwenye miaka kama 50 hivi. Nilimsalimia na
aliitikia, nilimsalimia mkewe pia. Yule bwana
aliniuliza kisa cha vurugu ile na nilimsimulia.
Aliniuliza sasa huko Arusha ningeishi vipi
wakati wa usaili wakati nimeibiwa fedha zote
na ningerudi vipi Dar. Nilimwambia nilikuwa
napanga namna ya kurudi Dar, kama huko
polisi ningeaminika.
Kama mzaha vile yule bwana aliniambia kuwa
angenipa fedha za kutumia huko Arusha na
nikirudi Dar nimrudishie fedha zake.
Nakumbuka alinipa shilingi 90 kwa ahadi
kwamba nikirudi Dar nimpelekee fedha zake
ofisini kwake. Alinielekeza ofisini kwake,
mtaa wa Nkuruma na kuniambia kuwa
ameamua kunisaidia kwa sababu kila
binadamu anahitaji msaada wa mwingine na
maisha haya ni mzunguko. Nilimshukuru na
kuondoka kukimbilia basini. Basi lilikuwa
linanisubiri mimi tu. Nilipanda ndani ya basi
na abiria wengine walinipa pole. Tuliondoka
Korogwe, lakini haikuchukua muda basi letu
lilipata tatizo la pancha ya gurudumu moja la
mbele. Ilibidi tuegeshe pembeni ili
litengenezwe. Baada ya matengenezo,
tuliondoka kuendelea na safari yetu.
Karibu na mji wa Same kwenye saa saba
usiku, basi letu lilisimama ghafla. Abiria
walisimama ndani ya basi na kulizuka aina ya
kusukumana. Huko nje kulikuwa na ajali.
Abiria tulishuka haraka na wengine huko
chini walishaanza kupiga mayowe, hasa
wanawake. Niliposhuka niliona gari ndogo
nyeusi ikiwa imebondeka sana na hapo
kando kulikuwa na maiti wawili.
Nilijua ni maiti kwa sababu walikuwa
wamefunikwa gubigubi. Halafu kulikuwa na
katoto kalikokuwa kanalia sana kakiwa
kamefungwa kanga kichwani. Tumwahishe
huyu mtoto hapo Same hospitali ameumia,
ingawa sio sana. Nilikatazama kale katoto ka
kiume kenye umri wa miaka kama mitatu.
Kalikuwa kameumie kwenye paji la uso, lakini
kalikuwa hai. Bila shaka wale walikuwa ni
wazazi wake, kalikuwa yatima tayari. Machozi
yalinitoka.
Baada ya kupata msaada na askari wa
usalama barabarani kuchukua maiti wale
tulipanda basini kuendelea na safari yetu.
Kale katoto kalichukuliwa na jamaa fulani
waliokuwa na Land Rover ya serikali
kukimbizwa hospitalini. Ndani ya Basi
mazungumzo yalikuwa ni kuhusu ajali ile tu,
hadi tunafika Arusha. Tulichelewa sana kufika
Arusha kwani tulifika kwenye saa tano
asubuhi, badala ya saa mbili .
Nililala kwenye hoteli rahisi na kufanya usaili
kesho yake. Ni hiyo kesho, baada ya usaili
niliponunua gazeti ambapo nilipata mshtuko
mkubwa ajabu. Kumbe wale watu wawili
waliokufa kwenye ajali ile ya Same walikuwa
ni yule bwana aliyenisaidia hela na mkewe.
Yule mtoto wao ndiye aliyeokoka. Niligundua
hilo baada ya kusoma jina lake na jina la
kampuni aliponiambia nimpelekee fedha zake
nikirudi Dar, pamoja na picha yake, mke na
mtoto. Nililia sana, kama mtoto.
Nillishindwa kujua ni kwa nini afe. Nilijiuliza
ni nani sasa angemlea mtoto yule? Yalikuwa
ni maswali yasiyo na majibu na pengine
maswali ya kijinga pia.
Nilijua kwamba nilikuwa na deni, deni la
shilingi tisini. Kwa wakati ule shilingi tisini
zilikuwa ni sawa na shilingi laki moja za sasa.
Kwa mara ya kwanza sasa nilijiuliza ni kwa
nini marehemu yule aliniamini nakuamua
kunipa fedha zile. Sikupata jibu.
Nilikata kipande kile cha gazeti la kingereza
kilichokuwa na habari ile. Nilichukuwa
kipande hicho na kukiweka kwenye Diary
yangu. Deni, Ningelipa vipi deni la watu?
Nilijikuta nikipiga magoti na kuomba mungu
anipe uwezo wa kuja kulilipa deni la mtu yule
mwema kwa njia yoyote. 'Mungu naomba uje
uniwezeshe kulilipa deni la marehemu kwa
sura na namna ujuavyo wewe. Nataka kulilipa
deni hili ili nami niwe nimemfanyia jambo
marehemu,' niliomba. Nilirejea Dar siku hiyo
hiyo.Kwa sababu ya mambo mengi na hasa
baada ya matokeo ya usaili ule kuwa mbaya
kwangu, nilijikuta nikiwa na mambo mengi
na kusahau haraka sana kuhusu mtu yule
aliyenisaidia mbaye ni marehemu.
Nilifanikiwa hata hivyo kupata nafasi ya
kusoma Chuo cha Saruji na baadae chuo cha
ufundi na hatimaye nilibahatika kwenda
nchini Uingereza. Mwaka 1991 nilianza
shughuli zangu.
Ilikuwa ni mwaka 1995 nikiwa ofisini
kwangu pale lilipokuwa jengo Nasaco ambalo
liliungua mwaka 1996, ambapo lilijengwa
upya na kubadilishwa jina na kuitwa Water
Front. Nikiwa nafanya kazi zangu niliambiwa
na sekratari wangu kwamba kulikuwa na
kijana aliyekuwa anataka kuniona. Nilimuuliza
ni kijana gani, akasema hamjui. Nilimwambia
amruhusu aingie. Kijana huyo aliingia ofisini.
Alikuwa ni kijana mdogo wa umri miaka
kama 17 au 18 hivi, mweupe mrefu kidogo.
Alikuwa amevaa bora liende , yaani
hovyohovyo huku afya yake ikiwa hairidhishi
sana.
Nilimkaribisha ilimradi basi tu, kwani niliona
atanipotezea bure muda wangu. Ni lazima
niwe mkweli kwamba sikuwa mtu mwenye
huruma sana na nilikuwa naamini sana
katika watu wenye pesa au majina.
Nilimuuliza, “nikusaidie nini kijana na
ukifanya haraka nitashukuru maana nina
kikao baada ya muda mfupi”. Nilisema na
sikuwa na kikao chochote , lakini nilitaka tu
aondoke haraka.
“Samahani mzee, nilikuwa na
shida…..nimefukuzwa shule na sina tena mtu
wakunisaidia kwa sababu …..nime….niko
….kidato cha pili na hivyo tu natafuta tu kama
atatokea mtu……..
Nilimkatisha. “Sikiliza kijana. Kama huna
jambo lingine la kusema, ni bora ukaniacha
nifanye kazi. Hivi unafikiri kama nikiamua
kumsaidia kila mtu aliyefukuzwa shule si
nitarudi kwetu kwa miguu! Nenda Wizara ya
Elimu waambie……Kwanza wazazi wako
wanafanya kitu gani, kwa nini washindwe
…..Kwa nini walikupeleka shule ya kulipia
kama hawana uwezo, wanataka sifa?”
“Hapana wazazi wangu walikufa na
ninasoma shule ya serikali. Nimekosa mahitaji
ya msingi na nauli ya kwendea shule. Nasoma
shule ya Kwiro, Morogoro. Shangazi ndiye
anayenisomesha, naye ana kansa na hivi sasa
hata kazi hafanyi….,” Alianza kulia. Huruma
fulani ilinijia na nilijiambia, kama ni nauli tu
na matumizi, kwa nini nisiwe mwema,
angalau kwa mara moja tu. “Baba na mama
walifariki lini?” Niliuliza nikijua kwamba,
watakuwa wamekufa kwa ukimwi, maana
kipindi kile ndipo fasheni ya ukimwi
ilipoanza, ambapo kila anayekufa
huhesabiwa kwamba kafa kwa ukimwi.
“Walikufa kwa ajali nilipokuwa mdogo sana,
nilipokuwa na miaka mitatu. Ndio shangazi
yangu akanichukua na kunilea hadi sasa
anakufa kwa kansa.” Yule kijana alilia zaidi.
Naomba nikwambie wewe msomaji
unayesoma hapa kwamba, kuna nguvu fulani
na sasa naamini kwamba ziko nyingi ambazo
huwa zinaongoza maisha yetu bila sisi kujua.
Kitu fulani kilinipiga akilini paaa! Nilijikuta
namuuliza yuel kijana. “Kwa nini umeamua
kuja kwangu, ni nani alikuelekeza hapa na
wazazi wako walikufa mwaka gani na wapi?”
Yule kijana alisema, “Nimeona nijaribu tu kwa
mtu yeyote ambaye anaweza kunisaidia, na
ndio nimejikuta nikiingia hapa,
sijui……..sikutumwa na mtu. Wazazi wangu
walikufa mwaka 1979 huko Same na mimi
wanasema nilikuwa kwenye ajali, nikaokoka.
Niliumia tu hapa.” Alishika kwenye kovu juu
ya paji lake la uso.
Nilihisi kitu fulani kikipanda tumboni na kuja
kifuani halafi niliona kama vile nimebanwa na
kushindwa kupumua. “Baba yako alikuwa
anaitwa nani?” “Alikuwa anaitwa
Siame….Cosmas Siame….” Niliinuka ghafla
hadi yule kijana alishtuka . Nilikwenda
kwenye kabati langu mle ofisini na kuchakura
kwenye droo moja na kutoka na diary.
Mikono ikinitetemeka, nilitoa kipande cha
gazeti ndani ya diary hiyo, nilichokuwa
nimekihifadhi.
“Ndio alikuwa anaitwa Cosmas Siame. Huyu ni
mtoto wake, ni yule mtoto aliyenusurika.”
Nilinong’ona. Nilijikuta nikipiga magoti na
kusali. “Mungu, wewe ni mweza na hakuna
kinachokushinda. Nimeamini baba kwamba
kila jema tunalofanya ni akiba yetu ya kesho
na kesho hiyo huanzia hapa duniani.” Halafu
nillinyamaza na kulia sana. Nililia kwa furaha
na ugunduzi wa nguvu zinazomgusa
binadamu kwa kila analofanya.
Nilisimama nikiwa nimesawajika kabisa.
Nilihisi kuwa mtu mwingine kabisa.
Nilimfuata yule kijana na kumkumbatia huku
nikiwa bado ninalia. “Mimi ni baba yako
mdogo, ndiye nitakyekulea sasa. Ni zamu
yangu sasa kukulea hadi mwisho” Naye alilia
bila kujua sababu na alikuwa
amechanganyikiwa kabisa. Nilirudi kwenye
kiti na kumsimulia kilichotokea miaka 17
iliyopita.
Tuliondoka hapo na kwenda kumwona
shangazi yake Ubungo, eneo la maziwa
ambako alikuwa amepanga chumba.
Kutokana na hali yake nilimhamishia kwangu,
baada ya kumsimulia kilichotokea. Huyo dada
yake Cosmas alifurahi sana hadi akashindwa
kuzungumza kwa saa nzima. Alifariki hata
hivyo mwaka mmoja baadae, lakini akiwa
ameridhika sana.
Kijana Siame alisoma na kumaliza Chuo Kikuu
na hivi sasa yuko nchini Australia anakofanya
kazi. Ukweli ni kwamba ni mwanangu kabisa
sasa. Naamini huko waliko Mbinguni wazazi
wake wanafurahia kile walichokipanda miaka
mingi sana nyuma. Lakini nami najiuliza bado.
Ilikuwaje Cosmas akanipa msaada ule? Halafu
najiuliza ni kitu gani kilimvuta mwanae Siame
hadi ofisini kwangu akizipita ofisi nyingine
zote? Nataka nikuambie, usiwe mbishi sana
bila sababu, kuna nguvu za ziada
zinazoongoza matokeo maishani
mwetu…………
*************MWISHO***********
*********
Namalizia kwa kusema haya
Maisha ni miujiza na usimwazie baya kwa kila mkosaji.
 Please press
share to spread this important message.

No comments:

Post a Comment