MBOWE ASEMA UJENGWE MFUMO MPYA KUSAIDIA CCM KUKABIDHI MADARAKA BILA VURUGU.
SERIKALI imetakiwa kuandaa mfumo wa kikatiba utakaowezesha chama cha
upinzani kuongoza iwapo kile kinachotawala kitaondolewa madarakani.
Kauli
hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipokuwa
akihutubia mikutano ya kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata
za Mpapa, wilayani Momba na Myovizi, Wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya.
Alisema
kutokana na vuguvugu la siasa za mabadiliko.
zinazoendelea nchini, ni
wakati mwafaka nchi ikawa na mfumo wa kikatiba na sheria kwa ajili ya
kusimamia mabadiliko ya uongozi kufanyika kwa amani ili kuepusha nchi
kuingia katika vurugu na mkanganyiko wa kisiasa.
Mbowe alisema
ingawa hiyo inaweza kuonekana kuwa ni dhana mpya, kutokana na umuhimu
wake kwa ajili ya mustakabali mwema wa Taifa, ni vyema Watanzania
wakaanza kuitafakari.
Alitola mifano wa Ghana ilivyopitia misukosuko
kutoka utawala wa Jerry Rawlings kwenda chama cha upinzani cha Rais John
Kufour.
Akiwanadi wagombea wa Chadema katika maeneo hayo, Mbowe
alisema ni hatari kwa nchi kama Tanzania ambayo sasa inapitia kwenye
wimbi kubwa la mabadiliko, kukosa mfumo huo wa kuhakikisha mabadiliko ya
mpito kutoka utawala wa Serikali moja kwenda nyingine yanafanyika kwa
amani na kulinda masilahi ya nchi bila vurugu.
“Ni muhimu sana kuwa na sheria itakayohakikisha 'transition' (kipindi cha mpito) kutoka Serikali ya chama fulani kwenda chama kingine au Serikali moja kwenda Serikali nyingine, kufanyika kwa amani na kwa kuhakikisha masilahi ya umma na nchi yanazingatiwa,” alisema na kuongeza:
“Lazima tuepuke
hali kama hiyo.
Wenzetu wale (Ghana) walijifunza, walipoingia madarakani
wakaamua kutunga sheria ya kusimamia ‘transition period’ kutoka uongozi
wa Serikali moja kwenda nyingine.”
“Watanzania wanaweza kujiuliza
kwa nini Marekani inachukua siku 72 kwa Rais kuapishwa na kukabidhiwa
rasmi mamlaka ya kuongoza nchi tangu achaguliwe?
Ni kwa sababu kuna vitu
vya muhimu sana vya kusimamiwa na kufanyiwa kazi kabla utawala mpya
haujakabidhiwa Ikulu.”
Mbowe alisema hapa nchini upo mfano mzuri
wa madhara ya kukosekana kwa sheria ya namna hiyo ya kusimamia kipindi
hicho cha mpito.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alidai kwamba
sehemu ya mabilioni ya ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa)
yalihamishwa kutokana na kukosekana kwa mfumo huo.
Mwenyekiti huyo
wa Chadema alisema wakati Marekani inachukua takriban siku 72 tangu
uchaguzi na uongozi mpya kukabidhiwa madaraka ya kuongoza nchi, Tanzania
inachukua wastani wa saa 48 pekee, akisema hali hiyo ni hatari kwa nchi
kwani, kuna masuala ya msingi ambayo yanahitaji muda wa kutosha katika
kufanya makabidhiano kutoka Serikali moja kwenda nyingine.
“Ni
wakati mwafaka kuanza kufikiria kuwa na mfumo huu wa kikatiba na
kisheria.
Huwezi kutumia saa 48 tangu uchaguzi kufanyika kumkabidhi Rais
mpya madaraka.
Kwanza kwa muda huo nani anasimamia kikamilifu
rasilimali za umma, nini hatma ya watumishi wa umma.
Kuna masuala ya
majeshi, nyaraka za siri na kila kitu, vitu ni vingi. Wenzetu walio
makini na nchi zao wanajua umuhimu wa masuala kama haya.
Wanapata muda
wa kufanya 'orientation' (uelewa wa mazingira), alisema Mbowe na
kuongeza:
“Ndiyo maana hapa kuna wakati watumishi wa Serikali wakaamua tu kuikumbatia CCM hata kama nao wameichoka, kwa sababu wanakuwa hawajui hatma yao ni nini kwenye Serikali au uongozi mpya, baada ya uchaguzi.
“Ghana katika kipindi hicho cha mpito kutoka
Serikali moja hadi nyingine wameweka utaratibu wa mamlaka inayoongozwa
na mtu ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa anasimamia rasilimali zote,
nyaraka zote, zinakuwa zimeandikishwa, zinajulikana zikoje.”
Alisema
lazima hatari hiyo izuiliwe kwa kuwa wakati Serikali mpya ilivyoingia
Ghana, waliokuwepo madarakani walichoma moto nyaraka muhimu na kuharibu
vitu, kitendo kilichosababisha Serikali iliyoingia madarakani kuhangaika
kuanza upya.
Alisema kutokana na hali kama hiyo ni lazima
wananchi waanze kudai mfumo huo kwani hivi sasa Katiba na sheria ziko
kimya kitu kinachoweza kusababisha siku moja mtu akakabidhi ukuta wa
Ikulu tu kukiwa hamna kitu ndani.
“Mfumo huo utahakikisha 'smooth exit' yaani wanaoondoka au anayeondoka aondoke kwa amani. Kwa sasa hakuna 'mechanism' (mfumo) yoyote ile, hakuna utaratibu, hakuna sheria, Katiba iko kimya. Tunataka 'smooth exit', 'smooth entry' (Kutoka kwa amani, kuongia kwa amani).”
“Watumishi wa umma wawe na uhakika wa
kuwepo kwa Serikali, bila hivyo nchi inaweza kuingia kwenye machafuko
kwa sababu tu watawala waliokuwepo hawataki kuondoka.”
Mwenyekiti
huyo yuko kwenye ziara ya kuwanadi wagombea udiwani wa chama hicho
katika kata mbalimbali za Mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Njombe na Iringa,
katika uchaguzi mdogo unaohusisha kata 29 nchini ambao umepangwa
kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment