Wednesday, January 29, 2014

DENI LA TAIFA LINAPAA, SERIKALINI NI MATANUZI

bot1 52cbf
Hivi karibuni The Citizen liliandika habari ya kushtua katika ukurasa wa mbele, likielezea wasiwasi wa wataalamu na mabingwa kadhaa wa masuala ya uchumi kuwa, Tanzania inakabiliwa na janga kubwa la mzigo wa madeni iwapo Serikali haitapunguza kasi ya mikopo isiyokuwa na tija katika kuinua uchumi. 
Onyo la wataalamu hao linatukumbusha jinsi janga la Deni la Taifa lilivyoligharimu Taifa kiuchumi katika miaka ya 90, ambapo karibu rasilimali zote ambazo Serikali ingezitumia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na pia kuziwekeza katika huduma muhimu za kijamii zilielekezwa katika kulipa madeni. Ni aibu na ukweli ulio mchungu kwamba ilipofika mwaka 2006, Deni la Taifa lilikuwa asilimia 70 ya Pato la Taifa, ingawa msamaha wa madeni ulipunguza kiwango hicho hadi asilimia 21 mwaka uliofuata.
Hata hivyo, kilichoendelea baada ya pale ni uthibitisho kwamba Serikali haikupata fundisho kutokana na janga hilo, kwani ilizidisha kasi ya kukopa kiasi kwamba
Deni la Taifa hivi sasa linakadiriwa kuwa kati ya asilimia 40 na 50 ya Pato la Taifa, ambalo linakadiriwa kuwa Sh50 trilioni. Ni vigumu kuamini kwamba Deni la Taifa limekua kwa kasi ya kutisha kutoka Sh10 trilioni mwaka 2005 hadi Sh27 trilioni mwishoni mwa mwaka uliopita.

Kama baadhi ya wataalamu wa masuala ya uchumi wanavyohadharisha, suala hapa siyo Serikali kukopa, bali ni kwamba mikopo hiyo inayokadiriwa kuwa Sh2 trilioni kila mwaka inachukuliwa kufanya kitu gani? Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zinaonyesha kwamba Deni la Taifa lilipaa kwa Tsh5 trilioni kati ya Januari na Oktoba mwaka uliopita.

Mtaalamu mmoja wa uchumi ametukumbusha jinsi miaka ya 70 Serikali ilivyokopa Sh96 bilioni kuanzisha Kiwanda cha Viatu Morogoro, lengo likiwa kuuza viatu nchini Italia. Kutokana na kufilisika kilibinafsishwa miaka ya 90 na hivi sasa majengo yake yamegeuzwa kuwa ghala, huku deni la uanzishwaji wa kiwanda hicho likiwa limelipwa kupitia kodi za wananchi. Mfano mwingine ni bajeti ya Sh122.4 bilioni ya kusambaza pembejeo za ruzuku kwa wakulima kwa mwaka 2011/12, ambapo Tsh89 bilioni zilikuwa ni mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imefichua uvundo na ufisadi mkubwa katika mfumo mzima wa pembejeo za ruzuku. Kwa hiyo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) inakutana leo kupokea na kujadili ripoti hiyo. Kwa mfano, katika Kijiji cha Lunyala
, wilayani Nkasi, mkoani Rukwa asilimia 70 ya wananchi walioorodheshwa kupata mbolea walikuwa bandia, huku Benki ya Dunia ikikaririwa ikisema asilimia 60 ya Bajeti ya pembejeo za ruzuku ililiwa na mafisadi.

Kinachosikitisha ni kwamba Deni la Taifa litalipwa na wananchi wote ingawa waliofaidika nalo ni mafisadi na viongozi wachache walio serikalini na mashirika ya umma. Lakini kinachosikitisha zaidi ni tabia ya Serikali kuendelea kukopa kwa lengo la kuendeleza matanuzi na matumizi makubwa yasiyo ya lazima.
Mfano mzuri ni ziara fupi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda mkoani Mtwara mwishoni mwa wiki, ambapo aliongozana na ujumbe mkubwa kupita kiasi na magari ya kifahari ya Serikali yasiyopungua 30. Sisi tunadhani unahitajika mjadala mpana wa kitaifa kuhusu Deni la Taifa.Chanzo: mwananachi.

No comments:

Post a Comment