Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid.PICHA|MAKTABA
Mbeya. Mfanyakazi
wa Kitengo cha Kuhifadhi Maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Eugene
Vurugu amemtisha Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid
kuwa ikitokea amefariki dunia akiwa mkoani Mbeya, basi maiti yake
italazwa kwenye sakafu hospitalini hapo.
Akizungumza
kwenye mkutano wa wafanyakazi na naibu waziri huyo mwishoni mwa wiki
iliyopita, Vurugu alisema kitengo hicho kimezidiwa na wingi wa maiti
zinazopelekwa hospitalini hapo.
Alisema kitengo hicho cha kina majokofu sita tu na hulazimika kuhifadhi miili kwa zamu ili angalau maiti zisiharibike.
“Hata wewe Waziri ukifa leo, hakuna pa kukuweka.
Utawekwa
sakafuni kusubiri maiti nyingine zipoe halafu utaingizwa ndani kwa
kuingizwa maiti mbili kwenye eneo la mtu mmoja,’’ alisema Vurugu.
Aliiomba Serikali ifanye haraka kuboresha kitengo hicho ili kuepusha tatizo la kuoza kwa miili ya marehemu.
Kumekuwa
na malalamiko kuhusu uchache wa majokofu ya kuhifadhia maiti katika
hospitali hiyo na baadhi ya watumishi walisema hali kuwa mbaya zaidi
inapotokea ajali ambayo inasababisha vifo vya watu wengi kwa wakati
mmoja.
Vurugu
alidokeza pia kuwapo kwa tatizo katika Idara ya Mifupa ya hospitali
hiyo, akisema wakazi wengi wanaofika hapo kwa matatizo hayo anawaona
wakiondoka kwenda Hospitali za Peramiho ya Ruvuma na Ikonda ya Makete
huku wengine wakienda kwa waganga wa jadi kuunga mifupa yao.
Vurugu
alizungumza baada ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dk
Humphrey Kiwelu kusoma taarifa ya utendaji mbele ya Naibu Waziri
iliyoonyesha hali iko shwari baada ya kudai kuwa hospitali hiyo imepiga
hatua kubwa kiutendaji na katika utoaji huduma kwa wagonjwa.
Dk
Kiwelu alisema hospitali yake ina mafanikio makubwa yakiwamo ya kuwa na
maabara ambayo imekubalika katika kiwango cha kimataifa na kwamba
majibu yanayotoka kwenye maabara hiyo kwa sasa yanakubalika hata
Uingereza na Marekani.
Hata hivyo, alisema hospitali hiyo haina mashine ya CT Scan licha ya kuiomba kutoka serikalini tangu 2003.
Akijibu
hoja mbalimbali za wafanyakazi, Dk Rashid aliwataka viongozi kujipanga
na kuchangua vipaumbele kutokana na mafanikio mazuri yanayoonekana
hospitalini hapo.
Alisema
kwa kuwa hospitali hiyo imeongeza mapato ya ndani kutoka Sh60 milioni
hadi Sh300 milioni kwa mwezi, ipo haja ya kutumia fedha hizo kuiboresha
kwa kuangalia vitendea kazi zaidi na masilahi ya watumishi wote.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment