Sunday, January 12, 2014

WATOTO WAWILI WAFA KWA KULIPUKIWA NA kitu KINACHODAIWA NI BOMU DAR

 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Engelbert Kiondo.
Watoto wawili wakiume wamekufa na mmoja kunusurika baada ya kulipukiwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu eneo la Jeshi la Wananchi nchini (JWTZ) huko Kimbiji, Kigamboni. Watoto hao  wanaotoka katika  familia tofauti wenye umri wa miaka nane na kumi walikutwa na mkasa huo juzi wakati wakiwa wanacheza maeneo hayo.

Mmoja wa ndugu wa marehemu ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, aliliambia NIPASHE kuwa, eneo la tukio kulikuwa na watoto watatu akiwamo mwenye umri wa miaka mitano ambaye alinusurika kwenye mlipuko huo.

Alimtaja mtoto aliyefariki kwa jina moja kuwa ni Yohana.

Akisimulia zaidi ndugu huyo alisema siku ya tukio watoto hao, walitoka nyumbani kuelekea eneo hilo la jeshi ambalo wanajeshi hulitumia kwa mazoezi ya kijeshi.


“Huwezi amini kutoka hapa nyumbani hadi huko walikolipukiwa ni mbali, yaani sijui walifikaje, ila ndiyo michezo ya watoto,”alisema.

Alieleza kuwa, watoto hao wakiendelea na michezo yao, walimuona nyani na kuanza kumkimbiza. Alisema baada ya kufika maeneo hayo ya jeshi waliona kitu kama gololi na kukiokota.

“Baada ya kuikokota wakaanza kunyang’anyana ndipo ulipotokea mlipuko na kuwajeruhi na kuwaua watoto wawili mmoja akiwa ni Yohana, yule wa miaka mitano aliokoka na kurudi nyumbani kuwajulisha kile kilichowatokea wenzake,” alisema.

Aidha, kutokana na tukio hilo miili ya watoto hao inaendelea kufanyiwa uchunguzi wa kina na inatarajiwa kuzikwa wiki ijayo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Engelbert Kiondo, alipopigiwa simu kuhusiana na tukio hilo, awali aliahidi kulifuatilia lakini baadaye alipopigiwa, ilipokelewa na mwanamke na kudai siyo ya kamanda.

Baadhi ya matukio ya milipuko au kuleta taharuki baada ya wananchi kufananisha chuma na bomu ni pamoja na Januari 2, mwaka huu taharuki ilitokea eneo la makutano ya barabara ya Morogoro na Shekilango, baada ya kuonekana kitu kilichofananishwa na bomu la kutupwa na mkono.

Tukio hilo lilisababisha wakazi wa eneo hilo, wafanyabiashara, wapita njia kupata hofu lakini baada ya polisi kulifanyia uchunguzi walibaini siyo bomu.

Aidha, kwa mwaka jana kuanzia mwezi Septemba, matukio yaliyotokea ni  pamoja na lile la wanafunzi wawili wa kidato cha kwanza, katika shule ya Sekondari Matombo mkoani  Morogoro, kunusurika kufa baada kulipukiwa na kujeruhiwa na kitu kilichosadikiwa kuwa ni bomu wakati wakitoka shule.

Mwezi Oktoba watoto wengine watatu wakazi wa Kijiji cha Likombora, Kata ya Mihumo wilayani Liwale, Mkoa wa Lindi walifariki baada ya kulipukiwa na kitu kinachosadikiwa kuwa bomu.

Tukio lilitokea ikiwa imepita wiki, baada ya mgambo wakiongozwa na mshauri wao, Meja Tiba kufanya mazoezi ya kulenga shabaha ya silaha huko kwenye Kijiji cha Kipule ambako mabomu matatu hayakulipuka na wakafanikiwa kuyaokota mawili na kuyateketeza.

Mwaka juzi katika kijiji cha Rugarama Kata ya Iyande wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, watoto watano walikufa baada ya kulipukiwa na bomu la kutupa kwa mkono walilookota wakati wakikusanya vyuma chakavu.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment