Saturday, January 11, 2014

MAJAJI, MAHAKIMU WAWEKWA KIKAANGONI

 
 Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman
Mahakama imeanza kutekeleza mpango kabambe wa kuondoa mrundikano wa kesi na kwa mara ya kwanza katika historia ya mhimili huo nchini, majaji na mahakimu wamewekewa malengo ya kesi wanazopaswa kusikiliza na kuzitolea uamuzi.
Habari zilizolifikia gazeti hili zilisema chini ya mkakati huo, majaji wa kanda za Mahakama Kuu zenye mrundikano wa kesi kwa muda mrefu, wametakiwa angalau kumaliza kesi 220 kwa mwaka.
Kadhalika kwa kesi mpya zinazofunguliwa, majaji wametakiwa kujitahidi kumaliza kesi hizo ndani ya miezi 24, wakati Mahakimu Wakazi na wale wa Wilaya wametakiwa kumaliza mashauri yanayopangiwa kuyasikiliza ndani ya miezi 18.
Vyanzo huru ndani ya mhimili huo, vimeliambia gazeti hili kuwa chini ya mkakati huo kabambe, mahakimu wa mahakama za mwanzo kote nchini wametakiwa kumaliza kesi mpya ndani ya miezi 12.
Ili kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa, wadau muhimu akiwamo Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, Jaji Kiongozi, Fakhi Jundu na Majaji wa Mahakama ya Rufani walikutana Desemba 2013, Bagamoyo Mkoa wa Pwani katika mkutano ulioweka mkakati wa utekelezaji wa uamuzi huo.
Mkutano huo uliofanyika chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, pia uliwashirikisha wawakilishi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), watendaji wakuu wa Mahakama hizo na viongozi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).
Katika kuanza utekelezaji wa mkakati huo, Msajili wa Mahakama Kuu, Ignas Kitusi na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Pantrine Kente walitembelea kanda mbalimbali kuhakiki wingi wa kesi zilizopo.
“Mheshimiwa Kitusi yeye alikwenda Kanda ya Moshi na Kente alikwenda Kanda ya Arusha na hivi tunavyoongea (jana) Kente anaelekea Kanda ya Moshi kuhakikisha mashauri ya rufaa,” ilidokezwa.
Gazeti hili lilipomtafuta Kitusi na kumuuliza kuhusu mkakati huo unaohusisha majaji na mahakimu kuwekewa malengo kwa ajili ya kupunguza mrundikano wa kesi alijibu kwa kifupi: “Ni kweli hicho kitu kipo.”
Kwa upande wake, Kente alisema hawajapata maagizo ya kesi ngapi zinatakiwa kumalizika ndani ya mwaka mmoja isipokuwa mchakato wa kukabiliana na mrundikano wa kesi unaendelea na utapatiwa ufumbuzi hivi karibuni.
Alisema kwa kuwa kesi za Mahakama ya Rufani lazima zisikilizwe na majaji watatu wanaangalia uwezekano wa kuwawezesha ili kukabiliana na tatizo hilo.
“Ndio tunajipanga namna Mahakama ya Rufani itakavyoweza kumaliza kesi nyingi kwa haraka, hili lipo kiufundi zaidi lakini tutalipatia ufumbuzi mapema iwezekanavyo,” alisema Kente.

Wakili apongeza
Mkakati huo umekuja wakati kukiwa na malalamiko ya kuwapo mrundikano na ucheleweshaji wa kesi katika mahakama nyingi nchini, huku nyingine zikiwa zimekaa zaidi ya miaka 10.
Wakili mashuhuri wa siku nyingi, Peter Shayo alitaka mhimili huo uende mbali zaidi ili Jaji apimwe kwa idadi ya mashauri anayoyasikiliza na kuyatolea uamuzi katika kipindi cha mwaka mzima.
“Tunapaswa tuwe na kitu kinaitwa Performance Contract by Judges (mkataba wa ufanisi kwa majaji) ili kigezo cha kuongezewa muda wa mkataba iwe ni idadi ya kesi alizosikiliza na kuziamua kwa mwaka,”alisema.
Wakili Shayo alisema utaratibu huo ndio unaotumika nchini Kenya kupima ufanisi wa majaji na Uganda nayo iko njiani kuanza kuutumia sambamba na nchi ya Zambia.
“Ingawa yako mazingira tofauti ambayo kesi inakuwa haijacheleweshwa na Hakimu au Jaji, lakini wakijua kwamba ufanisi wao utapimwa kwa njia hiyo itasaidia kuongeza ufanisi,”aliongeza Shayo.

No comments:

Post a Comment