Monday, January 20, 2014

RAIS KIKWETE AOMBOLEZA VIFO VYA WATU 13 WALIOFARIKI KWENYE AJALI MKOANI SINGIDA LEO. 20.01.14


DSC05820
Gari aina ya Noah T,730 BUX linavyoonekana baada ya kugongwa na Lori m koani Singida.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Perseko Kone kutokana na vifo vya watu wazima 12 na mtoto mmoja wa miezi minne vilivyotokea tarehe 20 Januari, 2014 kufuatia kugongana uso kwa uso kwa gari aina ya Toyota Noah lililokuwa limebeba abiria likitokea Itogi kwenda Singida na lori katika eneo la Isuna Mkoani Singida.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za vifo vya watu 13 akiwemo mtoto wa miezi minne waliofariki papo hapo katika eneo la ajali tarehe 20 Januari, 2014 baada ya gari aina ya Toyota Noah walilokuwa wakisafiria kutoka Itigi kwenda Singida kugongana uso kwa uso na lori katika eneo la Isuna”.
Rais Kikwete amesema inatia simanzi kuona ajali zikiendelea kutokea na kupoteza maisha ya watu wasio na hatia na hususan mtoto mdogo kama huyu wa miezi minne, kusababisha ulemavu wa kudumu kwa baadhi ya watu na uharibifu wa mali kutokana na makosa ya binadamu katika uendeshaji wa vyombo vya moto.
“Kufuatia ajali hiyo ya kusikitisha, ninakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Perseko Kone salamu zangu za rambirambi kutokana na msiba huo, na kupitia kwako, naomba unifikishie salamu zangu za rambirambi na pole nyingi kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo. Nawaomba wanafamilia wawe na moyo wa uvumilivu, subira na ujasiri hivi sasa wanapougulia machungu ya kupotelewa na ndugu zao”, amesema Rais Kikwete kwa masikitiko.
Aidha Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Mahala Pema Peponi Roho za Marehemu wote, na amewahakikishia wafiwa kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa.
Vilevile amemtakia ahueni kijana mmoja majeruhi wa ajali hiyo na aweze kupona haraka na kurejea katika hali yake ya kawaida na kuungana tena na ndugu na jamaa zake

No comments:

Post a Comment