RAIS JAKAYA KIKWETE.
SERIKALI
imetoa kauli kuhusu tuhuma zilizokuwa zikiwakabili baadhi ya mawaziri,
waliobatizwa jina la ‘Mawaziri Mizigo’, na hatua ambazo zimekuwa
zikichukuliwa kukabiliana na kero zilizosababisha wapewe jina hilo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana Ikulu Dar es Salaam, Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Safue, alisema mawaziri hao walituhumiwa kutokana na
changamoto zilizopo katika wizara zao; na si upungufu wao binafsi kama
viongozi.
Mawaziri
hao saba walitajwa katika ziara ya mikoani ya Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana na baadae walihojiwa katika kikao cha Kamati Kuu cha
chama hicho.
Miongoni mwa mawaziri waliohojiwa ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, ambaye sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Fedha.
Wengine
ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia.
Akijibu
swali kutoka kwa waandishi waliotaka kujua kwa nini mawaziri hao
walituhumiwa na wameendelea kuwepo katika baraza la mawaziri baada ya
mabadiliko ya jana, Balozi Sefue alisema baadhi ya changamoto
walizotuhumiwa zilikuwa nje ya uwezo wao.
Kilichowanusuru
“Kila wizara ina changamoto zake tofauti na wizara nyingine, wakati
mwingine tatizo ni fedha, sasa huwezi kumlaumu Waziri na hata Waziri wa
Fedha kama hakuna mapato, huwezi kumlaumu.
“Pia
Rais anaangalia Waziri ana mpango gani katika kukabiliana na changamoto
ya wizara yake…huwezi kumbadili Waziri anayefahamu tatizo na mwenye
mpango wa kulikabili na kumweka mpya ambaye hajui kabisa hilo tatizo,”
alifafanua Balozi Sefue.
Tayari
Bunge lilipitisha azimio la kumtaka Ghasia pamoja na naibu wake wawili,
Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa, kupima na kutafakari kama wanatosha
kusimamia wizara hiyo.
Kiini
cha Bunge kupitisha azimio hilo ni taarifa ya Bunge ya Hesabu za
Serikali, kubainisha kuwapo wizi, ubadhirifu na mtandao wa ufisadi ndani
ya Tamisemi. Hata hivyo, Waziri Ghasia alinukuliwa akisema hakuna
anayepaswa kunyooshewa kidole kwa matatizo yaliyopo Tamisemi.
Akifungua
warsha ya kujadili changamoto za uongozi wa Serikali za Mitaa Dodoma
hivi karibuni, Ghasia alisema kwa sasa kazi kubwa iliyoko ni kurekebisha
kasoro baada ya kufanyika utafiti juu ya matatizo ya Tamisemi.
Alisema
wizara yake inashughulikia matatizo hayo baada ya kupokea ripoti ya
utafiti, uliofanywa na Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute).
Udhaifu
wa waliotolewa Balozi Sefue alipotakiwa kufafanua kama uamuzi wa Rais
Kikwete kuwapumzisha kazi mawaziri watano, ulitokana na udhaifu wao na
kutakiwa kutaja udhaifu huo, Katibu Mkuu Kiongozi huyo alisema mawaziri
hao hawakuwa na udhaifu wowote.
Mawaziri
hao ni pamoja na Dk Terezya Huvisa, ambaye alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Rais (Mazingira). Naibu mawaziri waliopumzishwa kazi
pamoja na Dk Huvisa ni Gregory Teu, aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda na
Biashara na Philipo Mulugo, aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi.
Wengine
ni Benedict Ole-Nangoro, aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo
na Uvuvi na Goodluck Ole-Medeye, aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi.
Akielezea
sababu za kuwapumzisha, Balozi Sefue alifafanua kwamba kilichofanyika
ni kuimarisha Baraza, kutokana na upungufu uliosababishwa na kuachwa kwa
nafasi tano za wazi.
“Hata
katika timu ya mpira, wale wanaotolewa nje na kuwekwa benchi kabla ya
mpira kuisha, haina maana kuwa wana udhaifu, bali ni mbinu tu ya
kuimarisha kikosi,” alifafanua Balozi Sefue.
HABARILEO
No comments:
Post a Comment