Saturday, January 4, 2014

JWTZ latoa ufafanuzi wa ofisa wao anayetuhumiwa kuua

 
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limefafanua kuwa askari wake aliyedaiwa kuua raia alilazimika kufyatua risasi kujihami na watu waliodaiwa  kuwa ni vibaka waliomvamia na kumlazimisha kufungua milango ya gari lake.
 
Ofisa huyo, Meja Abdallah Mzee, alidaiwa kuua watoto wawili kwa risasi siku ya mkesha wa mwaka mpya katika mkasa uliotokea Pugu Kinyamwezi jijini Dar es Salaam.
 
Taarifa ya ufafanuzi ya JWTZ iliyotolewa Dar es Salaam jana ilisema kuwa Meja Mzee wakati anarudi nyumbani kwake saa 6.00 usiku akiwa anaendesha gari aina ya RAV4, alivamiwa na vibaka waliomzingira na kumlazimisha kufungua milango ya gari hilo.
 
Kitendo kilichoelezwa kwenye taarifa hiyo kuwa hakikuwa cha kawaida hali iliyomfanya ofisa huyo kujihami kwa kurusha risasi akihofia kudhuriwa na kuporwa gari.
 
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Habari Makao Makuu ya JWTZ , Meja Joseph Masanja, ilisema ofisa huyo alikuwa anarejea nyumbani kwake akitokea katika hospitali ya Amana na kwamba alivamiwa na vibaka hao eneo la Pugu Kinyamwezi na kwamba Meja Mzee alikuwa na bastola anayoimiliki kihalali.
 
“Alianza kufyatua risasi hewani kwa lengo la kujihami na kuwatawanya watu hao .Katika  tukio hilo ofisa huyo alifanikiwa kujinasua na kuondoka kwenye kusanyiko hilo huku akiamini kuwa watu hao wametawanyika,” ilisema taarifa hiyo ya jeshi kwa umma.
 
Katika tukio hilo inadaiwa kuwa watu wawili walipoteza maisha na wengine wawili kujeruhiwa.
 
Awali Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala Marieta Minangi, alisema mwanajeshi huyo anashikiliwa kwa tuhuma za kuwaua kwa kuwapiga risasi  watoto wawili na kujeruhi wengine wawili baada ya kundi la vijana waliokuwa wanasherehekea mwaka mpya kuzingira gari lake.
 
Minangi aliwataja marehemu hao kuwa ni Ibrahimu Mohamed (16) na Abubakar Hassan (14) wakati majeruhi ni Rupano Wanga (17) na Kassimu Abdul (16) 
 
 
CHANZO: NIPASHE 
 

No comments:

Post a Comment