Mfuasi wa Chadema akiwa chini baada ya ‘kukatwa mtama’ na mfuasi
mwingine wa chama hicho baada ya kutokea vurugu baina ya wafuasi
wanaounga mkono uongozi na wale wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe jana baada ya kuahirishwa kwa hukumu ya kesi ya mbunge huyo katika
Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam jana. Picha na Silvan Kiwale
Dar es Salaam.Wafuasi wa Chadema wanaomuunga
mkono aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe na
wanaounga mkono uongozi wa juu, jana walitwangana tena muda mfupi baada
ya kuondoka eneo la Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Tukio hilo limetokea huku Mahakama hiyo
ikiahirisha hadi leo, kutoa uamuzi wa maombi ya Zitto kuzuia kujadiliwa
na Kamati Kuu ya Chadema.
Katika maombi hayo namba 1 ya mwaka 2014, Zitto
ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, anaiomba Mahakama iizuie
Kamati Kuu ya Chadema kumjadili na au kuchukua uamuzi wowote kuhusu
uanachama wake hadi kesi yake ya msingi aliyoifungua mahakamani hapo
itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Uamuzi wa maombi hayo ulipangwa kutolewa jana na
Jaji John Utamwa ambaye hata hivyo, alisema alikuwa hajamaliza kuandika
uamuzi huo na kuahirisha shauri hilo hadi leo mchana.
Maombi hayo ya Zitto ya zuio la muda la kujadiliwa
na kuchukuliwa uamuzi wowote kuhusu uanachama wake yametokana na kesi
ya msingi aliyoifungua mahakamani hapo Januari 2, 2014, dhidi ya Bodi ya
Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Katika kesi hiyo, Zitto pia anaiomba Mahakama Kuu
imwamuru Katibu Mkuu wa Chadema ampatie mwenendo na taarifa za kikao cha
Kamati Kuu za kumvua nyadhifa zake zote alizokuwa nazo ndani ya chama
na iwazuie walalamikiwa kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake
ya ubunge wa Kigoma Kaskazini.
Mapigano
Baada ya kuahirishwa kwa shauri hilo, wanachama wa
makundi yote waliondoka eneo la Mahakama wakiendelea kuimba na
kushangilia lakini walipofika eneo la Mahakama ya Rufani ghafla walianza
kupigana ngumi na mawe. Baadhi yao walikamatwa na askari kutokana na
vurugu hizo.
Awali, wafuasi hao walifika mapema asubuhi katika viwanja vya Mahakama tayari kusikiliza uamuzi huo.
Ulinzi ulikuwa umeimarishwa na askari polisi
wakiwamo wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), waliokuwa na silaha
pamoja na mabomu ya machozi walikuwa wametanda.
Pia kulikuwa na askari wa Kikosi cha Mbwa pamoja na gari la maji ya kuwasha.
Licha ya kuwahi, ni wafuasi wachache walioruhusiwa
kuingia ndani ya u`kumbi wa Mahakama tena baada ya kuandikisha majina
yao huku wakitambuliwa na viongozi wao waliokuwapo.
Baada ya idadi iliyokuwa ikihitajika kutimia, wafuasi wengine waliambiwa wasubiri kutapata taarifa za uamuzi huo baadaye.
Wakiwa wanasubiri, walikuwa wakitambiana kwa maneno na nyimbo.
Kundi la Zitto lilikuwa na mabango yenye ujumbe
mbalimbali wa kumsifu na bendera za chama hicho pamoja na ngoma huku
likikejeli kundi linalounga mkono uongozi wa chama hicho.
Baadhi ya mabango yalisomeka ‘Zitto kama Mandela’, ‘Zitto Mkombozi.’
Baadhi ya maneno waliyokuwa wakiyatamka katika nyimbo zao ni pamoja na `Zitto Kwanza’, chama (Chadema) baadaye.
Wafuasi wa uongozi nao walikuwa na mabango
yaliyosomeka: ‘Hongera Mbowe kwa ujasiri,’ ‘Kunguru hafugiki’ na ‘Zitto
rudisha kadi yetu’.
Awali, kundi linalounga mkono uongozi lilidai
kwamba wanaomuunga mkono Zitto si wanachama halali wa chama hicho, bali
wamenunuliwa kwa lengo la kwenda mahakamani.
Tofauti na siku ya kwanza ya kusikilizwa kwa
maombi ya Zitto, ambayo kundi linalounga mkono uongozi lilidai kuwa
wafuasi wa Zitto wameandaliwa na CCM, jana liliwatuhumu kuwa
wameandaliwa na CUF.
Baadhi ya viongozi wa Baraza la Vijana Chadema
(Bavicha), walisikika wakilalamika kwa askari kuwa wafuasi hao wametoka
mitaani na wengine ni wa CUF.
CUF wakana tuhuma
Hata hivyo, CUF jana kimekana kuhusika na mgogoro
huo unaoendelea Chadema. Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Julius
Mtatiro alisema jana kuwa kuna taarifa zimesambaa kuwa CUF kilikuwa
kimeandaa vijana wa kwenda mahakamani jana kwa ajili ya kufanya vurugu.
“Wadau, waandishi wengi wa habari walinipigia
nithibitishe ikiwa CUF iliandaa makundi ya wanachama wakamshabikie ZZK
(Zitto) mahakamani leo (jana) hii. Taarifa ya namna hii pia imeenea
mitandaoni.
“Pia viongozi kadhaa wa Chadema wamenipigia kunijulisha kuwa
intelijensia yao imegundua kuwa vijana wa CUF wamepenyezwa na kwamba
wamevishwa T-shirt (fulana za M4C na mapanga,” alisema Mtatiro na
kusisitiza kuwa CUF hakijapanga wala kutuma makundi ya vijana kwenda
kumshabikia Zitto.
Alisema ikiwa wanachama wa CUF wameonekana mahakamani itakuwa ni kwa utashi na matakwa yao.
“Hatujawahi kukutana, kupanga wala kutuma vijana wa CUF wakasimamie upande wowote katika mgogoro huu.
Wakati wa fukuto la Hamad Rashid na CUF watu wengi
tu raia walifika mahakamani, hatukuhoji na kutafuta vyama vyao,
tuliamini ni Watanzania tu,” alisema Mtatiro na kuongeza:
“Ni vigumu kwa CUF kukataza wanachama wake
wasihudhurie kesi maarufu kama ile ya Babu Seya, Sheikh Ponda, Zitto
Kabwe, Samaki wa Magufuli na nyinginezo.”
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment