Friday, January 3, 2014

HAYA NDIO MATUKIO YALIYOTIKISA NA KUZUA GUMZO 2013



Zimebaki siku chache kabla ya kuuaga mwaka 2013, mwaka ambao umekuwa na matukio mengi yaliyoitikisa nchi ya Tanzania, huku mengine yakiipa sifa kubwa.
Historia ya Tanzania kuwa na Katiba Mpya itakayopatikana kutokana na maoni ya wananchi ilianza Desemba 31, 2011 wakati Rais Jakaya Kikwete akilihutubia taifa, alikiri wazi kuwa sasa inahitajika Katiba Mpya ili kuendana na wakati wa sasa.
Baadaye Rais Kikwete aliwateua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba na ilianza kazi yake ya miezi 18, kuanzia Mei 3, mwaka 2012.
Tume hiyo ilikusanya maoni ya wananchi nchi nzima na kuandaa rasimu ya kwanza ya Katiba ambayo iliitoa Juni 4, mwaka huu.
Baada ya kutolewa kwa rasimu hiyo wananchi walipewa muda wa kuipitia na kuitolea maoni katika Mabaraza ya Katiba ya wilaya, yaliyokaa kuanzia Julai 12 mpaka Septemba 2, mwaka huu.
Maoni hayo yalikusanywa na tume hiyo kwa ajili ya kuyachambua na kutoa rasimu ya pili ya Katiba ambayo inatarajiwa kutolewa Desemba 30, mwaka huu.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitakiwa kumaliza kazi ya kuandaa rasimu ya pili Desemba 15, mwaka huu, lakini Rais Kikwete aliiongezea siku 14 zaidi na hivyo kuifanya iweze kuendelea na kazi hadi Desemba 30.
Hatua hiyo ya Rais Kikwete kuiongezea muda tume hiyo ilikuwa ya pili, kwani mara ya kwanza tume hiyo iliomba kuongezewa muda wa siku 45, kuanzia Novemba Mosi hadi Desemba 15, mwaka huu
 
Kabla ya kuomba kuongezewa muda mara ya kwanza, tume ilitakiwa kukamilisha kazi yake Novemba 30.
Kwa uamuzi wake, wa kuiongezea Tume hiyo siku nyingine 14, Rais Kikwete ameiongezea tume hiyo jumla ya siku 59 kati ya 60 ambazo anaruhusiwa kisheria.
Kifo cha Dk Sengondo Mvungi
Hatua  ya Rais kuiongezea muda Tume ya Mabadiliko ya Katiba  ilitafsiriwa kama kutoa fursa kwa wajumbe wa tume hiyo kujipanga upya baada ya kifo cha mmoja wa wajumbe wa tume hiyo, Dk Sengondo Mvungi aliyefariki dunia Novemba 12, mwaka huu nchini Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa baada ya kujeruhiwa kwa mapanga na watu wanaotuhumiwa kuwa majambazi, nyumbani kwake mkoani Dar es Salaam.

Ujio wa Rais wa Marekani Barack Obama
Ni siku mbili za kihistoria ambazo zimeweka rekodi ya aina yake katika historia ya nchi hii, kuanzia maandalizi  ya ujio wake mpaka alivyowasili nchini Julai 1 na kuondoa Julai 3, mwaka huu.
Shughuli nyingi na barabara kadhaa zilifungwa ili kutoa nafasi kwa ugeni huo mkubwa uliojumuisha familia yake, wafanyakazi wa ikulu, walinzi na makachero wa usalama kutoka nchini Marekani.
Katika ziara yake hiyo, Rais aliwekea mkazo umuhimu ambao Marekani inauweka katika ushirikiano wetu wa kina na unaoendelea kuimarika na nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia mipango mbalimbali ikiwemo ile ya kuimarisha ukuaji wa uchumi, uwekezaji na biashara, uimarishaji wa taasisi za kidemokrasia na uwekezaji katika kizazi kipya cha viongozi wa Kiafrika.
Ziara ya Rais wa China, Xi Jinping
Ziara hii ilitokea ikiwa ni wiki mbili tangu achaguliwe Xi Jinping kuwa Rais wa China,  ambapo aliichagua Tanzania kuwa nchi ya kwanza kuitembelea barani Afrika.
Katika ziara hiyo Rais Jinping  alikutana na viongozi mbalimbali nchini, kusaini mikataba ya kidiplomasia 19, ukiwemo wa ujenzi wa Bandari wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Akiwa nchini Rais Jinping alitoa hotuba yake ya kwanza tangu achaguliwe kushika wadhifa huo, ambayo iligusia masuala ya kiuchumi, kisiasa sambamba na kueleza msimamo wa nchi yake kwa Tanzania na Afrika.
Rais huyo alikutana pia na jumuiya ya watu wa China na kutembelea makaburi ya wataalamu wa Kichina ambayo yapo Majohe, Ukonga ambako alitoa heshima zake kwa Wachina waliofariki dunia wakati wakijenga reli ya Tazara.
Bomu la Arusha
Mei 5, mwaka 2013 ni siku ambayo haitafutika katika historia ya Tanzania kutokana na tukio la kusikitisha la kutupwa kwa bomu kanisani, ambapo watu watatu walifariki dunia na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa.
Tukio hilo lilitokea mbele ya Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa nchini Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Montecillo, Askofu Mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo Kuu la Arusha, walipokuwa wakizindua jengo la Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti, Arusha.

Mgogoro wa gesi Mtwara
Maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara waliandamana wakipinga uamuzi wa Serikali kusafirisha gesi kwa njia ya bomba, kutoka mkoani hapo kwenda Dar es Salaam.
Maandamano hayo yaliyoratibiwa na vyama vya Chadema,CUF, NCCR-Mageuzi, Sau, Tanzania Labour Party (TLP), APPT- Maendeleo, ADC, UDP na DP yakishirikisha wananchi wa wilaya za mkoa huo, zikiwamo Tandahimba na Newala, yalianzia katika Kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara mjini kupitia barabara ya kwenda Msimbati eneo ambako gesi asilia inapatikana.
Kufuatia fujo na vurugu zilizotokea katika maandamano hayo risasi na mabomu yalirindima, hali iliyozua hofu na tafrani mkoani hapo.
Sakata la Sheikh Ponda
Tukio la kujeruhiwa kwa Katibu wa Jumuiya ya Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda ilikuwa miongoni mwa habari zilizoibua mjadala mzito huku kukiwepo na hali ya sintofahamu kama kiongozi alijeruhiwa kwa risasi au kitu chenye ncha kali.
Mkasa huo wa aina yake ulitokea Agosti 10, mwaka huu majira ya saa 12: 15 za jioni eneo la Barabara ya Tumbaku karibu na Fire, mkoani Morogoro mara baada ya kumalizika kwa Kongamano la Kiislamu lililofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja Cha Ndege, Kata ya Saba Saba.
Baada ya tukio hilo, uvumi ulisambaa maeneo mbalimbali nchini ukidai kuwa Shekhe Ponda amepigwa risasi na polisi na kufariki dunia.
Kuporomoka kwa ghorofa
Ilikuwa ni asubuhi ya Machi 29 ambapo jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa katika Mtaa wa Indira Gandhi  jijini  Dar es Salaam, liliporomoka na kusababisha vifo vya watu 36 na wengine kadhaa kufunikwa na kifusi.
Kuporomoka kwa ghorofa hilo kulizua huzuni, taharuki na simanzi kwa ndugu na jamaa waliofika kwenye eneo la tukio kutaka kufahamu nini kimetokea hali iliyosababisha kusimama kwa shughuli mbalimbali katikati ya jiji.
Matukio ya tindikali
Mwaka 2013 kumekuwa na matukio mengi wa watu kumwagiwa tindikali hususan upande wa Zanzibar, ambapo matukio kadhaa yaliripotiwa.
Julai 19 mwaka huu Said Mohamed Saad ambaye ni Mkurugenzi wa Home Shopping Center alimwagiwa tindikali na mtu asiyefahamika kisha kutokomea na kumuacha bilionea huyo katika maumivu makali.
Saad alipelekwa Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu lakini ilishindikana kutokana na madhara makubwa aliyoyapata kutokana na tindikali hiyo hali iliyosababishwa kupelekwa Ujerumani kwa matibabu zaidi.
Matukio mengine yalitokea Zanzibar kuhusisha  raia wawili wa Uingereza, Kate Gee na Kirstie Trup waliomwagiwa tindikali, eneo la Mji Mkongwe na Padri wa Parokia ya Machui, Anselmo Mwang’amba .
Siku chache baada ya tukio hilo lilitia doa nchi ya Tanzania katika ramani ya kimataifa, jeshi la Polisi upande wa Zanzibar lilitangaza kukamata lita 29 za tindikali.
Mauaji ya kutumia silaha
Mwaka huu pia kulikithiri kwa mauaji ya  kinyama kwa kutumia silaha ambapo watu kadhaa walijikuta wakipoteza maisha na wengine kujeruhiwa, kutokana na vitendo hivyo vilivyoonekana kushika kasi nchini.
Miongoni mwa matukio hayo ni mauaji ya Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Minara Miwili, Evarist Mushi ambaye alipigwa risasi na watu wasiofahamika asubuhi ya Februari 17 mwaka huu.
Mauaji mengine yalitokea Agosti 7 kwa mfanyabiashara maarufu wa madini Erasto Msuya kuuawa kwa kupigwa risasi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro. Msuya alikuwa anamiliki vitegauchumi kadhaa na kuaminika kama mfanyabiashara aliyekuwa akiongoza kwa utajiri Mirerani aliuawa kwa kupigwa risasi zaidi ya 20.
Tukio lingine la mauaji lillilotokea Oktoba 13  eneo la Kibamba ambalo kwa kiasi kikubwa lilihusishwa na  ugomvi wa  kimapenzi ambapo Mtangazaji wa Kituo cha ITV, Ufoo Saro alijeruhiwa kwa  risasi huku mama yake mzazi akipoteza maisha kutokana na shambulio lililofanywa na mzazi mwenzie aliyejulikana kama Anthery Mushi.
Operesheni Tokomeza
Operesheni  hii iliyolenga kupambana na vitendo vya ujangili dhidi ya wanyamapori ilianza rasmi Oktoba 5, mwaka huu katika hifadhi za taifa, mapori ya akiba na mbuga za wanyama huku ikishirikisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Idara ya Wanyamapori. Mawaziri wanne waliopoteza  nafasi zao kufuatia operesheni hiyo, nao ni Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Dk David Mathayo (Mifugo na Uvuvi), Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na JKT).

No comments:

Post a Comment