Mmkazi wa Ludewa, Mkoani Njombe, Yohana Nkwera (54) anadai kukatika miguu katika hali ya kushangaza.Yohana
anasema katika maisha yake amekuwa ni mwenye hofu kubwa baada ya
kukumbwa na tukio hilo la aina yake la kukatika miguu akiwa usingizini.
Anasema hadi sasa haelewi namna hasa tukio hilo lilivyomtokea, kwani
hakuhisi maumivu yoyote .Anasema
tukio hilo la aina yake lilimtokea mwaka 1992, lakini halikuwahi
kuandikwa wala kutangazwa, badala yake ni watu wachache waliokuwa
wakilifahamu.Anasema siku hiyo usiku alikwenda kulala kama ilivyo kawaida, alipoamka asubuhi alikuta miguu yake imekatika.Kilichomshangaza
zaidi ni kwamba hapakuwa na damu wala jeraha lilionekana. Palionekana
pana kovu, kana kwamba alikatika mguu muda mrefu uliopita.
Anasema
mara ya kwanza ulianza kupotea mguu wa kulia, hiyo ilikuwa ni mwezi
Machi, 1992. Kutokana na tukio hilo, ndugu zangu walifanya jitihada
mbalimbali ikiwemo kufanya maombi katika nyumba mbalimbali za ibada,
huku wengine wakienda kwa kuwaona waganga wa jadi.
“Kama binadamu wa kawaida ilichukua muda sana kuamini kilichotokea ndani ya maisha yangu na mguu wangu,” anasema.
Mwezi
mmoja baadaye yaani mwezi Aprili mguu wa kushoto nao ulikatika katika
mazingira yaliyo sawa na yale ya awali.Inaweza kuwa vigumu kuamini
lakini ulimwengu ndivyo ulivyo.
Anakumbuka
mazingira ya kukatika kwake yanahusishwa na imani za kishirikina kwa
sababu siku chache zilizopita kabla ya kukumbana na dhahama hiyo aliwahi
kukorofisha na mtu katika vilabu vya pombe za kienyeji anayesadikiwa
kufanya tendo hilo.
Baada ya
miaka saba kupita Yohana alipelekwa Hospitali Teule ya Ikonda wilayani
Makete kupata huduma za tatizo lake. Alifanikiwa kupata msaada wa
baiskeli ya magurudumu, ambayo aliitumia kwa miaka mitano.
Kwa sasa
baiskeli hiyo haifanyi kazi kutokana na watu wanaosadikiwa kuwa ni wezi
kuiba matairi na vyombo muhimu vinavyoiwezesha baiskeli hiyo kufanya
kazi.
Pamoja na
kupewa baiskeli hiyo na wasamaria wema, Yohana anakiri pia kuchongewa
viatu na hospitali hiyo ambavyo vinamuwezesha angalau kutembea umbali
mfupi.
Kutokana
na ulemavu huu wa kimiujiza, Yohana anakiri ndoto zake za maisha
hazijatimia mpaka leo na inawezekana zikawa zimepotea kabisa.
Mipango yake
Alipinga
mambo mengi yakiwemo kusoma na hata kufungua miradi ya maendeleo. Sasa
ni kama anaona haiwezekani tena kwa sababu hana uwezo thabiti wa kufanya
kazi; ukizingatia ni kijijini ambako kazi kubwa inayotegemewa kiuchumi
ni kilimo cha jembe la mkono.
Ulemavu
huo umesababisha ashindwe kuoa, kwani anasema katika ulimwengu wa sasa
ni ngumu kuoana na mtu kama huna uwezo wa kumhudumia.
Anasema
ilikuwa ni ngumu kwa ndugu kuamini kinachotokea lakini anawashukuru
wasamaria wema walioendelea kumhudumia mpaka pale alipoikubali hali yake
na kuanza kuishi katika huo mfumo mpya wa maisha.
Kwa sasa
Yohana anaishi na dada yake mkubwa aitwaye Lucy Nkwera akimsaidia kwa
mahitaji ya kila siku ikiwemo chakula na huduma za usafi na usalama kwa
jumla.
Akisimulia
kwa hisia, Yohana anakumbuka jinsi alivyokuwa katika hali ya uzima wa
miguu na kujitegemea, kwamba anashangaa sana kuona leo amekuwa ni mtu wa
kuomba msaada; kwa sasa msaada wake mkubwa ni dada yake huyo.
Lucy anasema, “Maisha ni magumu sana kwa kuwa anatakiwa kuwa karibu naye, kwani hakuna mwingine wa kumsaidia.”
Mbali na kupata huo ulemavu wa miguu, Yohana anaumwa ugonjwa wa kifafa, ambao nao aliupata baada ya kukatika miguu.
Ugonjwa huu unamfanya kupoteza fahamu mara kwa mara kitendo ambacho ni hatari kwa afya na maisha yake.
Anamshukuru
Lucy kwa kuendelea kumhudumia kwa sababu kwa mazingira ya kawaida ni
wachache wenye moyo wa huruma kiasi hicho, hasa kumhudumia mgonjwa
ambaye hatarajii kupona leo hata kesho.
Anashukuru pia ndugu zake kutoka maeneo mengine akisema kuwa nao wamekuwa wakija kumtaka hali na kumletea vyakula.
Anaishukuru Serikali ya Kijiji cha Ludewa anachoishi, kwa kumkumbuka na kumhudumia kwa kadiri wanavyoweza.
Anasema
kama Serikali na ndugu wasingekuwa wanamsaidia, huenda hali yake
ingekuwa ngumu zaidi na ilivyo sasa kwani kwa jumla afya yake ni dhaifu.
Ushauri wake
Yohana anawaomba watu kuachana na tabia za kunyanyapaa walemavu.Anasema baada ya kuwa na ulemavu, kuna marafiki zake walimtenga.
“Inauma
sana kuona kumbe wengine ni marafiki wa wakati wa raha...Ukiwa na
matatizo wanakukimbia, hii tabia si nzuri, ni lazima tuwe na moyo wa
kusaidiana wakati wote,” anasema Yohana.
Anaongeza
kuwa hata yeye hakupenda kuwa katika hali ambayo anayo sasa. Ndiyo
kusema kwamba yeyote anaweza kupatwa na lolote kabla ya hajafa,
tusinyanyasane. chanzo-MWANANCHI
No comments:
Post a Comment