WACHEZAJI
wa timu ya soka ya Mbeya City, wamepigwa marufuku kunyoa nywele za
pembeni na kuziacha za katikati 'kiduku' na wameambiwa atakayejitosa
kunyoa hivyo itakula kwake.
Mbali ya hilo, pia wamepigwa marufuku kufuga nywele na kuzisokota 'rasta'.
Kauli ya
marufuku hiyo imetolewa na Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Maka Mwalwisi na
kuungwa mkono na Katibu Mkuu, Emmanuel Kimbe, waliosema wachezaji wa
timu yao hawajafikia hatua ya kunyoa nywele kwa mfumo huo kama
wanavyofanya wachezaji wa timu nyingine.
Mwalwisi
alisema kuwa wachezaji wa Kitanzania wameiga mfumo huo kutoka kwa
wachezaji wa nje jambo ambalo kwao imekuwa ni vigumu kuhudumia nywele
zao kutokana na kipato kidogo wanachokipata.
"Kilichoruhusiwa
ni kunyoa upara, hayo mambo mengine ya 'kiduku' na 'dread' kwetu hayana
nafasi, kwanza uwezo wenyewe wa kuzihudumia hawana maana wakiweka hizo
'dread' zao wanakuwa kama wachafu," alisema. "Nywele zinahitaji matunzo
kama wanavyofanya wachezaji wa nje pia muda wa kwenda kuzihudumia
saluni, hapa Tanzania hata hao wanaofuga na kunyoa viduku uwezo wao
kifedha sio mkubwa, tumewaambia atakayenyoa hivyo atapewa adhabu kwa
mujibu wa taratibu zetu."
Alisema
kuwa kwao nidhamu ya ndani na nje ya uwanja ndiyo wanaipa kipaumbele
kuliko mambo mengine yoyote, suala ambalo liliungwa mkono na aliyekuwa
mwamuzi wa soka, Othman Kazi.
Kazi
alisema: "Tangu wapande daraja nimebahatika kuangalia mechi zao ila
sijawahi kuona timu yenye nidhamu kama Mbeya City, ingawa siwezi
kuzungumzia kiundani mechi yao na Yanga.
"Wachezaji
wa Mbeya City hawana tabia ya kumzonga mwamuzi pale anapotoa uamuzi
wake na hiyo ndiyo nidhamu inayotakiwa kwa wachezaji."
Katika
mechi ya timu hiyo dhidi ya Yanga iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam, Yanga ilishinda bao 1-0. Hicho kilikuwa kipigo cha kwanza
cha Mbeya City katika msimu wao wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania
Bara.Chanzo: mwanaspoti
No comments:
Post a Comment