WANAFUNZI
wa shule ya msingi na sekondari ya St Anne Marie Academy ya Dar es
Salaam, wamefanya vurugu zilizoambatana na uharibifu mkubwa wa mali
ikiwamo kuvunja vioo vya magari, mabweni, madarasa na kompyuta, chanzo
kikidaiwa kuwa ni hatua ya uongozi wa shule kuwapa walinzi mamlaka
makubwa ya kuwaadhibu.Mamlaka
hayo walidai yameendelea kujidhihirisha kwa muda mrefu ambapo usiku wa
kuamkia jana, mwanafunzi Loshilaa Emmanuel wa kidato cha sita, alipigwa
na mlinzi na kushonwa nyuzi kadhaa, jambo lililosababisha wanafunzi wa
bweni kuamka na kufanya vurugu za kuharibu mali baada ya kumkosa mlinzi
aliyedaiwa kumpiga mwenzao.Vurugu
hizo zinadaiwa kufanywa katika kipindi cha saa moja, kati ya saa nane
usiku na saa 10 alfajiri jana na tayari Polisi Mkoa wa Kinondoni
inashikilia wanafunzi tisa wanaodaiwa kuwa vinara wa vurugu hizo.
Wanane
kati yao ni wa kidato cha sita na mmoja ni wa kidato cha nne. Mali
zilizoharibiwa ambazo gazeti hili pamoja na kuelezwa, lilizishuhudia
shuleni hapo ni pamoja na kuvunjwa vioo vya magari 17 ya shule,
madirisha, taa na milango ya mbao katika madarasa yote hasa ya sekondari
na ofisi, kompyuta 40 kuharibiwa huku nyingine 16 mpya za mpakato
zikiibwa.
Viongozi
wa wanafunzi waliozungumza na gazeti hili shuleni hapo jana, kwa
nyakati tofauti walilaani vurugu hizo na kudai kuwa, lawama hazipaswi
kuishia kwa wanafunzi pekee hata kama wamefanya kosa kisheriam kwa kuwa
tukio hilo linahusisha malalamiko ya muda mrefu ambayo
hayajashughulikiwa yaliyojenga uhasama baina ya walinzi wa shule,
uongozi wa walimu na wanafunzi.
Miongoni
mwa malalamiko ni pamoja na Mkuu wa Shule ya Sekondari, Mary Msangi
kuwapa mamlaka walinzi wa shule hiyo yenye wanafunzi wa kutwa na bweni
kuanzia chekechea hadi kidato cha sita, kupiga wanafunzi wa sekondari
kipigo chochote wanapokosa kutii sheria za shule.
“Kumekuwa
na malalamiko ya muda mrefu ya wanafunzi kuhusu hawa maafande (walinzi)
wetu, usiku wanapokea hongo na kuruhusu wanafunzi watoke huku wengine
wakiwazuia, wengine wanaingiza vitu mpaka vileo, lakini wengine wakitaka
kutoka kunazuka ugomvi, ni kama wana njaa kali, sasa kuna adhabu
wanatoa zilizopitiliza ikiwamo vipigo,” alisema kiranja mkuu wa kiume wa
kidato cha sita, Innocent Mwombeki.
Kiranja
mkuu wa kiume wa kidato cha kwanza hadi cha nne, Hassan Haruni alisema
kuna matukio ya kupigwa wanafunzi hata kwa makosa ya kurekebishwa pekee
bila adhabu na kueleza kuwa, kabla ya tukio la jana, wanafunzi zaidi ya
wanne walishapigwa na walinzi.
“Mambo
yanakuwa mabaya zaidi kwa kuwa baadhi ya walimu viongozi wanahusika,
kwa mfano hivi karibuni Mkuu wa Shule (Msangi) alitangaza katika
mkusanyiko wa shule, kwamba amewapa mamlaka askari wapige wanafunzi ila
wamwachie roho,” alisema Emma Mhagama, kiranja mkuu wa kike wa kidato
cha kwanza hadi cha nne.
Mkuu
wa Shule Kiongozi Mkuu wa Shule Kiongozi, Johanssan Rwebugisa
aliliambia gazeti hili ofisini kwake kuwa, ni mapema kuthibitisha madai
hayo kwa kuwa mengi yalishashughulikiwa ingawa alikiri kuwa tukio la
mwanafunzi kupigwa na mlinzi usiku wa kuamkia jana haliwezi kuwafanya
wanafunzi washambulie shule nzima na kuharibu mali kama walivyofanya.
“Siwezi
kuwa na maelezo mengi, ila hii inaonekana kuwa ni jambo la muda
linalohitaji uchunguzi, hatutajua sababu hasa, kwa kuwa kama ni
malalamiko kuna utaratibu wa kuyawasilisha na kushughulikiwa na
hawajawahi kuyaleta kwangu, labda walipeleka kwa Mkuu wa Shule,” alisema
Rwebugisa.
Akielezea
kilichotokea, Rwebugisa alisema wanafunzi wa bweni, wengi wao wakiwa
kidato cha sita, walifanya vurugu baada ya kupata taarifa kwamba
mwanafunzi mwenzao aliyekuwa akijisomea, kapigwa na mlinzi.
Mwombeki
alisema hana uhakika kama ni kidato cha sita pekee walihusika na
vurugu, kwa kuwa saa nane usiku waliamshwa na wenzao kwenda kumsaidia
aliyejeruhiwa na mlinzi baada ya kupishana kauli, na wakiwa zahanati ya
shule, wanafunzi wa bweni wa vidato vya chini waliamka na kufanya vurugu
wakati wao wakiwa zahanati na mwenzao.
“Inaelezwa
Loshilaa alitaka kutoka nje, mlinzi akamzuia, wakaanza kubishana, ndipo
mlinzi akachukua shoka, upande wa mpini akampiga nao, tuliposikia
tuliamka ilikuwa saa nane usiku hivi, tukampeleka hospitali tukiwa wengi
kiasi, tulikaa nje kumsubiri, wazazi wake walipofika wakamchukua na
kumpeleka Kituo cha Afya cha Bochi, Kwa Musuguri, ndipo wengine wakaamka
na kuanza kuvunja mali,” alieleza Mwombeki.
Kiranja
wa kike wa Kidato cha Sita, Lidya Mkumbo alisema katika bweni la
wasichana la kidato cha sita, walishuhudia wanafunzi wa kiume waliokuwa
wamevaa kaptula bila mashati wakirusha mawe kwenye bweni lao na kuvunja
taa ndipo mwalimu mlezi alipowaamuru waingie ndani na kuwafungia mlango
kwa nje hadi saa moja asubuhi.
Mkumbo
alisema awali walitoka baada ya kuelezwa kuwa mlinzi anapigwa huku
baadhi ya wanafunzi wakidai kama ni mlinzi anapigwa ni bora aendelee
kupigwa, kwa kuwa hakukuwa na uhusiano mzuri kwa muda mrefu baina ya
walinzi na wanafunzi.
Mkuu
wa Wilaya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alitembelea
shuleni hapo jana akifuatana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni,
Camillius Wambura na kuagiza chanzo kitafutwe na uchunguzi zaidi
ufanywe, huku akielezea wasiwasi wake kuwa tukio hilo huenda likahusisha
pia ushawishi wa walimu kutokana na uharibifu uliofanywa na wanafunzi.
“Siamini
kama mwanafunzi mmoja kupigwa na mlinzi, adhabu inaweza kuwa ni
uharibifu huu wa mali, ingeingia akilini kama tungesikia mlinzi
kajeruhiwa baada ya kushambuliwa na wanafunzi kwa kumpiga mwenzao,
ingawa nalo ni kosa kisheria, lakini kuna mantiki kuliko la kushambulia
mali za shule namna hii, iko wapi nidhamu ya elimu?” Alihoji Rugimbana.
Alisema
kama mwekezaji wa shule hiyo akiamua kufunga mradi huo na kufungua
mwingine, hasara ni kwa Taifa, kutokana na mchango mkubwa wa sekta
binafsi katika elimu, hivyo alisisitiza wanafunzi kuheshimu maadili na
thamani kubwa ya ada wanayolipiwa na wazazi ama walezi wao kupata elimu
hiyo.
Ada
kwa sekondari katika shule hiyo inakaribia Sh milioni mbili kwa mwaka.
Kamanda Wambura alisema polisi imeimarisha ulinzi eneo hilo hasa
kutokana na kuwapo kwa wanafunzi watoto wa chekechea na shule ya msingi
ambao vurugu kama hizo huwaathiri zaidi zikitokea na kwamba wanaendelea
kuchunguza chanzo hasa cha tukio pamoja na thamani ya uharibifu wa mali.
Alitaja
wanafunzi waliokamatwa kuwa ni Marko Mkemi, Mandela Soka, Fabran
Fulena, Stanford Shomiki, Mwombeki Abdoni, Anyengise Frank, Amandus
Kimano, Godfrey Ndimila wote wa kidato cha sita na Emmanuel Mtesha wa
kidato cha nne. Msangi alipoulizwa kuhusu madai ya uongozi wa shule
kuwapa mamlaka walinzi ya kupiga wanafunzi, alisema msemaji pekee wa
shule kwa sasa ni Mkuu wa Shule Kiongozi ingawa alidai walinzi hao
hawana mamlaka hayo.
Mmiliki
wa Shule hiyo, Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza akizungumza
na gazeti hili kwa simu jana, alisema ameshtushwa na tukio hilo lakini
hawezi kueleza chochote kwa kuwa hajui chanzo na kuwa leo, kutakuwa na
mkutano wa dharura wa Bodi ya Shule, kuzungumzia suala hilo na hatua za
kuchukua.
No comments:
Post a Comment