Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
MABOSI wa
zamani wa mashirika ya umma, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), jana walipanda kizimbani kujibu
mashitaka yanayowakabili kutokana na uamuzi waliofanya walipokuwa
wakiongoza mashirika hayo.
Kaimu
Mkurugenzi wa TBS, Joseph Masikitiko, aliieleza mahakama kuwa, aliyekuwa
Mkurugenzi wa shirika hilo, Charles Ekelege, alitoa msamaha wa ada ya
utawala kwa kampuni mbili bila kufuata taratibu.
Masikitiko
alidai hayo wakati akitoa ushahidi katika kesi ya matumizi mabaya ya
madaraka na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh milioni 68,
inayomkabili Ekelege.
Ekelege
anadaiwa kusababisha hasara hiyo baada ya kuondoa ada ya asilimia 50
ambayo ni sawa na Sh milioni 68, kwa Kampuni za Jaffar Mohamed Ali na
Quality Motors bila idhini ya Bodi.
Akiongozwa
na Wakili Janeth Machulya kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru), Masikitiko alidai kuwa anazifahamu kampuni hizo kwa
kuwa zilikuwa zinafanya kazi ya ukaguzi wa magari kutoka nje kwa niaba
ya TBS.
Alidai
katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2009 akiwa Meneja wa Fedha na
Utawala, hajawahi kupokea wala kushughulikia barua za maombi ya
kuondolewa kwa ada ya utawala kutoka kampuni hizo mbili.
Kificho
Aidha
alidai hakujua kama kampuni hizo zilipewa msamaha wa ada, hadi alipopata
ripoti ya ukaguzi wa hesabu za nje ya mwaka 2008 hadi 2009, na kusikia
kwenye kikao cha Baraza la Utendaji ambalo kwa sasa ni Bodi ya
Wakurugenzi, cha Septemba 30 mwaka 2011.
Alidai
katika kikao hicho yeye akiwa mualikwa, walipata taarifa kuwa
Menejimenti ilitoa msamaha wa ada hiyo bila kupata kibali cha bodi hiyo,
ambapo bodi iliona walitoa msamaha huo kimakosa na kuwaonya wasirudie
tena.
Alidai
taratibu za kuomba msamaha wa ada ni kuwasilisha barua kwa Mkurugenzi,
kisha iende kwa Mhasibu Mkuu atakayeandika dokezo kwa Mkaguzi wa Ndani
ambaye ataangalia kama amekidhi vigezo vya kusamehewa, itapelekwa kwa
Meneja wa Fedha kisha Mkurugenzi ataipeleka Bodi ya Wakurugenzi kwa
ajili ya kuidhinishwa.
Akihojiwa
na Wakili Majura Magafu anayemtetea Ekelege, Masikitiko alidai kuwa,
Bodi haikusema kama Ekelege alifanya kosa, bali ilisema Menejimenti
ilifanya makosa kwa kutoa msamaha huo bila kupata kibali.
Inadaiwa
kuwa Machi 28, mwaka 2008 na Agosti 7, mwaka 2009, Ekelege alitumia
madaraka vibaya na kusamehe ada kampuni mbili kwa asilimia 50, ambayo ni
sawa na Sh milioni 68 bila idhini ya Baraza la Utendaji kinyume na
utaratibu wa TBS pia alilisababishia shirika hilo hasara ya fedha hizo.
Mataka
Meneja
Uendeshaji wa Kampuni ya Kuhifadhi Magari Yanayodaiwa Kodi, Bartholomew
Kijazi, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wanalidai
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) Sh milioni 206.4.
Kijazi
alidai hayo jana wakati akitoa ushahidi katika kesi ya kutumia vibaya
madaraka kwa kutangaza zabuni na ununuzi wa magari chakavu 26,
inayomkabili Mkurugenzi wa zamani wa shirika hilo, David Mattaka na
wenzake wawili.
Akiongozwa
na Wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro, Kijazi alidai kuwa wanaidai
ATCL fedha hizo kutokana na kuhifadhi magari tisa katika ghala lao
lililopo Mbagala, tangu 1998 hadi Novemba mwaka jana.
Alidai
kuwa Desemba 16, 2011 aliandaa ripoti ya mtiririko wa kuingiza na kutoa
magari 26 ya kampuni ya ATCL pamoja gharama za kuhifadhi na kukarabati,
baada ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kuomba ripoti
hiyo.
Alidai
wakati huo walikuwa wanaidai ATCL dola za Marekani 118,000 kutokana na
kuhifadhi magari hayo kwa miezi 39 kwenye ghala lao la Mbagala, ambapo
kati ya magari hayo, magari 15 yalitolewa na mengine tisa yamebaki
kutokana na kukosekana kwa fedha za kulipa ushuru wa forodha.
Alifafanua
kuwa kwenye ghala lao wanatoza kila gari dola 250 kwa mwezi na hadi
kufikia Novemba mwaka jana, walikuwa wakidai shirika hilo dola za
Marekani 129,000 ambayo ni sawa na Sh milioni 206.4.
Alidai
ATCL walihifadhi magari hayo katika ghala lao kuepuka gharama za
bandarini ambapo kwa siku wanatoza dola za Marekani 25 hadi 40 kulingana
na ukubwa wa gari na kwa mwezi ingekuwa dola 1,200.
Mbali
na Mattaka washitakiwa wengine ni Kaimu Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha,
Elisaph Ikomba na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani, William Haji.
Washitakiwa
wanadaiwa kula njama, matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia
Serikali hasara ya dola 143,442.75 za Marekani kwa kuagiza magari 26
chakavu kwa gharama ya Dola 809,300 kutoka Kampuni ya Bin Dalmouk Motors
ya Dubai bila kutangaza zabuni ya ushindani.
Aidha
wanadaiwa kuruhusu kununuliwa kwa magari hayo bila mkataba wa ununuzi
ambao umewekwa saini na wahusika na kuthibitishwa na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali na kuisababishia Serikali hasara baada ya kushindwa kulipia
kodi na kuchukua mkopo kwa ajili ya kuyakomboa na kuyatunza.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment