Wednesday, February 12, 2014

FUKWE ZA TANZANIA UCHOCHORO WA DAWA ZA KULEVYA

Baada ya kikosi kazi cha Jeshi la Polisi cha Kudhibiti Uharamia Baharini kukamata kilo 201 za dawa za kulevya aina heroini zilizokuwa zikiingizwa nchini kutoka Iran. Sasa imefahamika kuwa madawa ya kulevya yanapitishwa kwenye bahari ya hindi. Hii imethibotishwa  kwenye gazeti la MWANANCHI kutoa maelezo ya kina kuhusu madawa hayo.
 Polisi wa kikosi  kupambana na dawa za kulevya wakizifungua dawa hizo zilizokamatwa jana kwenye jahazi liitwalo Kunarak-Iran iliyokutwa katika bahari ya Hindi eneo la Tanzania ikiwa na Heroin kilo 201, pamoja na raia wa nane wa Iran na  wapakistan wanne.Picha na Michael Jamson
Gazeti la mwananchi linaeleza kuwa; wakati vita ya kupambana na biashara ya dawa za kulevya ikiendelea nchini, wasafirishaji wa dawa hizo wameanza kutumia fukwe ndogondogo za bahari nchini kuziingiza kutoka Mashariki ya mbali, gazeti hili limebaini.
Januari 10, mwaka huu saa 6:30 usiku, mwandishi wetu alishuhudia mzigo unaoaminika kuwa ni dawa za kulevya, ukishushwa kutoka kwenye boti, eneo la Salender Bridge, nyuma ya Kituo cha Polisi kilichopo eneo hilo.
Baada ya boti hiyo kutia nanga, walishuka watu zaidi ya 10; Wazungu wawili, Waafrika kadhaa na mmoja mwenye asili ya Asia na kuungana na wengine wanne ambao tayari walikuwa katika eneo hilo wakiwa ndani ya magari mawili.

Mara moja walianza kupakua mizigo iliyokuwa imefungwa kwenye maboksi na kupakia kwenye magari ambayo yalikuwa yameegeshwa mbali kidogo na ufukwe huo. Kazi hiyo ilichukua muda usiozidi nusu saa na baada ya mizigo kupakiwa, magari hayo moja likiwa ni Land Cruiser liliondoka na kuelekea upande wa Morroco na jingine aina ya Nissan liliondoka kwenda uelekeo wa Posta Mpya.
Wakati magari hayo yakiondoka kwa mwendokasi, boti iliyokuwa na mzigo huo nayo iling’oa nanga na kuelekea katikati ya Bahari ya Hindi.
Chanzo chetu kilisema mzigo ulioshushwa ni dawa za kulevya na kwamba boti hizo ndogo hufika eneo hilo hata mara mbili kwa wiki.
Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa dawa hizo huingizwa nchini kwa meli kubwa za mizigo, hasa zile zinazotoka Iran, Pakistan na Afganistan.
Ukamataji polisi
Mwandishi wetu aliwasiliana na polisi kuhusu njia hiyo ya kuingiza dawa za kulevya nchini na jeshi hilo kuahidi kutoa majibu baada ya kufanya ufuatiliaji. Kabla ya kutoa majibu juu ya ufuatiliaji huo, polisi ilikamata meli kutoka Iran ikiwa na kilo 201 za heroini katikati ya Bahari ya Hindi.
Msemaji wa Polisi, Advera Senso alisema kama taarifa hizo zingeripotiwa katika vyombo vya habari, ingekuwa vigumu kwa jeshi hilo kufanikisha kukamatwa kwa wahusika.
Katika wiki moja iliyopita, kilo 846 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh38 bilioni zimekamatwa kwenye mipaka ya Tanzania iliyoko katika eneo la Bahari Kuu, kiwango ambacho ni kikubwa katika rekodi ya kukamatwa kwa dawa za hizo.
Dawa hizo zilikamatwa kati ya Februari 2 na 5 mwaka huu. Kilo 350 za heroini zilikamatwa Februari 5 na wadhibiti wa dawa za kulevya wa Australia na kilo 265 za heroini zilikamatwa na wadhibiti wa kimataifa wa Canada, zote zikiwa zinaelekea Tanzania.

Dawa nyingine ni kilo 201 za heroini zilizokamatwa ndani ya mpaka wa Tanzania na Kikosi cha Polisi cha Wanamaji na kilo 30 zilizokamatwa Zanzibar.
Kamishna Msaidizi wa Tume ya Kuratibu Dawa za Kulevya, Aida Tesha alisema, kiasi hicho kikubwa kilikamatwa na wadhibiti wa bahari wa kimataifa walioshirikiana na wadhibiti wa Tanzania.
“Huu msimu ni wa wasafirishaji wa dawa za kulevya kwa njia ya maji. Ni wakati ambao wasafirishaji huleta dawa kwa wingi kwa sababu ya hali ya hewa. Ieleweke kuwa zinazokamatwa ni asilimia 10, tu. Wapo wengi ambao wanapita bila kubainika,” alisema Tesha.
Tesha alisema wadhibiti wa kimataifa wanapokamata dawa huziharibu majini ili kuwapa hasara wauzaji hao kwani wanapowaacha au kuzikabidhi kwa nchi zilizo mipakani, zinaweza kuwafikia watumiaji. Mkuu wa Interpol, Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile alisema hana taarifa za kina za kukamatwa kwa kiasi hicho cha dawa za kulevya isipokuwa wenzake wamemtumia taarifa hizo akiwa Algeria.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu alisema: “Nina taarifa za Kilo 201 za heroini, ambazo watuhumiwa wake 12 Raia wa Iran na Pakistan tayari wameshafikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka yao”.
DCI Mngulu alisema polisi wanaendelea na doria kwenye maeneo ya bahari kwa kutumia mbinu zote ili kuhakikisha tatizo hilo linapungua.
Kwa upande wake, Kamishna wa Kikosi cha Polisi cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema: “Ni kweli hicho ni kiasi kikubwa kukamatwa kwenye mipaka ya Tanzania na kinaonyesha kuwa watu hawa wanadharau mipaka yetu, pia kunaonyesha kuwa tunafanya misako mikali.”
Fukwe nyingine
Uchunguzi ulibaini kuwa fukwe nyingine ndogo za Dar es Salaam zinatumika kushusha dawa za kulevya bila kugundulika kwa urahisi na kukwepa nguvu nyingi za udhibiti ambazo zilikuwa zimewekwa katika viwanja vya ndege na mipaka ya barabara.
Miongoni mwa fukwe hizo ni Mbezi Jogoo, Dar es Salaam na eneo maarufu la Loliondo ya Kigamboni ambako pia kunadaiwa kuwa na vitendo vya kutisha vya ukahaba, biashara ya pombe haramu ya gongo na bangi.
Uchunguzi umebaini pia kuwa katika eneo la Loliondo, wavuvi hutumika kubeba dawa hizo kwa kutumia boti kutoka kwenye meli kubwa na kufikisha mizigo husika nchi kavu ambako hupokewa na watu maalumu na kuanza usambazaji.
Katika Pwani ya Bagamoyo, kiasi kikubwa cha dawa za kulevya hupitishwa na mara nyingi huwa zimefungashwa kama makopo ya samaki waliosindikwa.
Mkoani Mtwara, wasafirishaji hutumia fukwe ndogondogo kama za Mikindani kuingiza dawa hizo ambazo baadaye husafirishwa kupelekwa Msumbiji.
Katika Mkoa wa Lindi, maeneo ya Songo Mnara, Kilwa nayo yanatajwa kwamba yanatumika kuingiza dawa za kulevya kutoka Dar es Salaam na Zanzibar.
Uchunguzi wetu umebaini baadhi ya mbinu za kusambaza dawa hizo mitaani. Mizigo hufungwa kwenye khanga au matenga ili isitiliwe shaka na kisha kupelekwa mitaani kwa miguu na watu kati (middlemen) ambao hulipwa ujira kwa kazi hiyo.
Katika siku ambazo kuna wasiwasi au hofu ya kukamatwa, mizigo hufukiwa ardhini hadi hali inapotulia.
Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji, ACP Mboje Kanga alisema kwa Tanzania ni kazi ngumu kusimamia fukwe na uharamia unaofanyika, kwani ina fukwe zenye urefu wa kilometa 1,424.
Ripoti ya 2013 ya Kitengo cha Uhalifu na Dawa za Kulevya cha Umoja wa Mataifa (UNODC), inataja Bahari Kuu kuwa njia kuu zinazotumika kusafirisha dawa za kulevya hadi Tanzania hasa Tanga na Zanzibar, kisha kusafirishwa kwa boti ndogo kwenda Dar es Salaam na baadaye nchi za Kusini mwa Afrika.
Kadhalika, taarifa ya 2011 ya kitengo cha dawa za kulevya iliyochapishwa katika Ripoti ya Kitengo cha Dawa za Kulevya cha Marekani inaeleza kuwa, heroini huingia Tanzania kupitia Bahari ya Hindi ikitokea Afghanistan, Iran na Pakistan kupitia Dubai.
 MWANANCHI

No comments:

Post a Comment