MBIO za
urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimezidi kuibua mambo mapya,
baada ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kudai atachukua uamuzi
mgumu kama chama chake kitateua mgombea urais asiye na sifa.
Akizungumza
Radio Tumaini, mjini Dar es Salaam jana asubuhi, Sumaye alisema kama
CCM itafanya mambo ya ajabu kwa kuteua mgombea asiyekubalika wala kuwa
na sifa za kiongozi mwadilifu, atafungua ukurasa mpya.
"Nitachukua
uamuzi mgumu kama CCM watateua mgombea ambaye hana sifa ya kuwaongoza
Watanzania, nitachukua uamuzi mgumu, haiwezekani tukaongozwa na watu
wanaotoa fedha nyingi kila kukicha.
"CCM wakifanya mambo ya ajabu kwa kuchukua mtu ambaye ametoa fedha, nitatafuta njia nyingine," alisema.
Alisema hata siku moja hatakuwa na kinyongo kama atateuliwa mtu safi na mwenye moyo mweupe wa kusaidia Watanzania.
Alipoulizwa
swali kama atagombea urais, alisema "Mimi sisemi kama nagombea,
nakwambia muda ukifika nitasema tu, kwa wakati huu naomba tuendelee
kutulia kwanza.
"Muda
ukifika nitaamua nini cha kufanya, unajua unapotaka kuchukua uamuzi huu
kuna mambo mazito ambayo unapaswa kuyatafakari kwa undani zaidi.
"Miongoni
mwa mambo haya, ni kusaidia Watanzania kutoka walipo ili wapige hatua
moja mbele zaidi, kuachana na tabia ya mtu mmoja kujitajirisha kupita
kiasi," alisema Sumaye.
Alisema kama Watanzania wakimhitaji ili awasadie, atakuwa tayari kufanya hivyo.
"Muda
ukiwadia na Watanzania wakisema wananihitaji, basi nami nitakuwa tayari
kuwasaidia...jukumu hili linahitaji mtu mwenye busara sana," alisema
Sumaye.
Alipoulizwa
kuhusiana na hali ya CCM kwa sasa, alisema kuna tofauti kubwa katia ya
CCM ya mwaka 1977 na ya sasa ambayo imekuwa ikikumbwa na matukio mengi.
Akitoa
mfano, alisema: "Hivi sasa ukitaka kugombea lazima uwe na fedha, haya ni
mambo machafu ambayo CCM yetu ya miaka ya 77 haikuwapo kabisa.
"Nalisema hili kutoka moyoni mwangu, nimekuwa mbunge na mjumbe wa NEC kwa miaka 20, sijawahi kutoa rushwa wala kupokea.
"Ukiona
watu hao wanatoa rushwa, ujue moja, hawana uwezo wa kuongoza wananchi
wao na ndani ya mioyo yao hawana dhamira safi zaidi ya kutanguliza
maslahi yao.
"Nikikuhonga
leo ujue sina nia njema, sitakuhudumia pindi nitakapoingia madarakani,
nitaanza kwanza kutafuta namna ya kurudisha fedha zangu... hii ni vita
ambayo CCM tunapaswa kuipinga kwa nguvu zote," alisema Sumaye.
MUUNDO WA SERIKALI
Akizungumzia muundo wa Serikali, alisema yeye ni muumini wa muundo wa
serikali mbili siku zote na atendelea kusimamia ukweli huo.
"Haiwezekani
ndani ya taifa hili tukawa na serikali tatu, hivi Rais wa Jamhuri
ambaye anamiliki mali nyingi, akisema anamnyima Rais wa Tanganyika
misaada nini kitatokea... huu ndio mwanzo wa kuondoa utulivu wetu, tuwe
makini, tutaparanganyika," alisema Sumaye.
RUSHWA
Kuhusu rushwa, alisema wakati wa utawala wa awamu ya tatu, chini ya
Rais mstaafu Benjamin Mkapa, walipambana vya kutosha, ikiwa ni pamoja na
kuondoa kipengele cha takrima.
"Tumepambana
vya kutosha dhidi ya rushwa, hata takrima tulihakikisha inaondolewa
wakati ule baada ya kubaini uchaguzi wa serikali za mitaa ambao
ulijumuisha madiwani, ndiko hali hiyo ilikuwa imejikita.
"Nakumbuka
enzi za utawala wangu, niliagiza idara zote za serikali mikoani na
wilayani kukutana kwa saa moja kujadiliana masuala ya rushwa na ugonjwa
wa Ukimwi," alisema Sumaye.
MAWAZIRI MIZIGO
Akizungumzia utendaji kazi wa awamu yake, Sumaye alisema ndani ya Baraza la Mawaziri hakukuwa na mawaziri mizigo.
"Sikuwa na mawaziri mizigo kwenye utawala wangu, utaona hata umma kwa sehemu kubwa unakiri tulifanya kazi nzuri.
"Nakwambia ukiwa na mizigo unapaswa kuitua haraka sana kabla ya watu hawajakuona," alisema Sumaye.
WAPINZANI
Kuhusu vyama upinzani, Sumaye alisema vimekuwa na mchango mkubwa wa kuimarisha serikali katika utekelezaji wa mambo muhimu.
"Siku zote
nimekuwa muumini mkuu wa upinzani, wamekuwa kiungo muhimu, natamani
kuona wanaingia kwa wingi kwenye Bunge letu, michango yao
mizuri...nawaomba waendelee hivi hivi wasirudi nyuma," alisema Sumaye.
MBOWE
Kuhusu kauli ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Freeman Mbowe, kwamba Katiba itapatikana kwa ngumi, Sumaye
alisema kauli hiyo si nzuri, kwa sababu amani ikitoweka, si CCM wala
CHADEMA watakaopona.
"Nimemsikia
akiruka na helikopta zake huko mikoani na kusema atatumia nguvu, hivi
jamani leo amani ikitoweka, CCM na CHADEMA watapona?" Alihoji Sumaye.
Chanzo: mwananchi
No comments:
Post a Comment