Naibu
Waziri wa Fedha akiangalia Moja ya Mtumbi unaotumiaka kuvushia Biashara
za Magendo kwenye hiki kivuko haramu cha Timotheo kwenye Mto Songwe.
Naibu
Waziri wa Fedha Mh:Mwigulu Nchemba akifanya mahojiano na Vijana
waliokutwa wakivusha sukari kutoka Malawi kuja Tanzania.Vijana hao
wanadai wanalazimika kutumia njia hizi haramu kuvusha Sukari kutokana na
kuwa na mitaji midogo ya biashara zao,Hivyo kupita kwenye Kivuko Rasmi
cha Kasumulu wanakatwa Kodi Kubwa ambayo inawafanya wakose faida kwenye
Biashara yao.
Kyela. Zaidi
ya watu 10 wamenusurika kufa maji baada ya kujitosa ndani ya Mto
Songwe, wakihofia kukamatwa wakati wakivusha sukari ya magendo kutoka
nchi jirani ya Malawi.
Walikuwa
wanahofia kukamatwa na askari polisi waliokuwa wameongozana na Naibu
Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, wakati alipotembelea mpaka wa Tanzania
na Malawi wa Kasumulu, wilayani Kyela.
Katika tukio hilo, watu hao waliamua kuitupa majini, sukari na baiskeli moja waliyokuwa wakiitumia.
Tukio
hilo lilitokea juzi baada ya Naibu Waziri Nchemba na msafara wake,
kuwasili katika kivuko cha Timotheo, umbali wa kilometa tatu kutoka
ulipo mpaka rasmi wa Kasumulu.
Vijana hao walikuwa wanatumia mtumbwi wa jadi, kuvusha sukari hiyo kutoka Malawi na kuiingiza nchini.
Nchemba
alitembelea vivuko viwili kati ya 32 ambavyo ni njia za panya
zinazotumika katika kuvusha bidhaa za magendo na hivyo kulikosesha taifa
mapato.
Baada ya
kuvuka mto, baadhi ya vijana walitimua mbio na wengine walioshindwa
kuogelea, waliokolewa na kutolewa ndani ya maji kwa tabu.
Wakizungumza
baada ya kuokolewa, vijana hao walisema wanafanya biashara hiyo ya
magendo kwa lengo la kupata fedha za kujikimu na kuwasomesha watoto wao.
“Tunashindwa
kutumia mpaka halali kuingiza sukari hiyo nchini kwa sababu bidhaa hiyo
hairuhusiwi kisheria kuingizwa nchini. Pia hatuna uwezo wa kulipa
ushuru mkubwa na sisi mitaji yetu ni midogo, wengi wetu tuna mitaji ya
kuanzia kilo 20 hadi 100,”alisema mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja
la Lugano.
Alisema
pia baadhi ya vijana wanaovusha sukari hiyo, hawana mitaji ya kuendeshea
biashara hiyo na kwamba wanatumiwa na wafanyabiashara wakubwa kuingiza
sukari kwa magendo na kulipwa ujira kidogo unaowawezesha kujikimu.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kyela, Magreth Malenga
alisema changamoto kubwa katika kupambana na biashara ya magendo ya
sukari ni uhaba wa watumishi na vitendea kazi.
Pia kukosekana kwa sukari ya Tanzania katika maeneo mengi ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Alisema
wakati mwingine hushindwa kuweka mkazo wa kuzuia sukari hiyo kuingizwa
nchini kutokana na hali halisi kwamba wananchi hawana sukari mbadala kwa
sababu sukari ya Tanzania haipatikani kirahisi.
Kwa upande wake, Nchemba alisema amejionea ukubwa wa tatizo na kwamba Serikali italifanyia kazi ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
Pia
aliwataka vijana hao, kujiandaa kisaikolojia, ili kufanya biashara kwa
njia halali na zinazokubalika badala ya njia hiyo inayoweza kusababisha
matatizo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment