Ile
'safari ya Lowassa' imeibua mambo na mjadala mzito ndani na nje ya CCM.
Jambo la kujiuliza, je, safari hiyo ina urefu na vikwazo kiasi gani?
"Nimefarijika
sana leo kuwaona hapa marafiki zangu wengi. Ninapowatazama hadi machozi
yananitoka na kwa uwezo wa Mungu tutashinda kwani nyote mnajua nia na
ndoto yangu...WanaCCM msiwe na shaka, tutavuka kwa nguvu zetu... Wingi
wenu huu unanipa faraja katika safari yetu na kwa kumtegemea Mungu
tutashinda." ni kauli ya aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
Lowassa
alitangaza hivi karibuni kuanza rasmi kwa safari hiyo aliyoiita ya
matumaini ya ndoto zake, ambayo anasema itatimiza ndoto za Watanzania za
kupata elimu bure, majisafi na maendeleo ya uhakika.
Alitoa
kauli hiyo katika ibada ya shukrani na kuupokea mwaka mpya, katika
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),Usharika ya Monduli
Mjini mkoani Arusha.
Bila ya
kutaja safari hiyo ni ipi, Lowassa anawataka waliohudhuria ibada hiyo
waungane na kaulimbiu yake, 'Tulifurahi pamoja, tulihuzunika pamoja na
tutashinda pamoja'.
Hafla
hiyo ya kimkakati, ilihudhuriwa na baadhi ya wabunge, wengi wakiwa wa
CCM, wenyeviti wa mikoa kadhaa wa chama hicho, wakiongozwa na Mwenyekiti
wa Wenyeviti wa CCM, viongozi wa jumuiya za chama na wengineo.
Licha ya
kutoweka bayana aina ya safari anayoanza, Lowassa ni miongoni mwa
wanaCCM wanaotajwa kuwa wanaowania urais, kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Dalili
hizi za Lowassa kuutaka urais na kutafuta kabla ya kipenga kupulizwa,
zimeishtua CCM na kumtahadharisha kuwa atapoteza sifa ya kupitishwa
ifikapo 2015.
Safari tangu 1995
Tamaa ya
Lowassa kuutaka urais haikuanza leo wala jana, ni ya tangu 1995
alipojitokeza kwa mara ya kwanza. Mwaka huo alikuwa miongoni mwa
wagombea 17 wa CCM walioomba kuteuliwa kuipeperusha bendera ya chama
hicho.
Majina
hayo yalipaswa kujadiliwa na vikao vitatu vya CCM –Kamati Kuu,
Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu. Kikao cha kwanza kilikua ni Kamati Kuu
ambacho Mwenyekiti wake alikuwa Mwenyekiti wa CCM wakati huo, Ali Hassan
Mwinyi lakini Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa bado na
ushawishi na nguvu kubwa ndani ya chama hicho.
Nyerere
bila kumung'unya maneno, alisema wazi akiwataja wazi Lowassa na Waziri
Mkuu mstaafu, John Malecela kuwa hawakuwa wanafaa kugombea.
Nyerere
alisema Malecela alikuwa na madhambi mengi na kwamba alikuwa
ameyabainisha katika kitabu chake cha 'Uongozi na hatima ya Tanzania'
ambacho pia alielezea udhaifu wa Horace Kolimba, aliyekuwa Katibu Mkuu
wa CCM.Kuhusu Lowasa, habari zilizokaririwa kutoka kwenye kikao hicho,
zilisema Nyerere alihoji utajiri wake;
"Huyu
kijana wa miaka 42 tu amepata wapi utajiri wote huu? Licha ya kutetewa
na wapambe wake, Lowassa hakufanikiwa kupenya kwenye hasira za Nyerere.
Baada ya mchujo kufanyika kwa wagombea hao 17, jina la Benjamin Mkapa likaibuka kidedea na kuchukua nafasi hiyo.
Aluta continua
Licha ya Nyerere kumwengua katika kinyang'amyiro cha urais mwaka 1995, Lowasa hakukata tamaa.
Baada ya Mkapa kupitishwa na hatimaye kuwa rais, Lowassa alijiunga na Rais Jakaya Kikwete aliyeleta upinzani mkali.
Kundi
hilo ndilo lililomwezesha Rais Kikwete kupitishwa na CCM kugombea urais
mwaka 2005 huku Lowassa akiteuliwa kuwa waziri mkuu.
Hata hivyo, 'la kuvunda halina ubani', mwaka 2008, Serikali iliingia kashfa ya uzalishaji wa umeme tata wa kampuni ya Richmond.
Sakata
hilo lilipofikishwa bungeni, iliundwa Kamati iliyokuwa chini Waziri wa
wa sasa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ambayo hatimaye ripoti yake
ilitosha kabisa kumwengua Lowassa katika nafasi ya hiyo na hivyo Baraza
la Mawaziri kuvunjika.
Hilo
lilikuwa pigo la pili la Lowassa kisiasa. Bado hakukata tamaa. Licha ya
kutoweka wazi, Lowassa sasa anaonyesha kila dalili za kuutaka urais
ifikapo 2015.
Katika
jitihada hizo yeye na wapambe wake, wamefanya mambo mengi ikiwa pamoja
na kuweka mtandao mpana wa wafuasi na kuhakikisha kundi lake linaingiza
wajumbe wengi kwenye Halmashauri Kuu ya CCM na mkutano mkuu pia.
Mbinu
nyingine wanazotumia kujiweka karibu na makundi mbalimbali ya kijamii
kwa kutoa misaada ya aina mbalimbali, kuchangisha fedha makanisani na
misikitini, kutumia vyombo vya habari, mitandao ya jamii na baadhi ya
wabunge kumsafishia njia. Sasa ameanza kujiweka karibu vijana na hasa
waendesha bodaboda.Akizungumzia suala hilo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala anasema
mwendendo wa Lowassa hautoi sura nzuri kwa ndoto yake ya urais.
"Mimi
ukiniuliza, nitakwambia, Lowassa hafai kuwa rais... kwanza alishapewa
tamko na Mwalimu Nyerere mwaka 1995 akihojiwa kuhusu utajiri wake
ameupata wapi na hakujibu. Sasa amekumbwa na kashfa ile ya Richmond,
hadi akajiuzulu," anasema na kuongeza:
"Watanzania tuwe makini, uongozi siyo lelemama, tutaivuruga nchi yetu."
Profesa Mpangala amekikosoa Chama Cha Mapinduzi kwa kushindwa kuwadhibiti watu kama Lowassa.
"Hayo ni
mambo ya chama... kama kweli ameshaanza kujinasibu, basi amekosea
utaratibu wa chama, lakini hakichukui hatua. Hawa ndiyo walisema
watajivua gamba, wameshindwa. Wanasema tu taratibu zimekiukwa lakini
hawachukui hatua. Na Lowassa kwa kuwa ana utajiri na ushawishi mkubwa
anaweza kupitishwa na kushinda," alisema.
Hata
hivyo, kwa upande mwingine, Mhadhiri wa Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu
(Duce), Dk Kitila Mkumbo amemtia moyo Lowassa akisema anachokifanya
ndiyo utaratibu wa demokrasia.
"Sioni
kama Lowassa anatofauti na wana CCM wengine. Mengi yamesemwa juu yake
lakini huwezi kuyashika mkononi. Ameshafafanua hadharani kuwa kashfa ya
Richmond ilisababishwa na mfumo uliokuwapo, hivyo alijiuzulu kwa niaba
ya CCM," anasema Dk Mkumbo na kuongeza:
"Nashangaa
watu wanapozuiwa kujinadi kugombea urais mapema, huo ni ushamba. Mfumo
wa vyama vingi wa kiliberali tofauti na chama kimoja ambao ungesubiri
kutangazwa, unajiuza mwenyewe."
Akizungumzia zuio la Mwalimu Nyerere kwa Lowassa mwaka 1995, Dk Mkumbo anasema yalikuwa ni maoni yake binafsi.
"Mambo
mangapi yalisemwa na Mwalimu Nyerere na hatuyafuati? Ni kweli aliandika
katika kitabu chake cha 'Uongozi na Hatima ya Tanzania' lakini Lowassa
hayumo. Ni kweli alisema na tunamheshimu lakini hatulazimiki kuyafuata,"
anasema Dk Mkumbo.CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment