Wasomi na wanasiasa nchini wameupongeza uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba na kueleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ametumia busara kuwajumuisha wapingaji na wakosoaji wa kila jambo, ili wakatetee hoja zao katika bunge hilo kama watakavyofanya wawakilishiwa makundi mengine.
Mchungaji Christopher Mtikila. |
Tofauti na waliopongeza uteuzi huo, Mchungaji Christopher Mtikila kutoka Chama cha Democratic(DP) ambaye ameteuliwa katika bunge hilo ameuponda kwa kusema kuwa umejumuisha mambumbumbu wasio na uwezo wa kuutetea uhuru wa mtanganyika, kutokana na kuwa tayari kuubeba muungano ambao haupo.
Wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa za Tanzania waliotoa maoni ni pamoja na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) katika Idara ya Sayansi ya Siasa, Benson Bana na Robert Mkosamali aliyewahi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine mkoani Mwanza.
Bana alisema kuwa Rais Kikwete pamoja na mshirika wake Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohmed Shein wameonesha ukomavu wa kisiasa na busara ya hali ya juu kuwateua watu kama akina Mtikila ambao, kwa namna moja au nyingine, wangeweza kusumbua na kurudisha mchakato wote nyuma endapo majina yao yangeachwa.
Lakini, alipokuwa akiponda uteuzi huo, Mtikila alisema, "Uteuzi wangu hauna maana yoyote cha maana ni kutekeleza mahitaji ya uhuru wa wana wa Tanganyika, sijaona la msingi zaidi ya utanganyika kwa hiyo hata kama ningeachwa kwenye orodha ya wajumbe ingekuwa sawa tu".
Mtikila alisema hivyo kwa madai kuwa kundi lililoteuliwa kuwakilisha wasomi pamoja na makundi mengine yanayopinga utanganyika ni la watu mambumbumbu wasiojua kuwa hakuna muungano uliopo sasa, hivyo kung'ang'ania kuutetea na kuonesha dalili zote za kutoutetea utanganyika katika bunge hilo maalum.
"Mimi kwa mtazamo wangu ninaona kuwa structure (muundo) waliouweka ni wa kukaza gongo la utumwa kwa wana wa Tanganyika kwa sababu walipokonywa uhuru wao moja kwa moja, na wanachokwenda kukifanya katika bunge hilo maalum la katiba ni kuhalalisha muungano ambao haupo".
Mtikila alisema kuwa hawezi kuacha kichwa chake nyumbani akaenda katika Bunge hilo kuukanyaga utanganyika wake.
Hata hivyo, hakuweka wazi kama hatashiriki shughuli za bunge hilo lakini alifafanua hoja yake kuwa wanaodaiwa kuwa ni wasomi na wakongwe wa kisiasa katika uteuzi huo ni mambumbumbu walioshindwa kuutetea uhuru wa Tanganyika yao tangu awali.
Katika hoja nyingine, Bana alisema kuwa Rais Kikwete na Dk. Shein wametekeleza wajibu wao wa kulinda utaifa kwa kuhakikisha wameyagusa makundi yote kwa haki na usawa.
"Ni jambo la kupongezwa kwa sababu majina yalikuwa mengi sana na viongozi wetu hao kwa kuzingatia vigezo na sheria wameweza kuchagua wawakilishi wa kila kundi bila ubaguzi. Jambo hilo ni la heri kwa watanzania kwa kuwa litatusababishia tupate katiba inayokubalika kwa wengi,"Bana alisema na kuongeza kuwa wapingaji wa kila jambo hawatakuwa na nafasi ya kusema wamenyimwa nafasi ya kusema kwa kuwa nao wamejumuishwa katika kundi.
Mkosamali yeye alisema kuwa uteuzi ni mzuri kwa sababu umewakumbuka watu mashuhuri kama akina Mtikila wanaopigania Utanganyika ili wakatetee hoja zao.
Alisema kuwa kilichofanywa na viongozi hao ni kuondoa uwezekano wa kuwepo chuki au hali ya kundi fulani kuhisi limepuuzwa kwa kuwa kila lililopendekezewa majina liliguswa na kupewa nafasi kwa uwiano ulioeleweka tangu mwanzo wa mchakato.
"Kwa maana hiyo, kitakachozalishwa hapo kitakuwa kimejumuisha mawazo na maoni ya kila kundi hivyo kuwafanya watanzania wawe na katiba itakayokuwa na mambo yaliyokubaliwa kwa umoja. Hii ni hatua nzuri ya kuimarisha umoja wa watanzania.
Mbali na Mtikila, wanasiasa wengine waliotoa maoni ni pamoja na Mbunge wa Kilindi,Beatrice Shelukindo, Mbunge wa Igunga, Dalaly Kafumu na Mbunge waViti Maalum, Lediana Mng'ong'o waliosema kwa nyakati tofauti kuwa uteuzi wa wajumbe hao ni mafanikio kwa watanzania.
Shelukindo alisema kuwa utaifa umezingatiwa kwa kujumuisha makundi yote yaliyopendekezwa na kwamba hata wasomi hawajabaguliwa kutokana na ukweli kwamba wamejumuishwa kwenye ngazi zote.
"Kwa hili nampongeza Rais wetu kwa sababu amezingatia weledi pia. Binafsi kama mama, nimefurahishwa zaidi na jinsi alivyoweka usawa katika uchaguzi kwa kuzingatia jinsi. Ninahakika kwamba mjadala utazingatia matakwa ya watanzania",alisema Shelukindo.
Kwa upande wake, Kafumu alisema kuwa anaunga mkono uteuzi wa Rais na kumpongeza kwa kuwa haikuwa kazi rahisi kuteua majina kwa kuzingatia usawa na vigezo vingine vya jinsi bila kuacha kundi hata moja bila uwakilishi.
"Amemaliza sehemu ya kazi yake na kuridhisha watanzania wengi, shughuli iliyobaki ni yetu wabunge na wajumbe walioteuliwa kuhakikisha tunafanya kazi tunayopaswa kuifanya kwa umakini ili kuwaletea watanzania kinachostahili. Uteuzi umefanywa kwa busara ya hali ya juu na kwa kuzingatia utaifa, naauunga mkono", alisema.
Sambamba naye ni Mng'ongo aliyepongeza uteuzi huo kwa kusema kuwa umeonyesha njia ya mafanikio katika kazi wanayokwenda kuifanya katika bunge hilo maalum la katiba kwa sababu imejumuisha makundi yote bila ubaguzi.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri(KKKT), Alex Malasusa amewaomba watanzania wauheshimu uteuzi uliofanywa na Rais Kikwete kwa sababu umegusa makundi yote.
“Wauheshimu uteuzi kwani sisi tunamshukuru mungu na ieleweke kuwa kibinadamu mtu hawezi kumridhisha kila mtu hivyo watu wapokee uteuzi huu. Hii ni njia ya kwenda kwenye katiba sahihi ,”alisema Askofu Malasusa.
Naye Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema uteuzi huo ni mzuri kwa sababu umezingatia nafasi za watu mbalimbali na asilimia 99 wana sifa na kuongeza “hiyo asilimia moja tunamuachia mungu. Rais Kikwete amefanya kazi nzuri kwa kugusa makundi yote”.
Katika hatua nyingine, Katibu wa Jukwaa la Wahariri, Nevil Meena alisema kuwa uteuzi kwa ujumla ni mzuri ingawa kwa namna fulani umewaminya wanahabari kutokana na kuwa na wawakilishi kutoka katika taasisi za vyombo vya habari, ambao si wanahabari wa moja kwa moja.
"Wanahabari hatujapata uwakilishi wa moja kwa moja kwa sababu hakuna mwanahabari aliyeteuliwa kutoka katika kundi la wanahabari wanaofanya kazi ya uandishi wa habari ndani ya televisheni, redio au majarida zidi wamechukuliwa kutoka katika taasisi ambazo haziufanyi uandishi wa habari moja kwa moja. Hii kwetu ni kuminywa", alisema.
Kwa upande wa Msemaji wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Tumaini Makene alisema chama chake kinayachambua kwa makini majina ya wajumbe hao na baadaye kitatoa maoni rasmi ya chama hicho.
Rais Kikwete amefanya uteuzi wa wajumbe hao 201 kwa kuzingatia jinsia ambapo wanaume 101 na wanawake 100 kutoka orodha ya makundi aliyopelekewa. Makundi hayo ni pamoja na Taasisi zisizokuwa za serikali; Taasisi za kidini, taasisi za elimu; vyama vya siasa; walemavu, vyama vinavyowakilisha wafugaji, wavuvi na wakulima na watu wenye malengo yanayofanana
No comments:
Post a Comment