Tuesday, February 4, 2014

VITA YA URAIS CCM YAWAPELEKA MWINYI, MKAPA DODOMA

h11 8958d
KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inatarajiwa kukutana mjini Dodoma Jumapili wiki hii, huku Baraza la Ushauri linaloundwa na marais wastaafu, likitarajiwa kuwasilisha taarifa ya hali ya chama hicho. (HM)
Habari za kuaminika zilizopatikana kutoka vyanzo mbalimbali ndani ya CCM, zinasema Baraza la Ushauri, linaloundwa na marais wastaafu, linatarajia kutoa tamko zito kutokana na mwenendo unaoonyeshwa na makada wake.

Baraza hilo, linaundwa na wenyeviti na makamu wastaafu wa chama, likiongozwa na Mwenyekiti wake, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Katibu wake ni Pius Msekwa.
Wengine ni Rais mstaafu Benjamin Mkapa, Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amani Abeid Karume na Waziri Mkuu mstaafu, John Malicela.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya kuibuka malumbano yanayowahusisha makada wa chama hicho wanaotajwa kuwania mbio za urais mwaka 2015 kuanza harakati mapema.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka CCM, kiliiambia MTANZANIA kuwa kikao cha CCM, pamoja na mengine, kitatoa dira ya chama na kuweka mikakati ya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
"CCM itakutana Februari 9, mwaka huu kati ya mjini Dodoma au Dar es Salaam, lakini katika kikao hicho wajumbe wa Baraza la Ushauri la chama watakuwepo.
"Sijui watazungumza nini katika kikao hicho, huenda ikawa haya mambo yanayoendelea ndani ya chama hivi sasa, kwani tambua wajumbe wa baraza wanaweza kuomba kukutana na CC au NEC wakati wowote pale wanapoona inafaa," kilisema chanzo hicho.
Katika siku za hivi karibuni, makada wa CCM wameibuka na kuunga mkono hatua ya Katibu wa Uhamasishaji wa Chipukizi, Paul Makonda, ambaye alimtuhumu Waziri Mkuu wa zamani, EdwardLowassa, kuwa ameanza harakati za kuwania urais.
Baada ya kauli hiyo, Malecela naye aliibuka na kuutaka uongozi wa CCM kumchukulia hatua Lowassa.
Malecela alidai, Lowassa anakiyumbisha chama hicho kutokana na kampeni za kutaka kuwania urais wa 2015.
Alisema Sekretarieti ya CCM inapaswa kuwachukulia hatua kali makada wanaojipitisha maeneo mbalimbali nchini kwa nia ya kusaka urais, kabla ya chama hicho kupanga muda. Chanzo: mtanzania

No comments:

Post a Comment