DAWA ZISIZOFAA KWA MATUMIZI YA BINADAMU ZIKICHOMWA MOTO |
WANAWAKE wameshauriwa kuacha kutumia
sabuni za kunawia sehemu za siri ambazo hudaiwa kurejesha ubikira kwani
zina madhara makubwa ikiwemo kusababisha kansa ya shingo ya kizazi.
Mkaguzi wa Dawa na Mfamasia wa Manispaa ya Dodoma Daria Mwanuka alisema
hayo mwishoni mwa wiki katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi
wakati wa uteketezaji dawa, vipodozi na vyakula visivyofaa kwa matumizi
ya binadamu.
Kazi hiyo ilifanywa na Mamlaka ya
Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Kati. Alisema kumekuwa na sabuni
mbalimbali ikiwamo Kaisiki ambapo wanaoziuza wanadai zimekuwa
zikisababisha bikira iliyopotea kurudi kitu ambacho si kweli.
“Sabuni hizo zinapunguza tu majimaji
yaliyo sehemu za siri za mwanamke jambo ambalo husababisha wakati wa
kufanya mapenzi mwanaume kupata ugumu kwenye muingiliano kwa vile mwili
unakuwa umekataliwa kutoa maji na hivyo kuleta michubuko kitu ambacho ni
hatari hasa wenye maambukizi ya magonjwa,” alisema.
Alisema michubuko inapotokea ni rahisi
mwanamke kuambukizwa magonjwa ya zinaa hata virusi vya Ukimwi. Mtaalamu
huyo alisema sabuni hizo zinatengeneza hali fulani ukeni lakini haiwezi
kurejesha hali ya maumbile iliyopotea.
Alisema wanaotumia sabuni hizo wako
katika hatari kubwa ya kuambukizwa magonjwa na hata kupata saratani ya
shingo ya uzazi kwani kemikali zinazotumika katika kutengeneza sabuni
hizo zina athari kubwa kiafya.
Alisema ni vyema wanawake wakatambua
thamani yao na kuachana na matumizi ya sabuni hizo ambazo hazina manufaa
yoyote na badala yake zimekuwa na madhara makubwa kwao.
Kwa upande wake, Fredrick Luyangi ,
Mkaguzi wa dawa kutoka TFDA alisema matumizi ya sabuni hizo huleta
athari kubwa mwilini na wakati mwingine kutengeneza kansa taratibu bila
mhusika kufahamu.
Alisema sabuni hizo husababisha kansa ya
kizazi na kubainisha sabuni hizo licha ya kupigwa marufuku zimekuwa
zikiuzwa kwenye maduka ya vipodozi.
Alisema mara nyingi kwenye operesheni
zinazofanyika zimekuwa zikiondolewa sokoni lakini hata hivyo zimekuwa
zikiingizwa kwa wingi hali inayofanya zoezi la kudhibiti kuwa gumu.
Alisema ni muhimu kwa wanawake kuacha
matumizi ya sabuni hizo ambazo zina madhara makubwa sana kwao kwani
zikikosa wanunuzi zitaondoka sokoni.CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment