Wednesday, February 5, 2014
MBOWE AMJIBU JK kwa kuwapotosha wananchi!!!!!!!
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuacha kutafuta huruma ya Watanzania juu ya suala la Katiba na badala yake atumie nafasi hiyo kuwataka wabunge wake kuheshimu maoni ya wananchi.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema kuwa hotuba ya Rais Kikwete juzi kwamba Katiba haiwezi kupatikana kwa ngumi imejaa upotoshaji kwa wananchi.
“Huku ni kuwadanganya wananchi, pale hakuna ngumi wala vurugu yoyote, kila ibara iliyopo katika rasimu itajadiliwa ili upatikane mwafaka. Huku ni kukosa ukomavu wa kisiasa. Ni vema Rais Kikwete akaacha kuhangaika na wapinzani, badala yake awe tayari kuheshimu mawazo ya wananchi waliyotoa wakati wa kutoa maoni ya Katiba” amesema Mbowe.
Mbowe alisema kuwa Rais Kikwete ni mwanasiasa na mtu anayejaribu kupotosha hoja, kwani CHADEMA waliposema watapambana, hawakumaanisha kupigana ngumi kama alivyosema kiongozi huyo.
“Katiba ni ya wananchi, si ya chama chochote cha siasa, ndiyo maana hatukubali kuona mawazo ya wananchi yakishindwa kuheshimiwa,” alisema.
Alisema kuwa CHADEMA itahakikisha inashindana kwa hoja katika Bunge la Katiba litakaloketi hivi karibuni na iwapo hilo litashindikana watarudi kwa wananchi ambao ndio wenye uamuzi wa mwisho juu ya suala hilo.
“Wajumbe watakaoshiriki Bunge la Katiba ni 640 ambao hao si waamuzi wa mwisho na kama tutaona kuna suala lolote linaloenda kinyume, sisi tutakachokifanya ni kurudi kwa wananchi kuwaeleza juu ya kilichotokea na hao ndio wenye maamuzi ya mwisho katika kura ya maoni,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment