Thursday, February 6, 2014

MBUNGE WA CHADEMA NA DIWANI KORTINI KWA KUJERUHI MKOANI SHINYANGA

Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki (Chadema), Sylvester Kasulumbayi.

 Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki (Chadema), Sylvester Kasulumbayi na Diwani wa Kata ya Buselesele, Crispian Kagoma na watu wengine 14 wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kujeruhi katika vurugu zilizoibuka katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Kasulumbayi na wenzake 15, ambao wanaaminika kuwa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kahama saa 8.00 mchana jana na kusomewa mashtaka sita kila mmoja.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama, Gadiel Mariki, Mwendesha Mashtaka Shukrani Madulu alisema washtakiwa wote kwa pamoja walitenda makosa hayo Februari 4, mwaka huu.
Madulu aliiambia mahakama hiyo kuwa washtakiwa hao wakiongozwa na mbunge huyo walitenda kosa hilo la kuwashambulia kwa mapanga wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa kampeni za kuwania udiwani wa Kata ya Ubagwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.
Alisema mashtaka matano ni kushambulia na kujeruhi kwa mapanga, na moja la kuharibu mali, ikidaiwa kuwa katika vurugu hizo washtakiwa waliishambulia gari la CCM la wilaya hiyo na kuliharibu.
Washtakiwa wote walikana mashtaka yote na kuomba mahakama iwape dhamana ili waendelee na kampeni za kumnadi mgombea wao wa nafasi ya udiwani katika kata hiyo ya Ubagwe.
Maombi hayo yalipingwa na Mwendesha Mashtaka, akiiomba mahakama isitoe dhamana kwa kuwa hali za majeruhi watatu ni mbaya kwa kuwa tayari wamepelekwa kwenye Hospitali ya Rufaa na Bugando mkoani Mwanza, baada ya matibabu yao kushindikana wilayani Kahama.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mariki alikubaliana na hoja hiyo na kuahirisha kesi hiyo hadi leo ambapo kesi hiyo itasikilizwa.
Watuhumiwa wote walipelekwa mahabusu baada ya dhamana hiyo kuzuiliwa.
Waliojeruhiwa kwenye vurugu
Wafuasi watano wa CCM wilayani Kahama akiwamo ofisa mtendaji wa Kata ya Ubagwe walijeruhiwa kwa mapanga kwenye vurugu hizo.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Andrew Emmanuel alisema Masunga, Kamaro na Peter walisafirishwa kwenda Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.
Chanzo cha vurugu
Vurugu hizo zilitokea juzi saa moja usiku katika Kata ya Ubagwe muda mfupi baada ya wafuasi hao kumaliza kampeni zao za kumnadi mgombea wa CCM, Hamis Majogolo anayewania udiwani kwenye kata hiyo.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo, wafuasi hao walikumbwa na mkasa huo wakati wakiwa kwenye gari la CCM ambalo pia lilikuwa na watuhumiwa watatu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema waliokuwa wakipelekwa Kituo Kidogo cha Polisi Bulungwa.
Ilidaiwa watuhumiwa hao nao walidaiwa kufanya fujo kwenye mkutano wa Kampeni wa Chama cha Tadea ambacho pia kina mgombea anayewania nafasi hiyo.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa wanachama wa Chadema waliweka kizuizi kwa kutumia gari la Kasulumbayi kwenye barabara ya kuelekea kituo kidogo cha polisi.
Peter, ambaye ni dereva wa gari la CCM alisimulia kuwa walipofika kwenye kizuizi hicho walisimama, ndipo wafuasi wa Chadema waliposhuka kwenye gari la Mbunge huyo na kuanza kuwashambulia kwa mapanga wakitaka kuwaokoa wenzao watatu.
Watatu wakamatwa Njombe
Pia Jeshi la Polisi wilayani Njombe linawashikilia watu watatu wanaodaiwa kufanya fujo katika ofisi ya CCM ya tawi la Matalawe, Jumatatu iliyopita.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Fulgence Ngonyani alisema kuwa watu hao walikwenda kwa gari kwenye maeneo ya tawi hilo na kuanza kuchana picha za mgombea udiwani wa CCM, Menard Mlyuka.
Aliwataja watu waliokamatwa kuwa ni Award Karonga (40), Ally Mhagama (43) na Robert Mabu (24).
Mwananchi

No comments:

Post a Comment